Connect with us

Uchambuzi

Kuhamia Dodoma: Shs. 2 trilioni zinatoka katika bajeti gani?

Published

on

ZOEZI la serikali kuhamia Dodoma linaonekana kusuasua tofauti na lilivyoanza licha ya makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu wa wizara mbalimbali kuwa katika harakati za kuhamia Dodoma kabla ya Februari 28, 2017.

Inaelezwa kwamba, kusuasua kwa zoezi hilo lilinalotokana na agizo la Rais John Magufuli kumechangiwa na mambo mengi, kubwa zaidi likitajwa ‘kukurupuka’ kwa serikali bila kuangalia bajeti zake.

Wachambuzi wa masuala ya maendeleo wanaeleza kuwa, ili zoezi hilo likamilike, serikali inahitaji kati ya Shs. 1.5 trilioni hadi Shs. 2 trilioni, fedha ambazo ni nyingi na hazijaelekezwa kwenye bajeti yoyote, ikiwemo ile ya Wizara ya Sera, Uratibu na Bunge pamoja na Wizara ya Fedha na Mipango.

Badala yake, kauli ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu wa Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama kwamba bajeti ya kuhamishia makao makuu ya Serikali Dodoma litatatuliwa kwa kutumia posho za safari za mawaziri inaonekana ilikuwa ya kisiasa kuliko uhalisia.

“Bajeti tulizopanga, hasa ya 2016/17 sisi tunajua tulipanga nini, tunafahamu mapato yaliyopitishwa na Bunge yakoje. Kwa mfano, mimi Jenista (waziri) kwa mwaka huu mzima wa fedha nina mikutano minne Dodoma. Kwenye ile mikutano yote natakiwa kulipwa posho, maana yake ni kuwa napaswa nipate posho ya miezi mitano, sasa fedha hiyo ndiyo itakayoingizwa kwenye gharama za kuihamishia Serikali Dodoma,” alisema wakati akihojiwa nakituo cha luninga cha TBC1 Agosti 2016.

Waziri Mhagama hivi karibuni alirudia kusisitiza kwamba ni lazima wizara na idara za serikali ziwe zimehamia Dodoma ifikapo Februari 28, 2017 huku akiongeza kwamba hakuna tatizo la ofisi za watumishi.

“Hakuna tatizo la ofisi za watumishi wa wizara zote, kwani majengo yamekamilika na yapo katika hali nzuri tayari kwa ajili ya kuanza kutumiwa, hivyo wakuu husika wakiwamo mawaziri wahakikishe wanatakiwa kuhamia Dodoma,” alisema.

Lakini ratiba ya kuhamia huko iliyotangazwa Agosti 2016 na Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa, inakwenda kwa mwendo wa kinyonga ambapo hata hiyo awamu ya kwanza bado haijatekelezwa huku ukiwa umesalia mwezi mmoja tu.

Mbali ya makatibu na naibu makatibu wakuu, awamu hiyo ya kwanza ya inahusisha pia mawaziri wote pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu na wakuu wa idara kadhaa za kila wizara.

FikraPevu inatambua kwamba, kuhama haraka kwa wahusika katika awamu hiyo ya kwanza kutatoa fursa ya awamu nyingine kufuatia, ambapo kundi la pili linatakiwa lime limehamia Dodoma ifikapo Agosti 2017.

“Awamu ya pili itakuwa Machi 2017 na Agosti 2017 na kipindi hiki kitawapa fursa watendaji wa wizara mbalimbali kuweka bajeti zao za mwaka 2017 na 2018 na kuendelea kuwahamisha watumishi wake kuja Dodoma. Awamu ya tatu itakuwa kati ya Septemba 2017 na Februari 2018, ambapo wizara zitaendelea na uhamishaji wa watumishi wa idara zilizo ndani ya wizara zao,” Waziri Mkuu alikaririwa akisema mara baada ya Rais John Magufuli kutakaza nia ya kuhamishia serikali mjini Dodoma haraka.

Kwa mujibu wa mpango huo wa serikali, awamu ya nne itakuwa Machi 2018 mpaka Agosti 2018, awamu ya tano ni Septemba 2018 na Februari 2020, na awamu ya sita ni Machi 2020 na Juni 2020, ambayo itahusisha Ofisi ya Rais ikiongozwa na Rais na Makamu wa Rais ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kusuasua kwa uhamiaji huo kunawafanya wananchi ‘wafurahie’ mipango ya serikali inaposhindwa licha ya ukweli kwamba walikuwa wanaipongeza serikali ya awamu ya tano kwa kuthubutu kufanya kile ambacho kimeshindikana kwa miaka 43.

