Connect with us

Siasa

Kambi za wavuvi zatibua utulivu kwa wanafunzi

Published

on

Uvuvi katika Ziwa Victoria, umekuwa ukihusisha kambi nyingi za wavuvi zilizosheheni idadi kubwa ya wavuvi wenye umri mkubwa na mdogo wanaokadiriwa kufikia 182,741 huku kukiwa  na vyombo vya uvuvi vinavyokadiriwa kufikia 28,470 (hii ni kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi ya 2012/2013).

Pamoja na ukweli kuwa zao la samaki na sekta ya uvuvi kwa ujumla, huchangia katika upatikanaji wa lishe bora, ajira, kipato kwa wananchi na kwa taifa, hivyo kuchangia sana katika kuondoa umasikini kwa umma; lakini licha ya faida yote hiyo kazi hii kwa huku imegeuka janga.

Janga hili linatokana na wanafunzi wa kike na kiume kukacha na wakati mwingine kuacha shule kabisa na kujitumbukiza kwenye kambi hizo za wavuvi, kutokana na sababu mbalimbali; kubwa ikitajwa kuwa ni umasikini.

Kufuatia hali hiyo, mwandishi wa makala hii amepata nafasi ya kufanya uchunguzi kwenye baadhi ya kambi zinazotajwa kuathiriwa zaidi na hali hiyo, ambapo ametembelea kambi mbalimbali zilizoko katika fukwe za visiwa vya Rukuba, Mroba na Masakala.

Ziara hiyo ya uchunguzi pia ilimchukua hadi visiwa vya Ryamgasile, Iriga, pamoja na fukwe maarufu za Bukima na Burungu, maeneo yote hayo yakiwa katika wilaya za Musoma vijijini na Butiama mkoani Mara, ambako alipata nafasi ya kuhojiana na wavuvi wenyewe, wanafunzi, viongozi wa serikali, maofisa wa elimu, walimu na wazazi.

Katika uchunguzi huo, pamoja na mambo mengine amebaini kuwepo kwa tatizo la utumikishwaji na ajira haramu za watoto kwenye baadhi ya kambi za wavuvi, sambamba na ngono zisizo salama, mikesha ya madisco na miziki ya kienyeji maarufu kama ‘Mazinduke’ bila kusahau mikesha ya picha za ngono.

Uchunguzi huo pia umewashuhudia baadhi ya wavulana wakiwasaidia wavuvi kuwaondoa samaki kwenye nyavu, kushona na kurekebisha nyavu; huku wenzao wa kike wakijishughulisha na kuwapikia wavuvi, kusaga unga na kwenda kuchanja kuni kwa ajili ya matumizi ya kila siku kwenye kambi hizo za wavuvi.

Nyamweko Mjinja (13) na Nyakaji Robert (15) ni wanafuzi wa Shule ya Msingi Burungu, ambao niliwashuhudia wakifanya maandalizi ya chakula kwa ajili kambi moja ndogo ya wavuvi iliyoko Burungu, ambapo walidai kuwa hawafanyi uchuuzi wa chakula bali wanafanya kazi ya kupika katika kambi hiyo kwa ujira.

“Huwa tunawapikia wavuvi chakula na kusenya (kuchanja) kuni…,wakitupatia pesa tunatumia kununua nguo na mahitaji mengine;..tunalazimika kufanya hivyo kwa sababu wazazi hawana pesa ndiyo maana hatuendi hata shuleni.” anasema Nyakaji huku akiungwa mkono na mwenzake.

Kwa mujibu wa wanafunzi hao; wanadai wamekuwa wakilipwa ujira wa kati ya shilingi elfu mbili na elfu tatu kwa siku kwa ajili ya kazi hizo, huku pia wakiambulia samaki kidogo kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, hali inayowashawishi baadhi ya wazazi wasio na uwezo, kufumbia macho utoro wa watoto wao shuleni.

Shughuli zote hizo ni kwa malipo kiduchu ya kati ya sh. 1500/= hadi 2000/= kwa siku na samaki kidogo kwa ajili ya matumizi nyumbani, huku wenzao wa kiume wakidaiwa kujipatia ujira wa kati ya shilingi 4,000 na 5,000 kwa siku kwa kusaidia uvuvi, kufua nyavu na kuzikarabati.

