Connect with us

DATA

Elimu ya MEMKWA kupunguza idadi ya watoto wasiojua kusoma na kuandika

Published

on

Elimu ni haki ya msingi kwa kila mtoto, lakini kutokana na changamoto mbalimbali wapo watoto ambao hawakupata fursa ya kupata elimu ya msingi katika umri unaostahili.

Kwa kuzingatia kuwa elimu ni silaha muhimu kumkomboa  mtoto kifikra, serikali ilianzisha programu ya  Mpango wa Elimu ya Msingi Kwa Watoto Walioikosa (MEMKWA) ili kuwawezesha watoto kupata elimu  nje ya mfumo rasmi.

Programu ya MEMKWA ilianzishwa kwa majaribio kati ya mwaka 1999 hadi 2002 katika wilaya za Musoma Vijijini, Kisarawe, Ngara, Masasi na Songea Vijijini.  Programu hiyo ilipoonyesha mafanikio, mwaka 2003 serikali ilianzisha madarasa ya MEMKWA katika shule za msingi nchi nzima.

Elimu ya MEMKWA imegawanyika katika makundi rika mawili, ambapo kundi rika la kwanza hujumuisha watoto walio na umri kati ya miaka 10-13. Watoto hao husoma kwa miaka 2 hadi 4 kisha huruhusiwa kufanya mtihani wa darasa la nne (IV). Kundi rika la pili hujumuisha vijana walio na umri kati ya miaka 14 hadi 18.

Wanafunzi wanaofanya vizuri katika masomo yao huruhusiwa kujiunga katika elimu ya mfumo rasmi na kufanya mtihani wa darasa la saba, wakifaulu huendelea na elimu ya sekondari.

Dhima ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014 inajikita  kuinua ubora wa elimu na mafunzo na kuweka mifumo na  taratibu zitakazowezesha kupata idadi kubwa ya Watanzania  walioelimika na wanaopenda kujielimisha zaidi ili waweze kuchangia katika kufikia malengo ya maendeleo ya Taifa letu.

Licha ya ongezeko kubwa  la watoto wanaoandikishwa darasa la kwanza, bado idadi ya watoto walio katika elimu ya mfumo huu usio rasmi yaani MEMKWA ni kubwa ikilinganishwa na msisitizo wa serikali wa kuifanya elimu ya msingi kuwa bure na ya lazima.

Takwimu za Kituo Huru cha Serikali za mwaka 2016 zinaonyesha kuwa kulikuwa na wanafunzi 69,492 wa MEMKWA  kundi rika la kwanza nchi nzima.

Fikra Pevu imebaini mikoa 10 ambayo ilikuwa na wanafunzi wengi wa MEMKWA kwa mwaka 2016. Mikoa hiyo ni Geita, Kagera, Kigoma, Morogoro, Dar es salaam, Mwanza, Tabora, Rukwa, Tanga na  Singida. Mikoa hiyo ina wanafunzi kati ya 2,927 na 8,732.

Mikoa hiyo 10 iliyotajwa kuwa na wanafunzi wengi bado ina tofauti kubwa ya idadi ya wanafunzi kutoka mkoa mmoja hadi mwingine. Pia kanda ya Ziwa inaonekana kuwa na wanafunzi wengi zaidi ikilinganishwa na kanda nyingine za Kusini na Mashariki.

Mathalani mikoa ya Geita, Kagera na Mwanza ilikuwa na wanafunzi 18,163. Tofauti ya wanafunzi kati ya mkoa ya Geita na Kagera ni wanafunzi 2,784 huku mkoa wa Geita ukiwa unaongoza kwa kuwa na wanafunzi wengi wa MEMKWA ambao ni wanafunzi 8,732 ukifuatiwa na Kagera ambao una wanafunzi 5,948.

Tofauti hiyo ya wanafunzi 2,784 ni pungufu kidogo ya idadi ya wanafunzi 2,927 waliopo mkoa wa Tanga ambao ni miongoni mwa mikoa 10 yenye wanafunzi wengi wa MEMKWA. Lakini idadi ya wanafunzi waliopo mikoa ya Tabora na Kigoma  haitofautiani sana ikilinganishwa na mikoa mingine kama inavyoonyeshwa hapo juu kwenye kielelezo cha picha.