Serikali inashindwa kuweka wazi kuhusu bajeti itakayotumika kuhamishia utendaji wake Dodoma, suala ambalo ni la msingi kwa sababu bila fedha mipango yote itaendelea kuwa ya kisiasa.

Katika kipindi hiki ambacho uchumi umeonekana kulegalega, suala la bajeti ni muhimu kuzingatiwa ili ijulikane fedha zinazowahamisha watumishi zinatoka katika fungu gani.

Watawala waliomtangulia Rais Magufuli walishindwa kutekeleza suala hilo si kwa sababu hawakuwa na fedha, bali hawakuwa na dhamira.

Kwa miaka mingi iliyopita, suala la kuhamishia serikali Dodoma limechukuliwa na watawala kama mtaji wa kisiasa huku Watanzania wakiwa na shauku ya kuona utekelezaji.

Hakuna anayepinga hoja ya kuhamia Dodoma kwa sababu ni uamuzi wa muda mrefu na unaweza kuleta maendeleo, lakini kinachotia mashaka ni dhamira halisi ya utekelezaji wake ambayo safari hii imeanza kwa kasi na imezima ghafla.

Kila jambo la maendeleo lina faida na hasara zake, lakini katika kutekeleza maazimio ya serikali, mara nyingi ni vyema kuangalia faida kwa mipango endelevu kuliko kukwamishwa na changamoto.

Gharama za kuhamisha makao makuu ni kubwa kwa upande mmoja kwa sababu fedha zinatakiwa zipatikane ndani ya miaka minne iliyosalia, lakini kwa upande wa pili zinaweza kuwa ndogo kwa sababu ni za mara moja tu wala siyo kujirudiarudia.

Sote tunafahamu kuwa shughuli za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hufanyika Dodoma mara nne kila mwaka, ambapo kuna jumla ya vikao 182.

FikraPevu inatambua kwamba, katika vikao hivyo, ukiacha wabunge, kuna maofisa wengi wa serikali ambao husafiri kutoka Dares Salaam kwenda Dodoma kwa gharama za serikali.

Hawa ni mawaziri, watumishi wa wizara, wageni wa serikali, watumishi wa vyombo vingine vya serikali na kadhalika ambao wanaigharimu serikali nauli au mafuta na magari ya umma, malazi, chakula na posho mbalimbali za kuwa nje ya vituo vya kazi, achilia mbali matengenezo ya maghali kutokana na safari hizo pamoja na hatari ya usalama wa nyaraka za umma.

Ukiacha vikao hivyo vya Bunge, lakini zipo gharama nyingine za watumishi kusafiri katika miji hiyo kwa shughuli za serikali, ambazo ni gharama endelevu.

Tanzania haitakuwa ya kwanza kuhamisha makao makuu yake, kwani zipo nchi nyingi ambazo zimepata kufanya hivyo.

Tangu mwaka 1950 hadi 2000, nchi 13 zimeshabadilisha makao yao makuu ambazo ni Brazil (1956 – kutoka Rio de Janeiro kwenda Brasilia), Mauritania (1957 – kutoka Saint Louis (Senegal) kwenda Nouakchott), Pakistan (1959 – kutoka Karachi kwenda Islamabad), Botswana (1961 – kutoka Mafeking kwenda Gaborone), Libya (1963 – kutoka Benghazi kwenda Tripoli), Malawi (1965 – kutoka Zomba kwenda Lilongwe), na Belize (1970 – kutoka Belize City kwenda Belmopan).

Nyingine ni Nigeria (1975 – kutoka Lagos kwenda Abuja), Ivory Coast (1983 – kutoka Abidjan kwenda Yamoussoukro), Ujerumani (1990 – kutoka Bonn kwenda Berlin), Kazakhstan (1997 – kutoka Almaty kwenda Astana), na Malaysia (2000 – kutoka Kuala Lumpur kwenda Putrajaya).

Kuhamisha makao makuu ni moja ya njia sahihi za ujenzi wa dola na utambulisho wa kitaifa, lakini kutokana na mchakato wake kuwa mkubwa, viongozi wengi huhofia kuchukua hatua kutokana na gharama kubwa za kifedha, kijamii, na hata kisiasa.

