Connect with us

Siasa

Asilimia 48 ya wananchi wanataka mchakato wa katiba uanze upya

Published

on

Vuguvugu la kufufua mchakato wa Katiba Mpya limeendelea kujitokeza kwa sura mpya ambapo uchunguzi uliofanywa na Shirika la Twaweza unaoonyesha kuwa wananchi wengi wanataka katiba mpya inayoakisi matakwa yao.

Akiwasilisha matokeo hayo ya uchunguzi wa Sauti za Wananchi kuhusu Kukwama kwa Mchakato wa Marekebisho ya katiba leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Twaweza, Aidan Eyakuze amesema  wananchi wengi wanataka mchakato wa Katiba Mpya ufufuliwe lakini wanatofautiana katika njia za kuuendea mchakato wa kupatikana kwa katiba.

“Matokeo haya yanatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,745 kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara mwezi Juni hadi Julai 2017.  Asilimia 67 ya watanzania wanasema ni muhimu kwa Tanzania kupata katiba mpya” amesema Eyakuze.

Wananchi 2 kati ya 3 waliowahoji katika uchunguzi huo wamesema njia nzuri ya kufufua mchakato wa katiba ni kuanza upya na tume mpya. Hili kundi ni kubwa na linashauri mchakato wote wa awali uwekwe pembeni na Tume mpya ya kukusanya maoni iundwe na wananchi watoe maoni yao.

“Karibu nusu ya wananchi (48%) wanasema kuwa njia nzuri ya kufufua mchakato wa mabadiliko ya katiba ni kuanza mchakato huo mpya” amesema Eyakuze.

Wananchi wengine wamependekeza kuwa Rasimu ya Warioba (New Constitution) ambayo iliwasilishwa katika bunge la Katiba ndio ipigiwe kura na wananchi kwasababu wakati wa kukusanya maoni ilizingatia maoni mengi ya wananchi. Pia wameikataa Katiba ya Chenge iliyopendekezwa na wabunge wa Bunge la Katiba ambayo ilibeba maslahi mengi ya wanasiasa kuliko wananchi.

Aidan Eyakuze anaeleza kuwa “ Wananchi wawili kati ya kumi (18%) wanasema njia nzuri ni kwenda moja kwa moja na kuipigia kura rasimu ya Warioba. Wananchi waliokuwa na uelewa wa maana ya katiba walionesha kupendelea zaidi kufufua mchakato wa mabadiliko ya katiba kwa kupigia kura rasimu ya katiba ya Warioba; asilimia 25 ikilinganishwa na asilimia 18”

Lakini idadi ya wananchi wanaopendekeza rasimu ya Warioba ni ndogo ikilinganishwa na wale wanaosema mchakato uanze upya kwasababu uligubikwa na tofauti kubwa za kisiasa na hata kuharibu kazi yote aliyoanzisha Rais mstaafu Jakaya Kikwete. Hii inaweza kutafsiriwa kama kiu waliyonayo wananchi kuipata katiba mpya ambayo kwa sehemu inakwamishwa na wanasiasa ambao wanatetea maslahi yao ya kuendelea kushika dola.

Hisia hizo za wananchi zimeendelea kujitokeza katika uchunguzi huo ambapo mwananchi 1 kati ya 10 anasema ili tupate katiba mpya tumalizie mchakato wa kuipigia kura rasimu ya Chenge/ Katiba Pendekezwa. Katiba hiyo ilikataliwa na baadhi ya wabunge wa Bunge la Katiba ambapo walisusia mchakato huo baada ya maoni yao kukataliwa.

“Idadi ndogo ya asilimia 13 ya wananchi wanasema njia sahihi ni kuipigia kura rasimu ya Chenge/Katiba inayopendekezwa, wakati wananchi wachache sana (6%) wanasema mchakato uanze upya na Bunge jipya au rasimu ipelekwe bungeni ili wabunge wafanyie kazi toleo jipya”.

Hata hivyo, uchunguzi huo wa sauti za wananchi uliwauliza ni toleo gani litumike kama sehemu ya kuanzia majadiliano iwapo mchakato wa katiba utaanzishwa tena?

