Connect with us

Jamii

Mgomo UDSM: Serikali isikilize hoja badala ya kupiga mabomu

Published

on

Edward Mdaki — Migomo ya wanafunzi wa elimu ya juu nchini  vilivyolazimishwa kufunguliwa baada ya uchaguzi wa oktoba 2010, imefikia kilele . Ni kilele kwa sababu ilianzia kwingineko  na kwa madai yanayofanana. Kote walikogoma awali walikuwa wakilalamikia  ucheleweshwaji wa fedha za kujikimu kutoka bodi ya mikopo  (HESLB).

Wanafunzi wa chuo kikuu cha Dar-es-salaam sehemu ya mlimani ambao walianza  kuhamasishana kugoma siku ya alhamisi na siku iliyofuata kuanza maandamano kuelekea ikulu, wana madai tofauti. Hawa wanalo tatizo tofauti.Ingawa ni tatizo tofauti kimsingi  limewagusa wanafunzi wote wa elimu ya juu nchini.Wanaitaka serikali   iongeze fedha ya kujikimu wanayokopeshwa na serikali  kwa siku  kutoka  5,000 ya sasa hadi 10,000.

Wanafunzi wa UDSM wamepaza sauti. Serikali kama kawaida yake imeagiza wapigwe mabomu. Mabomu ndiyo msemaji wa serikali kwa kila tatizo inalopelekewa. Wakati  wa uchaguzi watu walipochoka kusubiri utangazwaji wa matokeo waliandamana , polisi wakapiga mabomu. Hayo yalitokea Mbeya mjini, Mbozi,  Arusha mjini, shinyanga mjini, Mwanza na kwingineko.

Mapema mwaka huu polisi walitumia ubabe wa aina ileile hadi kuua baadhi ya waandamanaji waliokuwa wakielekea kwenye uwanja wa mkutano wakiongozwa na viongozi wa CHADEMA. Hii ni huko Arusha.

Chuo kikuu cha Dodoma- UDOM   walipogoma kushinikiza hoja zilizo  wazi kabisa za kuwepo kwa mafunzo kwa vitendo walipigwa mabomu. Baada ya kupigwa mabomu mtoto wa mkulima ,Waziri mkuu Mizengo Pinda alikwenda huko na kukiri kuwa wanafunzi walikuwa na hoja ya msingi. Akaagiza ishughulikiwe.

Wanafunzi wa UDSM wameandamana kudai nyongeza ya fedha za kujikimu kwa siku,wamepigwa mabomu.Mawaziri Mh.Shukuru Kawambwa wa elimu na Mh.Shamsi Vuai Nahodha jumamosi wamekutana na menejimenti ya chuo na wawakilishi wa wanafunzi na kukiri kuwa madai ya wanafunzi ni ya msingi.Hapa tunajiuliza,je Serikali ni lazima ipige watu wake mabomu ndipo itambue uzito wa madai yao ya msingi?

Hili la upigaji mabomu tuliache kwanza maana linahitaji makala nzima kulijadili. Yafaa pia kuwapongeza polisi na wanajeshi wa Tunisia na Misri  walioapa kutokutumia nguvu dhidi ya waandamanaji waliomng’oa madarakani Ben Ali wa Tunisia na wanaomtaka Rais Hosni Mubaraka wa Misri aondoke pia.

Akitoa taarifa inayoonekana kuchelewa mno,mshauri wa wanafunzi wa UDSM, Dr. Martha Qorro amewataka wanafunzi kuacha mgomo na maandamano kwa kuwa wizara inayohusika na  mikopo katika serikali ya wanafunzi-DARUSO  tayari iko katika majadiliano na Serikali ili  kuweza  kutambua  gharama halisi ya maisha kwa siku sasa ili mabadiliko  yaingizwe katika mchakato wa bajeti ya 2011/2012.

