Connect with us

Siasa

Magufuli avitaka vyombo vya dola kuwafikisha mahakamani wanaobadili takwimu za serikali

Published

on

Rais John Magufuli amevitaka vyombo vya dola kuwafikisha mahakamani watu wanaobadilisha takwimu zinazotolewa na serikali na kuwapotosha watanzania.

Akitoa maagizo hayo Ikulu leo wakati wa kuwatunuku vyeti  wajumbe wa Kamati iliyokuwa inafanya mazungumzo na kampuni ya dhahabu ya Barrick ili kuongeza mapato ya madini, Rais Magufuli amesema watu wanaopingana na takwimu za hali ya uchumi na mapato wana lengo la kuichonganisha serikali na wananchi.

“Niwaombe watanzania tofauti na watu wengine wachache ambao kwao kubadilisha takwimu ni kitu cha kawaida muwapuuze, watu wa namna hiyo wapo tu kwasababu wanatutoa katika dira ya uchumi na lengo lao ni kuichonganisha serikali na wananchi”, amesema Rais Magufuli

Kauli ya Rais imekuja siku chache baada ya  baadhi ya wanasiasa kusikika  wakitofautiana na takwimu za serikali za hali ya uchumi na zile zinazoonyesha kuwa mapato yatokanayo na kodi yameongezeka na kudai kuwa takwimu hizo sio sahihi na haziendani na hali halisi ya uchumi wa wananchi wa kawaida.

Hivi karibuni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilitangaza kuwa  katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2017/2018 (Julai, Agosti na Septemba) imekusanya jumla ya trilioni 3.65 ambayo ni ongezeko la asilimia 1.2 ikilinganishwa na makusanyo ya kipindi hicho kwa mwaka uliopita. Na inatarajia kufikia lengo lake la kukusanya trilioni 17 kwa mwaka.

Kutokana na maoni hayo ya wananchi, Rais amemtaka Waziri wa Sheria na Katiba Prof. Palamagamba Kabudi  na vyombo vya dola kuwafuatilia watu hao ambao kwa nyakati tofauti wamekuwa wakibadilisha takwimu za serikali na kuwapotisha wananchi ili wafikishwe mahakamani kuthibitisha tuhuma zao.

“Lakini nafikiri vyombo vya dola na Prof. Kabudi wewe ndio Waziri wa Sheria muanze kuangalia watu wa namna hiyo ambao kwao ni kubadilisha takwimu. Unakuta mtu anazungumza makusanyo yameshuka wakati anajua kabisa si kweli. Watu wa namna hii wangekuwa wanapelekwa mahakamani wakathibitishe” amesema Rais na kuongeza kuwa,

“Katika hesabu za kawaida tu kama mapato yanashuka utaweza kusaini mkataba wa kujenga reli ya standard gauge yenye thamani ya zaidi ya trilioni 7 kutoka Dar es salaam hadi Morogoro kilometa 300 na kutoka Morogoro hadi Dodoma kilomita 426 na ni reli ya aina yake, utazipata wapi fedha kama makusanyo yameshuka”.

Kulingana na Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015 ambayo imefanyiwa maboresho katika kifungu cha 5 kinaeleza kuwa mtu yeyote ambaye atatoa au kuchapisha takwimu ambazo zinapingana na Sheria atakabiliana na adhabu ya kulipa faini isiyopungua milioni 5 au kufungwa jela kwa muda usiopungua mwaka mmoja au vyote kwa pamoja.

Kwa upande wake, Waziri wa Sheria na Katiba Prof. Palamagamba Kabudi amemshukuru Rais kwa kuiamini kamati hiyo aliyoiteua kufanya kazi ya kutetea maslahi ya taifa na kuhakikisha wananchi hawaibiwi tena katika sekta ya madini.

Amesema wataendelea kutoa ushirikiano na kwamba watachunguza maeneo mengine ya madini ya Almasi na Tanzanite ili kuihakikishia serikali mapato. Na amewataka watanzania kuendelea kuiamini serikali yao katika kuwaletea maendeleo wanayoyataka.

“Ukitaka kupima mafanikio aliyofikia mtu usiangalie kimo alichofika, bali uwezo wa shimo aliofikia”

Akizungumzia suala la kutoa vyeti kwa wajumbe walioshirika mazungumza na kampuni ya Barrick, Rais amesema watanzania hao wamefanya kazi nzuri ya kupigania maslahi ya taifa katika sekta ya madini. Mazungumzo hayo yaliwezesha kampuni ya Barrick kukubali kulipa fidia ya bilioni 700 kama hatua ya kuendelea na mazungumzo.

