Connect with us

Investigative

Kilio cha msitu wa Kimboza kusikika Dar

Published

on

WAKATI wananchi wa Dar es salaam wanaendelea kulalamika kuhusu upungufu mkubwa wa maji kwa matumizi ya binadamu na serikali ikinadi sera kwamba itawapatia wananchi maji ya kutosha ifikapo mwaka 2015 kwa kuboresha vyanzo vya maji, chanzo kimoja muhimu cha maji kinacholisha mto Ruvu kinaangamia kwa kasi kutokana na kukosa usimamizi.

Kwa spidi ya ukataji miti katika chanzo hicho, eneo hilo huenda likawa kipara miaka mitano ijayo na kuzidi kutia shaka kuhusu mapambano yaliyopangwa na serikali ya kukabiliana na  mabadiliko ya tabia nchi ambayo yanaanza kuonekana nchini kwa vyanzo vingi vya maji kunyauka.

Chanzo ambacho kinazungumzwa na ambacho kinagusa roho ya mto Ruvu , chanzo muhimu cha maji kwa wakazi wa Dar es salaam, kipo katika milima ya Uluguru, eneo la Matombo sehemu ya Mwarazi, kata ya Mkuyuni,  na kipo katika msitu wa Kimboza.

Upotevu wa msitu huu  licha ya kuwapo na mpango wa menejimenti ya misitu kitaifa na msitu wa kimboza ukiwamo unaashiria balaa kwa Dar es salaam. Ukiangalia hali inavyoendelea ni dhahiri kwamba Kimboza unafifia na mwangwi wake utasikika Dar es salaam kwa maji ya kutumia binadamu kuzidi kupungua hasa kutoka katika chanzo kikuu, Mto Ruvu.

Ukiingia katika mtandao wa kompyuta unaweza kuona umuhimu wa eneo hili kwa taifa ambalo limeachwa holela kwa sababu za ubinafsi na ufisadi kama ukiangalia sababu za kuendelea kufujika kwa msitu na kupoteza mazingira.

Kuna vyanzo vya kudumu vya maji ambayo mtiririko wake unaingia katika mto Ruvu ambao hutumiwa na watu takribani milioni 3 wa Dar es salaam. Vijiji vya jirani kama  Mwalazi,

Changa na Uponda hupata maji yao kutoka Kimboza na Palapala.

Hali ya uoevu inasaidia msitu huu kuwa katika mazingira ambayo kama ukitunzwa na wao wanatunza.

Pamoja na kuwa chanzo cha maji, Kimboza ina maeneo mazuri kwa utalii na maeneo kama Choka Wahawi,Dogo la njiwa,chemchem za Kimboza na eneo la kuzaliana kipepeo.

Maeneo haya yana mambo mengi ambayo yako tofauti yanayofaa kwa ajili ya utalii wa kitamaduni na pia kuelezea historia inayogusa jamii wa eneo hilo.

Jiografia ya Kimboza

Msitu huu wa Kimboza, kwa mujibu wa ofisa mali asili Ande Malango  upo wastani wa mita 619 kutoka usawa wa bahari, ndani ya vipimo vya ramani vya latitudo -7.03 (7″ 1′ 60 Kusini) na longitudo  37.78 (37″ 46′ 60 Mashariki), ikiwa ni kiasi cha kilomita  168  kutoka Dar es Salaam.

Awali msitu huu unaelezwa na wazee wa kimila wa hapo ulikuwa na maeneo maalumu yaliyotumika  kufanya matambiko mbalimbali ya kuomba hisani kwa miungu ya Kiluguru.

Msitu huu uliopo kilomita 60 kutoka manispaa ya Morogoro katika barabara ya kutoka Morogoro kwenda Kisaki kati ya Mkuyuni na Matombo hufikika kwa njia ya gari pia ni nyumbani kwa mijusi inayotoweka duniani, mijusi ya rangi ya Bluu (dwarf gecko-Lygodactus williamsii) lakini inaaminika nyakati zake pia kulikuwa na nguruwe pori,nyani,jongoo,nyoka na wadudu mbalimbali wanaotisha.

Ukiwa na mpaka wa kilomita 11 Mashariki mwa Milima ya Uluguru Kusini mwa Kibungo, msitu huu una mzunguko wa takribani kilomita za mraba 100, ambapo jumla ya hifadhi yake ni hekta 405 .

