Connect with us

Jamii

Dola yambana Mwandishi wa Habari wa Gazeti la Mwananchi

Published

on

MWANDISHI wa habari  anayeandikia gazeti la Mwananchi kutokea Arusha, Mussa Juma, ameanza kuandamwa na serikali na sasa uraia wake umeanza kuhojiwa huku yeye akihusisha hatua hizo na msimamo wake katika kazi zake.

Habari zilizothibitishwa na vyombo vya dola zimeeleza kwamba Mussa amekua akifuatiliwa kwa muda mrefu sasa kabla ya kuitwa na kuhojiwa rasmi na vyombo vya dola akituhumiwa kuwa uraia wake una utata.

Mbali ya kuandika habari za uchunguzi na zile za kisiasa, Mussa amekua mstari wa mbele katika kuwaunganisha waandishi wa habari mkoani Arusha na mikoa jirani ya Manyara na Kilimanjaro, lakini pia amekua kiungo na waandishi wageni wanaotembelea Arusha.

Imeelezwa moja ya sababu zilizochochea kuandamwa kwake ni mgogoro wa kisiasa katika Manispaa ya Arusha ambao Mussa amekua na msimamo usioyumba katika kuandika taarifa za mgogoro huo.

Juma aliyejipambanua kutoegemea upande wowote katika uandishi wake alisema  amekuwa akikwaruzana mara kwa mara na viongozi wa serikali wasiopendezwa na habari hizo ambao walimtumia ujumbe kumtaka ajihadhari kwani serikali ina mikono mirefu ikiamua itamshughulikia.

“Baada ya kuripoti kwa kina utata katika tukio la uchaguzi wa Meya na vurugu zilizosababishwa na maandamano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), mapema mwaka huu, nilianza kuandamwa na baadhi ya watendaji wa Idara ya Usalama wa Taifa ambao walinionya niache kuandika habari za matukio hayo la sivyo ‘nitakiona’,” alisema Mussa Juma.

Alisema awali mmoja wa maafisa wa ngazi ya juu wa Idara ya Usalama wa Taifa Kanda ya Kaskazini (jina linahifadhiwa kwa sasa) alituma mmoja wa waandishi wa habari mkongwe mjini Arusha Mwanaidi Mkwizu kumuonya Mussa asiendelee kuandika habari za mgogoro wa umeya kwa usalama wake kwani akiendelea yangemkuta makubwa.

“Baada ya kupokea ujumbe huo, nilimpigia simu afisa huyo ambaye alikiri kumtuma mwandishi huyo huku akidai alifanya hivyo kwa nia njema ya kunionya na kunihurumia kwa mabaya yaliyokuwa mbele yangu iwapo ningekaidi ushauri huo. Kwa ajili ya ushahidi nilirekodi mazungumzo yangu yote na afisa huyo,” alisema Mussa Juma

Alisema pamoja na tukio la umeya, afisa huyo pia alimtuhumu kuishambulia na kuiumbua serikali katika tukio la mgogoro wa jamii ya Wamaasai wa eneo la Lololiondo wilayani Ngorongoro na kampuni ya uwindaji wa kitalii ya Oterllo Business Co-oparation (OBC) na pia mgogoro wa Mashamba ya NAFCO wilayani Hanang.

Kilele cha vitisho na ujumbe alizotumiwa kilifika juzi baada ya maafisa wa Idara ya uhamiaji mkoani Arusha kufika ofisi za gazeti hili kumtafuta Musa na walipomkosa waliamua kumpigia simu yake ya kiganjani wakimtaka kufika ofisini kwao siku inayofuata, Agosti 23, mwaka huu, saa 3 asubuhi bila kumweleza sababu za wito huo.

Akiwa ameongozana na wakili wake, Shilinde Ngalula na mmoja wa wafanyakazi wa Mwananchi mkoani Arusha Peter Saramba, Mussa alifika ofisi za uhamiaji na kutakiwa kutoa maelezo lakini Ofisa huyo wa uhamiaji alikataa kufanya mahojiano wakati mwanasheria na mfanyakazi huyo ya mwananchi yupo, jambo lililozua mgogoro uliodumu saa mbili.

Hata hivyo baada ya mashauriano baina ya Mussa Juma na wakili huyo, ambaye ni mkuu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binaadamu mkoa wa Arusha, walikubaliana watoke nje ya ofisi na ndipo mahojiano yalianza na Mussa Juma kuandika maelezo.

