Connect with us

Uchunguzi

Bodaboda zasababisha vifo 6,700, majeruhi 36,700 katika miaka 10

Published

on

DAUDI Maliyatabu (35) amelala kitandani katika wodi Namba 4 Kibasila katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam huku akiugulia maumivu makali.

Hana uwezo wa kujigeuza kwa namna yoyote kwa sababu mguu wake wa kulia umevunjikia kwenye paja na mkono wa kushoto umevunjika pia huku kiwiko kikiwa kimesagika kutokana na ajali mbaya ya pikipiki (bodaboda) aliyoipata katika Kijiji cha Mtanana, Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma.

Anaieleza FikraPevu kwamba, kinachomuumiza zaidi siyo maumivu anayoyasikia, bali ni taarifa kuwa anatakiwa kukatwa mguu wa kulia kwa kuwa mfupa wake hauwezi kuunganishwa tena kutokana na kuvunjika vibaya.

Walau mkono wake wa kushoto utasalimika, ingawa atalazimika kufungwa vyuma maalum kwa sababu kiwiko kimesagika.

Daudi ni miongoni mwa maelfu ya watumiaji wa usafiri wa pikipiki, maarufu kama bodaboda, ambao wamepata ulemavu wa kudumu kutokana na ajali huku wengine wakipoteza maisha.

FikraPevu inafahamu kwamba, katika kipindi cha miaka 10 tangu mwaka 2006 hadi 2015 watu 6,743 wamefariki dunia kutokana na ajali 37,937 za bodaboda huku wengine 36,722 wakijeruhiwa na wengi wakipata ulemavu wa kudumu.

 “Nashukuru niko hai, lakini kwamba kuanzia sasa nimekwishakuwa mlemavu ni jambo ambalo linanitia simanzi kweli. Shughuli zangu zote zitasimama kwa sababu zilikuwa zinahitaji niwe na viungo kamili kuweza kuzitekeleza,” anasema Daudi, mkulima na mfanyabiashara wa nafaka katika Soko la Kibaigwa.

Akielezea namna ajali hiyo ilivyotokea, Daudi alisema kwamba, kubaki kwake hai ni majaliwa ya Mungu tu kwani aliamini siku kwamba ulikuwa ndio mwisho wake.

“Nilikuwa natoka nyumbani kwangu Kibaigwa nikiwa naendesha mwenyewe pikipiki yangu kuelekea Kongwa ili kwenda kununua karanga kwa wakulima. Nilipofika Mtanana, yapata kilometa tatu kutoka Kibaigwa nikakutana na lori ambalo liliacha njia na kuja upande wangu,” akaieleza FikraPevu.

Akaongeza: “Sikujua kilichoendelea, lakini walioshuhudia walisema kwamba niliingia chini ya uvungu wa lori ambako ndiko walikonitoa wakidhani nimekufa, lakini walipoona ninapumua kwa mbali wakanikimbiza Hospitali ya Wilaya ya Kongwa kabla ya kuletwa huku Muhimbili.”

Janga la taifa

Usafiri huo wa bodaboda, ambao awali ulionekana kama mkombozi kwa watumiaji wake kutokana na kupenya hata kwenye vichochoro na kuepuka foleni hivi sasa umegeuka janga kubwa la kitaifa badala ya unafuu wa ajira kwa vijana wa vijijini na mijini.

FikraPevu inatambua kwamba, tangu Aprili 2009 Serikali iliporuhusu pikipiki (bodaboda) zifanye kazi ya kusafirisha abiria na kurahisisha usafiri hasa kwenye misongamano kama mijini, vyombo hivyo vya usafiri vimekuwa balaa kwa kuongeza idadi ya ajali na vifo vinavyotokana na ajali hizo.

Ni nzuri kwa ajira na rahisi kwa usafiri, lakini kwa sasa zimeonekana kuwa hatari zaidi kwa uhai wa binadamu.

Wakati mauzo yakiendelea kupaa, idadi ya vifo vinavyohusiana na bodaboda nayo imeendelea kuongezeka kutoka vifo 89 mwaka 2006 hadi 971 mwaka 2015 huku idadi ya watu waliojeruhiwa kwenye ajali hizo nayo ikiongezeka kutoka 873 hadi 2,491 kwa kipindi hicho.

Takwimu ambazo FikraPevu inazo zinaonyesha kwamba, mwaka 2013 ndio uliokuwa na ajali nyingi za pikipiki, vifo pamoja na majeruhi ikilinganishwa na miaka mingine, ambapo jumla ya ajali 7,061 zilitokea na kusababisha vifo 1,138 na majeruhi 6,779 nchini Tanzania.