Ambapo Wananchi wanne kati ya kumi (38%) wanasema tuanze “ukurasa mpya” na wananchi watatu katika ya kumi (31%) wanasema rasimu ya Tume ya mabadiliko ya Katiba (rasimu ya Warioba) itumike.

Ili kukwepa gharama za kifedha na kupoteza muda kuanza mchakato wa kuunda tume mpya na kukusanya maoni, baadhi ya wananchi  (43%)walionesha kupendelea zaidi kufufua mchakato wa mabadiliko kwa kurejea kwenye rasimu ya katiba ya Warioba na kuanza hapo.

Maoni ya Wadau kuhusu uchunguzi

Msemaji  wa Chama Cha ACT-Wazalendo, Ado Shaibu amesema matokeo ya uchunguzi wa Twaweza ni muendelezo wa utamaduni wa kufanya tafiti za kisayansi ambazo zinaakisi hali halisi ya jamii yetu. Amesema kuwa kusitishwa kwa mchakato wa katiba mpya baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2015 kulizima sauti za wananchi ambao walitaka kusikika kwenye katiba.

“Katiba ni jambo la kimuafaka hata kama hatulipendi, msingi wa mambo yote katika nchi ni katiba. Utafiti huu umeonyesha wananchi wengi wanahitaji katiba mpya lakini mchakato mzima wa katiba mpya umezima sauti za wananchi”.

Ameongeza na kusema kuwa mchakato wa katiba ulikwama kwasababu ya kuibuka vikundi vyenye maslahi kutoka katika vyama vya siasa ambavyo vilikuwa vinapigania kushika madaraka.

Naye Katibu wa Itikadi, Siasa na Uenezi wa  CCM, Humphrey Polepole amesema uchunguzi huo wa Twaweza amegundua kuwa watanzania wengi wanataka ukatiba na sio katiba iliyoandikwa. Amesema mahitaji makubwa ya wananchi ni viongozi waadilifu wenye uwezo wa kusimamia rasilimali za nchi.

“Watanzania kwa takwimu hizi za Twaweza wanataka kuona Ukatiba (Constituonalism) kuliko katiba (Constitution) nchini. Watu wa kawaida wanataka viongozi waadilifu, wasiokula rushwa, wanaojua cheo ni dhamana huo ndio ukatiba” amesema Polepole,

“Ukatiba ni kuwekeana mifumo hata kama haikuandikwa mahali, kila mtu akielewa hii mifumo hakutakuwa na tatizo. Tunaweza kuaandaa katiba na kuiweka kwenye kitabu lakini bila Ukatiba hakuna atakayeifuata”.

Wakati huo huo amesema katiba ni muhimu kwa taifa lakini wao kama Chama Cha Mapinduzi wanaona sio wakati mwafaka wa kufufua mchakato wa katiba mpya na wataruhusu jambo hilo hapo baadaye.

Kwa upande wake Mjumbe wa Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA), Deogratius Bwire amesema suala katiba lisichukuliwe kisiasa kwasababu wananchi wanyonge wanahitaji katiba bora itakayowahakikishia upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii ikiwemo maji, elimu, huduma za afya na nishati.

“Wananchi wanaahidiwa vitu lakini hakuna sehemu inayompa nguvu ya kudai vitu vile wakinyimwa. Tunaposema tuwe na ukatiba wa kukubaliana bila maandishi, nini kitatokea pale makubaliano haya yatakaposahaulika?”

 

Kukwama kwa Mchakato Wa Katiba Mpya

Ikumbukwe kuwa mchakato wa kuipata katiba mpya ulianza miaka mingi iliyopita lakini ulipata nguvu mwaka 2011 baada ya wadau na wananchi kuishinikiza serikali kuanza mchakato huo.

Rais wa awamu ya nne Jakaya Kikwete alikubali na kuteua Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ilikusanya maoni kutoka kwa wananchi.