Mara nyingi miji mipya mikuu hushindwa kustawi kwa sababu hulazimu serikali kutumia gharama kubwa zaidi kuhamisha serikali yote na idara zake.

FikraPevu inaamini kwamba uamuzi wa serikali ni mzuri, lakini hata katika suala la bajeti inawezekana unakwamishwa na baadhi ya watendaji ambao wanaona dhahiri hakutakuwa na ‘upigaji dili’ ndefu za posho kama ilivyokuwa awali.

Tangu wazo la kuhamisha makao makuu kwenda Dodoma lilipokuja mwaka 1973 baada ya vikao kadhaa vya chama tawala cha wakati huo Tanzania Bara – Tanganyika African National Union (TANU) – idara karibu zote za serikali zimeshindwa kutekeleza uamuzi huo ambao baadaye ulitungiwa Sheria iliyounda Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu (CDA).

Visingizio visivyo na kichwa wala miguu ndivyo vilivyotawala na kukwamisha zoezi hilo ambalo siyo la kisiasa.

Wapo wanaosingizia kwamba mji wa Dodoma hauna miundombinu mizuri, lakini ni hao hao ambao kila mwaka huketi Bungeni kupitisha Bajeti kwa ajili ya CDA kuendeleza mji huo.

Barabara zimejengwa, ingawa siyo kwa wingi, lakini hakuna anayeweza kusingizia kwamba amechelewa kwa ajili ya foleni, maana atakuwa muongo.

Viwanja vimepimwa vya kutosha, maeneo ya umma yametengwa, lakini badala ya wakubwa hao kuhamia huko wengi wananunua viwanja vyao binafsi na kuendelea kuipuuza sheria inaiyowataka wahamishie serikali Dodoma.

Miundombinu mingi imeboreshwa katika mji huo na huduma za kijamii zinapatikana kwa urahisi tofauti na miaka 20 iliyopita kabla hata Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania halijahamishia vikao vyake huko mwaka 1996 kutoka kwenye ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam.

Wizara chache zina ofisi mbili; moja mjini Dodoma (‘makao makuu jina tu’) na Dar es Salaam. Wizara hizi ni Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi; Sera, Uratibu na Bunge), Wizara ya Fedha na Uchumi; Wizara ya Nishati na Madini; Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika; Wizara ya Mipango; na Wizara ya Maji na Umwagiliaji. Mawaziri karibu wote wana nyumba zao (Rest House) kule Area D na nyingine Kilimani, sijui kisingizio ni nini?

Maswali mengi ya msingi yanaendelea kujitokeza kuhusu dhamira halisi ya serikali kuhamia huko wakati tayari ilikwishatangaza kujenga nyumba 80 za wizara kadhaa jijini Dar es Salaam.

Mtu angeweza kufikiri kwamba, lingekuwa ni wazo jema kwa serikali kujenga nyumba hizo 80 mjini Dodoma kama kuonyesha nia yake ya kuhamishia serikali huko.

Kila mwaka wa fedha, Serikali kupitia Wizara ya Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa hutenga mamilioni ya fedha za walipa kodi kwenye bajeti kwa ajili ya CDA.

Aliyekuwa Waziri wa Nchini katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Phillip Marmo, alisema mwaka 2008 kwamba serikali ilikuwa imetenga Shs. 2.4 bilioni kwa ajili ya uendelezaji makao makuu kwa bajeti ya mwaka wa fedha 2008/09, kulinganisha na Shs. 400 milioni za bajeti ya mwaka 2005/06. Fedha hizo, alisema, zingetumiwa na CDA kwa ajili ya upimaji wa viwanja 10,000 huko Nzuguni, Mnadani na Mkalama na tayari vimekwishapimwa.

Mara nyingi fedha hizi hufujwa na maofisa wasio waadilifu na pengine ndiyo maana wamekuwa wakikwepa suala la kuhamia Dodoma kwa kuwa hawawezi kuzipata tena, jambo ambalo wakati fulani limewafanya wakurugenzi wa CDA kuachia ngazi kutokana na ubadhilifu.

Watanzania wanaamini uamuzi huo siyo mbaya, lakini ni vyema serikali ikaweka wazi bajeti hiyo inatoka fungu gani, maana yawezekana likawa ni agizo la kisiasa kama yalivyotokea maagizo mengine miaka iliyopita.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Jamii

Siri iliyofichika mauaji ya wanandoa nchini

Published

on

Hivi karibuni tumeshuhudia matukio kadhaa ya vifo kwa wanandoa, aidha mume kumuua mke wake au mke kumuua mume wake.