Kwakuwa wakazi wengi wa maeneo yanayopakana na kambi za uvuvi, huendesha maisha yao kwa kutegemea  shughuli za uvuvi, hali hiyo imeonekana kuwavutia siyo tu wanafunzi, bali hata walimu wao ambao baadhi wanamiliki zana za uvuvi ikiwa ni pamoja na kumiliki baadhi ya kambi za kuvulia samaki, hivyo kwa kiasi fulani kuathiri ratiba za masomo.

“Hata walimu tuna zana zetu za uvuvi kama sehemu ya kujiingizia kipato cha ziada ingawa haihusiani na ratiba yangu shuleni…, bahati mbaya hapa kwetu wanafunzi wengi wamekuwa watoro na wengine hata kuacha shule kwa sababu ya kushamiri kwa shughuli za uvuvi na tatizo la umasikini.” Anasema mwalimu Malima Ng’aranga wa Shule ya Msingi Burungu.

Hali kama hiyo pia iko katika kisiwa cha Rukuba hasa Shule ya Msingi Rukuba yenye wanafunzi 800, ambapo inadaiwa karibu asilimia 20% ya wanafunzi ama ni watoro wa kudumu ama wameacha shule kabisa kwa sababu ya kukimbilia kwenye kambi za wavuvi.

“Unajua kambi hizi za wavuvi ni hatari sana kuwa jirani na shule, wanafunzi wanapewa mimba, wanakesha kwenye miziki na picha za ngono…, hapa shuleni tuna wanafunzi takribani mia nane lakini zaidi ya 160 hawaonekani shuleni  kwa sababu kama hizo.” Anasema mwalimu Hamisi Maiga.

Aidha kumeripotiwa pia kuwepo kwa vitendo vya ngono, mimba zisizotarajiwa na maambukizi ya magonjwa ya zinaa miongoni mwa wanafunzi, ambapo takwimu zinaonesha katika shule mbili za msingi za Majita na Irugwa pekee, zaidi ya wanafunzi 15 walishindwa kumaliza shule kwa sababu za ujauzito katika kipindi cha kati ya mwaka 2011 na 2013. Hii ni kwa mujibu wa walimu wakuu wa shule hizo; Mwalimu Raymond kimaro (Majita) na Victor Luginya (Irugwa).

Kulingana na hali aliyoishuhudia mwandishi huyu ni kwamba, mikesha kwenye madisco na picha za video za ngono, hutawaliwa kwa kiasi kikubwa na baadhi ya wanafunzi wa kike na kiume, sanjari na wavuvi wanaotumia kila aina ya kilevi kutokana na vipato vikubwa vya pesa zinazotokana na shughuli za uvuvi.

John Mwanjara ni mmiliki wa Duka la Dawa Muhimu katika kisiwa kikubwa cha Irugwa; yeye anasema kuwa wateja wake wakubwa huja kununua dawa zinazohusiana na magonjwa ya zinaa, huku akitanabaisha kwamba matumizi ya mipira ya kuzuia uzazi (condom), ya kiume na kike ni madogo sana.

“Nimekuwa naifanya biashara hii ya kuuza madawa ya binadamu kwa muda mrefu sana hapa kisiwani, lakini licha ya kushamiri kwa vitendo vya ngono na ulevi bado matumizi ya kinga ya ngono ni madogo sana…, hapa siyo salama …huwenda hata maambukizi ya ukimwi yakawa ni makubwa.” Anasema Mwanjara.

Nilitinga ofisini kwa Afisa Mtendaji wa Kata ya Bukima, kutaka kujua serikali kwa upande wake inalizungumziaje tatizo hilo; ambapo pamoja na majibu mengine, afisa huyo alikiri kuwepo kwa changamoto hiyo kwa wanafunzi na walimu wanaopakana na kambi za wavuvi.

Aidha alilalamikia pia kutokuwepo kwa Vituo vya Polisi karibu na maeneo hayo ya kambi za wavuvi, jambo linalopelekea baadhi ya watu kutokujali sheria na amri za serikali, licha ya kuwa wapo baadhi ya watendaji wadogo wadogo wa serikali ambao hujinufaisha kutokana na kambi hizo, hivyo kujikuta wakishindwa kuchukua hatua yoyote dhidi ya wavuvi wanaokiuka sheria za nchi.