Rais wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli

Awamu nyingine  itahusisha kamati ndogo ambayo itaendelea na mazungumzo na wawakilishi wa kampuni hiyo ili kufikia muafaka wa kugawana faida ya 50/50 baada ya kodi zote kulipwa na kuiwezesha serikali kumiliki hisa za 16% na kupata kodi ya 70%.

Makubaliano hayo yamezua mijadala miongoni mwa wananchi huku wengine wakisema haiwezekani serikali yenye hisa 16% kupata faida ya 50/50. Wananchi wengine wanaona serikali imepiga hatua nzuri kwa kuongea na wawekezaji hao ili kuongeza mapato yatakayosaidia kuboresha huduma za kijamii.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe hivi karibuni alikaririwa na vyombo vya habari juu ya makubaliano ya serikali na Kampuni ya Barrick kuipa Tanzania fidia ya bilioni 700 na kugawana faida 50 kwa 50 licha ya serikali kumiliki hisa za asilimia 16, alisema suala hilo haliwezekani na serikali inapaswa kuwaambia ukweli wananchi juu ya mchakato mzima wa upatikanaji wa mapato katika sekta ya madini.

“Tanzania changamoto zake ni mbili tu kwenye sekta ya madini, umiliki na mfumo wa kodi ya kimataifa. Mfumo wa kodi ya kimataifa unayaruhusu makampuni kufungua makampuni dada kwenye nchi zenye kodi ndogo (tax haven)” amesema Zitto na kuongeza kuwa,

“Hapana sivyo, huwezi kuwa na hisa ya 16% ukapata faida ya 50% haiwezekani, haipo kokote duniani lakini unaweza kama ukimfanya muwekezaji kuwa mkandarasi sababu utamlipa fee yake na wala sio jambo la ajabu tunafanya hivyo kwenye sekta ya mafuta. Tuna mfumo maalumu wa kugawana faida”

Katika hatua nyingine, Prof. Florens Luoga ambaye alikuwa miongoni mwa wajumbe wa kamati hiyo, ameteuliwa na Rais kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) akichukua nafasi ya Prof. Benno Ndulu ambaye anamaliza muda wake wa utumishi.

Hafla hiyo ya kuwatunuku vyeti wajumbe wa kamati walioshiriki mazungumzo na Barrick imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini, vyama vya siasa na watendaji wa serikali wakiwemo mawaziri. 

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Siasa

Sakata la waraka wa Maaskofu KKKT lang’oka na Msajili Mambo ya Ndani

Published

on

Waziri wa Mambo ya Ndani Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Usajili wa Jumuiya za Kidini na Vyama vya Kijamii, Merlin Komba ili kupisha uchunguzi wa barua iliyoandikwa ukilitaka Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kufuta waraka ilioutoa Machi mwaka huu.

Barua iisambazwa kwenye mitandao ya kijamii ikiitaka KKKT kuufuta waraka wa Pasaka uliotolewa Machi 24 mwaka huu vinginevyo hatua kali za sheria zitachukuliwa dhidi ya kanisa hilo.

Waraka huo uliopewa jina la ‘Taifa letu amani yetu’ ulisainiwa na maaskofu 27 wa kanisa hilo. Ulijikita kujadili masuala ya jamii, uchumi, siasa, katiba mpya na matukio ambayo yako kinyume na kile lilichokiita tunu na misingi ya Taifa.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Waziri Nchemba amesema Serikali haipingani na dhehebu lolote na pale ambapo kuna uhitaji wa kufanyia kazi jambo kuhusu taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo taratibu huwa zinatumika kuzungumza na sio kama ilivyofanywa taarifa hiyo inayosambaa.

“Serikali inalinda uhuru wa kuabudu na waumini hivyo huo waraka una maudhui kama matatu, ni barua batili na tunaendelea kuchunguza kama imetengenezwa basi imetengenezwaje, kwani haujapita kwetu.” amesema Waziri Mwigulu.

Kutokana na msimamo huo wa serikali, Waziri Nchemba, amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Usajili wa Jumuiya za Kidini na Vyama vya Kijamii, Merlin Komba, kupisha uchunguzi wa barua iliyoandikwa kwa maaskofu wa KKKT.