Maelezo ya uraia wake kwa kujaza fomu maalumu kuonyesha jina lake, jina la wazazi wake, ndugu zake na mahali walipozaliwa.

Maelezo hayo yaliandikwa mbele ya mkuu wa upelelezi wa Idara ya uhamiaji mkoa wa Arusha, Embrosy Mwanguku ambaye baada ya kuyapitia alimruhusu kuondoka kwa maelezo kuwa akihitajika ataitwa.

Afisa huyo, hata hivyo,wakati akichukuwa maelezo ya Mussa Juma, alikiri kumfahamu kama rafiki yake kwa muda mrefu lakini anachofanya ni kutekeleza maagizo ya ngazi za juu.

“Mimi na Mussa hatuna matatizo, tunafahamiana muda mrefu na hatuna matatizo na ndio sababu suala hili tangu mwezi wa kwanza tumekuwa tukifuatilia ili tumhoji  tukaambiwa yupo Samunge tukamsubiri hadi amerudi”alisema Mwanguku.

Wakati mwandishi aliyetumwa kumfikishia ujumbe juma alikiri alipozungumza jana kwa njia ya simu, Ofisa anayetuhumiwa kuhusika katika tukio hilo hakuweza kupatikana jana baada ya kutokuwepo ofisini kwake na hata simu yake ya kiganjani ilikuwa haipatikana. Juhudi za kumtafuta zinaendelea ili kuthibitisha iwapo hatua hii ya sasa dhidi ya Mussa Juma ni utekelezaji wa onyo lake.

Akizungumza mara baada ya kuhojiwa Mussa Juma alisema anaamini uhamiaji wametumwa na wakubwa zao kumfuatilia kutokana na masuala ya kisasa na utekelezaji wa kazi zake za uandishi.

“Sasa naweza kusema maisha yangu yapo hatarini kwani kuna mengi yametokea tangu uchaguzi mkuu na hata kabla ambayo yanatokana na vitisho ya dola lakini naamini nilichokuwa nafanya na ambacho ntaendelea kufanya kuwa sawa na sikiuki maadili ya uandishi wa habari,”alisema Mussa Juma.

Alisema kama vyombo vya dola vinaona kuwa uandishi wake na mwenendo ya gazeti la Mwananchi si sahihi kuna taratibu za kufuata ili madai yao yafanyiwe kazi.

“Nimekuwa mwandishi kwa zaidi ya miaka 15 sasa sijawahi kushitakiwa  kwa kuandika habari zozote za uchochezi au kupotosha sasa nashangaa vitisho dhidi yangu,” alisema Mussa Juma.

Continue Reading
8 Comments

8 Comments

 1. Gordon

  24/08/2011 at 11:15 pm

  Serikali ina matatizo makubwa kuliko kumfuatilia Mwandishi. Hivi hii ni akili kweli? Na hao wanaotumwa wanasema wanatimiza maagizo ya Mabwana zao. Hivi wakiambiwa wafanye Ubakaji watakubali? Upumbavu gani huu jamani ktk nchi inayojidai ina Demokrasia!

 2. Chriss

  25/08/2011 at 1:02 pm

  Nadhani ile dhana ya kusema kwamba mamlaka ya Tanzania imekuwa kichwa cha mwenda wazimu imepata uhalali wake. Sina shaka juu ya haya yanayofanywa juu ya mwandishi Musa, kwamba ni agizo la chama tawala kwa sababu mamlaka iko chini ya serikali ya chama (CCM). Naweza kuthibitisha hili kwa dhana ile ya kuwa hata mgogoro wa kisiasa na maafa yaliyotokea Arusha chanzo chake ni CCM, angalia hata initiator wa mgogoro wa ardhi na ule wa wafugaji kati ya wamasai na mwekezaji vyote viko chini ya viongozi wa serikali inayokingiwa kifua na CCM, na kadhalika na kadhalika. But time will tell!