“Ni kweli tunazo taarifa za matukio kama hayo huko kwenye kambi za wavuvi, lakini sasa  baadhi ya wazazi na watendaji wadogo wadogo wa serikali, wamekuwa wakishindwa kuwachukulia hatua watu kama hao, kutokana na ama kutokuwepo vituo vya polisi ama rushwa ya pesa na kitoweo kutoka kwa wavuvi” anasema Mtendaji Kata huyo, Tumaini Mugeta.

Kwa kuhitimisha uchunguzi wake, mwandishi wa makala hii alifika pia ofisini kwa Afisa Elimu Shule za Msingi, Musoma Vijijini, Boniphace Magesa ambaye hakukiri moja kwa moja wala kukanusha kuwepo kwa tatizo hilo, ingawa alikiri kuwepo kwa utoro, ufahuru duni na kudorora kwa kiwango cha elimu katika maeneo hayo.

Magesa anadai kuwa hilo tatizo lilikuwepo kwa kiasi kikubwa hapo siku za nyuma, lakini baada ya kufuatilia na kuhimiza uwajibikaji kwa walimu wanaofundisha kwenye maeneo hayo,  ikiwa ni pamoja  na kutishia kuwachukulia hatua wazazi wa wanafunzi wanaotorokea  kwenye kambi za wavuvi, walau tatizo hilo lina unafuu kidogo.

“Nipe nafasi nikutafutie data kamili kuhusiana na changamoto hiyo, kwa sasa sina taarifa sahihi kuhusiana na swali lako, lakini hayo uliyoyasema yanaweza kuwa na  ukweli…, siku za nyuma hali ilikuwa mbaya lakini tumekemea kemea kufuatia kukithiri kwa utoro na kushuka kwa kiwango cha ufahuru,…, walau sasa hali siyo mbaya sana,… anyway nipe nafasi nitakutafutia data kamili…” anasema Magesa.

Pamoja na Sera ya Elimu ya Mwaka 1995 sambamba na sheria ndogo ndogo (by- lows) kuwabana  wazazi dhidi ya kutowapeleka watoto shule na kufuatilia maendeleo yao kielimu, bado sheria hizo zimekuwa zikipuuzwa na baadhi ya watendaji wa Serikali na wazazi, licha ya kusimamiwa kwa karibu na Kamati za Shule zinazowajumuisha pia wazazi hao hao!.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Siasa

Sakata la waraka wa Maaskofu KKKT lang’oka na Msajili Mambo ya Ndani

Published

on

Waziri wa Mambo ya Ndani Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Usajili wa Jumuiya za Kidini na Vyama vya Kijamii, Merlin Komba ili kupisha uchunguzi wa barua iliyoandikwa ukilitaka Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kufuta waraka ilioutoa Machi mwaka huu.

Barua iisambazwa kwenye mitandao ya kijamii ikiitaka KKKT kuufuta waraka wa Pasaka uliotolewa Machi 24 mwaka huu vinginevyo hatua kali za sheria zitachukuliwa dhidi ya kanisa hilo.

Waraka huo uliopewa jina la ‘Taifa letu amani yetu’ ulisainiwa na maaskofu 27 wa kanisa hilo. Ulijikita kujadili masuala ya jamii, uchumi, siasa, katiba mpya na matukio ambayo yako kinyume na kile lilichokiita tunu na misingi ya Taifa.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Waziri Nchemba amesema Serikali haipingani na dhehebu lolote na pale ambapo kuna uhitaji wa kufanyia kazi jambo kuhusu taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo taratibu huwa zinatumika kuzungumza na sio kama ilivyofanywa taarifa hiyo inayosambaa.

“Serikali inalinda uhuru wa kuabudu na waumini hivyo huo waraka una maudhui kama matatu, ni barua batili na tunaendelea kuchunguza kama imetengenezwa basi imetengenezwaje, kwani haujapita kwetu.” amesema Waziri Mwigulu.

Kutokana na msimamo huo wa serikali, Waziri Nchemba, amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Usajili wa Jumuiya za Kidini na Vyama vya Kijamii, Merlin Komba, kupisha uchunguzi wa barua iliyoandikwa kwa maaskofu wa KKKT.

“Hivyo basi, namsimamisha Msajili wa hizo taasisi kupisha uchunguzi na ikithibitika ni za Wizara tuweze kujua maana jambo hilo halijapita kwa Waziri, Katibu Mkuu na wala si maelekezo ya serikali,” amesema.