Katiba hiyo ilipitia michakato mbalimbali na ilipofika katika Bunge la Katiba ulikwama kutokana na  wabunge wa bunge hilo kushindwa kufikia muafaka na kuipitisha Katiba ya Warioba. Mabadiliko kadhaa yalifanyika katika Katiba ya Warioba na baadaye ikaitwa Katiba Pendekezwa ambayo inatajwa kuacha maoni mengi ya wananchi.

Hata alipoingia madarakani Rais John Magufuli hakuonyesha nia ya kuendeleza mchakato huo wa kuwapatia wananchi katiba mpya kwa madai kuwa katiba siyo kipaumbele chake.

Hata hivyo makundi mbalimbali zikiwemo  Asasi za Kiraia na wanaharakati wameendelea kupaza sauti kuishinikiza serikali kukamilisha mchakato wa kupatikana kwa katiba mpya.

Katika kuendeleza majadiliano ya katiba, Shirika la Twaweza limekuja na matokeo ya uchunguzi ambao ulihusisha sauti za wananchi ambao wamesema wananchi wengi wanapenda kuona mchakato wa katiba mpya ukifufuliwa na kukamilishwa kwa wakati.

Inaeelezwa kuwa Afrika Kusini na Kenya ndio nchi pekee ambazo zina katiba bora miongoni mwa ncho zote barani Afrika ambapo zimezingatia zaidi uhuru wa wananchi katika kujieleza, kupata taarifa na kujenga mifumo imara ya kitaasisi ambayo inaendeshwa kwa uwazi na ukweli.

 

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Siasa

Sakata la waraka wa Maaskofu KKKT lang’oka na Msajili Mambo ya Ndani

Published

on

Waziri wa Mambo ya Ndani Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Usajili wa Jumuiya za Kidini na Vyama vya Kijamii, Merlin Komba ili kupisha uchunguzi wa barua iliyoandikwa ukilitaka Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kufuta waraka ilioutoa Machi mwaka huu.

Barua iisambazwa kwenye mitandao ya kijamii ikiitaka KKKT kuufuta waraka wa Pasaka uliotolewa Machi 24 mwaka huu vinginevyo hatua kali za sheria zitachukuliwa dhidi ya kanisa hilo.

Waraka huo uliopewa jina la ‘Taifa letu amani yetu’ ulisainiwa na maaskofu 27 wa kanisa hilo. Ulijikita kujadili masuala ya jamii, uchumi, siasa, katiba mpya na matukio ambayo yako kinyume na kile lilichokiita tunu na misingi ya Taifa.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Waziri Nchemba amesema Serikali haipingani na dhehebu lolote na pale ambapo kuna uhitaji wa kufanyia kazi jambo kuhusu taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo taratibu huwa zinatumika kuzungumza na sio kama ilivyofanywa taarifa hiyo inayosambaa.

“Serikali inalinda uhuru wa kuabudu na waumini hivyo huo waraka una maudhui kama matatu, ni barua batili na tunaendelea kuchunguza kama imetengenezwa basi imetengenezwaje, kwani haujapita kwetu.” amesema Waziri Mwigulu.

Kutokana na msimamo huo wa serikali, Waziri Nchemba, amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Usajili wa Jumuiya za Kidini na Vyama vya Kijamii, Merlin Komba, kupisha uchunguzi wa barua iliyoandikwa kwa maaskofu wa KKKT.

“Hivyo basi, namsimamisha Msajili wa hizo taasisi kupisha uchunguzi na ikithibitika ni za Wizara tuweze kujua maana jambo hilo halijapita kwa Waziri, Katibu Mkuu na wala si maelekezo ya serikali,” amesema.

Hata hivyo, amewatoa hofu viongozi wa dini kutokana na sakata hilo na kuwataka waendelee na majukumu yao huku ikitahadharisha jamii kuwa makini na taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

“Tunawaomba viongozi wa dini waendelee na kazi zao, nasema jamii iwe macho na taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya jamii na wasifanyie kazi taarifa hizo. Viongozi wa dini wasiwe na taharuki na taarifa hizo, hazina baraka za Serikali na wasisite kuwasiliana na Serikali kujua uhalali wake,” amesema.