 3. ntagunga

  26/08/2011 at 11:50 am

  hiyo ndo serikali tuliyonayo, kuna haja ya kuibadilisha

 4. Zoka

  27/08/2011 at 5:17 am

  Ikumbukwe mwaka 2010,Gazeti la mwanahalisi lili fungiwa kwa muda kwa kushutumiwa kuandika habari za uchochezi wa chuki kwa ananchi dhidi ya serikali.Muda si mrefu Gazeti mwananchi likatishiwa kufungwa kwa kosa kama hilo.
  Tilisha shuhudia K ubenea alichofanyiwa kwa kumwagiwa kemikali.Bado Jery Muro anashutumu serikali kumfanyia uhuni wa kesi bandia pitia Waziri wa zamani wa mabo ya ndani Lawrence Masha alikuwa anamtishia kumpoteza alipo umbua uozo wa rushwa ktkm jeshi la polisi.
  Dkt Slaa alisha ushutumu usalama wa taifa kuwa umemsaidia kikwete kumuibia kura.
  Sasa Ndugu yangu MUSSA Juma usiogope kwani umma upo nawewe kama vijijini na hitaji la maji,
  Alafu wewe unajua utovu wa nidhamu wa serikali hivyo fanya kazi tumalizie kuamsha umma ili 2015 tuiondoe erikali iliyo dhalimu kwa haki na za masikini mwisho wao umefika misri walimyoa wao sisi wetu tumesha mwekea maji asubiri kipara,nandani ya cku15 mafisadi watajua uchungu wa jasho la walala hoi walilo vuja kwao na kwa wazungu pitia ukoloni mamboleo wanao usaidia kwa vigezo vya uwekezaji na ubinafsishaji bandia.
  Ni dhambi kubwa kwa vyombo vya usalama kusaidia kunyamazisha wasema kweli,ila kwa ukweli tutaushinda wongo.PA1 Mussa mapaka kaanani.

 5. BERNARD KOMBA

  19/09/2011 at 7:29 pm

  Mussa Juma kwa sababu ya kutetea haki kwake mnampa kesi ya kutokuwa raia wa Tanzania, Mbona wengine mnawapa mpaka nyadhifa za juu katika uongozi wa nchi yetu na uhamiaji wanajua mnajifanya misukule,siku moja ankula huu

 6. BERNARD KOMBA

  19/09/2011 at 7:33 pm

  Hadhi ya usalama wa Taifa inaporomoka kwa kasi hata kama mna LICENCE TO KILL use it wisely, msimtishie kijana huyo kwani waandishi wanafanya kazi ya kitume na ndio hao walioandika vitabu vitakatifu, DONT DISTUREB THEM, naomba usalama wa taifa kumuombea maisha marefu mwandishi huyo na tunategemea ulinzi wenu juu ya maisha yake.

 7. HAMIS HAMAD

  03/01/2012 at 6:28 pm

  Naomba kujua hii issue ya Mwandishi Mussa Juma imeishia wapi ?

 8. bado niponipo

  03/01/2012 at 10:14 pm

  kazi kwelikweli

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Afya

Watumishi wa afya 200 kupatiwa mafunzo ya utoaji dawa ya usingizi kuokoa maisha wajawazito

Published

on

Kufuatia upungufu wa wataalamu wa dawa za usingizi (anaesthesia), serikali itatoa mafunzo ya dawa za usingizi kwa watumishi wa afya 200 katika vituo vya afya vya upasuaji wa dharura kwa akina mama wajawazito.

Hatua hiyo inakuja ikiwa imepita miezi 6 baada ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kutangaza kuanza kutoa shahada ya dawa ya usingizi (Bsc. Anaesthesia Nursing).

Katika taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano serikalini cha Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, inaeleza kuwa mafunzo hayo yatatolewa sambamba na uboreshaji wa huduma ya upasuaji wa dharura kwa wajawazito ili kuokoa maisha ya wanawake na watoto ambao hufariki kwa kosa huduma muhimu za uzazi kwenye vituo vya afya.

“Mkakati wa kuhakikisha huduma za afya kwa akina mama wajawazito zinakuwa salama na uhakika kwa kuandaa rasilimali watu, miundombinu ya majengo na vifaa vitakavyowezesha huduma hizi ikiwemo upasuaji wa dharura kwa akina mama wajawazito wakati wa kujifungua,” imeeleza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya, vifo 556 vitokanavyo na uzazi kwa kila viumbe hai 100,000 huripotiwa kila mwaka katika maeneo mbalimbali nchini. Maana yake ni kwamba watoto na wajawazito hufariki hasa wakati wa mama akijifungua.

Aidha, serikali itaboresha vituo vya afya 288 vya serikali vilivyopo nchini ili kuviwezesha kutoa huduma ya dharura ya upasuaji kwa wajawazito ambapo waaguzi katika vituo hivyo watapatiwa mafunzo ya dawa za usingizi ili kuokoa maisha ya akina mama na watoto wachanga.