Katika taarifa yake hiyo kwa wanafunzi aliyoitoa siku ya ijumaa wakati maandamano yakiendelea, Dr. Quorro  anasema viwango vya fedha za kujikimu  kwa siku vimekuwa vikibadilishwa kama ifuatavyo;

Ø   Hadi kufikia mwaka 2005/2006 wanafunzi walikuwa wakikopeshwa sh. 2500/=  kwa siku.

Ø  Mwaka 2006/2007 kiwango hichio kilipandishwa hadi sh. 3500/= kwa siku na

Ø  Mwaka 2007/2008, kiwango hicho kilipandishwa hadi sh. 5000/=  wanayoendelea kukopeshwa hadi sasa.Hii inamaana kuwa fedha wanayopewa kwa siku imebaki sh. 5000/= kwa miaka mine iliyopita.

Ni aibu  kubwa kwa taifa linalotaka kujenga jamii yenye amani,haki na usawa kusubiri maandamano ndipo serikali  ielewe kuwa sh.5000/= zilizomuwezesha mwanafunzi kujikimu kwa  siku  miaka mine iliyopita  leo hazitoshi.Ipo aibu nyingine, ikiwa Dr. Qorro ambaye ni mshauri wa wanafunzi UDSM alijua kuwepo kwa mchakato wa kubadili kiwango hiki,kwa nini hakuwapa taarifa wanafunzi?  Au thamani ya taarifa hizi ilikuwa sawa na matokeo ya ubunge huko Mbulu,Rombo,Shinyanga mjini,Ilemela,Nyamagana na kwingineko?

Tujiulize swali  jingine .Ni mara ngapi serikali imeboresha mishaara ya wafanyakazi wake kuanzia mwaka 2007/2008 hadi leo kwa madai ya kupanda kwa gharama za maisha ? Hawa wanafunzi kulikoni? Ni vigezo gani vinavyohitajika kubainishwa ili kuwezesha fedha yao ya kujikimu kuongezwa? Je wanayo maduka yao yenye bei tofauti? Hoteli,mabasi yao je? Yaani je wapo kweye Tanzania nyingine tofauti yenye kuhitaji utafiti  tofauti na ule unaowahusu watanzania wasiokuwa wanafunzi?

Kuna hoja nyingine. Mwaka 2007/2008 wakati kiwango cha sh. 5000/= kikiidhinishwa kwa siku kila mwanafunzi alikuwa na hakika ya malazi katika hostel za vyuo.Serikali imeongeza idadi ya wanafunzi chuoni hapo kwa kasi ya ajabu bila kuongeza hosteli za kuwawezesha wanafunzi hao kupata malazi kwa gharama nafuu. Hili limefanyika hivyo  katika vyuo vyote nchini vya umma na visivyokuwa  vya umma. Fedha  ya malazi kwa kila mwanafunzi hujilipia kutoka katika  kiwango hicho hicho cha sh.5000/= anazopewa kwa siku sambamba na nauli yake,chakula,maji sabuni na mahitaji mengine yote. Kwa sasa mwenye uhakika wa malazi katika hosteli za chuo UDSM ni mwanafunzi wa mwaka wa kwanza.Wengine wote hupaswa kupanga vyumba mtaani ambako bei ya chumba kwa mwezi inafika Tsh.50,000/=

Kuna hoja nyingine ndani ya maandamano haya:

Wanafunzi wa elimu ya juu wanafikiri,wanatafiti na kufanya uchambuzi wa mambo mengi ya kijamii, kisiasa,kiuchumi na kiutamaduni. Wanaangalia namna  serikali inavyowatendea wao na kuwapendelea wengine. Wanashangaa serikali inayowafanya waishi kwa shida huku  ikijiandaa kulipa Dowans sh.94 bilioni. Wanaona usimamizi wa rasilimali  za taifa haufanywi kwa usahihi.

Wakati wao wakiishi kwa shida UDSM wameshuhudia rais kikwete akiongoza kikao cha kamati kuu  mchana na kuidhinisha malipo ya billion 94 Dowans na usiku akiendesha harambee ya kukusanya sh. 1 bilioni ya kujenga hostel ya chuo hicho.Hapa wanaona serikali inakosa umakini.