“Hivyo basi, namsimamisha Msajili wa hizo taasisi kupisha uchunguzi na ikithibitika ni za Wizara tuweze kujua maana jambo hilo halijapita kwa Waziri, Katibu Mkuu na wala si maelekezo ya serikali,” amesema.

Hata hivyo, amewatoa hofu viongozi wa dini kutokana na sakata hilo na kuwataka waendelee na majukumu yao huku ikitahadharisha jamii kuwa makini na taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

“Tunawaomba viongozi wa dini waendelee na kazi zao, nasema jamii iwe macho na taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya jamii na wasifanyie kazi taarifa hizo. Viongozi wa dini wasiwe na taharuki na taarifa hizo, hazina baraka za Serikali na wasisite kuwasiliana na Serikali kujua uhalali wake,” amesema.

Waziri Nchemba amesema waraka wa viongozi wa dini uliotolewa miezi iliyopita ni jambo lililopita na hakukuwa na haja ya kuendeleza malumbano yasiyo na tija kwenye jamii.

Katika waraka wa ujumbe wa pasaka uliosomwa katika makanisa ya Kilutheri kote nchini Tanzania na kusambaa katika mitandao ya kijamii, baraza hilo limeorodhesha mambo kadhaa ambayo wameyataja kuwa ndio tishio la umoja na amani ya nchi hiyo.

Utekwaji wa watu wa hivi karibuni, utesaji, kupotea kwa watu, mashambulizi ya silaha dhidi ya viongozi wa kisiasa, muaji yenye mwelekeo wa kiitikadi, vitisho, ubambikiziaji wa kesi, na matumizi mabaya ya vyombo vya dola dhidi ya wananchi ni baadhi tu ya mambo yaliyotajwa katika waraka huo.

Lakini pia Watanzania wamekuwa na hisia tofauti kuhusu viongozi wa dini kuzungumzia hali ya kisiasa nchini. Waraka wa KKKT ulikuja mwezi mmoja baada ya ule wa maaskofu wa kanisa katoliki ambao nao ulionya juu ya kuminywa kwa haki ya kufanya shughuli za kisiasa kama mikutano ya hadhara na maandamano.

Baada ya nyaraka hizo mbili kutolewa na Maaskofu, baadhi ya mambo yaliyokuwa yakilalamikiwa yalipata ufumbuzi ikiwemo kupungua kwa mauaji na uteswaji wa raia kulikuwa kunafanywa na watu wasiojulikana.

Continue Reading

Jamii

Waziri Mkuu Majaliwa: Hatutangazi nyongeza ya mshahara hadharani kuepusha athari kwa jamii

Published

on

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameweka wazi kuwa serikali haitatangaza nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa umma hadharani ili kuepusha athari kwa jamii ikiwemo kupanda kwa bei ya bidhaa.

Akizungumza leo Bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalumu (CHADEMA), Susan Lymo ambaye alitaka kufahamu kwanini Serikali imewanyima au imeshindwa kuwalipa watumishi wa umma nyongeza ya mishahara ambayo ni haki yao ya msingi kulingana na miaka waliyokaa kazini.

Akijibu swali la Mbunge huyo, Waziri Mkuu Majaliwa amesema Serikali ina utaratibu wa kutoa nyongeza ya mishahara kwa watumishi wake lakini haitangazi kwa wananchi wote kama ambavyo imekuwa ikifanyika kwenye sherehe za wafanyakazi za Mei Mosi kila mwaka.

Amesema Serikali ikitangaza mishahara hadharani inaweza kusababisha usumbufu kwa watu wasio watumishi wa umma na inaweza kupandisha bei ya bidhaa na kuathiri mwenendo wa mahitaji ya wananchi sokoni.

Nyongeza za mishahara ambazo zinatangazwa hadharani, mara nyingi zina athari yake sio kwamba Serikali haikusudii kutoa nyongeza ya mshahara kwa mwaka, lakini unapotumia Mei Mosi kutangaza nyongeza ya mshahara unaleta athari kwenye jamii kwasababu vitu vinaweza vikapanda bei, vikawasumbua hata na wananchi ambao hawalipwi mshahara,” amesema Waziri Mkuu.

Amebainisha kuwa siyo lazima Serikali itangaze hadharani kila inapoongeza mishahara kwa watumishi wa umma lakini ifahamike kuwa Serikali ina utaratibu wake mzuri wa kuboresha stahiki za wafanyakazi wake kila mwaka.

