Connect with us

Afya

Likizo ya uzazi kwa wanaume na mgongano wa sheria, mila na wanasiasa

Published

on

Jukumu la kumlea na kumtunza mtoto ni la wazazi wote wawili yaani baba na mama. Matunzo hayo yanaanza mama anapokuwa mjamzito mpaka siku ya kujifungua.

Katika siku za mwanzo za kuzaliwa mtoto, inashauriwa wawazi wote wawili kuwa karibu na mtoto ili kujenga msingi mahusiano mazuri ya upendo kwa kichanga. Ili jambo hilo lifanikiwe wazazi watalazimika kuacha majukumu mengine  na kutumia  muda mwingi kukaa na mtoto.

Dhana hiyo imeleta mjadala na mitazamo tofauti katika jamii hasa kwa wanaume ambao ni wafanyakazi wa kuajiriwa kwamba wanapaswa kuacha majukumu yao kwa muda na kuungana na mtoto. Hapo ndipo linakuja suala la kupata likizo ya uzazi kwa wanaume (paternity leave).

Kulingana na Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004 ya Tanzania inatoa likizo ya siku tatu kwa mwanaume na miezi mitatu kwa mwanamke kwa ajili ya uzazi hasa mtoto akizaliwa.

Licha ya sheria mbalimbali duniani kutoa mwongozo wa likizo ya uzazi kwa wanaume bado kumekuwepo na mkanganyiko wa mawazo kuhusu dhana hiyo.

Wabunge nchini Nigeria wamekataa kupitisha muswada wa likizo ya hiari ya uzazi kwa wafanyakazi wa  sekta ya umma na binafsi. Mswada huo ulioshindwa kusomwa kwa mara ya pili bungeni hivi karibuni.

Ili muswada uwe sheria nchini Nigeria, unatakiwa usomwe mara ya kwanza na ya pili, kisha utapitiwa na kamati ya Bunge na kusomwa tena kwa mara ya tatu kabla rais hajatia saini.

Kukataliwa kwa muswada huo kulitokana na sababu za asili na kitamaduni. Wakazi wengi wa Nigeria wanajihusisha na ndoa za wake wengi. Baadhi ya wabunge waliopinga muswada huo wanaamini kuwa mwanaume mwenye wake wengi atalazimika kuchukua likizo nyingi kwa mwaka ili kuwahudumia wake zake wakati wamejifungua.

Uhusiano wa baba na mtoto huamarika ikiwa atapata muda wa kukaa naye

Siyo mara ya kwanza kwa wabunge hao kuzuia miswada inayozingatia usawa wa kijinsia. Machi 2016, walizuia pia muswada ambao ulidhamiria kuondoa ubaguzi  wa kijinsia kwenye siasa, elimu na ajira.

Mtazamo wa wabunge wa Nigeria hautofautiani sana na raia wa Marekani ambao wanaona mwanaume hapaswi kupewa kabisa likizo ya uzazi na wengine wanaenda mbali zaidi na kutaka hata mwanamke asipate kabisa likizo hiyo.

Kulingana na utafiti uliofanywa na taasisi ya Pew mwaka 2017 ulibaini kuwa mtu 1 kati ya 7 (asilimia 15) wa Marekani alisema akina baba wasipewe likizo ya uzazi kabisa. Na asilimia 3 ya raia wa Marekani wanafikiri kuwa hata mama aliyejifungua hapaswi kupewa kabisa likizo ya uzazi na malipo.

Mtazamo wa likizo ya uzazi kwa wanaume, pia umeganyika kulingana na vyama vya siasa. Utafiti huo unaeleza kuwa wanachama wa chama cha ‘Republican’ ambao wana mawazo huru wanasema likizo hiyo siyo lazima. Mwanachama 1 kati ya 4 (26%) wa Republican ambaye ni Mhafidhina anafikiri mwanaume hapaswi kabisa kuondoka kazini kwa ajili ya masuala ya uzazi.

Lakini asilimia 13 tu ya wanachama wenye msimamo wa kawaida wanakubaliana na dhana hiyo huku asilimia 91 ya wanachama wa chama cha ‘Democrat’ hawakubaliani na na wanaume kunyimwa likizo ya uzazi.

Pia imebainika kuwa upinzani wa likizo hiyo unakuwa mkubwa kadiri mtu anavyozidi kuwa mtu mzima. Mathalani Wamerikani wenye umri wa miaka 65 na kuendelea  ambao kwa asilimia 36 walisema sio lazima kupewa likizo hiyo. Lakini  wanaume waliopata watoto wachanga wanaona ni muhimu kupata likizo ili wajumuike na familia zao kuimarisha upendo.