Ni bahati mbaya kuwa jeshi letu la polisi lilifundishwa intelijensia ya unabii na utabiri wa kutokea vurugu katika maandamano pekee. Ikiwa  lingejifunza intelijensia  ya kubaini hoja  za wanaotaka kuandamana lingeitaka serikali kutoa majibu kabla ya kuwepo kusudio la maandamano. Ni kwa ajili ya udhaifu wa intelijensia ya polisi na serikali kwa ujumla hoja hizo na nyingine zifuatazo hazina majibu ila waandamanaji watapigwa mabomu.

Ukosefu wa ajira:  serikali imeasisi mpango wa shule ya sekondari kwa kila kata. Ikahimiza wanafunzi wasome ualimu.Watu wakaitikia wito. Katika hali ya ajabu imeajiri baadhi tu ya walimu hawa huku shule zikikosa walimu. Waliokosa ajira sasa hivi wataungana na wanaomaliza vyuo mwaka huu. Wote wataandamana baadaye mwaka huu kudai ajira serikalini. Natarajia watapigwa mabomu. Miaka inakwenda haraka, 2012 itafika,wengine watahitimu tena, Serikali itasema uchumi haujakuwa kwa kasi iliyotarajiwa huku ikiingia mikataba feki na hivyo itashindwa kuajiri. Wataandamana kudai ajira nao watapigwa mabomu. Wanafunzi waliomaliza kidato cha nne mwaka  2010 katika shule ya Benjamini Mkapa katikati ya jiji kati yao 282 wamepata sifuri. Hawa watawakusanya wenzao waliofeli hapa DSM, wataungana na wahitimu wa vyuo walionyimwa ajira ili wawafundishe kuwaponya wasifeli; wataungana na machinga waliozuiwa kuuza bidhaa wanapopataka ili mradi hawavunji sheria; wataungana na wafanyakazi wasiopandishwa  madaraja kazini; wataungana na waliochagua Kimau akashinda lakini mshindi akatangazwa kuwa ni Njuguna, wote hawa kwa pamoja wataunda jeshi la waandamanaji wasiokuwa na silaha.

Wote wataunganishwa na wimbo  unaowakilisha mahitaji yao. Kwamba wamechoka kuongozwa na viongozi wasiojali maslahi ya wanyonge. Intelijensia ya jeshi na serikali  yake haizioni hoja hizi ila wakati wa maandamano watatabiri vurugu. Na hivyo watawapiga mabomu waandamanaji.

Serikali makini  haisubiri maandamano ya jinsi hii yatokee. Hujitahidi kutenda vitendo visivyozalisha  majeruhi wa tabaka tawala kwenye tabaka tawaliwa.

Waandamanaji wa UDSM walisikika wakisema nguvu ya umma haijawahi kushindwa na jeshi lolote duniani. Tuangalie mifano ya Afrika kusini na India enzi za  Mahatma Ghandhi, Tunisia, Ufaransa, Urusi, China, Irani ya Ayatolla Khomenei  na Kwingineko.

Watu wenye njaa hujua kuwa wanakaribiwa na kifo.Huona heri kuwaambia watawala tuna njaa  wakawaua  kama hawataki kuwasikiliza kuliko kukaa kimya na kufa kwa njaa. UDSM wanasema wanakufa  njaa kwa sababu  sh. 5000/= ya mwaka 2007 leo  mwaka 2011 haitoshi. Je mabomu ndilo jawabu lao?

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Afya

Watumishi wa afya 200 kupatiwa mafunzo ya utoaji dawa ya usingizi kuokoa maisha wajawazito

Published

on

Kufuatia upungufu wa wataalamu wa dawa za usingizi (anaesthesia), serikali itatoa mafunzo ya dawa za usingizi kwa watumishi wa afya 200 katika vituo vya afya vya upasuaji wa dharura kwa akina mama wajawazito.

Hatua hiyo inakuja ikiwa imepita miezi 6 baada ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kutangaza kuanza kutoa shahada ya dawa ya usingizi (Bsc. Anaesthesia Nursing).