Ni matukio ya kusikitisha ambayo yameripotiwa sehemu mbalimbali Tanzania ikiwemo Mkuranga, Pwani, Dodoma and Tabora. Mauaji haya yamezua maswali mengi huku kila mmoja akitoa tafsiri yake kwa namna anavyoiona hali.

Nimesikiliza maoni ya watu mbalimbali wakijaribu kudadavua ni kitu gani kimetokea mpaka vifo hivi vimetokea; maoni mengi yamekuwa ni kukosa hofu ya Mungu na wengine wakiamini ni nguvu za kishirikina.

Ningependa kutoa maelezo ya kitaalamu kwa nini matukio haya hutokea na nini kifanyike kuzuia aina hii ya matukio kutokea katika ndoa zetu.

Nianze kwa kusema taaluma yangu ni sayansi ya jamii ambayo nimejikita katika Saikolojia ya Binadamu (Human Psychology) na Ushauri Nasihi (Counseling). Naamini kwa taaluma hii niko sehemu sahihi kueleza tatizo hili.

Mauaji kwa wanandoa sio swala jipya duniani na pia linatokea kwa kiwango kikubwa kila mwaka. Dk. Aaron Ben-Zeeve katika kitabu chake In the Name of Love: Romantic Ideology and its Victims cha mwaka 2008 anaeleza kuwa takriban asilimia 40 ya wanawake huuawa na waume zao na asilimia 6 ya wanaume huuawa na wake zao kila mwaka duniani.

Takwimu hizo zinadhihirisha wazi kuwa tatizo kubwa liko kwa wanaume kuliko wanawake. Sababu zifuatazo zinaweza kueleza chanzo cha tatizo hili:

Niweke wazi kwamba, sababu za mauaji kutokea ni mchanganyiko wa mambo mengi kwa wakati mmoja, hivyo sababu nitakazozieleza hapa hazina maana ndiyo hizo tu bali zitatoa mwanga kwanini tatizo hutokea.

Nikianza kwasababu za kijamii, makuzi ya watoto wa kiume na watoto wa kike ni tofauti sana karibu jamii zote duniani. Jamii nyingi duniani humkuza mtoto wa kiume na kumfanya kujua yeye ni shujaa, mlinzi na kuwa yuko juu ya mwanamke.

Wanaume wengi tunajiona wajasiri, wenye nguvu na wanawake wako chini yetu hivyo tunaweza kufanya lolote kwao.

                                    Wanaume wengi tunajiona wajasiri, wenye nguvu na wanawake wako chini yetu

Makuzi haya ya jamii yanakwenda moja kwa moja kushawishi saikolojia ya mwanaume, hata katika ndoa. Mwanaume huonesha nguvu zake kwa mwanamke (Masculinity). Hivyo kunakuwa na mpaka baina ya mwanamke na mwanaume.

Hapa tunashuhudia matukio ya mara kwa mara ya wanaume kupiga wake zao kila kukicha. Hii halitokei bahati mbaya kwani makuzi ya jamii yameshawishi saikolojia ya mwanaume na kumfanya mwenye nguvu na anaweza kusahihisha kosa la mwanamke kwa kutumia nguvu na sio mjadala au mazungumzo.

Mjadala kwa wanaume ni dalili ya udhaifu na hii ni dalili ya kuwa na matatizo ya kisaikolojia.

Nitoe mfano mdogo tu, binti mwenye umri wa miaka 21 akitaka kwenda dukani usiku anaogopa sana, ila akisindikizwa na mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 7 anajisikia amani kabisa na uoga hutoweka.

Saikolojia hii inaruhusu amani kwenye mwili wako kwa kuwa tayari mapokeo ya jamii yamekuaminisha kuwa mwanaume ni mwenye nguvu na mlinzi.

Nikigeukia katika upande wa pili wa saikolojia unaochangia vifo kwa wanandoa. Binadamu wote tumeumbwa na nafsi mbili (personality) ambazo ni nafsi imara (strong personality) na nafsi dhaifu (weak personality).

Mtu mwenye nafsi imara ni yule anayeweza kupata msukosuko katika maisha, akaumia ila asikate tamaa akakubali mabadiliko na kuwa tayari kuishi nayo na kufanya vyema zaidi hapo mbele.