Utekelezaji wa mafunzo hayo ni matokeo ya ushirikiano wa Wizara ya Afya na Mfuko wa Pamoja wa Afya ambapo zaidi ya sh1,079 bilioni zimepatikana kufakisha mafunzo hayo ya dawa ya usingizi kwa wauguzi na matabibu waliopo kwenye vtuo vya afya nchini.

“Fedha hizo zitasomesha watumishi wapatao 200, kati ya watumishi hao 100 watapata mafunzo yao katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na MOI, watumishi 50 watafanya mafunzo katika hospitali ya KCMC, na 50 watafanya mafunzo hayo kwenye hospitali ya Bugando,” imefafanua taarifa ya wizara.

Lengo la serikali ni kuhakikisha ifikapo 2019 na kabla ya 2020 vituo vyote vya afya vinavyomilikiwa na serikali vinakuwa na watumishi maalum wa kutoa huduma ya dawa ya usingizi kwaajili ya wapasuaji wasiopungua wawili kwa kila kituo.

Mafunzo hayo ya mwaka mmoja ni mpito wakati serikali ikiendelea kukamilisha taratibu za kurasimisha utoaji wa shahada ya kwanza ya kutoa dawa ya usingizi katika Chuo cha MUHAS katka mwaka huu wa 2018/2019.

Hali halisi ya huduma ya dawa za usingizi nchini
Takwimu za wizara ya Afya zinaonyesha kuwa kuna upungufu mkubwa wa madaktari wenye utaalamu wa kutoa dawa ya usingizi hasa wakati wa huduma ya upasuaji ambapo kwa sasa waliopo ni asilimia 1.2 tu ya mahitaji yote.

Ili kuweza kukidhi mahitaji yote ya huduma hiyo wanahitajika madaktari 2000, lakini waliopo sasa ni madaktari 30 pekee.

Kufuatia changamoto hiyo Januari 31, mwaka huu wadau mbalimbali wa afya na elimu walikutana na kujadili namna ya kuondoa changamoto hiyo na kupendekeza mtaala utakaotumika kufundishia kozi ya Aesthesia kabla ya kuupeleka kwa Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU).

” Ni kweli kumekuwepo kwa changamoto hiyo ya watalaamu wa dawa hizo lakini sasa mpango huu ukikamilika maana yake tutaongeza idadi ya madaktari kamili maana hawa waliopo wengi ni wale ambao wamesoma kozi kwa mwaka mmoja au miwili.

” Mafunzo yakianza kutolewa hapa chuoni Muhimbili wataweza kuchukua wanafunzi 200, Bugando 50 na KCMC 50 jambo ambalo litaongeza idadi kubwa ya watalaamu ili kuweza kufikia lengo letu la kuwa na wataalamu 2000 nchi nzima,” alinukuliwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Mpoki Ulisubisya.

Continue Reading

Jamii

Waziri Mkuu Majaliwa: Hatutangazi nyongeza ya mshahara hadharani kuepusha athari kwa jamii

Published

on

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameweka wazi kuwa serikali haitatangaza nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa umma hadharani ili kuepusha athari kwa jamii ikiwemo kupanda kwa bei ya bidhaa.

Akizungumza leo Bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalumu (CHADEMA), Susan Lymo ambaye alitaka kufahamu kwanini Serikali imewanyima au imeshindwa kuwalipa watumishi wa umma nyongeza ya mishahara ambayo ni haki yao ya msingi kulingana na miaka waliyokaa kazini.

Akijibu swali la Mbunge huyo, Waziri Mkuu Majaliwa amesema Serikali ina utaratibu wa kutoa nyongeza ya mishahara kwa watumishi wake lakini haitangazi kwa wananchi wote kama ambavyo imekuwa ikifanyika kwenye sherehe za wafanyakazi za Mei Mosi kila mwaka.

Amesema Serikali ikitangaza mishahara hadharani inaweza kusababisha usumbufu kwa watu wasio watumishi wa umma na inaweza kupandisha bei ya bidhaa na kuathiri mwenendo wa mahitaji ya wananchi sokoni.

Nyongeza za mishahara ambazo zinatangazwa hadharani, mara nyingi zina athari yake sio kwamba Serikali haikusudii kutoa nyongeza ya mshahara kwa mwaka, lakini unapotumia Mei Mosi kutangaza nyongeza ya mshahara unaleta athari kwenye jamii kwasababu vitu vinaweza vikapanda bei, vikawasumbua hata na wananchi ambao hawalipwi mshahara,” amesema Waziri Mkuu.