 

Tanzania na Ulaya wasimama kidete

Wakati raia wa Nigeria na Marekani kwa sehemu wakipinga likizo ya uzazi kwa wanaume, wananchi wa Ulaya na Tanzania wanakubaliana na kuwepo kwa likizo hasa katika mtazamo wa usawa wa kijinsia.

Aliyewahi kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango ya Maendeleo ya Zanzibar, Omar Yussuf Mzee amewahi kusema kuwa likizo ya uzazi kwa akina baba pindi wake zao wanapojifungua inasaidia ulezi wa wazazi wawili baina ya mama na baba.

“Hatua hii itasaidia kuondokana na ile dhana kwamba suala la afya ya uzazi linamhusu mama pekee. Lakini hatua hii inategemewa iwe chachu ya kuwashirikisha akina baba katika harakati  zote za huduma ya afya ya uzazi na mtoto,” alinukuliwa Waziri Mzee.

Kwa mujibu wa jalida la Business Insider, linaeleza kuwa nchi ya Sweden ndio ina sera nzuri ya likizo ya uzazi ambapo inatoa likizo ya siku 480 kwa wazazi waliopata mtoto kwa mara ya kwanza inayoambatana na malipo ya asilimia 80 ya mshahara wa kawaida.

Wanaume wametengewa siku 90 (miezi 3) likizo ya malipo ya uzazi. Wanaopewa kipaombele ni akina baba ambao wanapata mtoto kwa mara ya kwanza. Sweden wanaamini kuwa likizo hiyo inaimarisha uhusiano kati ya baba na mtoto wakati ambao wazazi wote wawili wameelekeza macho yao kwa kumlea.

Nchini Norway, akina baba wanapata likizo ya wiki 0 hadi 10, huku wanaume wa Finland wanapewa wiki 8 lakini mtoto akifikisha miaka 3 baba anaweza kuchukua likizo ya malezi. Akina baba wa Slovenia nao wana siku 90 za likizo ambazo huambatana  na malipo ya asilimia 100 kwa siku 15 za mwanzo. Lakini likizo inaweza kuanza hata kabla mama hajajifungua.

Nchi za Ulaya zimefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuimarisha usawa wa kijinsia kwenye sekta ya afya ya mama na mtoto.

Licha ya mitazamo tofauti ya likizo ya uzazi kwa wanaume, tafiti nyingi zimethibitisha wazi kuwa likizo hiyo ni njia nzuri ya kurejesha na kuimarisha upendo na muunganiko wa familia.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Afya

Watumishi wa afya 200 kupatiwa mafunzo ya utoaji dawa ya usingizi kuokoa maisha wajawazito

Published

on

Kufuatia upungufu wa wataalamu wa dawa za usingizi (anaesthesia), serikali itatoa mafunzo ya dawa za usingizi kwa watumishi wa afya 200 katika vituo vya afya vya upasuaji wa dharura kwa akina mama wajawazito.

Hatua hiyo inakuja ikiwa imepita miezi 6 baada ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kutangaza kuanza kutoa shahada ya dawa ya usingizi (Bsc. Anaesthesia Nursing).

Katika taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano serikalini cha Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, inaeleza kuwa mafunzo hayo yatatolewa sambamba na uboreshaji wa huduma ya upasuaji wa dharura kwa wajawazito ili kuokoa maisha ya wanawake na watoto ambao hufariki kwa kosa huduma muhimu za uzazi kwenye vituo vya afya.

“Mkakati wa kuhakikisha huduma za afya kwa akina mama wajawazito zinakuwa salama na uhakika kwa kuandaa rasilimali watu, miundombinu ya majengo na vifaa vitakavyowezesha huduma hizi ikiwemo upasuaji wa dharura kwa akina mama wajawazito wakati wa kujifungua,” imeeleza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya, vifo 556 vitokanavyo na uzazi kwa kila viumbe hai 100,000 huripotiwa kila mwaka katika maeneo mbalimbali nchini. Maana yake ni kwamba watoto na wajawazito hufariki hasa wakati wa mama akijifungua.