Waziri Nchemba amesema waraka wa viongozi wa dini uliotolewa miezi iliyopita ni jambo lililopita na hakukuwa na haja ya kuendeleza malumbano yasiyo na tija kwenye jamii.

Katika waraka wa ujumbe wa pasaka uliosomwa katika makanisa ya Kilutheri kote nchini Tanzania na kusambaa katika mitandao ya kijamii, baraza hilo limeorodhesha mambo kadhaa ambayo wameyataja kuwa ndio tishio la umoja na amani ya nchi hiyo.

Utekwaji wa watu wa hivi karibuni, utesaji, kupotea kwa watu, mashambulizi ya silaha dhidi ya viongozi wa kisiasa, muaji yenye mwelekeo wa kiitikadi, vitisho, ubambikiziaji wa kesi, na matumizi mabaya ya vyombo vya dola dhidi ya wananchi ni baadhi tu ya mambo yaliyotajwa katika waraka huo.

Lakini pia Watanzania wamekuwa na hisia tofauti kuhusu viongozi wa dini kuzungumzia hali ya kisiasa nchini. Waraka wa KKKT ulikuja mwezi mmoja baada ya ule wa maaskofu wa kanisa katoliki ambao nao ulionya juu ya kuminywa kwa haki ya kufanya shughuli za kisiasa kama mikutano ya hadhara na maandamano.

Baada ya nyaraka hizo mbili kutolewa na Maaskofu, baadhi ya mambo yaliyokuwa yakilalamikiwa yalipata ufumbuzi ikiwemo kupungua kwa mauaji na uteswaji wa raia kulikuwa kunafanywa na watu wasiojulikana.

Continue Reading

Jamii

Waziri Mkuu Majaliwa: Hatutangazi nyongeza ya mshahara hadharani kuepusha athari kwa jamii

Published

on

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameweka wazi kuwa serikali haitatangaza nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa umma hadharani ili kuepusha athari kwa jamii ikiwemo kupanda kwa bei ya bidhaa.

Akizungumza leo Bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalumu (CHADEMA), Susan Lymo ambaye alitaka kufahamu kwanini Serikali imewanyima au imeshindwa kuwalipa watumishi wa umma nyongeza ya mishahara ambayo ni haki yao ya msingi kulingana na miaka waliyokaa kazini.

Akijibu swali la Mbunge huyo, Waziri Mkuu Majaliwa amesema Serikali ina utaratibu wa kutoa nyongeza ya mishahara kwa watumishi wake lakini haitangazi kwa wananchi wote kama ambavyo imekuwa ikifanyika kwenye sherehe za wafanyakazi za Mei Mosi kila mwaka.

Amesema Serikali ikitangaza mishahara hadharani inaweza kusababisha usumbufu kwa watu wasio watumishi wa umma na inaweza kupandisha bei ya bidhaa na kuathiri mwenendo wa mahitaji ya wananchi sokoni.

Nyongeza za mishahara ambazo zinatangazwa hadharani, mara nyingi zina athari yake sio kwamba Serikali haikusudii kutoa nyongeza ya mshahara kwa mwaka, lakini unapotumia Mei Mosi kutangaza nyongeza ya mshahara unaleta athari kwenye jamii kwasababu vitu vinaweza vikapanda bei, vikawasumbua hata na wananchi ambao hawalipwi mshahara,” amesema Waziri Mkuu.

Amebainisha kuwa siyo lazima Serikali itangaze hadharani kila inapoongeza mishahara kwa watumishi wa umma lakini ifahamike kuwa Serikali ina utaratibu wake mzuri wa kuboresha stahiki za wafanyakazi wake kila mwaka.

Suala la nyongeza ya mishahara liko Serikalini na Mhe Rais ameishawahakikishia wafanyakazi atawaongeza mishahara na sio lazima litangazwe hadharani. Mshahara ni suala la mtu binafsi hata ukiongezwa leo kuwa tumeitangaza leo tumeongeza mshahara kwa kiwango hiki. Ukifanya hivi tayari umeleta kupanda kwa gharama’” amebainisha Waziri Mkuu.

Ameongeza kuwa mkakati wa Serikali ni kupunguza gharama za mahitaji kwenye masoko ili kuzuia mfuko wa bei za bidhaa.