Aidha kwa sensa ya mwaka 2000 kwa mujibu wa takwimu zilizopo msitu huu unazungukwa na watu zaidi ya 28,159.

Kukiwa na haja kubwa ya nishati inayotokana na kuni hapo zamani kwa mujibu wa mzee  Mohamed Hassan (72) kulikuwa na siku maalumu ya kuokota kuni na mara nyingine kuusafisha msitu huo ili kuepusha mioto isiteketeze msitu huo.

Vurugu zilizopo sasa ambazo zimeacha wazi msitu huo zinafanyika pamoja na kuwapo kwa sheria ya usimamizi wa mazingira sura ya 1921 ya mwaka 2004 kifungu cha 75 ambacho kinahitaji waziri mwenye dhamana kushrikiana na wizara nyingine kuratibu mazingira.

Wakati wizara ya mali asiuli inaonekana kudorora katika hili, watu wa maji walipaswa kuelewa umuhimu wa msitu huu na kuianza kuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba kuna watu wanaoangalia maisha ya misitu kwa kuzingatia mutakabali wa  nchi katika kufikia malengo ya milenia 2015 na malengo ya muda mrefu (2025).

Japo sekta ya misitu ndiyo inayotegemewa sana kuhimili mabadiliko ya tabianchi na kuwapo kwa mikakati mbalimbali ya kukabiliana na hilo vitendo vinavyojitokeza wakati wa kuutembelea msitu wa Kimboza kunainyooshea kidole serikali kwa kushindwa kutoa usimamizi wa maeneo yaliyohifadhiwa (protected area Management Systems-PAMs).

Kwani ukitoka katika maeneo ya ndani ya kijiji cha Kibungo na kupiga hatua za kwenda ndani zaidi katika msitu huo unaanza kuona mabadiliko ambayo si sahihi, mabadiliko ambayo ni kazi ya binadamu ya kufyeka misitu hata ile miti michanga.

Hali hiyo pamoja na kuwakera wanamazingira na kamati ya kijiji cha Kimboza kianachoshughulikia mahusiano na serikali katika utunzaji wa msitu huo,wao wamesema hawafikirii kusaidia kuhifadhi msitu huo na hawajihesabu kama wao ni sehemu ya hifadhi hiyo.

Sababu za kutoshiriki uhifadhi

Msitu huu ambao ni hifadhi kwa mujibu wa sheria unatakiw akuwashirikisha wananchi katika kuhakikisha kila kitu kinaenda vyema.Hii inatokana na sera iliyopo na ulinzi shirikishi na pia kuwapatia kipato wananchi wanaolinda msitu huo.

Sania Kambi , mmoja wa wakazi wa jirani na msitu huo,katika mazungumzo na mwandishi wa habari hizi alielezea uchungu wake kuona msitu wa hifadhi ya Kimboza uliopo kijiji cha Mwarazi kata ya Mkuyuni wilaya ya Morogoro unavyotoweka.

“Ukiutazama kwa nje unauona kama upo,wajanja kwelikweli waliokuwa wanakuja kukata miti, lakini ndani hakuna mti kuna viwanja vya kuchezea mpira” alisema Sania ambaye alisema hali hiyo inatokana na serikali kuususa msitu huo muhimu ambao unahifadhi vyanzo kadha vya mito inayotitirisha maji yake kwenda mto  Ruvu.

Kutokana na kukosekana kwa uangalizi wa bwana miti, msitu huo sasa unaanza kutoweka taratibu na hata vyanzo vya maji vinaanza kunyauka.

Alielekeza kuwa kutokana na kukosa bwana miti na hasa kamati inayoshughulikia msitu huo, watu wamekuwa wakiingia katika msitu huo na kukata miti hovyo na hivyo kuufanya msitu huo kubakia wazi.

“Kwa sasa msitu huu uko wazi, miti iko kwa nje tu lakini ndani kuko wazi kabisa, hii inasikitisha sana na inatia uchungu’’ alisisitiza Sania.

Alisema pamoja na kukosa bwana miti huyo kwa miaka minne sasa lakini pia kamati ya mazingira ya kijiji ambaye yeye pia ni miongoni mwa wajumbe wamesusia kufanya ulinzi  na usimamizi wa msitu huo kwa madai kuwa hawanufaiki na kitu chochote.