Lakini mtu mwenye nafsi dhaifu ni yule anayepitia msukosuko akaumia, akakata tama, akashindwa kuishi na mabadiliko na kuona hakuna namna ya kuendelea kuishi na mabadiliko hayo.

Wengi wetu tumepita huko na tunazidi kupita katika hizi nafsi mbili. Kwa maelezo hayo wanaume wengi wanaoishia kuwauwa wanawake zao mara nyingi wanakuwa na nafsi dhaifu ambazo huwaonyesha wako katika hali mbaya na hawawezi kutoka hapo walipo.

Wivu wa mapenzi ni sababu ya mauaji ya wanandoa

Nafsi hii hujidhihirisha kwa mapenzi waliyonayo kwa mwanamke husika kwamba ni mazito mno hivyo yanawapelekea wafanye vitu vya hatari.

Tafiti nyingi za saikolojia zinaonesha wale wanaowauwa wake zao husikika wakisema; nilimpenda sana huyu mwanamke kaniumiza, ama yeye ndio alikuwa nuru ya maisha yangu, kaififisha, ama wengine husema ni kwa sababu ya mapenzi ndio maana nimefanya haya.

Japo utetezi wa mapenzi hapo juu haukubaliki kisaikolojia ila tafiti zinaonesha nafsi dhaifu inayoandamwa na msongo wa mawazo wa muda mrefu humfanya mtu kupanga tukio la mauaji kwa kuwa haoni kama kuna njia mbadala zaidi ya kifo.

Kwa ufafanuzi zaidi, msongo wa mawazo (stress) hutokana na hali ya mazingira yanayokuzunguka kutokuendana na matarajio ya ubongo wako. Mfano, ulitegemea mpenzi wako ni mwaminifu (hali ya ubongo wako) ila ukamkuta na mtu mwingine (hali ya mazingira) hapo msongo wa mawazo hutokea kwani hakuna usawa baina ya ubongo na mazingira yako.

Kwa mantiki hii ni kwamba, kuweza kuwa na nafsi imara ni lazima tujifunze namna ya kufanya hivyo kwa kuwaona wataalamu wa saikolojia na ushauri nasahi. Ama wakati mwingine, kuzungumza na watu wenye uzoefu na jambo ambalo unalipitia kama vile wabobezi katika maswala ya ndoa, biashara, elimu na mengineyo.

Mantiki hapa ni kwamba, wakati mwanadamu anapokuwa na tatizo lazima apate suluhisho, sasa kwenye suluhisho hapo maamuzi ndipo hutofautiana kwa wengine huona ni mwisho wa dunia na wengine huona mwanga mwisho wa safari.

Nini kifanyike katika hali kama hii? Nitaeleza kwa uchache japo suluhisho linaweza kuwa la aina mbalimbali, ila kitaalamu ningeshauri tufanye hili:

Ndoa ni taasisi kama ilivyo taasisi nyingine, inahitaji ujuzi, uvumilivu, utashi na uelewa. Misukosuko ya ndoa ni mikubwa kwa kuwa inahusisha hisia hivyo hata namna ya kuitatua inahitaji hisia imara hususani nafsi imara kuweza kuliendea tatizo kwa umakini.

Kitu kikubwa ambacho tunaweza kufanya kama wanandoa, tujenge tabia endapo matatizo yanakuwa makubwa tuende kuwaona wataalamu wa ushauri nasahi ama wanasaikolojia ambao wamefunzwa namna ya kufanya kazi na msongo wa hisia (Emotional Stress).

Wataalamu hawa hutoa maelekezo ambayo yanaweza kumjenga mtu na kufanya nafsi dhaifu kuwa imara.

Kwa wale ambao wanaona ni gharama kwenda kwa wataalamu wa saikolojia na ushauri nasahi waende kwa wanandoa wakongwe waliokaa kwenye ndoa kwa muda mrefu wanaweza kuzungumza na kuweza kumfanya mtu aone kuna mwanga mwisho wa safari badala ya kukata tamaa na kuchukua maamuzi magumu ya kumuua mwenzi wako.

Nihitimishe kwa kusema, saikolojia ya mwanadamu yeyote yule inahitaji matunzo na matibabu ya mara kwa mara kama vile mwili wa binadamu unavyokwenda kwa tabibu kupimwa na kupatiwa dawa. Wengi wetu hupuuza umuhimu huu na mwishowe tunatenda mambo mabaya bila kujua tu wagonjwa.

