Connect with us

Afya

Maambukizi ya UKIMWI yanapogeuka janga kwa wakulima Tanzania

Published

on

Kilimo ni sekta ya uzalishaji ambayo huchangia kukuza pato na kuimarisha uchumi la taifa. Tanzania ikiwa ni nchi inayotegemea kilimo kama uti wa mgongo wa uchumi wake, mipango na mikakati mbalimbali imetekelezwa na serikali ikishirikisha  wadau wa maendeleo kuboresha kilimo ili kiwe cha manufaa.

 Changamoto iliyopo sasa ni kupata teknolojia na nguvukazi ya kuendeleza rasilimali za nchi na kutengeneza mazingira mazuri ya kukuza kilimo nchini.  Nguvu kazi ya kilimo kwa sehemu inaathiriwa ugonjwa wa UKIMWI ambao haujapata dawa wala kinga. Idadi kubwa wanaoathirika na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI ni vijana na wanawake ambapo hali hiyo huathiri ukuaji wa sekta ya kilimo nchini   

Kulingana na Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya Ukimwi Tanzania (THIS) ya mwaka 2016/2017  unaonyesha vijana wenye umri wa miaka 15-24 wanapata maambuki ya ugonjwa huo kwa asilimia 1.4, kwa wanawake wenye umri wa miaka 15 hadi 64 maambukizi hayo yako juu kwa asilimia 6.5.

Kutokana na maambukizi hayo mapya, uwezekano wa nguvu kazi kwenye ya kilimo ikapungua hasa kwa wanawake ambao wanachangaia asilimia 43 ya nguvu kazi katika sekta hiyo.

 

Maambukizi ya Viruzi vya UKIMWI yanavyoathiri kilimo

Utafiti uliofanywa na Taasisi ya  Sayansi ya Kijamii ya Afrika Mashariki na Kusini (OSSREA) mwaka 2012 unaeleza  maambukizi ya VVU katika mikoa ya Mbeya, Lindi, Kigoma, Morogoro, Tabora na Kagera yamechangia kwa sehemu kubwa kurudisha nyuma maendeleo ya kilimo Tanzania.

Prof. Honest Ngowi ambaye alishiriki katikia utafiti huo anasema matokeo makuu yanaonyesha kwamba janga la VVU/UKIMWI linaathiri sekta ya kilimo katika mikoa iliyochunguzwa kwa namna mbalimbali, “ Namna mojawapo ni upotevu wa nguvukazi mashuhuli, zalishi na yenye nguvu moja kwa moja  au namna isiyo ya moja kwa moja ambayo hutokea mda mfupi na mrefu”.

Anasemaa kuwa nguvukazi inapotea kwa njia ya maradhi na hatimaye vifo; muda unaotumika katika kutoa huduma na msaada na kuhudhuria misiba. Pia watu wanaokimbia makwao kutokana na unyanyapaa na ubaguzi na kuepuka kuwahudumia wagonjwa, yatima na wajane

Utafiti huo uliolenga kutafuta njia ya kukuza nguvu kazi ya taifa kwenye kilimo unaeleza kuwa  athari nyingine ni mazao pungufu kutokana kupungua kwa eneo linalolimwa na mifugo. Pamoja na mambo mengine, ukosefu wa rasilimali watu, fedha na halisi za kutosha kutumia ardhi iliyopo kwa ajili ya kilimo kwa sababu ardhi hutumiwa zaidi  kwa mazishi kwa kuwa idadi ya vifo inaongezeka kila mwaka.

Kupungua kwa mifugo ni matokeo ya wananchi kuuza mazao ili kulipia gharama za matibabu, matunzo na msaada kwa ndugu walio na maambukizi ya VVU au ugonjwa wa UKIMWI. Hali hii hupunguza uzalishaji hasa katika jamiii za wafugaji ambao hutegemea machungo kwa kutembea umbali mrefu kutafuta marisho na maji kwa ajili ya mifugo.

 

Ukataji wa Miti
Miongoni mwa athari za mda mrefu ni mabadiliko ya hali ya hewa na mazingira. Kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya majeneza yaliyotengenezwa kwa miti, miti mingi zaidi bado inakatwa kutoa malighafi kwa utengenezaji wa majeneza.