Aidha, serikali itaboresha vituo vya afya 288 vya serikali vilivyopo nchini ili kuviwezesha kutoa huduma ya dharura ya upasuaji kwa wajawazito ambapo waaguzi katika vituo hivyo watapatiwa mafunzo ya dawa za usingizi ili kuokoa maisha ya akina mama na watoto wachanga.

Utekelezaji wa mafunzo hayo ni matokeo ya ushirikiano wa Wizara ya Afya na Mfuko wa Pamoja wa Afya ambapo zaidi ya sh1,079 bilioni zimepatikana kufakisha mafunzo hayo ya dawa ya usingizi kwa wauguzi na matabibu waliopo kwenye vtuo vya afya nchini.

“Fedha hizo zitasomesha watumishi wapatao 200, kati ya watumishi hao 100 watapata mafunzo yao katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na MOI, watumishi 50 watafanya mafunzo katika hospitali ya KCMC, na 50 watafanya mafunzo hayo kwenye hospitali ya Bugando,” imefafanua taarifa ya wizara.

Lengo la serikali ni kuhakikisha ifikapo 2019 na kabla ya 2020 vituo vyote vya afya vinavyomilikiwa na serikali vinakuwa na watumishi maalum wa kutoa huduma ya dawa ya usingizi kwaajili ya wapasuaji wasiopungua wawili kwa kila kituo.

Mafunzo hayo ya mwaka mmoja ni mpito wakati serikali ikiendelea kukamilisha taratibu za kurasimisha utoaji wa shahada ya kwanza ya kutoa dawa ya usingizi katika Chuo cha MUHAS katka mwaka huu wa 2018/2019.

Hali halisi ya huduma ya dawa za usingizi nchini
Takwimu za wizara ya Afya zinaonyesha kuwa kuna upungufu mkubwa wa madaktari wenye utaalamu wa kutoa dawa ya usingizi hasa wakati wa huduma ya upasuaji ambapo kwa sasa waliopo ni asilimia 1.2 tu ya mahitaji yote.

Ili kuweza kukidhi mahitaji yote ya huduma hiyo wanahitajika madaktari 2000, lakini waliopo sasa ni madaktari 30 pekee.

Kufuatia changamoto hiyo Januari 31, mwaka huu wadau mbalimbali wa afya na elimu walikutana na kujadili namna ya kuondoa changamoto hiyo na kupendekeza mtaala utakaotumika kufundishia kozi ya Aesthesia kabla ya kuupeleka kwa Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU).

” Ni kweli kumekuwepo kwa changamoto hiyo ya watalaamu wa dawa hizo lakini sasa mpango huu ukikamilika maana yake tutaongeza idadi ya madaktari kamili maana hawa waliopo wengi ni wale ambao wamesoma kozi kwa mwaka mmoja au miwili.

” Mafunzo yakianza kutolewa hapa chuoni Muhimbili wataweza kuchukua wanafunzi 200, Bugando 50 na KCMC 50 jambo ambalo litaongeza idadi kubwa ya watalaamu ili kuweza kufikia lengo letu la kuwa na wataalamu 2000 nchi nzima,” alinukuliwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Mpoki Ulisubisya.

Continue Reading

Afya

Vyakula hivi vitakulinda dhidi ya athari za kiafya za uchafuzi wa hewa

Published

on

Tunaishi katika ulimwengu unaokabiliwa na athari kubwa za mabadiliko ya hali ya hewa. Moja ya athari hizo ni kuongezeka kwa joto na kupungua kwa mvua katika maeneo mbalimbali. Athari hizi zinagusa moja kwa moja afya ya binadamu.

Ripoti ya mabadiliko ya hali ya hewa ya mwaka 2017 imeonesha kuwa kuongezeka kwa joto kunaathiri afya ya binadamu kwa kiasi kikubwa. Ripoti hiyo inatoka kundi la vyuo mbalimbali na mashirika tofauti ya Umoja wa Mataifa inasema watu wengi wanaathirika na joto pamoja na mlo hafifu sambamba na kusambaa kwa magonjwa.

Moja ya kisababishi cha mabadiliko ya hali ya hewa ni uchafuzi wa anga. Uchafuzi wa anga ni kuchanganyika kwa hewa asili katika anga na vitu kama vile moshi, majivu, gesi za kemikali katika hali na kiwango ambacho huathiri sifa ya hewa na kusababisha madhara kwa binadamu na viumbe vingine.