Pia tofauti hiyo inajitokeza kwa mkoa wa Iringa wenye wanafunzi wachache kabisa na Geita yenye wanafunzi wengi Tanzania Bara. Mkoa wa Iringa ulikuwa na wanafunzi 252 tu ikilinganishwa na Geita yenye wanafunzi 8,732.

Iringa inajumuishwa katika mikoa 10 kati ya 26 ambayo ilikuwa na wanafunzi wachache kabisa wa MEMKWA. Mikoa mingine  ni Kilimanjaro, Simiyu, Songwe, Dodoma,Lindi, Mbeya, Manyara, Katavi  na Njombe.

Mikoa hiyo 10  yenye wanafunzi wachache ilikuwa na jumla ya wanafunzi 10,907, ambapo ni juu kidogo ya mkoa mmoja wa Geita wenye wanafunzi 8,732. Licha ya Simiyu kuwa katika kanda moja na mazingira yanayofanana na Geita bado mkoa huo uko miongoni mwa mikoa yenye idadi ndogo ya wanafunzi.

 

Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ina wanafunzi wachache ambapo haitofautiani sana na mikoa ya Kanda ya Kaskazini hasa mikoa ya Kilimanjaro na Manyara. Ukitazama kwa makini kwa kila kanda kuna mikoa yenye idadi kubwa na ndogo ya wanafunzi wa MEMKWA.

Hali hii inaweza kuashiria utofauti uliopo katika uandikishaji wa watoto kwa darasa la kwanza na idadi ya wanafunzi ambao wanachelewa kuanza shule.  Pia wapo wanafunzi  wanaodondoka njiani  na kushindwa kuendelea na masomo.

Changamoto Zilizopo

Wadau wa elimu wanasema maeneo ambayo yanaongoza kuwa na wanafunzi wengi wa MEMKWA, sababu ni kuwa baadhi ya wazazi wanakataa kuwaandikisha watoto wao shule wakiwa katika umri mdogo.

Wanatumia kigezo hicho kwa kudai kuwa baadhi ya shule ziko mbali na makazi wanayoishi, hivyo huwalazimu wanafunzi kutembea umbali mrefu kuzifuata shule na watoto wadogo hawawezi kufika huko shuleni kwa kuhofia usalama wao.

“Wazazi wengi wanakataa kuwapeleka watoto wao shule kwasababu shule ziko mbali, hivyo wanasubiri wakue na kufikia umri wa kujitegemea ndipo waanze kwenda shule” anasema Faustin Clement mkazi wa Geita.

Kauli hiyo inathibitishwa na Mwanachama wa  shirika la HakiElimu, Profesa Suleman Sumra katika utafiti wake alioutoa katika Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET) ambapo anasema;

“Ni wazi kwamba agizo la kuandikisha watoto kuanza shule wakiwa na umri wa miaka saba limepuuzwa. Kama ilivyokuwa siku za nyuma, wazazi wengi huwaona watoto hao bado wadogo na hivyo kuweka kipaumbele katika kuwaandikisha shule wenye umri mkubwa kwanza”, anafafanua zaidi,

“ Wazazi wengi wanashauri suala la umri liwe wazi kwa kuangalia mazingira na utamaduni wa watu. Baadhi ya sehemu, umbali wa ilipo shule kulinganisha na makazi ni mkubwa mno kuliko uwezo wa kutembea wa mtoto wa miaka saba”.

Kutokana na changamoto mbalimbali, hivyo zinawazuia watoto kuanza darasa la kwanza kwa wakati, elimu ya MEMKWA huwa njia pekee ya mtoto kuipata elimu ya msingi lakini sio wote wanaofanikiwa kuingia katika elimu hiyo.