Hata hivyo, amewatoa hofu viongozi wa dini kutokana na sakata hilo na kuwataka waendelee na majukumu yao huku ikitahadharisha jamii kuwa makini na taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

“Tunawaomba viongozi wa dini waendelee na kazi zao, nasema jamii iwe macho na taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya jamii na wasifanyie kazi taarifa hizo. Viongozi wa dini wasiwe na taharuki na taarifa hizo, hazina baraka za Serikali na wasisite kuwasiliana na Serikali kujua uhalali wake,” amesema.

Waziri Nchemba amesema waraka wa viongozi wa dini uliotolewa miezi iliyopita ni jambo lililopita na hakukuwa na haja ya kuendeleza malumbano yasiyo na tija kwenye jamii.

Katika waraka wa ujumbe wa pasaka uliosomwa katika makanisa ya Kilutheri kote nchini Tanzania na kusambaa katika mitandao ya kijamii, baraza hilo limeorodhesha mambo kadhaa ambayo wameyataja kuwa ndio tishio la umoja na amani ya nchi hiyo.

Utekwaji wa watu wa hivi karibuni, utesaji, kupotea kwa watu, mashambulizi ya silaha dhidi ya viongozi wa kisiasa, muaji yenye mwelekeo wa kiitikadi, vitisho, ubambikiziaji wa kesi, na matumizi mabaya ya vyombo vya dola dhidi ya wananchi ni baadhi tu ya mambo yaliyotajwa katika waraka huo.

Lakini pia Watanzania wamekuwa na hisia tofauti kuhusu viongozi wa dini kuzungumzia hali ya kisiasa nchini. Waraka wa KKKT ulikuja mwezi mmoja baada ya ule wa maaskofu wa kanisa katoliki ambao nao ulionya juu ya kuminywa kwa haki ya kufanya shughuli za kisiasa kama mikutano ya hadhara na maandamano.

Baada ya nyaraka hizo mbili kutolewa na Maaskofu, baadhi ya mambo yaliyokuwa yakilalamikiwa yalipata ufumbuzi ikiwemo kupungua kwa mauaji na uteswaji wa raia kulikuwa kunafanywa na watu wasiojulikana.

Continue Reading

Jamii

Waziri Mkuu Majaliwa: Hatutangazi nyongeza ya mshahara hadharani kuepusha athari kwa jamii

Published

on

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameweka wazi kuwa serikali haitatangaza nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa umma hadharani ili kuepusha athari kwa jamii ikiwemo kupanda kwa bei ya bidhaa.

Akizungumza leo Bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalumu (CHADEMA), Susan Lymo ambaye alitaka kufahamu kwanini Serikali imewanyima au imeshindwa kuwalipa watumishi wa umma nyongeza ya mishahara ambayo ni haki yao ya msingi kulingana na miaka waliyokaa kazini.

Akijibu swali la Mbunge huyo, Waziri Mkuu Majaliwa amesema Serikali ina utaratibu wa kutoa nyongeza ya mishahara kwa watumishi wake lakini haitangazi kwa wananchi wote kama ambavyo imekuwa ikifanyika kwenye sherehe za wafanyakazi za Mei Mosi kila mwaka.

Amesema Serikali ikitangaza mishahara hadharani inaweza kusababisha usumbufu kwa watu wasio watumishi wa umma na inaweza kupandisha bei ya bidhaa na kuathiri mwenendo wa mahitaji ya wananchi sokoni.

Nyongeza za mishahara ambazo zinatangazwa hadharani, mara nyingi zina athari yake sio kwamba Serikali haikusudii kutoa nyongeza ya mshahara kwa mwaka, lakini unapotumia Mei Mosi kutangaza nyongeza ya mshahara unaleta athari kwenye jamii kwasababu vitu vinaweza vikapanda bei, vikawasumbua hata na wananchi ambao hawalipwi mshahara,” amesema Waziri Mkuu.

Amebainisha kuwa siyo lazima Serikali itangaze hadharani kila inapoongeza mishahara kwa watumishi wa umma lakini ifahamike kuwa Serikali ina utaratibu wake mzuri wa kuboresha stahiki za wafanyakazi wake kila mwaka.