Alisema kuwa  miaka mitano iliopita idara ya maliasili   ilikuwa ikiwashirikisha kikamilifu ikiwa ni pamoja na kuwapatia fedha kama motisha kwa ajili ya kazi hiyo ya ulinzi katika msitu huo wa hifadhi.

‘’ Kwa sasa wanakijiji hawafanyi doria katika msitu huu , tumekataa tamaa kabisa, idara ya maliasili haitupi kitu, ‘’ alisema.

Kwa maelezo ya Sania, manufaa waliyokuwa wakiyategemea ni ya malipo ya fedha kutoka kwa idara ya mali asili pale ambapo wanawatuma watu na vibali kwenda kukata miti, hali ambayo kwa sasa haipo.

Pamoja na ukweli kuwa msitu huo ni sehemu ya baraka kubwa ya Tanzania ambapo hekta milioni 33.5 ni eneo la misitu, upotevu wa misitu wa takribani hekta 91,276 pia  unahesabika katika kuangalia kasi ya uharibifu wa mazingira ambapo pia msitu wa kimboza upo.

Wakati maeneo mengine upotevu wa misitu husababishwa na ukataji miti kwa ajili ya kilimo na makazi, malisho ya mifugo, uchomaji moto, uchomaji wa mkaa na uvunaji usio endelevu wa mazao ya misitu kwa ajili ya biashara, vibali vya mali asili za uvunaji wa hifadhi hii ndio chanzo kikuu, kwani hakuna mifugo huko na wala wakulima hawajavamia.

Kitendo cha idara ya maliasili kutoa vibali vya kukata miti bila kijiji kupewa fungu lake kusaidia  maendeleo ya kijiji kumewavunja moyo wa kujitolea wanakijiji kulinda msitu huo kwa kufanya doria za mara kwa mara ili pamoja na mengine kuzuia mioto na watu kukata miti .

Kuna sababu nyingi za wananchi kukataa jukumu ambao wamepewa la kuuhami msitu huo kwa manufaa ya pande zote mbili yaani kijiji na serikali kuu ambayo inaona eneo hilo kama eneo linalohifadhi chemchemi.

Baadhi ya maagizo ya serikali yamechangia wananchi kuususa kwa kuwa hawakuwa wanajua watafaidika nini ni magogo yaliyokatwa katika msitu huo kwa dai la kupunguza minyonya maji (miti) ili kuibakisha ile ya asili.

Agizo hilo wananchi walilifanyia kazi lakini kabla hawajajua kunatokea nini, miti hiyo ilisombwa na watu waliokuwa na vibali na wao wakaambulia patupu.

Hayo yalisemwa na Sania Kambi ambaye pia alithibitisha kwamba agizo hilo lilitolewa hivi karibuni na idara ya Maliasili wilaya ya Morogoro .Agizo hilo lilikuwa ni kuondoa minyonya maji hiyo miti aina ya misedelea ambayo inakausha maji sambamba na kutokomeza miti ya asili.

Miiko imekiukwa Kimboza

Mohamed Hassan (72)Mzee huyu ambaye ni mkazi kijiji cha Mwarazi hajawahi kutoka nje ya kijiji chake tangu kuzaliwa, lakini sasa anaona kama vile anapita katika kipindi kigumu na anashutumu watu waliokataa kutii miiko ya kuingia msitu wa Kimboza na kuwasababishia matatizo makubwa ya mvua na upatikanaji wa maji.

“Haikuwahi kutokea kwa mtu yeyote  kuingia ndani ya msitu huo akiwa na silaha yenye ncha kali  kama vile kisu, panga shoka na hata upinde” alisema mzee huyo na kuongeza kwamba sasa hivi watu wanaingia na malori wanakata miti hovyo , wanachukua magogo na mizimu imekasirika.

Ukizungumza na mzee huyu kukupa historia ya msitu anakuwa na mengi ya kuyasema . Lakini katika makubwa ambayo ndiyo yanamfanya awe na huzuni ni mabadiliko ya hali ya hewa ambapo sasa maji ni kidogo na mvua ni haba na hali ya kupotea kwa wanyama ambao walikuwa na kawaida ya kukaa katika msitu huo.