Hata hivyo, Waziri Mkuu Mjaliwa amesema Serikali inaendelea kufanya sensa ya watumishi wote nchi nzima na zoezi hilo likikamilika itaboresha nyongeza ya mwaka, nyongeza ya mishahara na upandishaji wa madaraja.

Awali katika swali lake, Mbunge Lyima amesema Serikali inakiuka Sheria ya Utumishi wa Umma ya kuwapatia watumishi stahiki zao na kuwapunguzia motisha ya kufanya kazi kwa ufanisi katika maeneo yao ya kazi na kuathiri mafao baada ya kustaafu.

Hoja ya Mbunge huyo ni muendelezo wa malalamiko ya watumishi dhidi ya Serikali kwamba hawajapata stahiki zao tangu ilipoanza zoezi la ukakiki wa watumishi wa umma mwaka 2015. Katika zoezi hilo watumishi zaidi ya 9,000 walibainika kutokukidhi vigezo vya utumishi na hivyo kuondolewa kazini.

Huenda kauli aliyoitoa Waziri Mkuu leo Bungeni inaweza ikatofautiana na ile ya Rais John Magufuli aliyoitoa wakati wa sherehe za Mei Mosi, 2018 mijini Iringa ambapo alinukuliwa akisema hawezi kutoa nyongeza ya mishahara akidai Serikali haina fedha.

Kwangu mimi ninafikiria hizi pesa tunazotoa kwa ajili ya elimu bure ni nzuri kuliko fedha hizo kuzipeleka kuongezea mishahara, naona bora kuwapa mikopo wanafunzi wa vyuo vikuu kuliko kuongezea wafanyakazi mishahara,

Nikisema nitaongeza hizo pesa mimi nitazitoa wapi? naogopa kusema uongo. Hata mimi napenda kupandishiwa mshahara lakini kwa hali halisi ya sasa hivi lazima niwaeleze ukweli,” alinukuliwa Rais Magufuli.

Hata hivyo alibainisha kuwa kabla ya kuondoka madarakani ataboresha maslahi ya wafanyakazi wa umma, “Nawaahidi, kipindi changu cha urais hakitaisha kabla sijapandisha mishahara kwa wafanyakazi, kupandisha kwangu haitakuwa kwa shilingi elfu kumi, itakuwa ni kupandisha kwelikwel.”

Continue Reading

Jamii

Maaskofu KKKT wapewa siku 10 kufuta waraka

Published

on

Serikali imetoa siku 10 kwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), kuufuta kwa maandishi waraka wao waliotuoa Machi 24 mwaka huu na kisha kuujulisha Umma kwa njia mbalimbali walizotumia kuusambaza.

Kanisa la KKKT kupitia Baraza lake la Maaskofu lilitoa waraka uliopewa jina la ‘Taifa Letu Amani Yetu’ wakati wa Pasaka ambao mbali na masuala ya kiroho, ulibainisha mambo kadhaa yanayogusa mstakabali wa taifa.

Katika mitandao ya kijamii leo imesambazwa barua yenye kumbukumbu no. SO.748/25 inayoonyesha imeandikwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama Wizara ya Mambo ya Ndani kwenda kwa Mwenyekiti /askofu Mkuu wa KKKT iliyoandikwa Mei 30, 2018 ikitoa maelekezo ya kufutwa waraka huo ndani ya siku 10 tangu ilipoandikwa barua hiyo.

Ikiwa na kichwa cha habari ‘Ujumbe wa Baraza la Maaskofu wa KKKT’ barua hiyo inaeleza baraza hilo halitambuliki kisheria katika ofisi ya msajili.

“Unaelekezwa kuufuta waraka husika kwa maandishi na kuujulisha umma kuwa taasisi yako haikuwa na haina uwezo kisheria kufanya kile mlichokifanya. Maandishi hayo yaufikie umma wa Watanzania kwa kupitia vyombo vya habari na njia zingine zilezile zilizotumika kuufikisha waraka ule mliouita ‘Ujumbe wa Baraza la Maaskofu KKKT’.