Suala la nyongeza ya mishahara liko Serikalini na Mhe Rais ameishawahakikishia wafanyakazi atawaongeza mishahara na sio lazima litangazwe hadharani. Mshahara ni suala la mtu binafsi hata ukiongezwa leo kuwa tumeitangaza leo tumeongeza mshahara kwa kiwango hiki. Ukifanya hivi tayari umeleta kupanda kwa gharama’” amebainisha Waziri Mkuu.

Ameongeza kuwa mkakati wa Serikali ni kupunguza gharama za mahitaji kwenye masoko ili kuzuia mfuko wa bei za bidhaa.

Hata hivyo, Waziri Mkuu Mjaliwa amesema Serikali inaendelea kufanya sensa ya watumishi wote nchi nzima na zoezi hilo likikamilika itaboresha nyongeza ya mwaka, nyongeza ya mishahara na upandishaji wa madaraja.

Awali katika swali lake, Mbunge Lyima amesema Serikali inakiuka Sheria ya Utumishi wa Umma ya kuwapatia watumishi stahiki zao na kuwapunguzia motisha ya kufanya kazi kwa ufanisi katika maeneo yao ya kazi na kuathiri mafao baada ya kustaafu.

Hoja ya Mbunge huyo ni muendelezo wa malalamiko ya watumishi dhidi ya Serikali kwamba hawajapata stahiki zao tangu ilipoanza zoezi la ukakiki wa watumishi wa umma mwaka 2015. Katika zoezi hilo watumishi zaidi ya 9,000 walibainika kutokukidhi vigezo vya utumishi na hivyo kuondolewa kazini.

Huenda kauli aliyoitoa Waziri Mkuu leo Bungeni inaweza ikatofautiana na ile ya Rais John Magufuli aliyoitoa wakati wa sherehe za Mei Mosi, 2018 mijini Iringa ambapo alinukuliwa akisema hawezi kutoa nyongeza ya mishahara akidai Serikali haina fedha.

Kwangu mimi ninafikiria hizi pesa tunazotoa kwa ajili ya elimu bure ni nzuri kuliko fedha hizo kuzipeleka kuongezea mishahara, naona bora kuwapa mikopo wanafunzi wa vyuo vikuu kuliko kuongezea wafanyakazi mishahara,

Nikisema nitaongeza hizo pesa mimi nitazitoa wapi? naogopa kusema uongo. Hata mimi napenda kupandishiwa mshahara lakini kwa hali halisi ya sasa hivi lazima niwaeleze ukweli,” alinukuliwa Rais Magufuli.

Hata hivyo alibainisha kuwa kabla ya kuondoka madarakani ataboresha maslahi ya wafanyakazi wa umma, “Nawaahidi, kipindi changu cha urais hakitaisha kabla sijapandisha mishahara kwa wafanyakazi, kupandisha kwangu haitakuwa kwa shilingi elfu kumi, itakuwa ni kupandisha kwelikwel.”

Continue Reading

Jamii

Maaskofu KKKT wapewa siku 10 kufuta waraka

Published

on

Serikali imetoa siku 10 kwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), kuufuta kwa maandishi waraka wao waliotuoa Machi 24 mwaka huu na kisha kuujulisha Umma kwa njia mbalimbali walizotumia kuusambaza.

Kanisa la KKKT kupitia Baraza lake la Maaskofu lilitoa waraka uliopewa jina la ‘Taifa Letu Amani Yetu’ wakati wa Pasaka ambao mbali na masuala ya kiroho, ulibainisha mambo kadhaa yanayogusa mstakabali wa taifa.

Katika mitandao ya kijamii leo imesambazwa barua yenye kumbukumbu no. SO.748/25 inayoonyesha imeandikwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama Wizara ya Mambo ya Ndani kwenda kwa Mwenyekiti /askofu Mkuu wa KKKT iliyoandikwa Mei 30, 2018 ikitoa maelekezo ya kufutwa waraka huo ndani ya siku 10 tangu ilipoandikwa barua hiyo.

Ikiwa na kichwa cha habari ‘Ujumbe wa Baraza la Maaskofu wa KKKT’ barua hiyo inaeleza baraza hilo halitambuliki kisheria katika ofisi ya msajili.