Utafiti huo unabainisha kuwa athari za mda mrefu na haziwezi kuonekana mapema lakini hali hii ikiendelea bila kuthibitiwa mapema kwa namna nzuri inaweza kusababisha uharibifu wa mazingira ambao kwa upande wake utaathiri mazao katika sekta ya kilimo kwa sababu kilimo cha Tanzania kinategemea zaidi mvua ambayo inaathiriwa na ukataji wa miti na maendeleo ya viwanda duniani.

 

Njia Mahususi kuongeza tija
Prof.  Ngowi anaendelea kusema njia mahususi zinahitajika kupunguza athari hasi za VVU na UKIMWI katika sekta ya kilimo ni kupunguza athari ya muda unaotumiwa na nguvukazi ya kilimo kwenye masuala yanayohusiana na UKIMWI.  badala ya kutumia muda huo kwenye kilimo, kuna haja ya kuwa na watu wenye ujuzi maalumu wanaotoa huduma ambazo zinatolewa na wakulima wadogowadogo.

“Kwa mfano, watoa huduma za matunzo wenye ujuzi maalumu walioajiriwa majumbani wanapaswa kuchukua nafasi ya wakulima wanaotoa huduma kwa msingi wa kujitolea’, ameshauri.

Anapendekezwa kwamba kadri inavyowezekana shughuli zinazolenga kushughulikia masuala mbalimbali ya VVU  zinapaswa kutekelezwa wakati zinapokuwa  athari hasi ndogo kabisa kwenye sekta ya kilimo, kwa mfano, katika njia muhimu za shughuli za UKIMWI kama vile semina na maonyesho ya kuigiza zinapaswa kuepukwa kadri inavyowezekana.

Watu wanashauriwa kuzika maiti kwenye ardhi ya uzalishaji mdogo wa mazao  na kuepuka kutumia nafasi kubwa kupita kiasi cha makaburi. Lakini kutokana na utakatifu wa suala lenyewe la kuzika wafu katika jamii nyingi za Tanzania, inatambuliwa wazi kwamba katika kuzika mwili kinachofanyika kwanza ni kuipa heshima kubwa ikiwa ni pamoja na kuzika katika ardhi nzuri ya kilimo katika uwanja wa kaya kama inavyotumiwa zaidi na wakazi wa Kilimanjaro na Bukoba.

Anaeleza kuwa kiasi cha nguvukazi kinachaoathiriwa na janga hili kinapaswa kidhibitiwe kuongeza juhudi za kusambaza dawa za kurefusha maisha kwa waathirika ili kupunguza athari katika sekta ya kilimo na kupata watu ambao watanufaika na uzalishaji wa mazao.
 

Athari za Kisaikolojia
Imegundulika kuwa watu walio na maambukizi ya VVU pia hupata athari za kisaikolojia na hivyo kushindwa kufanya shughuli nyingine za uzalishaji. Juhudi za wataalamu wa kutoa ushauri na nasaha zinapaswa kuongezwa ili kuwaelimisha watu kuwa  UKIMWI sio mwisho wa maisha na mtu anaweza kuendelea na shughuli za kilimo ambacho kitamuingizia kipato na kuimarisha afya yake.

Wakati wote tumekuwa tukisikia viongozi na wadau wa afya wakitaja athari hasi za Ukimwi lakini upande wa pili kuna athari chanya ambazo zinahitaji ulinganifu ili kuleta matokeo yaliyo na tija katika maendeleo ya taifa.

“Athari chanya zinaweza kutokea kwa njia ya uwekezaji wa mapato yanayotokana na sekta ya kilimo. Katika muktadha
wa mambo kujizidisha, sehemu ya mapato kutokana na ushiriki katika shughuli za VVU na UKIMWI, kama zilivyo aina nyingine za mapato zinatumiwa katika kununua mazao mbalimbali ya kilimo hasa chakula kutegemea muelekeo alionao mtu. Wanaopata mapato kwa njia hii huwa soko kwa wale wanaozalisha katika sekta ya kilimo na hivyo kuchangia ukuaji wa sekta hii”, anaeleza Prof. Ngowi katika utafiti huo.