Suala la nyongeza ya mishahara liko Serikalini na Mhe Rais ameishawahakikishia wafanyakazi atawaongeza mishahara na sio lazima litangazwe hadharani. Mshahara ni suala la mtu binafsi hata ukiongezwa leo kuwa tumeitangaza leo tumeongeza mshahara kwa kiwango hiki. Ukifanya hivi tayari umeleta kupanda kwa gharama’” amebainisha Waziri Mkuu.

Ameongeza kuwa mkakati wa Serikali ni kupunguza gharama za mahitaji kwenye masoko ili kuzuia mfuko wa bei za bidhaa.

Hata hivyo, Waziri Mkuu Mjaliwa amesema Serikali inaendelea kufanya sensa ya watumishi wote nchi nzima na zoezi hilo likikamilika itaboresha nyongeza ya mwaka, nyongeza ya mishahara na upandishaji wa madaraja.

Awali katika swali lake, Mbunge Lyima amesema Serikali inakiuka Sheria ya Utumishi wa Umma ya kuwapatia watumishi stahiki zao na kuwapunguzia motisha ya kufanya kazi kwa ufanisi katika maeneo yao ya kazi na kuathiri mafao baada ya kustaafu.

Hoja ya Mbunge huyo ni muendelezo wa malalamiko ya watumishi dhidi ya Serikali kwamba hawajapata stahiki zao tangu ilipoanza zoezi la ukakiki wa watumishi wa umma mwaka 2015. Katika zoezi hilo watumishi zaidi ya 9,000 walibainika kutokukidhi vigezo vya utumishi na hivyo kuondolewa kazini.

Huenda kauli aliyoitoa Waziri Mkuu leo Bungeni inaweza ikatofautiana na ile ya Rais John Magufuli aliyoitoa wakati wa sherehe za Mei Mosi, 2018 mijini Iringa ambapo alinukuliwa akisema hawezi kutoa nyongeza ya mishahara akidai Serikali haina fedha.

Kwangu mimi ninafikiria hizi pesa tunazotoa kwa ajili ya elimu bure ni nzuri kuliko fedha hizo kuzipeleka kuongezea mishahara, naona bora kuwapa mikopo wanafunzi wa vyuo vikuu kuliko kuongezea wafanyakazi mishahara,

Nikisema nitaongeza hizo pesa mimi nitazitoa wapi? naogopa kusema uongo. Hata mimi napenda kupandishiwa mshahara lakini kwa hali halisi ya sasa hivi lazima niwaeleze ukweli,” alinukuliwa Rais Magufuli.

Hata hivyo alibainisha kuwa kabla ya kuondoka madarakani ataboresha maslahi ya wafanyakazi wa umma, “Nawaahidi, kipindi changu cha urais hakitaisha kabla sijapandisha mishahara kwa wafanyakazi, kupandisha kwangu haitakuwa kwa shilingi elfu kumi, itakuwa ni kupandisha kwelikwel.”

Continue Reading

Jamii

Maaskofu KKKT wapewa siku 10 kufuta waraka

Published

on

Serikali imetoa siku 10 kwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), kuufuta kwa maandishi waraka wao waliotuoa Machi 24 mwaka huu na kisha kuujulisha Umma kwa njia mbalimbali walizotumia kuusambaza.

Kanisa la KKKT kupitia Baraza lake la Maaskofu lilitoa waraka uliopewa jina la ‘Taifa Letu Amani Yetu’ wakati wa Pasaka ambao mbali na masuala ya kiroho, ulibainisha mambo kadhaa yanayogusa mstakabali wa taifa.

Katika mitandao ya kijamii leo imesambazwa barua yenye kumbukumbu no. SO.748/25 inayoonyesha imeandikwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama Wizara ya Mambo ya Ndani kwenda kwa Mwenyekiti /askofu Mkuu wa KKKT iliyoandikwa Mei 30, 2018 ikitoa maelekezo ya kufutwa waraka huo ndani ya siku 10 tangu ilipoandikwa barua hiyo.

Ikiwa na kichwa cha habari ‘Ujumbe wa Baraza la Maaskofu wa KKKT’ barua hiyo inaeleza baraza hilo halitambuliki kisheria katika ofisi ya msajili.