Continue Reading

Kimataifa

Uuzaji, umiliki wa silaha Rwanda usiwe sababu ya kuvuruga amani Afrika

Published

on

Hivi karibuni Rwanda imebadili Sheria yake ya mwaka 2009 iliyokuwa inakataza umiliki na uuzwaji wa silaha za moto. Sheria mpya ya silaha za moto nchini humo inaruhusu wananchi kumiliki silaha na pia watu binafsi kufungua maduka ya uuzwaji wa silaha za moto.

Sheria inaenda mbali zaidi na kuruhusu uwekezaji wa viwanda vya silaha za moto nchini Rwanda.

Serikali ya Rwanda imetetea uamuzi huo kwa kusema ni wakati sahihi kwa raia wake kumiliki silaha na kudai kuwa itasimaia vizuri sekta hiyo ili isilete madhara.

Hatua hii ya kubadili Sheria na kuruhusu watu binafsi kuwa na maduka ya kuuza silaha za moto na pia kuruhusu uwekezaji katika viwanda vya silaha za moto imeamsha hisia tofauti za wananchi na wachambuzi mbalimbali masuala ya usalama Afrika.

Nchi zetu za Afrika bado zinakabiliwa na changamoto lukuki ikiwamo usalama, vita vya wenyewe kwa wenyewe, ujambazi uliokithiri, ugaidi, fujo katika chaguzi na mambo mengine mengi.

Haya na mengine mengi yanaleta hofu endapo ubinafsishaji holela unafanyika katika silaha za moto. Hapa najaribu kufikiria matokeo ya mbele zaidi, kwani madhara yake yanaweza yasiwe sasa ila katika muda mrefu ujao tunaweza kuyaona kwa wingi.

Nieleze wasiwasi wangu katika uamuzi huo wa kubinafsisha sekta ya silaha za moto. Kwanza kabisa sio wananchi kumiliki silaha, hili halina tatizo sana kwani hata Tanzania tunafanya hivi lakini kupitia kwa taasisi za Serikali.

Wasiwasi mkubwa nilionao ni kubinafsisha silaha za moto kuuzwa katika masoko huria na wawekezaji kuwekeza katika sekta hiyo.

Najaribu kutafakari, Je, hitaji la wananchi lilikuwa silaha za moto kana kwamba kulikuwa na upungufu kiasi cha kuruhusu watu kuwekeza katika sekta hiyo?

Je, ajenda hii haina msukumo wowote kutoka kwa mabepari ambao biashara yao kubwa ni uuzaji wa silaha za moto na wanatafuta masoko mapya Afrika?

Duka la silaha za aina mbalimbali

Twakimu za Taasisi ya Utafiti ya Stockholm International Peace (SIPRI) za mwaka 2015 zinaonesha kuwa makampuni makubwa kumi bora ya utengenezaji wa silaha za moto duniani, nane yanatoka Marekani, moja Italia na lingine Umoja wa Ulaya.

Takwimu hizi pia zinaonesha nchi zinazouza silaha za moto kwa wingi duniani ni pamoja na Marekani, Urusi, China, Ufaransa, Ujerumani, Uingereza, Uhispania, Italia, Ukraine na Israeli.

Taarifa ya SIPRI ya mwaka 2012 zinaeleza kuwa nchi kumi bora zinazoagiza silaha kwa wingi duniani ni India, Saudi Arabia, Umoja wa Kiarabu, China, Australia, Aljeria, Uturuki, Iraq, Pakistani, Vietnam. Katika orodha hii, utaona nchi za Afika ni chache sana kwani nyingi huagiza silaha kwa kiwango kidogo na nyingine hufanya biashara kwa magendo.

Kwa takwimu hizo hapo juu, ni dhahiri sasa mabepari hawa wanatafuta mahala pa kuwekeza viwanda vyao vya silaha za moto na Afrika ni chaguo lao kwa wakati huu.

Hata hivyo, Hii inaweza kuwa fursa nzuri kwa Rwanda kwani watapata wawekezaji wengi katika sekta hii ila waathirika wa silaha hizi za moto ni majirani ambao inatupasa tukae chonjo sasa.

Marekani kama mfano duniani imekuwa muhanga mkubwa wa Sera na Sheria zake za ubinafsishaji wa silaha za moto ambapo upatikanaji wa silaha umekuwa rahisi kiasi kwamba maduka binafsi yanauza silaha hizo.