Chanzo cha ajali za bodaboda

Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani linaeleza kwamba, chanzo kikubwa cha ajali za bodaboda ni ukosefu wa elimu ya usalama barabarani kwa waendesha pikipiki na kukosa sifa ya kumiliki leseni ya udereva inayothibitisha kuhudhuria mafunzo katika vyuo vinavyotambulika na serikali  na kufuzu mafunzo ya uendeshaji wa pikipiki. 

“Tatizo hili limesababisha waendesha pikipiki kutozijua sheria na kanuni za Usalama Barabarani sambamba na kutozijua alama za barabarani, uendeshaji wa hatari kwa kupenyeza katikati ya magari na kuyapita (careless overtakings), mwendo kasi, kutovaa kofia ngumu, na upakiaji wa abiria zaidi ya mmoja (mshikaki),” zimefafanua ripoti nyingi za Hali ya Uhalifu nchini zinazotolewa na Jeshi la Polisi kila mwaka. 

Ripoti hizo, ambazo FikraPevu inazo nakala zake, zimeeleza vilevile kwamba, ajali zitokanazo na waendesha pikipiki zimekuwa zikisababishwa na udhibiti hafifu wa uagizaji na uingizaji wa pikipiki hapa nchini kwa mamlaka zinazohusika.

“Hakuna Sera ya kudhibiti vyombo hivi, jambo ambalo limepelekea kuwa na wafanya biashara wengi wa pikipiki na wingi wa pikipiki unaosababisha kila mtu kuwa na uwezo wa kumiliki hasa kwa vijana wasio na ajira na kuzitumia kibiashara baada ya serikali kuruhusu vyombo hivyo kutumika kusafirisha abiria,” zinaeleza ripoti hizo.

FikraPevu inafahamu kwamba, uagizaji wa pikipiki umeongezeka kwa kiwango kikubwa kutoka uingizaji wa pikipiki 20,117 mwaka 2006 hadi pikipiki 113,610 mwaka 2010 na idadi hiyo imeendelea kuongezeka kila wakati.

Aidha, miundo mbinu nayo imetajwa kuwa chanzo kingine kwani haikidhi matumizi ya vyombo vya moto kwa nafasi.

“Hii inatokana na barabara nyingi za mjini kuwa nyembamba sana na kusababisha ajali za magari kugongana na pikipiki kutokea mara kwa mara na waathirika wakubwa wakiwa ni wapanda pikipiki,” zinaongeza ripoti hizo kila wakati.

Mathalani, katika kipindi cha mwaka 2011 kulikuwa na ajali za pikipiki 5,384 ikilinganishwa na ajali 4,363 zilizotokea mwaka 2010 sawa na ongezeko la 23%, ambapo vifo vilikuwa 945 ikilinganishwa na vifo 683 sawa na ongezeko la 38%, na majeruhi 5,506 ikilinganishwa na majeruhi 4,471 sawa na ongezeko la 23%. 

Kati ya Januari na Juni tu mwaka 2012, jumla ya ajali 2,641 zilikuwa zimetokea zilizosababisha vifo 487 na majeruhi 2,706, huku wengi wa waathirika wakiwa ni vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa.

Ingawa takwimu zinaonyesha kwamba idadi ya ajali hizo imekuwa ikipungua, lakini bado haijaleta matumaini chanya kwani bado roho za wengi zinaendelea kupukutika huku wengine wakiachwa na ulemavu wa kudumu.

Mwaka 2015 kwa mfano, idadi ya ajali ilikuwa 2,749 kulinganisha na ajali 4,304 mwaka 2014 ikiwa ni upungufu wa ajali 1,555 sawa na asilimia 36.1.

Hata hivyo, ajali hizo kwa mwaka 2015 zilisababisha vifo 971 ikilinganishwa na vifo 957 mwaka 2014 , likiwa ni ongezeko la vifo 14, sawa na asilimia 1.5.

Majeruhi kwa mwaka 2015 walikuwa 2,491 kulinganisha na majeruhi 4,016 mwaka 2014, ukiwa ni upungufu wa majeruhi 1,525, sawa na asilimia 38.

Mnamo Mei 2011, aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Said Ally Mwema, alikiri kwamba bodaboda zimekuwa janga kubwa la taifa kutokana na kuwa chanzo kikuu cha ajali nchini Tanzania.