“Unaelekezwa kuufuta waraka husika kwa maandishi na kuujulisha umma kuwa taasisi yako haikuwa na haina uwezo kisheria kufanya kile mlichokifanya. Maandishi hayo yaufikie umma wa Watanzania kwa kupitia vyombo vya habari na njia zingine zilezile zilizotumika kuufikisha waraka ule mliouita ‘Ujumbe wa Baraza la Maaskofu KKKT’.

Hata hivyo, barua hiyo imetoa onyo kali kwa taasisi hiyo dini nchi kutekeleza agizo mara moja la sivyo itachukuliwa hatua za kisheria.

“Maelekezo haya yatekelezwe ndani ya siku kumi tangu kupokea kwa barua hii vinginevyo hatua kali zaidi za kisheria zitachukuliwa dhidi ya taasisi hii,” inasema barua hiyo.

Ikumbukwe kuwa  waraka huo ulisainiwa na maaskofu 27 wa kanisa hilo nchini na kutaja baadhi ya mambo hayo kuwa ni pamoja na utekaji, utesaji, kupotea kwa watu, mashambulizi ya silaha dhidi ya viongozi wa kisiasa, mauaji yenye mwelekeo wa kiitikadi, vitisho, ubambikiziaji wa kesi, na matumizi mabaya ya vyombo vya dola dhidi ya wananchi.ni hali ya kijamii na kiuchumi, maisha ya siasa, na masuala mtambuka likiwamo suala la Katiba Mpya.

Waraka uliongeza pia kwamba uhuru wa kujieleza, kutoa na kupokea habari umeendelea kutoweka nchini huku ukionya kubanwa na hatimaye kuelekea kupungua kwa uhuru wa Bunge, Mahakama, na Tume ya Uchaguzi, ukisema hatua hii ni pamoja na kudhoofishwa kwa serikali za Mitaa.

Lakini kabla ya KKKT kutoa waraka wao, Kanisa Katoliki nalo lilitoa waraka kama huo likionya baadhi ya mambo ikiwemo uminywaji wa misingi ya demokrasia ya vyama vingi na uhuru wa kujieleza.

Baada ya kusambaa kwa waraka huo, yalijitokeza mambo mengi ikiwemo kutofautiana na kwa mawazo ya wananchi kuhusu wajibu wa viongozi wa dini katika kutoa ushauri, kuonya au kukemea pale mambo yanapoenda mrama.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa na Maaskofu wa KKKT

Hata hivyo, barua hiyo imepokelewa kwa hisia tofauti na watumiaji wa mitandao ya kijamii ikizingatiwa kuwa suala hilo lilijadiliwa na kupita, iweje linaibuka tena wakati huu ambapo kuna utulivu na yale mambo waliyoyapigia kelele na maaskofu  yamepungua ikiwemo kuteswa, kupotea kwa watu na vitisho dhidi ya viongozi wa kisiasa.

 

Wananchi bado wanawaamini viongozi wa dini

Wadau mbalimbali wa masuala ya kijamii wamesema kama kweli barua hiyo imetolewa na serikali, inaweza kuchochea taharuki zaidi kwa waumini wa kanisa hilo na wananchi kwasababu linagusa moja kwa moja imani zao.

Amebainisha kuwa bado waumini wengi wana imani na viongozi wao dini na kwamba yale wanayotamka yanakuwa na nia njema kwa jamii yao. Na katika muktadha huo serikali inapaswa kuwa makini ili kuepusha matatizo zaidi yanayoweza kutokea.

Akizungumza na FikraPevu, Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena amesema kama serikali ilibaini kuna tatizo kwenye usajili wa Baraza la Maaskofu la KKKT ingekaa na wahusika na kulimaliza kuliko kujitokeza hadharani na kuendeleza jambo ambalo limepita.

“Mimi namwamini Mungu kuliko serikali na viongozi wangu wa dini hasa Maaskofu. Hivyo serikali inapaswa kuwa makini na mambo yanayogusa imani za watu. Katika hili walipaswa kutafakari sana jinsi ya kushughulika nalo. Vinginevyo halina afya kwa ustawi wa taifa letu,” amesema Meena.

Amesema Maaskofu walitimiza wajibu wao wa kuonya kabla mambo hayajaharibika na serikali inapaswa kuyafanyika kazi yale yalyotajwa kwenye waraka au kukaa kimya ili kuepusha migongano isiyo na faida kwa taifa.

Continue Reading

Muhimu Kusoma