Rafiki wa Elimu kutoka mkoa wa Mara, Juma Richard anasema elimu ya MEMKWA ni njia mojawapo ya kufuta ujinga kwa wanafunzi walioshindwa kuingia katika elimu ya mfumo rasmi. Anashauri kuwekwa kwa mipango endelevu ambayo itawawezesha watoto kupata elimu bila kikwazo chochote.

“Watanzania tunaiona elimu ya MEMKWA kama haina msaada kabisa kwetu lakini ifike mahali tukumbuke kwamba Mwalimu Nyerere alipigana kufa na kupona kuhakikisha tunafuta ujinga nchini na mbinu kubwa aliyotumia ni kuhakikisha waliokosa elimu wanapata elimu bila kujali umri wao na alifanikiwa kwa kiwango kikubwa sana”. Anasema Richard.

Matamko na Ripoti Mbalimbali

Ripoti ya shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ya mwaka 2015 inaonyesha kuwa takribani watoto Milioni 58 wameshindwa kujiunga na shule na milioni 100 kati yao wameshindwa kuhitimu  elimu ya msingi duniani kote.

Tanzania bado ina idadi kubwa ya watoto ambao hawako shuleni na wanatakiwa kupatiwa elimu ili kujenga taifa la watu walioelimika.

Kwa mujibu wa takwimu za Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) za mwaka 2012 zinaonyesha kuwa Tanzania ina jumla ya vijana wa umri wa miaka 7-17 Milioni 3.5 waliopo nje ya shule, ambapo kati yao Milioni 2.5 wanahitaji elimu ya Sekondari na Milioni 1 wanahitaji Elimu ya msingi.

Mafanikio Ya MEMKWA

Kwa mwaka 2013 wanafunzi 4,170 wa MEMKWA walichaguliwa kujiunga darasa la tano huku wengine 1,576 waliofanya mtihani wa darasa la saba walijiunga na elimu ya sekondari mwaka 2012. Pia Serikali imeimarisha mafunzo kwa walimu wanaofundisha wanafunzi wa MEMKWA ili kupunguza idadi ya watoto wasiojua kusoma na kuandika.

"Vilevile wizara imeandaa Mwongozo wa Ufundishaji wa KKK (Kusoma, Kuandika na Kuhesabu) kwa watoto wanaosoma nje ya mfumo rasmi kwa lengo la kuwasaidia  walimu watakaofundisha  madarasa ya Elimu Nje ya Mfumo Rasmi". anasema Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Njalichako akiwa bungeni hivi karibuni.

Programu ya MEMKWA inapaswa  kuimarishwa kwa kuongeza rasilimali watu na miundombinu ili kuhakikisha wanafunzi waliokosa elimu ya msingi wanapata fursa ya kusoma kama watoto wengine katika shule za msingi na sekondari.

Dira Maendeleo ya Taifa, 2025 (The Tanzania Development Vision) inalenga kuwa na taifa la watu wenye elimu ya kati na ya juu ili kuwa na watendaji kazi wenye uwezo wa kushughulikia kikamilifu changamoto za kimaendeleo.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

DATA

Maambukizi  ya Ukimwi yanavyoshamirisha yatima shule za msingi Iringa, Mbeya

Published

on

Mikoa ya Iringa, Mbeya na Njombe imetajwa kuongoza kwa idadi kubwa ya wanafunzi yatima wanaondikishwa katika shule za mingi, jambo linaloweza kuongeza gharama za matunzo kwa watoto hao.

Kulingana na uchambuzi wa takwimu za Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) za mwaka 2016 zinaeleza kuwa mkoa wa Iringa ulishika nafasi ya kwanza kitaifa kwa kuwa na wanafunzi  29,062 yatima sawa na asilimia 14.4% ya wanafunzi wote wa shule za msingi kwa mwaka huo.

Iringa ilikuwa na wanafunzi  wa shule za msingi wapatao 202,113 lakini kati ya hao mwanafunzi 1 kati ya 10 alikuwa ni yatima.

Kulingana na Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009, mtoto anahesabika kuwa ni yatima endapo atafiwa na mzazi mmoja au wote wawili. Kimsingi anakosa matunzo au upendo wa mzazi mmoja au wote wawili ambapo inaweza kuwa ni changamoto kwa ukuaji wake hasa katika upatikanaji wa elimu.