Amebainisha kuwa siyo lazima Serikali itangaze hadharani kila inapoongeza mishahara kwa watumishi wa umma lakini ifahamike kuwa Serikali ina utaratibu wake mzuri wa kuboresha stahiki za wafanyakazi wake kila mwaka.

Suala la nyongeza ya mishahara liko Serikalini na Mhe Rais ameishawahakikishia wafanyakazi atawaongeza mishahara na sio lazima litangazwe hadharani. Mshahara ni suala la mtu binafsi hata ukiongezwa leo kuwa tumeitangaza leo tumeongeza mshahara kwa kiwango hiki. Ukifanya hivi tayari umeleta kupanda kwa gharama’” amebainisha Waziri Mkuu.

Ameongeza kuwa mkakati wa Serikali ni kupunguza gharama za mahitaji kwenye masoko ili kuzuia mfuko wa bei za bidhaa.

Hata hivyo, Waziri Mkuu Mjaliwa amesema Serikali inaendelea kufanya sensa ya watumishi wote nchi nzima na zoezi hilo likikamilika itaboresha nyongeza ya mwaka, nyongeza ya mishahara na upandishaji wa madaraja.

Awali katika swali lake, Mbunge Lyima amesema Serikali inakiuka Sheria ya Utumishi wa Umma ya kuwapatia watumishi stahiki zao na kuwapunguzia motisha ya kufanya kazi kwa ufanisi katika maeneo yao ya kazi na kuathiri mafao baada ya kustaafu.

Hoja ya Mbunge huyo ni muendelezo wa malalamiko ya watumishi dhidi ya Serikali kwamba hawajapata stahiki zao tangu ilipoanza zoezi la ukakiki wa watumishi wa umma mwaka 2015. Katika zoezi hilo watumishi zaidi ya 9,000 walibainika kutokukidhi vigezo vya utumishi na hivyo kuondolewa kazini.

Huenda kauli aliyoitoa Waziri Mkuu leo Bungeni inaweza ikatofautiana na ile ya Rais John Magufuli aliyoitoa wakati wa sherehe za Mei Mosi, 2018 mijini Iringa ambapo alinukuliwa akisema hawezi kutoa nyongeza ya mishahara akidai Serikali haina fedha.

Kwangu mimi ninafikiria hizi pesa tunazotoa kwa ajili ya elimu bure ni nzuri kuliko fedha hizo kuzipeleka kuongezea mishahara, naona bora kuwapa mikopo wanafunzi wa vyuo vikuu kuliko kuongezea wafanyakazi mishahara,

Nikisema nitaongeza hizo pesa mimi nitazitoa wapi? naogopa kusema uongo. Hata mimi napenda kupandishiwa mshahara lakini kwa hali halisi ya sasa hivi lazima niwaeleze ukweli,” alinukuliwa Rais Magufuli.

Hata hivyo alibainisha kuwa kabla ya kuondoka madarakani ataboresha maslahi ya wafanyakazi wa umma, “Nawaahidi, kipindi changu cha urais hakitaisha kabla sijapandisha mishahara kwa wafanyakazi, kupandisha kwangu haitakuwa kwa shilingi elfu kumi, itakuwa ni kupandisha kwelikwel.”

Continue Reading

Jamii

Maaskofu KKKT wapewa siku 10 kufuta waraka

Published

on

Serikali imetoa siku 10 kwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), kuufuta kwa maandishi waraka wao waliotuoa Machi 24 mwaka huu na kisha kuujulisha Umma kwa njia mbalimbali walizotumia kuusambaza.

Kanisa la KKKT kupitia Baraza lake la Maaskofu lilitoa waraka uliopewa jina la ‘Taifa Letu Amani Yetu’ wakati wa Pasaka ambao mbali na masuala ya kiroho, ulibainisha mambo kadhaa yanayogusa mstakabali wa taifa.

Katika mitandao ya kijamii leo imesambazwa barua yenye kumbukumbu no. SO.748/25 inayoonyesha imeandikwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama Wizara ya Mambo ya Ndani kwenda kwa Mwenyekiti /askofu Mkuu wa KKKT iliyoandikwa Mei 30, 2018 ikitoa maelekezo ya kufutwa waraka huo ndani ya siku 10 tangu ilipoandikwa barua hiyo.

Ikiwa na kichwa cha habari ‘Ujumbe wa Baraza la Maaskofu wa KKKT’ barua hiyo inaeleza baraza hilo halitambuliki kisheria katika ofisi ya msajili.