Pia athari chanya za moja kwa moja huwa kitega uchumi katika uzalishaji wa mazao ya chakula yanayohitajika kama lishe maalumu kwa waathirika wa VVU. Zinaweza kuwa kitega uchumi kwa malengo ya kibiashara katika kilimo cha mimea inayoweza ikawa na ubora wa lishe au dawa katika muktadha wa tiba ya UKIMWI.

 Nguvu ya pamoja baina ya wadua wote wa kilimo na masuala ya jamii ili kuwa na takwimu za kutosha katika kupima ukuaji wa kilimo nchini kwa kuwa athari za Ukimwi huwakumba wakulima ambao idadi yao ni kubwa katika nchi na wanategemewa kuzalisha mazao kwa ajili ya viwanda, chakula na matumizi mengine.

Watunga sera hawana budi kuitazama sekta ya kilimo kwa mtazamo mpana ili kukabiliana na changamoto za janga la UKIMWI ambazo zinaligharimu taifa rasilimali nyingi. Kazi hii sio ya watunga sera pekee bali ni ya kila mwananchi kutazama
mabadiliko yaliyoletwa na janga hili katika kilimo na kuchukua hatua stahiki.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Afya

Watumishi wa afya 200 kupatiwa mafunzo ya utoaji dawa ya usingizi kuokoa maisha wajawazito

Published

on

Kufuatia upungufu wa wataalamu wa dawa za usingizi (anaesthesia), serikali itatoa mafunzo ya dawa za usingizi kwa watumishi wa afya 200 katika vituo vya afya vya upasuaji wa dharura kwa akina mama wajawazito.

Hatua hiyo inakuja ikiwa imepita miezi 6 baada ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kutangaza kuanza kutoa shahada ya dawa ya usingizi (Bsc. Anaesthesia Nursing).

Katika taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano serikalini cha Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, inaeleza kuwa mafunzo hayo yatatolewa sambamba na uboreshaji wa huduma ya upasuaji wa dharura kwa wajawazito ili kuokoa maisha ya wanawake na watoto ambao hufariki kwa kosa huduma muhimu za uzazi kwenye vituo vya afya.

“Mkakati wa kuhakikisha huduma za afya kwa akina mama wajawazito zinakuwa salama na uhakika kwa kuandaa rasilimali watu, miundombinu ya majengo na vifaa vitakavyowezesha huduma hizi ikiwemo upasuaji wa dharura kwa akina mama wajawazito wakati wa kujifungua,” imeeleza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya, vifo 556 vitokanavyo na uzazi kwa kila viumbe hai 100,000 huripotiwa kila mwaka katika maeneo mbalimbali nchini. Maana yake ni kwamba watoto na wajawazito hufariki hasa wakati wa mama akijifungua.

Aidha, serikali itaboresha vituo vya afya 288 vya serikali vilivyopo nchini ili kuviwezesha kutoa huduma ya dharura ya upasuaji kwa wajawazito ambapo waaguzi katika vituo hivyo watapatiwa mafunzo ya dawa za usingizi ili kuokoa maisha ya akina mama na watoto wachanga.

Utekelezaji wa mafunzo hayo ni matokeo ya ushirikiano wa Wizara ya Afya na Mfuko wa Pamoja wa Afya ambapo zaidi ya sh1,079 bilioni zimepatikana kufakisha mafunzo hayo ya dawa ya usingizi kwa wauguzi na matabibu waliopo kwenye vtuo vya afya nchini.

“Fedha hizo zitasomesha watumishi wapatao 200, kati ya watumishi hao 100 watapata mafunzo yao katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na MOI, watumishi 50 watafanya mafunzo katika hospitali ya KCMC, na 50 watafanya mafunzo hayo kwenye hospitali ya Bugando,” imefafanua taarifa ya wizara.