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa siyo Iringa pekee ndiyo yenye idadi kubwa ya wanafunzi yatima lakini mikoa yote inayounda kanda ya Nyanda za Juu Kusini iko kwenye nafasi ya juu kabisa miongoni mwa mikoa 5  ya Tanzania bara yenye yatima wengi.

Nafasi ya pili inashikwa na mkoa wa Njombe ambao ulikuwa na wanafunzi  yatima 19,794 sawa na asilimia 12.7, ikifuatiwa na Mbeya (41,956) sawa na 11.3%. Mkoa wa nne ni Pwani (26,545) sawa na 10.4% na nafasi ya tano ni Kagera (45431) sawa na asilimia 9.8.

Mikoa hiyo mitano inaunda jumla ya asilimia 44.2  ya wanafunzi wote  731,536 yatima waliokuwepo katika shule za msingi kwa mwaka wa 2016. Hiyo ni sawa na kusema kuwa watoto 4 wa mikoa hiyo mitano kati ya 10 ya Tanzania bara ni yatima.

Lakini iko mikoa ambayo imefanikiwa kuwa na idadi ndogo ya wanafunzi  yatima ikiwemo Manyara ambayo ilikuwa na wanafunzi 15,854 sawa na 6.2% ikifuatiwa na Kigoma (6.5%),  Singida na Mtwara ambazo zote kwa pamoja zilikuwa na 6.7 %. Na mkoa wa tano toka chini ni Lindi (6.8%).

Nini kiini cha kuwepo utofauti mkubwa wa kimkoa wa uwepo wa wanafunzi yatima katika shule za msingi za serikali na binafsi nchini?

ASILIMIA ZA WANAFUNZI YATIMA KATIKA SHULE ZA MSINGI KIMKOA- 2016

 

Wadau waelezea dhana hiyo

Wadau wa afya na masuala ya elimu ya jamii wanaeleza kuwa kuna uhusiano mkubwa wa ugonjwa wa UKIMWI na uwepo wa wanafunzi wengi au wachache yatima katika maeneo mbalimbali nchini.

 Kulingana na takwimu za Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) za mwaka 2017 zinaeleza kuwa mikoa ya Mbeya, Njombe na Iringa ambayo ina wanafunzi wengi yatima ndiyo vinara wa maambukizi ya Virusi vya Ukimwi nchini.

Kwa muktadha huo idadi ya wazazi wanaofariki kwa maradhi hayo nayo ni kubwa; uwezekano wa watoto wengi kubaki au kuondokewa na wazazi wote wawili ni mkubwa. VVU husambazwa zaidi kwa njia ya ngono (Uasherati na uzinzi), Matumizi ya pombe na dawa za kulevya, kutakasa wajane na baadhi ya mila na desturi. Ugonjwa huo hauna dawa wala kinga.

TACAIDS inaeleza kuwa  mkoa wa kwanza ni Njombe wenye  asilimia 14.8 ikifuatiwa na Iringa kwa asilimia 9.1 na Mkoa wa Mbeya unashika nafasi ya tatu kwa asilimia 9. Lakini imebainika kuwa mikoa yenye wanafunzi yatima wachache katika shule ina viwango vidogo vya maambukizi ya UKIMWI. Mafano  Manyara (1.5%) na Lindi (2.9%).

Msemaji wa Tacaids, Glory Mziray, wakati akiongea na wanahabari alisema maeneo watanzania walioonesha kuwa na ufahamu sahihi wa elimu kuhusu Virusi vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi wanafikia asilimia 60 jambo linalosababisha kuwepo mwamko mdogo wa kubadili tabia katika maeneo yenye maambukizi makubwa ya maradhi hayo.