“Unaelekezwa kuufuta waraka husika kwa maandishi na kuujulisha umma kuwa taasisi yako haikuwa na haina uwezo kisheria kufanya kile mlichokifanya. Maandishi hayo yaufikie umma wa Watanzania kwa kupitia vyombo vya habari na njia zingine zilezile zilizotumika kuufikisha waraka ule mliouita ‘Ujumbe wa Baraza la Maaskofu KKKT’.

Hata hivyo, barua hiyo imetoa onyo kali kwa taasisi hiyo dini nchi kutekeleza agizo mara moja la sivyo itachukuliwa hatua za kisheria.

“Maelekezo haya yatekelezwe ndani ya siku kumi tangu kupokea kwa barua hii vinginevyo hatua kali zaidi za kisheria zitachukuliwa dhidi ya taasisi hii,” inasema barua hiyo.

Ikumbukwe kuwa  waraka huo ulisainiwa na maaskofu 27 wa kanisa hilo nchini na kutaja baadhi ya mambo hayo kuwa ni pamoja na utekaji, utesaji, kupotea kwa watu, mashambulizi ya silaha dhidi ya viongozi wa kisiasa, mauaji yenye mwelekeo wa kiitikadi, vitisho, ubambikiziaji wa kesi, na matumizi mabaya ya vyombo vya dola dhidi ya wananchi.ni hali ya kijamii na kiuchumi, maisha ya siasa, na masuala mtambuka likiwamo suala la Katiba Mpya.

Waraka uliongeza pia kwamba uhuru wa kujieleza, kutoa na kupokea habari umeendelea kutoweka nchini huku ukionya kubanwa na hatimaye kuelekea kupungua kwa uhuru wa Bunge, Mahakama, na Tume ya Uchaguzi, ukisema hatua hii ni pamoja na kudhoofishwa kwa serikali za Mitaa.

Lakini kabla ya KKKT kutoa waraka wao, Kanisa Katoliki nalo lilitoa waraka kama huo likionya baadhi ya mambo ikiwemo uminywaji wa misingi ya demokrasia ya vyama vingi na uhuru wa kujieleza.

Baada ya kusambaa kwa waraka huo, yalijitokeza mambo mengi ikiwemo kutofautiana na kwa mawazo ya wananchi kuhusu wajibu wa viongozi wa dini katika kutoa ushauri, kuonya au kukemea pale mambo yanapoenda mrama.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa na Maaskofu wa KKKT

Hata hivyo, barua hiyo imepokelewa kwa hisia tofauti na watumiaji wa mitandao ya kijamii ikizingatiwa kuwa suala hilo lilijadiliwa na kupita, iweje linaibuka tena wakati huu ambapo kuna utulivu na yale mambo waliyoyapigia kelele na maaskofu  yamepungua ikiwemo kuteswa, kupotea kwa watu na vitisho dhidi ya viongozi wa kisiasa.

 

Wananchi bado wanawaamini viongozi wa dini

Wadau mbalimbali wa masuala ya kijamii wamesema kama kweli barua hiyo imetolewa na serikali, inaweza kuchochea taharuki zaidi kwa waumini wa kanisa hilo na wananchi kwasababu linagusa moja kwa moja imani zao.

Amebainisha kuwa bado waumini wengi wana imani na viongozi wao dini na kwamba yale wanayotamka yanakuwa na nia njema kwa jamii yao. Na katika muktadha huo serikali inapaswa kuwa makini ili kuepusha matatizo zaidi yanayoweza kutokea.

Akizungumza na FikraPevu, Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena amesema kama serikali ilibaini kuna tatizo kwenye usajili wa Baraza la Maaskofu la KKKT ingekaa na wahusika na kulimaliza kuliko kujitokeza hadharani na kuendeleza jambo ambalo limepita.

“Mimi namwamini Mungu kuliko serikali na viongozi wangu wa dini hasa Maaskofu. Hivyo serikali inapaswa kuwa makini na mambo yanayogusa imani za watu. Katika hili walipaswa kutafakari sana jinsi ya kushughulika nalo. Vinginevyo halina afya kwa ustawi wa taifa letu,” amesema Meena.

Amesema Maaskofu walitimiza wajibu wao wa kuonya kabla mambo hayajaharibika na serikali inapaswa kuyafanyika kazi yale yalyotajwa kwenye waraka au kukaa kimya ili kuepusha migongano isiyo na faida kwa taifa.

Continue Reading

Muhimu Kusoma

Copyright © 2020 FikraPevu.com