“Pikipiki kama chombo cha usafirishaji, kimekuwa kikitumiwa na wananchi katika shughuli mbalimbali kama njia rahisi zaidi katika kusafirisha abiria na mizigo kote mijini na vijijini. Licha ya nia njema ya Serikali ya kuwapunguzia wananchi adha ya usafiri, pikipiki hizi zimekuwa chanzo kikubwa cha ajali za barabarani,” alikaririwa akisema.

Tofauti na miaka ya nyuma ambapo vituo vya polisi vilijaa magari yaliyokamatwa kwa makosa mbalimbali, hivi sasa vituo hivyo vimesheheni bodaboda kana kwamba ni karakana au mahali pa mauzo.

Bodaboda zilizokamatwa kwa makosa mbalimbali ikiwemo ajali zikiwa katika kituo cha polisi.

Aidha, hospitali nyingi nchini idadi kubwa ya majeruhi wa ajali inaelezwa ni wale waliopata ajali za bodaboda, ambao kwa sasa wamekuwa wengi kuliko uwezo wa hospitali zenyewe.

Zinauzwa kama ‘toi’, kwetu biashara

Uchunguzi unaonyesha kwamba, pikipiki nyingi zilizozagaa nchini zimeingizwa kutoka China zikiuzwa kwa bei nafuu zaidi na zimekuwa kama ‘toi’, ambapo yeyote anaweza kuzipata hata kwa Shs. 1.5 milioni.

FikraPevu inafahamu kwamba, pikipiki hizo ambazo zimejaa kwenye soko kwa bahati mbaya ziko kwenye mikono isiyo sahihi, kwani wengi wa madereva ni vijana ambao hawana mafunzo sahihi ya udereva, achilia mbali kuwa na leseni.

Mara nyingi wanaendesha bila kuvaa kofia ngumu ambazo wamezifunga kama mapambo, wanavunja sheria zote za usalama barabara, wanachojua ni kuwasha na kuvuta mafuta, na wengi wanabeba abiria zaidi ya mmoja (mishikaki), mambo ambayo yanatokea mbele ya macho ya askari wa usalama barabarani.

Uhusiano wa kiuchumi kati ya China na Tanzania umeongeza kasi ya uingizaji wa bidhaa mbalimbali nchini Tanzania, zikiwemo bodaboda kwa kipindi cha miaka 15 iliyopita.

FikraPevu inafahamu kwamba, usafirishaji na uingizaji wa bidhaa kati ya China na Tanzania kwa mwaka 2001 ulikuwa Dola za Marekani 93.4 milioni tu, lakini kufikia mwaka 2010 ulikuwa Dola za Marekani 1.65 bilioni, ambalo ni ongezeko kubwa na limezidi kukua kadiri miaka inavyosonga mbele.

Aidha, miaka 15 nyuma kulikuwa na makandarasi 12 tu kutoka China na mameneja na wahandisi 240 wa Kichina, lakini kufikia mwaka 2010 pekee kulikuwa na kampuni zaidi ya 30 za Kichina zilizokuwa na wataalam takriban 3,000 kutoka China na wafanyakazi wa Kitanzania zaidi ya 30,000 zikishughulika na ujenzi wa barabara, madaraja, huduma za maji, majengo, mawasiliano na miradi mingine ya miundombinu.

Mwishoni mwa karne iliyopita, migahawa na gereji za Kichina ilikuwa ikihesabika jijini Dar es Salaam, lakini kwa sasa kuna wawekezaji takriban 300 kutoka China waliowekeza zaidi ya Dola 200 milioni wakiwa na viwanda vinavyotengeneza viatu, vyombo vya plastiki na kadhalika.

Hali hiyo haishangazi kuona wingi wa bodaboda nchini, kwani Watanzania nao wameona milango ya kufuata bidhaa China iko wazi na huko wananunua vitu kwa bei nafuu, vingi kati ya vitu hivyo vikiwa havina ubora stahiki kwa kuwa vimetengenezwa katika viwanda vidogo ambavyo vimetapakaa katika miji mingi huko China.