Alibainisha kuwa njia mojawapo ya kupunguza maambukizi ya Ukimwi ni tohara kwa wanaume. Njia hiyo napunguza maambukizi ya Ukimwi kwa asilimia 60 na kusisitiza kuwa ipo haja ya kutoa elimu zaidi juu ya uelewa wa ugonjwa huo ili watoto wapate matunzo ya wazazi wote wawili.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi ya Vijana ya YOPOCODE, Alfred Mwahalende amesema mila, ushirikina na kugombania mali ni sababu nyingine inayoongeza watoto yatima shuleni.

“Sababu zingine ni masuala ya kishirikina ambayo hayazungumzwi sana. Katika maeneo ambayo tumekutana na wanavijiji wanaseama baba alirogwa kutokana na mali ili ndugu zake warithi. Wengine wanatafuta utajiri kwa kutoa ndugu zao kafara.” Ameeleza Mwahalende.

Amebainisha kuwa elimu itolewe kwa jamii juu ya kuwatunza watoto yatima na jinsi ya kujikinga na maradhi yote yanayosababisha vifo kwa wazazi ambao wanawajibika kuwalea na kuwasomesha watoto.

“Ninachoweza kusema ni elimu  itolewe lakini pia Asasi zinazoshughulika na masuala ya watoto yatima zione njia ya kuweka sawa kuimarisha na kuwapokea watoto wengi kwenye vituo vyao.” Amesema Mwahalende.

Continue Reading

Afya

Bajeti ya afya 2018/2019 bado tegemezi, yafyekwa kwa asilimia 20

Published

on

Imeelezwa kuwa kuna uwezekano mkubwa kwa watanzania kukosa huduma bora za afya kwa mwaka wa fedha 2018/2019 kutokana na kupunguzwa kwa bajeti ya  Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa asilimia 20.

Hayo yamebainika leo bungeni mjini Dodoma wakati waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akiwasilisha makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019 ambapo amesema wameomba Serikali iwapatie billion 893.4 kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya wizara hiyo.

“Mhe. Mwenyekiti jumla ya fedha kuu ambayo ninaomba Bunge lako tukufu lipitishe katika mafungu yote mawili kwa mwaka 2018/2019 sh. Bilioni 893.4,” amesema Waziri Ummy.

Kiasi hicho cha fedha kilichoombwa kimepungua kutoka trilioni 1.1 za mwaka wa fedha wa 2017/2018 ambapo zimepungua bilioni 171.6  na kufikia bilioni 893.4 mwaka 2018/2019 sawa na asilimia 20.

Waziri Ummy amesema kati ya fedha hizo ambazo wizara yake inaomba, fedha zitakazoelekezwa kwenye matumizi ya miradi ya maendeleo zitakuwa Tsh. bilioni 561.75 sawa na asilimia zaidi 60 ya fedha zote, ambapo matumizi ya kawaida yatagharimu bilioni 304. 47.

“Kwa upande wa matumizi ya kawaida kwa mwaka 2018/2019 wizara ikadiria kutumia kiasi cha sh. Bilioni 304,473,476 (bilioni 304.47) kwa ajili ya matumizi ya kawaida. Kati ya fedha hizo sh. Bilioni 88,465,756 (bilioni 88.46) zitatumika kwajili ya matumizi mengineyo na sh. Bilioni 216,720,000 (bilioni 216.72) zitatumika kwajili ya mishahara ya watumishi,” amesema waziri Ummy na kuongeza kuwa,

“Kwa upande wa miradi ya maendeleo wizara inakadiria kutumia sh. bilioni 4.91 kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Kati ya fedha hizo, sh. Bilioni 1.5 ni fedha za ndani na sh. Bilioni 3.41 ni fedha za nje.” amesema waziri Ummy.

Kwa muktadha huo, bajeti ya afya itategemea fedha za wahisani kwa asilimia 60 kugharimia miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya, zahanati, ukarabati wa majengo na ununuzi wa vifaa tiba na dawa. Hata fedha bilioni 4.91  iliyoelekezwa kwenye miradi ya maendeleo bado ni ndogo.

Changamoto iliyopo ni kwamba fedha za wahisani wakati mwingine huchelewa kufika au zinaweza zisiingie kabisa nchini kutoka na masharti ambayo yanaweza kuathiri utolewaji wa huduma za afya.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii, Peter Serukamba amesema  serikali haina nia ya dhati ya kuinua sekta ya afya kwasababu bajeti inayotengwa kila mwaka ni ndogo na haikidhi mahitaji ya wizara ya afya.