Hata hivyo, barua hiyo imetoa onyo kali kwa taasisi hiyo dini nchi kutekeleza agizo mara moja la sivyo itachukuliwa hatua za kisheria.

“Maelekezo haya yatekelezwe ndani ya siku kumi tangu kupokea kwa barua hii vinginevyo hatua kali zaidi za kisheria zitachukuliwa dhidi ya taasisi hii,” inasema barua hiyo.

Ikumbukwe kuwa  waraka huo ulisainiwa na maaskofu 27 wa kanisa hilo nchini na kutaja baadhi ya mambo hayo kuwa ni pamoja na utekaji, utesaji, kupotea kwa watu, mashambulizi ya silaha dhidi ya viongozi wa kisiasa, mauaji yenye mwelekeo wa kiitikadi, vitisho, ubambikiziaji wa kesi, na matumizi mabaya ya vyombo vya dola dhidi ya wananchi.ni hali ya kijamii na kiuchumi, maisha ya siasa, na masuala mtambuka likiwamo suala la Katiba Mpya.

Waraka uliongeza pia kwamba uhuru wa kujieleza, kutoa na kupokea habari umeendelea kutoweka nchini huku ukionya kubanwa na hatimaye kuelekea kupungua kwa uhuru wa Bunge, Mahakama, na Tume ya Uchaguzi, ukisema hatua hii ni pamoja na kudhoofishwa kwa serikali za Mitaa.

Lakini kabla ya KKKT kutoa waraka wao, Kanisa Katoliki nalo lilitoa waraka kama huo likionya baadhi ya mambo ikiwemo uminywaji wa misingi ya demokrasia ya vyama vingi na uhuru wa kujieleza.

Baada ya kusambaa kwa waraka huo, yalijitokeza mambo mengi ikiwemo kutofautiana na kwa mawazo ya wananchi kuhusu wajibu wa viongozi wa dini katika kutoa ushauri, kuonya au kukemea pale mambo yanapoenda mrama.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa na Maaskofu wa KKKT

Hata hivyo, barua hiyo imepokelewa kwa hisia tofauti na watumiaji wa mitandao ya kijamii ikizingatiwa kuwa suala hilo lilijadiliwa na kupita, iweje linaibuka tena wakati huu ambapo kuna utulivu na yale mambo waliyoyapigia kelele na maaskofu  yamepungua ikiwemo kuteswa, kupotea kwa watu na vitisho dhidi ya viongozi wa kisiasa.

 

Wananchi bado wanawaamini viongozi wa dini

Wadau mbalimbali wa masuala ya kijamii wamesema kama kweli barua hiyo imetolewa na serikali, inaweza kuchochea taharuki zaidi kwa waumini wa kanisa hilo na wananchi kwasababu linagusa moja kwa moja imani zao.

Amebainisha kuwa bado waumini wengi wana imani na viongozi wao dini na kwamba yale wanayotamka yanakuwa na nia njema kwa jamii yao. Na katika muktadha huo serikali inapaswa kuwa makini ili kuepusha matatizo zaidi yanayoweza kutokea.

Akizungumza na FikraPevu, Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena amesema kama serikali ilibaini kuna tatizo kwenye usajili wa Baraza la Maaskofu la KKKT ingekaa na wahusika na kulimaliza kuliko kujitokeza hadharani na kuendeleza jambo ambalo limepita.

“Mimi namwamini Mungu kuliko serikali na viongozi wangu wa dini hasa Maaskofu. Hivyo serikali inapaswa kuwa makini na mambo yanayogusa imani za watu. Katika hili walipaswa kutafakari sana jinsi ya kushughulika nalo. Vinginevyo halina afya kwa ustawi wa taifa letu,” amesema Meena.

Amesema Maaskofu walitimiza wajibu wao wa kuonya kabla mambo hayajaharibika na serikali inapaswa kuyafanyika kazi yale yalyotajwa kwenye waraka au kukaa kimya ili kuepusha migongano isiyo na faida kwa taifa.

Continue Reading

Muhimu Kusoma

Copyright © 2020 FikraPevu.com