Lengo la serikali ni kuhakikisha ifikapo 2019 na kabla ya 2020 vituo vyote vya afya vinavyomilikiwa na serikali vinakuwa na watumishi maalum wa kutoa huduma ya dawa ya usingizi kwaajili ya wapasuaji wasiopungua wawili kwa kila kituo.

Mafunzo hayo ya mwaka mmoja ni mpito wakati serikali ikiendelea kukamilisha taratibu za kurasimisha utoaji wa shahada ya kwanza ya kutoa dawa ya usingizi katika Chuo cha MUHAS katka mwaka huu wa 2018/2019.

Hali halisi ya huduma ya dawa za usingizi nchini
Takwimu za wizara ya Afya zinaonyesha kuwa kuna upungufu mkubwa wa madaktari wenye utaalamu wa kutoa dawa ya usingizi hasa wakati wa huduma ya upasuaji ambapo kwa sasa waliopo ni asilimia 1.2 tu ya mahitaji yote.

Ili kuweza kukidhi mahitaji yote ya huduma hiyo wanahitajika madaktari 2000, lakini waliopo sasa ni madaktari 30 pekee.

Kufuatia changamoto hiyo Januari 31, mwaka huu wadau mbalimbali wa afya na elimu walikutana na kujadili namna ya kuondoa changamoto hiyo na kupendekeza mtaala utakaotumika kufundishia kozi ya Aesthesia kabla ya kuupeleka kwa Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU).

” Ni kweli kumekuwepo kwa changamoto hiyo ya watalaamu wa dawa hizo lakini sasa mpango huu ukikamilika maana yake tutaongeza idadi ya madaktari kamili maana hawa waliopo wengi ni wale ambao wamesoma kozi kwa mwaka mmoja au miwili.

” Mafunzo yakianza kutolewa hapa chuoni Muhimbili wataweza kuchukua wanafunzi 200, Bugando 50 na KCMC 50 jambo ambalo litaongeza idadi kubwa ya watalaamu ili kuweza kufikia lengo letu la kuwa na wataalamu 2000 nchi nzima,” alinukuliwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Mpoki Ulisubisya.

Continue Reading

Afya

Vyakula hivi vitakulinda dhidi ya athari za kiafya za uchafuzi wa hewa

Published

on

Tunaishi katika ulimwengu unaokabiliwa na athari kubwa za mabadiliko ya hali ya hewa. Moja ya athari hizo ni kuongezeka kwa joto na kupungua kwa mvua katika maeneo mbalimbali. Athari hizi zinagusa moja kwa moja afya ya binadamu.

Ripoti ya mabadiliko ya hali ya hewa ya mwaka 2017 imeonesha kuwa kuongezeka kwa joto kunaathiri afya ya binadamu kwa kiasi kikubwa. Ripoti hiyo inatoka kundi la vyuo mbalimbali na mashirika tofauti ya Umoja wa Mataifa inasema watu wengi wanaathirika na joto pamoja na mlo hafifu sambamba na kusambaa kwa magonjwa.

Moja ya kisababishi cha mabadiliko ya hali ya hewa ni uchafuzi wa anga. Uchafuzi wa anga ni kuchanganyika kwa hewa asili katika anga na vitu kama vile moshi, majivu, gesi za kemikali katika hali na kiwango ambacho huathiri sifa ya hewa na kusababisha madhara kwa binadamu na viumbe vingine.

Baadhi ya vitu na vitendo huathiri vibaya anga letu. Baadhi ya vitu hivyo ni kama gesi na moshi unaotoka kwenye viwanda, moshi kutoka kwenye magari, marashi, dawa ya kuuwa wadudu shambani na kadhalika.

Lakini umewahi kujiuliza kuwa aina ya chakula unachokula kinaweza kukusaidia kukabiliana na athari za kiafya zinazotokana na uchafuzi wa hewa?

Wanasayansi katika utafiti wao uliotolewa hivi karibuni, wanaeleza ulaji wa chakula cha Mediterania ( Mediterranean diet) chenye matunda mengi, mbogamboga, nafaka isiyokobolewa, samaki, maharage jamii ya soya, mafuta ya mizeituni na mayai yanaweza kuwalinda watu dhidi ya athari za afya zinazotokana na uchafuzi wa hewa.