Baadhi ya vitu na vitendo huathiri vibaya anga letu. Baadhi ya vitu hivyo ni kama gesi na moshi unaotoka kwenye viwanda, moshi kutoka kwenye magari, marashi, dawa ya kuuwa wadudu shambani na kadhalika.

Lakini umewahi kujiuliza kuwa aina ya chakula unachokula kinaweza kukusaidia kukabiliana na athari za kiafya zinazotokana na uchafuzi wa hewa?

Wanasayansi katika utafiti wao uliotolewa hivi karibuni, wanaeleza ulaji wa chakula cha Mediterania ( Mediterranean diet) chenye matunda mengi, mbogamboga, nafaka isiyokobolewa, samaki, maharage jamii ya soya, mafuta ya mizeituni na mayai yanaweza kuwalinda watu dhidi ya athari za afya zinazotokana na uchafuzi wa hewa.

Wanasayansi hao kutoka Shule kuu ya Udaktari ya NYU ya Marekani, walichambua data za watu takribani 550,000 wenye wastani wa umri wa miaka 62 kwa miaka zaidi ya 17 ambapo waliwapanga watu hao kwenye makundi kulingana na ulaji wao unaoendana na chakula cha Mediterania na kulinganisha na muda waliokaa kwenye hewa iliyochafuliwa.

Walibaini kuwa watu ambao walizingatia kula vyakula vilivyotajwa hapo juu walikuwa na uwezekano mkubwa wa kuepuka magonjwa na vifo vinavyotokana na uchafuzi wa hali ya hewa. Magonjwa hayo ni yale ya mfumo wa upumuaji, moyo na kansa.

                                   Vyakula  jamii ya Mediterania

Vyakula hivyo jamii ya Mediterania vina uwezo mkubwa wa kukabiliana na vimelea vya maambukizi ya magonjwa kwa mtu ambaye atazingatia kwa usahihi kutumia katika maisha yake.

Uchafuzi wa hewa unasababisha athari mbaya za kiafya kupitia hewa ukaa na mlo wa Mediterania una virutubisho muhimu kupambana na vimelea vya magonjwa,” anasema Mwandishi Mtafiti wa utafiti huo, Chris Lim wa Chuo cha NYU.

Lim anasema vyakula vya aina nyingine vinaweza kusaidia kukabiliana na athari hiyo. “Nilipoangalia kila mchanganyiko wa chakula cha Mediterania, kina matunda, mbogamboga na mafuta yanayoweza kupambana na athari za hewa chafu,” anasema.

Utafiti kuhusu ulaji kama unaweza kuzuia athari za kiafya za uchafuzi wa hewa bado haujahakikiwa na kukubalika kisayansi. Lakini utafiti huo sio wa kwanza kutafuta uhusiano wa mlo na athari za kiafya za uchafuzi wa hali ya hewa.

Wakala wa Uhifadhi wa Mazingira wa Marekani (U.S. Environmental Protection Agency (EPA)) unatafiti kama mlo unaweza kumlinda mtu dhidi ya athari za uchafuzi wa mazingira. Pia wanatafiti ili kujiridhisha kama virutubisho hivyo vinaweza kutumika badala ya dawa za kitabibu na kwa kiasi gani mtu anatakiwa apate virutubisho hivyo kumhakikishia usalama dhidi ya uchafuzi huo.

Hata hivyo, bado watu wanashauriwa kutumia zaidi matunda na mbogamboga kwenye milo yao ya kila siku ili kupata faida mbalimbali za kiafya.

Continue Reading

Afya

Ulaji mbaya wa chakula watajwa kusababisha kansa ya matiti kwa wanawake

Published

on

Thamani ya maisha haiko kwenye muonekano wa mtu na vitu vinavyomzunguka bali kwenye chakula anachokula kila siku ili kuwa na afya njema. Lakini umewahi kujiuliza, chakula kinawezaje kupunguza uwezekano wa kufa kutokana na magonjwa ikiwemo kansa?

Utafiti mpya uliofanyika huko Marekani umebaini kuwa kwa sehemu mlo kamili unaweza kupunguza hatari ya kufa kwa kansa.

Mtafiti Dk. Rowan Chlebowski wa Kituo cha Taifa cha Uuguzi cha City of Hope na wenzake walichambua takwimu za wanawake 48,000 waliosajiliwa katika mpango wa Afya ya Mwanamke unaoratibiwa katika vituo 40 nchini Marekani.