Yeye anasema kwa miaka takribani 30 iliyopita ilikuwa ni vigumu kuingia katika msitu wa Kimboza kutokana si tu na imani iliyoachwa na wazee kuwa msitu huo ulikuwa ni wa mizimu ambayo ingeweza kuleta neema au balaa  kwa jamii kama mambo hayatafuatwa,na pia unene wa msitu ambao ulikuwa hautoi nafasi hata ya kupiga hatua za kawaida za mtu mzima.

Mzee Mohammed alikuwa anasimulia,uharibifu wa msitu kutokana na kukatwa hovyo kwa miti huku akionesha visiki vinavyoashiria aina ya miti iliyopo ukubwa wake na ukaribu wa miti iliotengeneza msitu mnene wenye kiza .

Kwa anayependa mazingira hali hiyo inakupa taabu kubwa.Uthibitisho wa shaka za Mzee Mohamed  zinaonekana wazi kwani ukifuata mipaka ya awali ya msitu unabaini kwamba unaweza kuingia ndani hata na pikipiki hali ambayo.

Kwa msitu uliokuwa umeshiba hadi kufikia kuingia na pikipiki ni dhahiri kwamba hali ni mbaya unajiuliza shida hii imeanza lini?

“Kwa miaka kumi sasa hali imekuwa mbaya zaidi,na katika mazingira ya sasa hali itakuwa mbaya zaidi”  unaweza kukubaliana na hali hii baada ya kugundua kwamba kuna vitu haviko sawasawa katika msitu huo,vipara vya hapa na pale vilionekana wazi pamoja na visiki.

Hekta zilizoharibiwa ambazo zinasababisha msitu kuwa na vipara hazioneshi kuwa ni tatizo la utafutaji wa nishati bali uchukuaji wa magogo ambao unaaminika unafanywa na watumishi wa idara ya misitu. Kuna sababu za kufanya hivi kwani wanaokuja kukata miti wakiulizwa huwa wakali na wala hawataki kuguswa na kusema wana vibali vya kuvuna, huku wakionesha karatasi vivuli.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kibungo Musa Chande alielezea jinsi ya watu wanaopewa vibali kuja kukata miti katika msitu hao wanavyoteketeza  msitu huo ambao ni urithi wa taifa na wananchi kwa ujumla.

“Unakuta wanapoangusha mti mkubwa ule mti unadondokea katika miti midogo na  kuiua,  lakini pia magari wanaingiza hadi ndani ya msitu kwa ajili ya kuchukua magogo waliokata nayo yanaharibu kwa kiasi kikubwa” alisema mwenyekiti huyo.

Akifafanua zaidi anasema kuwa kwa takribani miaka minne sasa hakuna bwana miti katika eneo hilo hali inayochangia pia kuwepo kwa uharibifu huo.

“Kwa sasa watu wanaingia katika msitu huu bila utaratibu , hakuna bwana miti wa kuwadhibiti wala , hakuna anayesimami uhifadhi wa msitu huo” alisema.

Kimboza yenye programu zinazoshindwa kutoka ukoloni

Kimboza inateketea huku kukiwa na sera na kanuni za kitaifa na za mahali pale, wenyeji wa pale waluguru walikuwa wanazungumzia kutokata miti kwa sababu za kimila na matambiko, lakini katika kusaidia kuwa na utaratibu serikali  iliingiza msitu huo katika hifadhi kwa kutumia sera ya taifa ya misitu ya mwaka 1998 kupitia sheria ya Misitu na mipango ya kuendelkeza misitu.

Katika sera kumeainishwa wazi kwamba wanavijiji ndio nao watahusika katika kulinda na kujipatia faida kutokana na misitu hiyo. kwa kuzingatia sera kunakuwapo na kamati ambayo inashauriana na misitu kuangalia namna ya kuendesha msitu huo.

Inafaa kuelewa kuwa hasira za wanakijiji zinatokana na watawala kudharau makubaliano yaliyofikiwa ya kutengeneza menejimenti ya uendeshaji baada ya Kimboza kutangazwa katika gazeti la serikali kupitia (GN) 417 ya  11/7/1964.

Msitu huu kimsingi unamilikiwa na serikali kuu kupitia,Mali asili na utalii na mtawala wa kwanza wa msitu huu ni Meneja wa misitu wa wilaya ya Morogoro.