FikraPevu inaona kwamba, jambo pekee ambalo linapaswa kufanyika kudhibiti wimbi la ajali ni kwa Jeshi la Polisi kusimamia sheria na kuwakamata wahalifu na kuwafikisha mahakamani, lakini pia kuwahimiza vijana kwenda kupata mafunzo ili kujiajiri kupitia bodaboda, biashara ambayo imewanufaisha wengine wengi.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Jamii

Vigogo Halmashauri za Monduli, Karagwe, Biharamulo kikaangoni upotevu wa milioni 171.8 za miradi ya maji

Published

on

Maji ni uhai. Ni uhai kwasababu  yanabeba dhana nzima ya mwanadamu yeyote kuishi na kufanya shughuli zingine za maendeleo. Pia maji ni uhai kwasababu yanagusa sekta zote za uzalishaji, popote utakapokwenda utahitaji maji. Hiyo ndiyo thamani ya maji.

Ni dhahiri kuwa jambo lolote linalofanyika kwa nia ya kuvuruga au kuhalibu mfumo wa upatikanaji wa maji safi na salama, linalenga kuuawa uhai wa binadamu. Kuanzia kwenye uhalibifu wa mazingira, vyanzo vya maji, ukosefu wa rasilimali fedha na watu kutekeleza miradi ya maji hadi kukosekana kwa utashi wa kisiasa kuhakikisha wananchi wanapata maji ya uhakika.

Katika makala hii tunajadili matumizi mabaya ya fedha za miradi ya maendeleo katika baadhi ya halmashauri za wilaya nchini ambazo zimetumia vibaya fedha na kuwahatarishia uhai wakazi wa maeneo yao.

Halmashauri hizo ni Monduli, Karagwe na Biharamulo ambazo  zimekiuka makubaliano ya mkataba wa utekelezaji wa miradi ya maji na kusababisha milioni 171.8 kutumika kwa matumizi ambayo hayakukusudiwa.

Halmashauri hizo 3 katika mwaka wa fedha unaoishia Juni 2017 zilikuwa zinatekeleza miradi ya maji chini ya ufadhili wa Mfuko wa Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP). Fedha za mfuko wa WSDP hutolewa na nchi wahisani au mashirika ya kimataifa kuhakikisha wananchi hasa maeneo ya vijijini wanapata maji safi na salama.

Wahisani hao wanaongozwa na dhamira kuu; maji ni uhai na binadamu popote alipo ni lazima aypate ili aweze kuishi. Lakini wapo baadhi ya watendaji katika halmshauri hizo kwa kujua au kutokujua wanahujumu miradi inayofadhiliwa na wahisani hao.

Tabia hiyo inatajwa kuwa kikwazo kwa wafadhili kuendelea kuwasaidia wananchi kupata maji kwasababu kukosekana kwa utashi wa kisiasa  kwa baadhi ya watendaji ambao kwa namna moja ama nyingine wanatumia tatizo la maji kama mtaji wa kujinufaisha kisiasa na kupata nafasi za uongozi serikalini.

Kulingana na Mkataba wa makubaliano (MoU) wa uanzishaji wa Mfuko wa WSDP aya ya 9.2.2 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2013 inaeleza kuwa, “Serikali imekubali kusamehe kodi zote zilizowekwa moja kwa moja au zisizo za moja kwa moja kwenye matumizi yote yanayostahili ya bidhaa, kazi na huduma za kifedha chini ya WSDP”.

Lakini halmashauri za  wilaya za Monduli mkoani Arusha; Karagwe na Biharamulo mkoani Kagera zilikiuka kifungo hicho na kutoza kodi yenye thamani sh. Milioni 171.8 kwenye miradi minne ya maji iliyofadhiliwa na mfuko wa WSDP ambayo haikupaswa kukatwa.

Kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka wa fedha unaoishia Juni 2017 inaeleza kuwa katika halmashauri ya Wilaya ya Monduli ilibainika mikataba miwili ambayo ilitozwa kodi yenye thamani ya sh. Milioni 87.7 kutoka kwenye miradi ya maji ambayo haikustahili kulipa kodi katika wilaya hiyo.

“Nimebaini mikataba miwili, Na. LGA/004/2016/17/RWSSP/W/14 na Na. LGA/004/2016/17/RWSSP/W/10 katika Halmashauri ya Wilaya Monduli Mkoani Arusha, ambapo kiasi cha VAT (ongezeko la thamani) Sh. 87,765,679 kililipwa kwa ajili ya miradi ya maji iliyosamehewa kodi”, imeeleza ripoti hiyo ambayo ilitolewa na CAG, Prof. Mussa Assad wiki iliyopita.

Halmashauri za Karagwe na Biharamulo nazo zilifuata mkondo ule ule wa Monduli kwa kutoza kodi ya sh. Milioni 84.035 kwenye miradi miwili ya maji iliyokuwa ikitekelezwa na mfuko wa WSDP katika wilaya zao.