Tangu mwaka 2011, kumezuka matukio mengi ya watu kupigwa risasi katika shule na maeneo yenye mikusanyiko ya watu. Matukio haya nchini Marekani yanazidi kila mwaka na sasa wananchi wameanza kuipigia kelele sheria ya silaha za moto ibadilishwe.

Ugumu wa kubadili Sheria hizi nchini Marekani unatokana na ukweli kwamba ni biashara inayoingiza kipato kikubwa kwa makampuni ya nchi hiyo. Takwimu za SIPRI za mwaka 2012 zinakadiria kuwa mapato ya jumla ya makampuni 100 makubwa ya uuzaji wa silaha za moto yanafika Dola za Marekani 395 bilioni.

Kwa hakika hii ni biashara kubwa inayoweza kuipatia nchi mapato. Na sasa tunaweza kushuhudia Rwanda ikiwa moja ya nchi inayoweza kufaidika na mpango huu wa ubinafsishaji sekta ya silaha za moto.

Lakini fursa hiyo ya Rwanda kutengeneza silaha inapaswa kuangaliwa kwa jicho la tatu ili isiwe chanzo cha kuchochea machafuko katika nchi za Afrika, ikizingatiwa kuwa bado bara hilo halijatulia; ziko nchi kama Sudan ya Kusini, Somalia, Congo DRC, Jamhuri ya Kati, Burundi ambazo zinakumbwa na mizozo ya kisiasa.

Nchi hizo zinaweza kutumia silaha zinazouzwa Rwanda kuendeleza mapigano katika nchi zao. Katika hili serikali ya Rwanda inapaswa kuweka mfumo madhubuti wa kusimamia utengenezaji na uuzaji wa silaha hizo ili zisivurue amani ya Afrika.

Continue Reading

Siasa

Ubinafsishaji wa demokrasia unavyodidimiza maendeleo Afrika Mashariki

Published

on

Wagiriki wana tafsiri yao demokrasia kama ‘uongozi wa watu’. Na tafsiri ya kisasa inaelezeaza demokrasia zinasema ni mfumo wa serikali unaoongozwa na watu moja kwa moja ama kwa kutumia wawakilishi wanaotokana na wao wenyewe.

Tunashuhudia ubinafsishaji wa demokrasia katika bara la Afrika na hasa ukanda wa Afrika Mashariki. Wananchi wamekuwa mihuri ya watawala katika kupitisha maamuzi yao ili kutoa uhalali wa ubinafsishaji huu.

Tumeshuhudia Burundi, nchi mwanachama wa Afrika Mashariki ikitumia wananchi kuhalalisha ukomo wa uongozi kwa kupiga kura kubadilisha katiba kutoka miaka 5 hadi miaka 7 kwa muhula mmoja.

Hili limetokea baada ya Uganda nao kubadilisha katiba yao mwaka 2017 kuondoa ukomo wa umri kwa Rais wa kugombea wa miaka 75. Lakini kabla ya hapo mwaka 2005, mabadiliko ya katiba yalifanyika na kuondoa ukomo wa mihula ya uongozi yakimruhusu rais Yoweri Museveni kuendelea kugombea.

Mabadiliko mengine ya katiba yalifanyika Rwanda ambapo wananchi walipiga kura mwaka 2017 kumruhusu rais Paul Kagame kuhudumu mihula mingine miwili kila muhula ukiwa na miaka 7.

Sudan ya Kusini nako mambo sio shwari, kwani walipaswa kuwa na uchaguzi mwaka 2015 ambapo ungekuwa uchaguzi wao wa kwanza tangu kupata uhuru ila haukufanyika kutokana na mgogoro unaondelea. Bunge la nchi yao likafanya mabadiliko kwenye katiba yao ya mpito ya mwaka 2011 ili kuongeza muda wa uchaguzi mpaka mwaka 2018 mwezi wa saba.

Nchi wanachama pekee ambao ni Tanzania na Kenya bado zimekuwa imara zikiheshimu katiba zao na kuzingatia mihula ya uongozi. Ni jambo zuri kuona nchi hizi mbili bado ziko imara, lakini ni jambo la kuwa waangalifu kwani nchi hizi zinaweza kutumbukia katika mkumbo wa nchi zingine wanachama na kubadili katiba zao.