“Unaelekezwa kuufuta waraka husika kwa maandishi na kuujulisha umma kuwa taasisi yako haikuwa na haina uwezo kisheria kufanya kile mlichokifanya. Maandishi hayo yaufikie umma wa Watanzania kwa kupitia vyombo vya habari na njia zingine zilezile zilizotumika kuufikisha waraka ule mliouita ‘Ujumbe wa Baraza la Maaskofu KKKT’.

Hata hivyo, barua hiyo imetoa onyo kali kwa taasisi hiyo dini nchi kutekeleza agizo mara moja la sivyo itachukuliwa hatua za kisheria.

“Maelekezo haya yatekelezwe ndani ya siku kumi tangu kupokea kwa barua hii vinginevyo hatua kali zaidi za kisheria zitachukuliwa dhidi ya taasisi hii,” inasema barua hiyo.

Ikumbukwe kuwa  waraka huo ulisainiwa na maaskofu 27 wa kanisa hilo nchini na kutaja baadhi ya mambo hayo kuwa ni pamoja na utekaji, utesaji, kupotea kwa watu, mashambulizi ya silaha dhidi ya viongozi wa kisiasa, mauaji yenye mwelekeo wa kiitikadi, vitisho, ubambikiziaji wa kesi, na matumizi mabaya ya vyombo vya dola dhidi ya wananchi.ni hali ya kijamii na kiuchumi, maisha ya siasa, na masuala mtambuka likiwamo suala la Katiba Mpya.

Waraka uliongeza pia kwamba uhuru wa kujieleza, kutoa na kupokea habari umeendelea kutoweka nchini huku ukionya kubanwa na hatimaye kuelekea kupungua kwa uhuru wa Bunge, Mahakama, na Tume ya Uchaguzi, ukisema hatua hii ni pamoja na kudhoofishwa kwa serikali za Mitaa.

Lakini kabla ya KKKT kutoa waraka wao, Kanisa Katoliki nalo lilitoa waraka kama huo likionya baadhi ya mambo ikiwemo uminywaji wa misingi ya demokrasia ya vyama vingi na uhuru wa kujieleza.

Baada ya kusambaa kwa waraka huo, yalijitokeza mambo mengi ikiwemo kutofautiana na kwa mawazo ya wananchi kuhusu wajibu wa viongozi wa dini katika kutoa ushauri, kuonya au kukemea pale mambo yanapoenda mrama.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa na Maaskofu wa KKKT

Hata hivyo, barua hiyo imepokelewa kwa hisia tofauti na watumiaji wa mitandao ya kijamii ikizingatiwa kuwa suala hilo lilijadiliwa na kupita, iweje linaibuka tena wakati huu ambapo kuna utulivu na yale mambo waliyoyapigia kelele na maaskofu  yamepungua ikiwemo kuteswa, kupotea kwa watu na vitisho dhidi ya viongozi wa kisiasa.

 

Wananchi bado wanawaamini viongozi wa dini

Wadau mbalimbali wa masuala ya kijamii wamesema kama kweli barua hiyo imetolewa na serikali, inaweza kuchochea taharuki zaidi kwa waumini wa kanisa hilo na wananchi kwasababu linagusa moja kwa moja imani zao.

Amebainisha kuwa bado waumini wengi wana imani na viongozi wao dini na kwamba yale wanayotamka yanakuwa na nia njema kwa jamii yao. Na katika muktadha huo serikali inapaswa kuwa makini ili kuepusha matatizo zaidi yanayoweza kutokea.

Akizungumza na FikraPevu, Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena amesema kama serikali ilibaini kuna tatizo kwenye usajili wa Baraza la Maaskofu la KKKT ingekaa na wahusika na kulimaliza kuliko kujitokeza hadharani na kuendeleza jambo ambalo limepita.

“Mimi namwamini Mungu kuliko serikali na viongozi wangu wa dini hasa Maaskofu. Hivyo serikali inapaswa kuwa makini na mambo yanayogusa imani za watu. Katika hili walipaswa kutafakari sana jinsi ya kushughulika nalo. Vinginevyo halina afya kwa ustawi wa taifa letu,” amesema Meena.

Amesema Maaskofu walitimiza wajibu wao wa kuonya kabla mambo hayajaharibika na serikali inapaswa kuyafanyika kazi yale yalyotajwa kwenye waraka au kukaa kimya ili kuepusha migongano isiyo na faida kwa taifa.

Continue Reading

Muhimu Kusoma

Copyright © 2020 FikraPevu.com