Wanasayansi hao kutoka Shule kuu ya Udaktari ya NYU ya Marekani, walichambua data za watu takribani 550,000 wenye wastani wa umri wa miaka 62 kwa miaka zaidi ya 17 ambapo waliwapanga watu hao kwenye makundi kulingana na ulaji wao unaoendana na chakula cha Mediterania na kulinganisha na muda waliokaa kwenye hewa iliyochafuliwa.

Walibaini kuwa watu ambao walizingatia kula vyakula vilivyotajwa hapo juu walikuwa na uwezekano mkubwa wa kuepuka magonjwa na vifo vinavyotokana na uchafuzi wa hali ya hewa. Magonjwa hayo ni yale ya mfumo wa upumuaji, moyo na kansa.

                                   Vyakula  jamii ya Mediterania

Vyakula hivyo jamii ya Mediterania vina uwezo mkubwa wa kukabiliana na vimelea vya maambukizi ya magonjwa kwa mtu ambaye atazingatia kwa usahihi kutumia katika maisha yake.

Uchafuzi wa hewa unasababisha athari mbaya za kiafya kupitia hewa ukaa na mlo wa Mediterania una virutubisho muhimu kupambana na vimelea vya magonjwa,” anasema Mwandishi Mtafiti wa utafiti huo, Chris Lim wa Chuo cha NYU.

Lim anasema vyakula vya aina nyingine vinaweza kusaidia kukabiliana na athari hiyo. “Nilipoangalia kila mchanganyiko wa chakula cha Mediterania, kina matunda, mbogamboga na mafuta yanayoweza kupambana na athari za hewa chafu,” anasema.

Utafiti kuhusu ulaji kama unaweza kuzuia athari za kiafya za uchafuzi wa hewa bado haujahakikiwa na kukubalika kisayansi. Lakini utafiti huo sio wa kwanza kutafuta uhusiano wa mlo na athari za kiafya za uchafuzi wa hali ya hewa.

Wakala wa Uhifadhi wa Mazingira wa Marekani (U.S. Environmental Protection Agency (EPA)) unatafiti kama mlo unaweza kumlinda mtu dhidi ya athari za uchafuzi wa mazingira. Pia wanatafiti ili kujiridhisha kama virutubisho hivyo vinaweza kutumika badala ya dawa za kitabibu na kwa kiasi gani mtu anatakiwa apate virutubisho hivyo kumhakikishia usalama dhidi ya uchafuzi huo.

Hata hivyo, bado watu wanashauriwa kutumia zaidi matunda na mbogamboga kwenye milo yao ya kila siku ili kupata faida mbalimbali za kiafya.

Continue Reading

Afya

Ulaji mbaya wa chakula watajwa kusababisha kansa ya matiti kwa wanawake

Published

on

Thamani ya maisha haiko kwenye muonekano wa mtu na vitu vinavyomzunguka bali kwenye chakula anachokula kila siku ili kuwa na afya njema. Lakini umewahi kujiuliza, chakula kinawezaje kupunguza uwezekano wa kufa kutokana na magonjwa ikiwemo kansa?

Utafiti mpya uliofanyika huko Marekani umebaini kuwa kwa sehemu mlo kamili unaweza kupunguza hatari ya kufa kwa kansa.

Mtafiti Dk. Rowan Chlebowski wa Kituo cha Taifa cha Uuguzi cha City of Hope na wenzake walichambua takwimu za wanawake 48,000 waliosajiliwa katika mpango wa Afya ya Mwanamke unaoratibiwa katika vituo 40 nchini Marekani.

Awali wanawake wote walipata vipimo na hakuna aliyegundulika kuwa na kansa ya matiti lakini 20,000 kati yao walishauriwa kubadilisha mlo na kupunguza ulaji wa mafuta kwa asilimia 20 katika milo yao ya kila siku.

Pia waliambiwa wale zaidi matunda, mbogamboga na nafaka zisizokobolewa. Wanawake wengine hawakupewa maelekezo yoyote ya kuzingatia mlo kamili lakini walifundishwa kuhusu lishe nzuri na mlo wenye afya.