Hivi karibuni minong’ono ilianza nchini Tanzania kutoka kwa baadhi ya watu na wabunge waliotaka mabadiliko ya katiba yatakayoruhusu Rais kuhudumu kwa muda mrefu zaidi. Ila Rais John Magufuli alizima mjadala huo na kusema wazi hana nia ya kufanya hivyo kwani anaheshimu katiba ya nchi na hawezi kuivunja.

Niwakumbushe kuwa Tanzania sio mara ya kwanza kuwa na minong’ono ya kuongeza muda wa Rais kusalia madarakani. Katika kitabu cha Mwalimu Nyerere kijulikanacho kama “Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania” Mwalimu alieleza wazi ya kuwa kulikuwa na minong’ono kutoka kwa watu na wabunge ambao walitaka Rais Ali Hassan Mwinyi asalie madarakani kwa muhula mmoja zaidi. Mwalimu alikiri wazi kuwa alihuzunishwa na jambo hilo kisha alimwendea Rais Mwinyi ili aweze kufunga mjadala huo ili kuweza kuheshimu matakwa ya katiba.

Kwa nchi ambazo zimefanikiwa kuongeza ukomo wa uongozi wamefanya hivyo kwa kisingizio cha maslahi ya kisiasa ya baadhi ya watu ambao wana uchu wa madaraka. Ukweli unabaki  kuwa, wananchi wanatumika kupitisha ajenda za viongozi ambao wameamua kubinafsisha demokrasia kwa matakwa yao binafsi.

Ubinafsishaji huu wa demokrasia unadhihirisha maovu yake kwa kuongezeka kwa migogoro, ukosefu wa amani na uvunjifu wa haki za binadamu katika nchi zilizowageuka wananchi wao na kuishia kujinufaisha wao wenyewe.

Kwa kuzingatia ubinafsishaji huu wa demokrasia Afrika, baraza la Umoja wa Afrika liliazimia mwaka 2007, kuwa na Mkataba wa Afrika juu ya Demokrasia, Uchaguzi na Utawala kama unavyojulikana kwa kiingereza “The African Charter on Democracy, Elections and Governance”.

Mkataba huu unajumuisha jumla ya wananchama 54 wa Umoja wa Afrika ambao ulianza rasmi Februari 15, 2012. Kati ya wanachama hao 54, waliotia sahihi na Kuridhia mkataba huo ni wanachama 10 tu ikiwamo Rwanda kwa Afrika Mashariki.

Wanachama waliotia sahihi bila kuridhia ni 28 ikiwamo Kenya, Uganda na Burundi kwa Afrika Mashariki. Wanachama ambao hawajatia sahihi wala kuurudhia ni 16 ikiwamo Tanzania.

Mkataba huo umekuja kama suluhisho la miaka mingi la utawala mbovu hususani chaguzi zisizo huru na haki, uvunjifu wa haki za binadamu, ushiriki hafifu wa wananchi katika serikali zao, na mabadiliko ya serikali bila kufuata katiba.

Mkataba huo unalenga kuimarisha ahadi na utayari wa nchi wananchama wa Umoja wa Afrika unaotaka kuwe na thamani ya demokrasia, heshima kwa haki za binadamu, uongozi wa sheria, ukuu wa katiba na mfumo thabiti wa katiba katika mipangilio ya dola.

Haya yote yamelenga kuwapa nguvu nchi wanachama kuweza kuwa walezi kwa wengine endapo makubaliano haya yatavunjwa. Ila mpaka sasa ubinafsishaji wa demokrasia unaendelea licha ya mkataba huo kupitishwa mwaka 2012.

Nitoe rai kwa Waafrika wenzangu tupaze sauti kwa nchi zetu kutia sahihi na kuridhia mkataba huu ili tuweze kuimarisha demokrasia Afrika. Tukumbuke kuwa mkataba huu umetokana na sisi waafrika wenyenye sio ile aina ya mikataba ambayo inatokana na misukumo ya nchi za Magharibi ambayo mara nyingi inakuwa na ajenda binafsi.

Kwa kuhitimisha, Afrika ni yetu sote na sisi wananchi tuna jukumu la kuhakikisha tunaimarisha demokrasia yetu wenyewe kwa kuzingatia matakwa yetu kwa kuwakumbusha viongozi wetu kwamba tumewapa madaraka ya kusimamia hoja zetu na sio matakwa yao binafsi.

Continue Reading

Muhimu Kusoma

Copyright © 2020 FikraPevu.com