“Uchambuzi wa kamati umebaini fedha zilizotengwa kwaajili ya utekelezaji wa shughuli wizara kwa mwaka wa fedha 2017/18, ni kiasi kidogo ambacho hakiridhishi na kinyume na matarajio ya Mpango wa Bajeti ambao Bunge na Serikali tulikubaliana,” alisema Serukamba.

Licha ya bajeti ya afya kupungua kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019 kwa asilimia 20, fedha za bajeti iliyopita ya 2017/2018 hazikufika zote kwenye wizara hiyo jambo lilikwamishwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya sekta hiyo.

Serukamba amesema, mpaka kufikia Februari mwaka huu, Serikali ilikuwa imetoa Sh. bilioni 576.52 pekee kati ya Sh. trilioni 1.1 zilizokuwa zimetengwa kwaajili ya Bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2017/18,.

Kutokana na bajeti ndogo ya wizara ya afya, wabunge wameshauriwa kuijadili na kuangalia uwezekano wa kuishawishi Serikali kuongeza fedha kwa wizara hiyo ikizingatiwa ni sekta muhimu kwa ustawi wa wananchi ili kuwahakikishia wananchi afya bora.

Continue Reading

Afya

Mgawanyo usio sawa wa hospitali, zahanati unavyokwamisha huduma za afya kwa wananchi

Published

on

Imeelezwa kuwa watanzania watalazimika kusubiri kwa muda mrefu ili kupata huduma bora za afya kutokana na uchache wa vituo vya kutolea huduma hizo ambavyo haviendani na ongezeko la idadi ya watu nchini.

Hali hiyo ni tofauti na matakwa ya Sera ya Afya ya mwaka 2007 ambayo inasisitiza kuwa serikali inawajibika  kuinua hali ya afya ya wananchi wote na hasa wale walioko kwenye hatari zaidi, kwa kuweka mfumo wa huduma za Afya utakaokidhi mahitaji ya wananchi na kuongeza umri wa kuishi wa watanzania.

Lakini watanzania wengi hawafaidiki na tamko la Sera ikizingatiwa kuwa idadi ya watu inaongezeka sana kuliko maboresho na ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya nchini. Vituo hivyo vinajumuisha hospitali, vituo vya afya na zahanati ambazo vinatakiwa kujengwa kwenye vijiji, kata na ngazi ya wilaya na mkoa.

Kwa mujibu wa data za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) za mwaka 2017 zinaonyesha kuwa vituo vya kutolea huduma za afya viliongezeka kutoka 6,321 mwaka 2010 hadi kufikia 7,680 mwaka 2016, ambapo ongezeko hilo ni sawa na vituo 1,359 (14%) tu  kwa miaka saba na wastani wa vituo 194 kila mwaka.

Idadi ya vituo hivyo haiendani na ongezeko kubwa la watu. Kulingana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 Tanzania ilikuwa na watu milioni 45 na hadi kufikia mwaka 2016 inakadiriwa ilikuwa na watu zaidi milioni 50.

Kwa mtazamo wa kawaida ni kwamba karibu nusu ya wananchi hawapati na huduma bora za afya ikiwemo upatikanaji wa vituo vya kutolea huduma za afya, jambo linaloweza kuwaweka katika hatari ya kupoteza nguvukazi ya taifa na hata maisha.

Hata hivyo, bado ziko juhudi mbalimbali zinazofanyika kuhakikisha huduma hizo zinawafikia wananchi katika maeneo yao. Takwimu za NBS zinaeleza kuwa hadi mwaka 2016 kulikuwa na zahanati 6,658 ambazo zilikuwa na kliniki 89 za mama na mtoto. Lakini changamoto ni kwamba zahanati nyingi zinakabiliwa na upungufu wa madaktari, dawa, vifaa tiba na uchakavu wa miundombinu.