Taarifa ya CAG inafafanua kuwa “Nimebaini pia mikataba miwili katika Halmashauri za Wilaya Karagwe na Biharamulo yenye namba LGA/033/W/2016/17/W/NT/07 na LGA/032/2016-2017/HQ/WSDP/W/76 LOT 03 ambapo kodi ya ongezeko la thamani (VAT) yenye thamani ya Sh. 84,035,685 ilijumuishwa katika gharama ya miradi ya maji iliyosamehewa kodi.”

Kwa vyovyote vile katika miradi hiyo mitatu kuna harufu ya ufisadi, kama miradi hiyo haikutakiwa kulipa kodi fedha hizo zimeenda wapi?. Na kama serikali ilipokea hizo fedha ilitumia vigezo gani kwasababu masharti ya mkataba ambao serikali ilisaini hayaruhusu kodi ijumuishwe kwenye gharama za mradi wa maji.

Kiasi cha milioni 171.8 kukatwa kodi huenda kimewakosesha wananchi katika maeneo mengine kupata huduma ya maji. Kwa mafano fedha hiyo ingetumika vizuri ingeweza kujenga miradi mingine ya kusambaza maji katika halmashauri hizo na kuwapunguzia wananchi tatizo la upatikanaji wa maji.

 

Nini kifanyike…

CAG katika ripoti yake ameonyesha kusikitika na mwenendo  huo wa baadhi ya watendaji wa halmashauri kutozingatia maadili ya kazi zao. Amebainisha kuwa tabia hiyo ikiendelea inaweza kuwakatisha tamaa wafadhili kuendelea kutoa fedha za misaada.

“Kwa maoni yangu, malipo ya VAT kwa miradi iliyosamehewa kodi yanapunguza uwezo wa Halmashauri kugharamia miradi mingine. Aidha, kutofuata MoU kunakatisha tamaa nia za wafadhili kuendelea kutoa ruzuku katika miradi mingine.”, amesema CAG, Prof. Assad katika ripoti yake.

Kwa kutambua kuwa fedha zilizopotea ni nyingi, Makatibu Tawala wa halmashauri za wilaya hizo 3 wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria kwa kitendo chao cha kukwamisha upatikanaji wa huduma muhimu ya maji kwa wananchi.

“Napendekeza kwamba, katika siku zijazo Uongozi wa Halmashauri ufuate mkataba wa makubaliano uliosainiwa. Aidha, Afisa Masuuli achukuliwe hatua kwa ulipaji wa VAT katika miradi iliyosamehewa kodi,” ameshauri CAG, Prof. Assad.

Continue Reading

Afya

Ubakaji, ulawiti watoto usifumbiwe macho Kinondoni

Published

on

Na Daniel Samson

Kulingana Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 sehemu ya pili (II) inatoa wajibu na majukumu ya mzazi katika kumlea mtoto ambapo inaeleza kuwa “Kila mzazi atakuwa na wajibu na majukumu yaliyowekwa ama na sheria au vinginevyo kwa mtoto wake ambayo yatajumuisha wajibu wa kumlinda mtoto dhidi ya utelekezwaji, ubaguzi, vurugu, unyanyasaji, madhara ya kimwili na kiakili na ukandamizaji”

Ni tofauti na matakwa ya sheria, wako baadhi ya wazazi ambao wanawafanyia watoto wao ukatili wa aina mbalimbali na kukiuka jukumu la msingi la kuwalinda na kuwatengenezea mstakabali mzuri wa maisha.

Lucy (4) (jina hilo sio halisi) ni miongoni mwa watoto wengi duniani ambao wamefanyiwa ukatili wa kijinsia na watu ambao wanapaswa kuwalinda na kuhakikisha wanakuwa na furaha wakati wote.

Lucy alibakwa na baba yake mzazi aliyetambulika kwa jina la Clement (40) (jina la pili tumelihifadhia). Tukio hilo lilitokea kata ya Bunju B wilaya ya Kinondoni ambapo alimsababishia maumivu makali sehemu zake za siri.

“Baba aliniingiza vidole huku chini, amekuwa akinifanyia muda mrefu. Aliniingiza chumbani akanilaza kitandani na kufungua zipu na kutoa dudu”,amesema Lucy na kuongeza kuwa baba yake alimuingilia nyumbani kwao Bunju B ambako wanaishi kwenye nyumba ya kupanga.