Afisa mali asili wa wilaya Ande Malango alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na kudai kuwa wao kama idara ya maliasi hawahusiki kutoa vibali vyovyote na kwamba wanaotoa vibali ni serikali kuu kupitia mkurugenzi wa misitu.

Hata hivyo alilalamikiwa  utaratibu uliopo wa kufanya kazi ndio umekuwa ukisababisha kuzorota kutokana na wao kuwajibika kwa halmashauri badala ya serikali kuu ambayo ndio inahusika moja kwa moja na misitu.

Alisema kuwa hali hiyo imekuwa ikiwapa ugumu wa kazi hasa pale inapotokea watu wameingia katika msitu na kuharibu wanashindwa kufanya kazi kama zimamoto kutokana na kutokuwa na vitendea kazi na badala yake kutegemea kwa mgurugenzi na hivyo mara nyingine kukwama.

Pia alisema kuwa fedha wanazokusanya wao hawazitumii moja kwa moja na badala yake zinapelekwa serikali kuu  na kupatia kiais kidogo ambacho hakikidhi mahitaji.

Aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Morogoro Said Thabiti Mwambungu alisema kuwa mara nyingi uharibufu huo wa mazingira unachangiwa kutokana na watu wanaozunguka katika maeneo hayo kutokuwa na uzalendo wa kutunza rasilimali zao.

Hali hiyo unaweza kuiona hata katika miaka kabla ya kuondoka katika ukoloni.

Inajulikana kwamba Mafuriko ya mwaka 1918 yaliyotokea katika msitu huu yalisababisha kuwapo kwa njaa na njaa nyingine ilitokea mwaka 1940 ambayo wenyeji wanaita kibangarazi ilisababisha kuwapo na ulaji wa nazi na ni mwaka huu ambapo mipaka ya hifadhi hii ilifanyika.

Tatizo kubwa lililoelezwa miaka hiyo ni kutokana na kutokuwapo na menejimenti ya eneo hilo,hali iliyofanya serikali kuanaza kuangalia eneo hilo.

Juhudi zilizofanywa mwaka 1955, serikali ilianza  kushawishi wananchi kulima matuta ili kuzuia mmomonyoko wa udongo, lakini ushawishi huo ulileta madhara makubwa kwa kuwa wananchi waliuana na programu ilifutwa.Lakini mwaka 1961  mvua nyingi zilinyesha tena na maporomoko ya ardhi yalitokea.

Na katika mazingira hayo kulileta haja ya uwajibikaji mdogo kwa watu wanaotakiwa kusimamia rasilimali hizo ndio unapelekea uharibifu huo na kudai kuwa  kama serikali watashughulikia  ili kukomesha hali hiyo.

Hata hivyo Mwaka 1998 serikali iliamua kupitisha sera mpya ya misitu , sera hiyo ilisisitiza zaidi ushirikishwaji wa wananchi katika kutunza  na kuendeleza misitu na kwamba hiyo ilitokana na upungufu mkubwa wa wataalamu wa misitu uwezo mdogo  wa serikali kifedha kusimamia misitu yote  sambamba na upungufu mkubwa wa vitendea kazi katika kutekeleza sera hiyo.

John kimario meneja wa hifadhi ya misitu wilaya ya Morogoro  kutokana na upungufu huo serikali iliteua mikoa minne  ya Tanga ,Kilimanjaro, Arusha na  Morogoro ambapo katika mkoa wa Morogoro  ilichaguliwa ikiwamo msitu wa Kimboza .

Aliongeza kuwa msitu wa hifadhi ya kimboza ukawa kwenye mpango wa ushirikishwaji wa ambao wanakijiji walihusika zaidi katika shughuli za ulinzi, usimamizi  na uendelezaji wa msitu wa hifadhi na kwamba wakati wautekelezaji  huo vijiji vilivyopakana na msitu huo  yaani Changa, Mwarazi Kibangile na uponda  waliandaa sheria  ndogo  ambazo zinatumika hadi sasa.

Alisema wakati huo wanakijiji walikuwa wakinufaika  zaidi na kazi zilizokuwa zikifanyika za kufyeka na kutengeneza barabara  za mioto ambapo fedha zake zilikuwa zikitolewa na serikali  ambapo kwa sasa serikali haitoi bajeti hiyo hali iliopelekea wananchi  kuwa na ushiriki mdogo katika utunzaji wa msitu huo.