Kimsingi Sera ya Afya inaelekeza kuwa kila kijiji kinapaswa kuwa na zahanati yake ili kuhakikisha wananchi hawatembei umbali mrefu kufuata huduma kwasababu afya ni huduma muhimu ya kijamii na inapaswa kupewa kipaombele.

Kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2012, Tanzania ina vijiji 19,200  Ambavyo vinahudumiwa na zahanati 6,658 na hivyo basi kuna upungufu wa zaidi ya zahanati 12,000 ili kukidhi mahitaji ya wakazi wa vijiji vyote.

Kumekuwa na mabadiliko ya kuongezeka na kupungua kwa zahanati nchini. Mathalani mwaka 2013 kulikuwa zahanati 5,680 na mwaka uliofuata wa 2014 zilipungua hadi kufikia 6,002 na sababu kubwa ni  baadhi ya zahanati ni kutotimiza masharti na matakwa ya mwongozo wa matibabu nchini na hivyo kulazimika kufungwa. Juhudi zilifanyika na idadi ya zahanati ziliongezeka hadi kufikia 6,549 mwaka 2015 na mwaka uliofuta wa 2016 zilifikia 6,658.

Kinachotokea ni kwamba wingi wa vituo vya kutolea huduma za afya  unapungua kutoka ngazi ya kijiji, tarafa, wilaya hadi kitaifa. Hali hii inaweza kusababishwa na uhaba wa rasilimali fedha na watu, ubora wa huduma kwenye hospitali husika.

Mwaka 2016, kulikuwa na vituo vya afya 759 nchini kote ambapo ni sawa na kusema kuwa kila mkoa ulikuwa na vituo takribani 29. Kimsingi huduma zinazotolewa kwenye vituo vya afya zina hadhi ya juu ukilinganisha na zahanati kwasababu vinahudumia watu wengi zaidi na vinatakiwa kuwa na vifaa vya kisasa na huduma kama vile upasuaji na kliniki za mama na mtoto.

Idadi ya zahanati zilizoko nchini ni mara 9 ya vituo vya afya ambavyo vinategemewa kuwasaidia wagonjwa ambao hawajapata matibabu ya uhakika kwenye zahanati. Changamoto inayojitokeza ni kuwa vituo hivyo vinaelemewa na idadi kubwa ya wagonjwa wanaotoka ngazi ya chini na kwa vyovyote vile baadhi yake vitakuwa havina huduma bora za matibabu.

Pia vituo vya kutolea huduma za afya hupungua zaidi katika ngazi ya mkoa hadi kitaifa. Mwaka 2016 kulikuwa na hospitali 263 za wilaya, mkoa na rufani. Hizi ndio hospitali pekee zinazotegemewa na watanzania zaidi ya milioni 50 nchi nzima kupata matibabu.

Pengo kati ya vituo vya afya na hospitali sio kubwa sana ukilinganisha na zahanati ambazo ni nyingi lakini huduma zake hazilingani na hospitali nyingine za ngazi ya wilaya na mkoa.

Na utaratibu uliopo ni kwamba mgonjwa anatakiwa kutibiwa ngazi ya juu ikiwa tu zahanati na vituo vya fya vimeshindwa kumpatia matibabu yanayotakiwa. Kwa utaratibu huo vituo vya afya na hospitali nyingi huelemewa na wagonjwa kutokana na uwekezaji mdogo na  huduma zisizoridhisha kwenye zahanati.

Kutokana na hali halisi ya upatikanaji wa huduma za afya nchini, serikali na wadau wanapaswa kuongeza juhudi za kuboresha na kujenga vituo na hospitali ili kukidhi ongezeko la watanzania ambao wanatakiwa kuwa na afya bora zitakazosaidia katika ujenzi wa taifa.

Ujenzi na maboresho hayo ni muhimu yakaenda sambamba na tathmini ya huduma zinazotolewa, idadi ya vituo ili kuyasaidia maeneo yenye uhitaji mkubwa wa huduma za afya.

Continue Reading

Muhimu Kusoma

Copyright © 2020 FikraPevu.com