Akihojiwa na mwandishi wa makala haya Lucy amesema baba yake alimkataza kuwa asimuambie mtu yoyote lakini maumivu yalipozidi alimwambia mama yake aitwaye Beatrice (jina la pili tunalihifadhi kwa ajili ya usalama)

Beatrice anasema aligundua kuwa mtoto wake ameingiliwa wakati akimuogesha ambapo alikuwa akilalamika kwamba anapata maumivu sehemu za siri.

“Nilimuuliza tatizo nini lakini hakuniambia akabaki analia na kuonyesha sehemu zake za siri”, amesema Beatrice na kuongeza kuwa alimuita mama Vena ambaye wanaishi pamoja katika nyumba yao ambapo walimchunguza na kukuta ameharibiwa sehemu zake za siri.

“Nikampandisha juu ya kiti nikwambia wapi panauma? Ebu nionyeshe akapanua miguu. Nikamuuliza mbona uko hivi kuna tatizo gani huku mbona kuna damu, kulikuwa na michubuko, maana kulikuwa kwekundu kote…”, Amesema Mama Vena.

“Nikamuuliza  mbona uko hivi umefanyaje? Akaniambia baba amefanya hivi, baba alifungua zipu akatoa dudu akaingia huku”, amebainisha Mama Vena.

Anasema usiku huo huo, aliambatana na Beatrice hadi kwa kaka yake (Clement) ambaye anaishi mtaa wa Idara ya Maji kata ya Bunju B ili wasaidiwe kumkamata mtuhumiwa. Walifanya kikao ambapo walianza kumtafuta Clement ambaye tayari alikuwa ameondoka nyumbani baada ya kutekeleza unyama huo.

Familia hiyo haikutaka kulifikisha suala hilo kwenye vyombo vya dola na ili kumnusuru mtuhumiwa. Inaelezwa kuwa msimamo huo wa familia ulipata nguvu kwasababu Beatrice, mke wa Clement ilikataa kumfikisha mme wake polisi kwa kuhofia kukosa matunzo.

Mama Vena anasema siku tatu baada ya tukio hilo alitoa taarifa kwenye ofisi ya serikali ya mtaa wa Idara ya Maji na kutaka suala hilo lifikishwe polisi.

 Lucy aliyefanyiwa udhalilishaji wa kingono na baba yake mzazi

 

 Kesi yafikishwa Polisi

Kutokana na shinikizo la majirani, Beatrice, aliripoti tukio hilo kwenye kituo cha Polisi cha Mabwepande ambako huko jalada la kesi ya ubakaji lilifunguliwa Novemba pili 2017.

Beatrice alipewa Fomu ya Polisi (PF3) ambapo alimpeleka mtoto huyo hadi hospitali ya Mwananyamala iliyopo Wilaya ya Kinondoni kwa ajili ya vipimo.  Alionana na daktari na Lucy alifanyiwa vipimo viwili, cha Maambukizi ya virusi vya UKIMWI na kile cha kuingiliwa kimwili.

Majibu ya daktari  yalionyesha dhahiri kuwa mtoto huyo amenajisiwa na sehemu zake za siri zimeharibiwa na majibu ya kipimo cha maambukizi ya UKIMWI yamefanywa kuwa siri ili kutoharibu upelelezi wa kesi hiyo ambayo iko polisi.

Siku hiyo hiyo aliwasilisha majibu hayo kwa Mkuu wa Kituo Cha Polisi Cha Mabwepande, ambapo majibu yalipokelewa kwa ajili ya ushahidi. Upelelezi wa tukio hilo unaendelea ili kumkamata mtuhumiwa Clement ambaye alitoroka kusikojulikana baada ya kupata taarifa kuwa anatafutwa na polisi.

 

 Ukubwa wa Tatizo la ubakaji

Katika kuangazia ukubwa wa tatizo la ubakaji katika Manispaa ya kinondoni, Chama Cha Wanahabari Wanawake  (TAMWA), kimeshirikiana na mwanadishi wa makala haya ili kuibua na hatimaye kutoa suluhu juu ya njia sahihi ya kukomesha vitendo hivi.

Kwa mujibu wa takwimu za Jeshi la Polisi Tanzania (2016) zinaonyesha kuwa katika kipindi cha miezi saba ya kwanza ya mwaka 2016 yaani kuanzia Januari hadi Julai, Kinondoni ambayo Kipolisi ni Mkoa ilikuwa inaongoza kwa kuwa na kesi 187 za ubakaji katika kipindi hicho huku ikifuatiwa na Mbeya (177), Morogoro (160),  Pwani (159), Temeke (139) na Ilala (109).