Idara ya misitu  tangu mwaka 2007 haijatoa fedha za kufyeka mpaka wa kimboza  na hivyo kusababisha wananchi kukosa hamasa  na moyo wa kutunza msitu huo.

Hata hivyo meneja huyo alibainisha kuwa hakuna takwimu zozote zinazoonyesha kuwa msitu huo wa hifadhi wa kimboza umetoweka kwa kiasi gani huku  akisisitiza kuwepo na mikakati ya kuendeleza ushirikishwaji kwa wananchi wa vijiji hivyo  ili kuweza kusimamia na kulinda raslimali.

Kauli za mtendaji huyu zinaashiria wazi kwamba hajawahi kufika kujionea hali halisi ya Kimboza, msitu ambao nitegemeo kwa wengi lakini ukinyambuka kwa kasi huku watendajii wakibaki maofisini wakiangalia makaratasi yao.

Pamoja na kuwepo kwa sheria za misitu na sera na ushirikishaji wa wananchi eneo hili lina matatizo makubwa ya uharibifu kutokana na  vibali vinavyotolewa lakini bado katika sheria ipo lakini pia sheria ndogo za kijiji ambazo zinatakiwa kuingizwa katika sheria kuu haipo.

 

Kulikuwa na makubaliano ya kijiji  na serikali kuu kuhusu utunzaji wa msitu lakini je hoja ya wananchi kutojua mapato ni tatizo la nani hasa ni serikali au menejimenti.

Katika miaka ijayo huenda kukawa na tatizo kubwa la nishati na sehemu ya kuabudia kama zamani alivyosema Mzee Mohammed pengine huzuni ya mzee Mohamed na uchungu wa Bi kambi unaweza kuangaliwa kwa upana zaidi kwa kuwa na utekelezaji wa sheria, makubaliano na mipango mikakati ya kuhimili mabadiliko ya tabia nchi, sivyo mwangwi wa Kimboza utasikika Dar e s salaam kwa nguvu kubwa, maji yatakapoanza kuwa bidhaa adimu.

Continue Reading
2 Comments

2 Comments

 1. CHarles Ng'atigwa

  21/04/2012 at 11:51 pm

  Kuna kiasi cha ukweli kuhusu matatizo ya usimamizi shirikishi wa msitu huu. Tatizo hili lipo kwenye misitu karibu yote na linafanyiwa kazi. Mwezi december nilikuwa huko kupata mawazo kuhusu usimamizi wa msitu huo na jamii, pamoja na changamoto hizo bado wanafanya doria. Waliomba sinema Janiaru wakaipata ili kuwajengea uwezo zaidi wa kulinda msitu.

  Kuna mkakati wa kupunguza miti ya cedrela inawezekana ndicho kinachoonekana kwa sasa.

 2. peter Mwenda

  20/10/2012 at 7:58 pm

  nawapongezeni kwa kazi yenu yenye tija kwa jamii,jitahidini kuturushia matukio kama hayo hata sisi ili tusaidiane kuelimisha jamii

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Investigative

‘UBESHI’: Safari ya Vijana Kuifikia Almasi Mwadui-Shinyanga

Published

on

MAJUZI nilikuwa katika utafiti wa namna gani Madini ya Almas yanayopatikana katika Mji Mdogo wa Maganzo Wilayani Kishapu mkoani Shinyanga umewanufaisha wananchi wanaozunguka Mgodi wa Almasi wa Mwadui.

(more…)

Continue Reading

Investigative

Hofu ya Usalama kwa wafanyakazi GGM Yatanda

Published

on

SIKU chache baada ya moto kuzuka ndani ya mgodi wa Geita (GGM) na kuteketeza mali zenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 25,hofu kubwa ya kupoteza maisha imeibuka kwa uongozi na wafanyakazi wa mgodi huo.

(more…)

Continue Reading

Investigative

If we can’t give people’s priorities the attention they deserve, why ask them to prioritize?

Published

on

In a move intended to empower the citizens and give them mandate to decide on their own development priorities, the government adopted the decentralization policy.

(more…)

Continue Reading

Muhimu Kusoma

Copyright © 2020 FikraPevu.com