Baada ya miaka nane ya kuwafuatilia wanawake hao, watafiti hao waliangalia idadi ya kansa ambazo wanawake hao walitibiwa na zile ambazo zilisababisha vifo. Walibaini kuwa wanawake ambao walitumia kiasi kidogo cha mafuta walikuwa na hatari ndogo ya kufa kwa kansa ya matiti kwa asilimia 22, ukilinganisha na wanawake wengine.

Pia wanawake hao walipunguza kwa asilimia 24 hatari ya kufa kwa kansa zingine ikiwemo kwa 38%  magonjwa ya moyo ikilinganishwa na wanawake wa kundi ambalo walipata elimu ya mlo.

“Tunachokiona ni matokeo halisi,” anasema Dk. Chlebowski. Tafiti za awali ziliangalia madhara kabla ya uchunguzi wa kansa, lakini utafiti huu ulichambua kwa kiasi gani mlo unaweza kumuathiri mtu baada ya uchunguzi.

“Tulichobaini ni kuwa ushauri wa mlo baada ya uchunguzi wa kansa ya matiti ulikuwa muhimu kuliko kabla ya uchunguzi.”

                        Ulaji wa matunda na mboga unasaidia kupunguza hatari ya kupata kansa

Hata hivyo, utafiti huo ulibaini kuwa wanawake ambao wanazingatia kutumia kiasi kidogo cha mafuta katika maisha yao wana nafasi kubwa ya kuepuka kansa ya matiti.

Kutokana na idadi ya watu walioshirikishwa kwenye utafiti huo, Dkt. Chlebowski anasema wazo la kuhusisha mlo katika programu ya matibabu lilikuwa ni muhimu ili kupata matokeo chanya katika kukabiliana na kansa ya matiti kwa wanawake.

Watafiti hao wanaendelea na uchunguzi ili kufahamu kama ulaji wa chakula unaweza kuwa sehemu ya matibabu ya kansa ya matiti. “Inahamasisha kwasababu tunajaribu kuziba pengo kati ya mtindo wa maisha na mchakato wa kibaiolojia uliopo nyuma ya ugonjwa huo.”

 

Kansa ya matiti

Saratani ya matiti ni ugonjwa ambao huwapata wanawake na unatokana na athari za chembe ndogo ama seli kwenye matiti na matokeo yake ni kwamba hubadili mfumo wa kawaida wa kukua na kuongezeka.

Mabadiliko haya huanza polepole na yanaweza yakachukua muda mrefu hadi mtu kuweza kujua kama ana matatizo hayo. Ikiwa katika hatua hizo za mwanzo kwa kawaida huwa hakuna maumivu jambo hilo ni moja ya mambo ambayo huchangia baadhi ya wagonjwa kubaini tatizo hilo wakati tayari limekomaa.

Ni kutokana na sababu hizo, wanawake hutakiwa kuchunguza afya zao mara kwa mara kwasababu ugonjwa huweza kutibiwa kirahisi iwapo utabainika mapema.

Miongoni mwa dalili za saratani ya matiti ni uvimbe kwenye matiti ama makwapani. Titi kubadilika kiumbo, titi kutoa majimaji yaliyochanganyika na damu ama chuchu kuingia ndani.

Zipo aina mbalimbali za tiba na mojawapo ni upasuaji. Upasuaji huu kwa kawaida hufanywa katika hatua za mwanzo. Njia nyingine ni tiba ya mionzi au kupewa dawa. Jambo la kukumbukwa ni kwamba ugonjwa huu unaweza kusababisha kifo iwapo hautabainika mapema na kupatiwa tiba mwafaka.

Njia ambayo mtu aweza kujilinda asiathirike na saratani hii ya matiti ni kujichunguza mara kwa mara ili kubaini mapema na kupatiwa dawa.

Mwanamke anapaswa kuchunguzwa mara moja kwa mwaka ili kuona kama ameathirika na ugonjwa huo au la.

Continue Reading

Muhimu Kusoma

Copyright © 2020 FikraPevu.com