Pia Takwimu za Jeshi hilo zinaonyesha kuwa matukio ya ubakaji nchini Tanzania yameongezeka kutoka 6,985 mwaka 2016 na kufikia matukio 7,460 mwaka 2017 na ongezeko hilo ni asilimia 6.8.  Makosa ya kunajisi yalikuwa 16 kwa mwaka 2016 na yaliongezeka hadi kufikia 25 mwaka uliofuata

Kinondoni inatajwa kuwa na matukio mengi ya ubakaji kwa sababu kuna mwamko wa watu kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo kuwaripoti  watuhumiwa wa vitendo hivyo ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ali Hapi ameitaka jamii kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa sahihi za matukio ya ubakaji, “ Jeshi la Polisi limejipanga ili kila aliyepatikana na hatia ya ubakaji achukuliwe hatua”.

 

Ustawi wa Jamii

Mshauri na Mtaalamu wa Saikolojia kutoka Taasisi ya Ustawi wa Jamii Tanzania, Zainabu Rashidi amesema ubakaji una athari nyingi kwa watoto ambapo zinaweza kuendelea hadi ukubwani.

Amesema mtoto aliyebakwa hujiona duni na mpweke na hufikia hatua ya kujitenga na kuogopa kucheza na wenzake kwa sababu jamii humnyooshea kidole ambapo hujiona mwenye hatia.

“Athari kubwa ni kwamba mtoto anakuwa mnyonge, mpweke na anakosa hamu ya kushiriki na wenzake katika mambo mengine kwa sababu vitendo vya ubakaji katika jamii vinatafsiriwa kama aibu na unyonge. Na haijalishi mtoto amebakwa na nani? Jamii huanza kumnyoshea kidole kwamba Yule mtoto alibakwa”,  amesema Mtaalamu huyo na kuongeza kuwa,

“Anapokuwa mtu mzima anaendeleza tabia ambazo ni mbaya, anaweza kufanya vitendo vya kikatili, kulipiza kisasi, kumchoma mtoto mikono na mwingine anaweza kufikia hatua ya kuchanganyikiwa”.

Ameitaka jamii kujenga utamaduni wa kutoa taarifa na kuwasaidia waathirika wa ubakaji kwa kuwapeleka Ustawi wa Jamii ili wapate tiba ya kisaikolojia na kurejea katika hali ya kawaida.

                                            Beatrice, mama wa Lucy  aliyebakwa na baba yake mzazi

 

Msimamo wa Serikali dhidi ya Ukatili

Serikali kupitia Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt Faustine Ndungulile ameitaka jamii kutoyafumbia macho matukio ya ubakaji aidha inapaswa kutoa taarifa ili watuhumiwa wachukuliwe hatua za kisheria.

“Kupaza sauti katika kupinga ukatili wa kijinsia na kuondokana na utamaduni wa kukaa kimya dhidi ya vitendo vya kikatili na madhara yake yanamgusa kila mmoja katika ngazi tofauti”, amesema Dkt. Ndungulile.

Hata hivyo, Serikali imezifanyia maboresho Sera na Sheria ikiwemo  Sheria ya Elimu sura 353 ambayo inatoa adhabu ya kifungo kisichopungua miaka 30 kwa mtu yeyote atakayembaka na kumpa mimba mwanafunzi wa shule ya Msingi au Sekondari.

Pia Serikali imeanza utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa kutokomeza Ukatili dhidi ya wanawake na watoto unaojumuisha sekta zote zinazohusu wanawake na watoto kwa lengo kuzuia aina zote za ukatili.

 

 Nini Kifanyike?

Ili kupunguza au kuyamaliza matukio haya, jamii inapaswa kuacha tabia ya kuwalinda wabakaji lakini wanatakiwa kuwafikisha kwenye vyombo vya dola ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Pia kuboresha sheria na sera ikiwemo Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 ambayo inatoa mwanya kwa watoto kuolewa katika umri mdogo. Mabadiliko hayo yaambatane na mikakati ya kitaifa ya kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vyote vya ukatili ukiwemo ubakaji na ulawiti.

Continue Reading

Afya

Waendesha bodaboda wanachangia asilimia 13 ya mimba za utotoni nchini

Published

on

  • Kuna uhusiano gani kati ya bodaboda na ongezeko la mimba za utotoni kwa wasichana wanaosafiri umbali mrefu kwenda shule?