Awali wanawake wote walipata vipimo na hakuna aliyegundulika kuwa na kansa ya matiti lakini 20,000 kati yao walishauriwa kubadilisha mlo na kupunguza ulaji wa mafuta kwa asilimia 20 katika milo yao ya kila siku.

Pia waliambiwa wale zaidi matunda, mbogamboga na nafaka zisizokobolewa. Wanawake wengine hawakupewa maelekezo yoyote ya kuzingatia mlo kamili lakini walifundishwa kuhusu lishe nzuri na mlo wenye afya.

Baada ya miaka nane ya kuwafuatilia wanawake hao, watafiti hao waliangalia idadi ya kansa ambazo wanawake hao walitibiwa na zile ambazo zilisababisha vifo. Walibaini kuwa wanawake ambao walitumia kiasi kidogo cha mafuta walikuwa na hatari ndogo ya kufa kwa kansa ya matiti kwa asilimia 22, ukilinganisha na wanawake wengine.

Pia wanawake hao walipunguza kwa asilimia 24 hatari ya kufa kwa kansa zingine ikiwemo kwa 38%  magonjwa ya moyo ikilinganishwa na wanawake wa kundi ambalo walipata elimu ya mlo.

“Tunachokiona ni matokeo halisi,” anasema Dk. Chlebowski. Tafiti za awali ziliangalia madhara kabla ya uchunguzi wa kansa, lakini utafiti huu ulichambua kwa kiasi gani mlo unaweza kumuathiri mtu baada ya uchunguzi.

“Tulichobaini ni kuwa ushauri wa mlo baada ya uchunguzi wa kansa ya matiti ulikuwa muhimu kuliko kabla ya uchunguzi.”

                        Ulaji wa matunda na mboga unasaidia kupunguza hatari ya kupata kansa

Hata hivyo, utafiti huo ulibaini kuwa wanawake ambao wanazingatia kutumia kiasi kidogo cha mafuta katika maisha yao wana nafasi kubwa ya kuepuka kansa ya matiti.

Kutokana na idadi ya watu walioshirikishwa kwenye utafiti huo, Dkt. Chlebowski anasema wazo la kuhusisha mlo katika programu ya matibabu lilikuwa ni muhimu ili kupata matokeo chanya katika kukabiliana na kansa ya matiti kwa wanawake.

Watafiti hao wanaendelea na uchunguzi ili kufahamu kama ulaji wa chakula unaweza kuwa sehemu ya matibabu ya kansa ya matiti. “Inahamasisha kwasababu tunajaribu kuziba pengo kati ya mtindo wa maisha na mchakato wa kibaiolojia uliopo nyuma ya ugonjwa huo.”

 

Kansa ya matiti

Saratani ya matiti ni ugonjwa ambao huwapata wanawake na unatokana na athari za chembe ndogo ama seli kwenye matiti na matokeo yake ni kwamba hubadili mfumo wa kawaida wa kukua na kuongezeka.

Mabadiliko haya huanza polepole na yanaweza yakachukua muda mrefu hadi mtu kuweza kujua kama ana matatizo hayo. Ikiwa katika hatua hizo za mwanzo kwa kawaida huwa hakuna maumivu jambo hilo ni moja ya mambo ambayo huchangia baadhi ya wagonjwa kubaini tatizo hilo wakati tayari limekomaa.

Ni kutokana na sababu hizo, wanawake hutakiwa kuchunguza afya zao mara kwa mara kwasababu ugonjwa huweza kutibiwa kirahisi iwapo utabainika mapema.

Miongoni mwa dalili za saratani ya matiti ni uvimbe kwenye matiti ama makwapani. Titi kubadilika kiumbo, titi kutoa majimaji yaliyochanganyika na damu ama chuchu kuingia ndani.

Zipo aina mbalimbali za tiba na mojawapo ni upasuaji. Upasuaji huu kwa kawaida hufanywa katika hatua za mwanzo. Njia nyingine ni tiba ya mionzi au kupewa dawa. Jambo la kukumbukwa ni kwamba ugonjwa huu unaweza kusababisha kifo iwapo hautabainika mapema na kupatiwa tiba mwafaka.

Njia ambayo mtu aweza kujilinda asiathirike na saratani hii ya matiti ni kujichunguza mara kwa mara ili kubaini mapema na kupatiwa dawa.

Mwanamke anapaswa kuchunguzwa mara moja kwa mwaka ili kuona kama ameathirika na ugonjwa huo au la.

Continue Reading

Muhimu Kusoma

Copyright © 2020 FikraPevu.com