Gazeti la The Guardian la Tanzania, linawaweka waendesha bodaboda kama kiini cha ongezeko la mimba za utotoni nchini Tanzania. Kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa hivi karibuni, waendesha bodaboda wanachangia asilimia 13 ya mimba za utotoni nchini.

Matumizi ya bodaboda, ama pikipiki kwaajili ya biashara, yameongezeka sana nchini Tanzania hasa pale ambapo ni ngumu kupata usafiri mwingine. Umaarufu wake unasababishwa na upatikanaji mgumu wa usafiri pamoja na bei nafuu za pikipiki; na huwa zinaendeshwa na vijana wadogo waliotoka kumaliza tu elimu ya sekondari.

Kwa mujibu wa utafiti huo, wasichana wadogo, hasa wale wa vijijini, wako katika mazingira hatarishi zaidi kushawishika kingono kwasababu inawabidi kusafiri umbali mrefu kwenda shule. Gazeti la Financial Times linasema, baadhi ya wasichana huishi umbali wa hadi kilometa 15 kutoka shuleni, hivyo huwalazimu kupanda bodaboda badala za kutembea umbali huo.

Kwakuwa hawana fedha za kutosha kuwalipa waendesha bodaboda hao, huishia kulala nao kama njia ya malipo. Wanapopata ujauzito kwa jinsi hii, huishia kufukuzwa shuleni.

 

Swali hapa ni je, mimba ngapi za utotoni ambazo zinasababishwa na waendesha bodaboda nchini Tanzania?

PesaCheck imefanya uchunguzi na kubaini ya kwamba, madai ya kuwa waendesha bodaboda wanachangia ongezeko la mimba za utotoni Tanzania ni kweli kwa kiasi kikubwa kwa sababu zifuatazo:

Utafiti wa Taifa kuhusu Vichocheo na Madhara ya Ndoa za Utotoni nchini Tanzania, unafafanua kwamba wasichana kutoka kaya masikini ni kundi hatarishi kwasababu ya hali yao ya kiuchumi. Kukosa mahitaji yao ya msingi, kama kuweza kulipia usafiri, kunawafanya iwe rahisi kunyanyaswa kingono.

Ni ngumu kujua idadi kamili ya mimba zilizosababishwa na waendesha bodaboda. Lakini, kilicho bayana ni kwamba wasichana waishio vijijini nchini Tanzania ni kundi hatarishi la kunyanyaswa kingono na watu wanaohusika na usafiri sehemu mbalimbali nchini.

Watoto wengi hukumbana na changamoto mbalimbali wanapokuwa njiani kwenda na kutoka shule. Baadhi ya makondakta hukataa kuwachukua kwasababu wanalipa nauli ndogo. Safari ya kwenda na kutoka shule huwaweka watoto katika mazingira hatarishi. Ripoti ya “Ukatili Dhidi ya Watoto Tanzania” inaonyesha kwamba kati ya wasichana wanne waliotoa taarifa ya kufanyiwa ukatili wa kijinsia, mmoja kati yao ilimtokea akiwa anaenda shule, aidha kwa usafiri wa umma au akiwa anatembea.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Ukatili Dhidi ya Watoto Tanzania (2011), msichana 1 kati ya 25 mwenye umri wa miaka 13 hadi 17 amewahi kupewa pesa au zawadi ili afanye ngono. Ripoti hii inaonyesha kwamba asilimia 23 ya wasichana wananyanyaswa kijinsia wakiwa wanaenda au kutoka shule.

Hivyo, madai ya kwamba waendesha bodaboda wanachangia ongezeko la mimba za utotoni nchini Tanzania ni kweli kwa kiasi kikubwa. Kuna ushahidi unaoonyesha kuwa wasichana wanaotoka kwenye kaya masikini, hasa walioko vijijini, wanapata shinikizo kubwa kulipia usafiri wao kingono. Kwa kuwanyanyasa wasichana hao, waendesha bodaboda huwaongezea ugumu ambao tayari wanao.

Matokeo yake, maamuzi ya kuwafukuza shule wasichana waliopata ujauzito huleta matokeo hasi. Kunawafanya wakose nafasi ya kupata elimu ambayo wangeihitaji kujikwamua na umasikini. Hivyo, huwaweka katika hali hatarishi zaidi.

 

Makala hii imeandikwa na PesaCheck Fellow Belinda Japhet, Mwandishi na Mshauri Mtaalamu wa maswala ya mawasiliano.

Continue Reading

Muhimu Kusoma

Copyright © 2020 FikraPevu.com