Katika taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano serikalini cha Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, inaeleza kuwa mafunzo hayo yatatolewa sambamba na uboreshaji wa huduma ya upasuaji wa dharura kwa wajawazito ili kuokoa maisha ya wanawake na watoto ambao hufariki kwa kosa huduma muhimu za uzazi kwenye vituo vya afya.

“Mkakati wa kuhakikisha huduma za afya kwa akina mama wajawazito zinakuwa salama na uhakika kwa kuandaa rasilimali watu, miundombinu ya majengo na vifaa vitakavyowezesha huduma hizi ikiwemo upasuaji wa dharura kwa akina mama wajawazito wakati wa kujifungua,” imeeleza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya, vifo 556 vitokanavyo na uzazi kwa kila viumbe hai 100,000 huripotiwa kila mwaka katika maeneo mbalimbali nchini. Maana yake ni kwamba watoto na wajawazito hufariki hasa wakati wa mama akijifungua.

Aidha, serikali itaboresha vituo vya afya 288 vya serikali vilivyopo nchini ili kuviwezesha kutoa huduma ya dharura ya upasuaji kwa wajawazito ambapo waaguzi katika vituo hivyo watapatiwa mafunzo ya dawa za usingizi ili kuokoa maisha ya akina mama na watoto wachanga.

Utekelezaji wa mafunzo hayo ni matokeo ya ushirikiano wa Wizara ya Afya na Mfuko wa Pamoja wa Afya ambapo zaidi ya sh1,079 bilioni zimepatikana kufakisha mafunzo hayo ya dawa ya usingizi kwa wauguzi na matabibu waliopo kwenye vtuo vya afya nchini.

“Fedha hizo zitasomesha watumishi wapatao 200, kati ya watumishi hao 100 watapata mafunzo yao katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na MOI, watumishi 50 watafanya mafunzo katika hospitali ya KCMC, na 50 watafanya mafunzo hayo kwenye hospitali ya Bugando,” imefafanua taarifa ya wizara.

Lengo la serikali ni kuhakikisha ifikapo 2019 na kabla ya 2020 vituo vyote vya afya vinavyomilikiwa na serikali vinakuwa na watumishi maalum wa kutoa huduma ya dawa ya usingizi kwaajili ya wapasuaji wasiopungua wawili kwa kila kituo.

Mafunzo hayo ya mwaka mmoja ni mpito wakati serikali ikiendelea kukamilisha taratibu za kurasimisha utoaji wa shahada ya kwanza ya kutoa dawa ya usingizi katika Chuo cha MUHAS katka mwaka huu wa 2018/2019.

Hali halisi ya huduma ya dawa za usingizi nchini
Takwimu za wizara ya Afya zinaonyesha kuwa kuna upungufu mkubwa wa madaktari wenye utaalamu wa kutoa dawa ya usingizi hasa wakati wa huduma ya upasuaji ambapo kwa sasa waliopo ni asilimia 1.2 tu ya mahitaji yote.

Ili kuweza kukidhi mahitaji yote ya huduma hiyo wanahitajika madaktari 2000, lakini waliopo sasa ni madaktari 30 pekee.

Kufuatia changamoto hiyo Januari 31, mwaka huu wadau mbalimbali wa afya na elimu walikutana na kujadili namna ya kuondoa changamoto hiyo na kupendekeza mtaala utakaotumika kufundishia kozi ya Aesthesia kabla ya kuupeleka kwa Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU).

” Ni kweli kumekuwepo kwa changamoto hiyo ya watalaamu wa dawa hizo lakini sasa mpango huu ukikamilika maana yake tutaongeza idadi ya madaktari kamili maana hawa waliopo wengi ni wale ambao wamesoma kozi kwa mwaka mmoja au miwili.

” Mafunzo yakianza kutolewa hapa chuoni Muhimbili wataweza kuchukua wanafunzi 200, Bugando 50 na KCMC 50 jambo ambalo litaongeza idadi kubwa ya watalaamu ili kuweza kufikia lengo letu la kuwa na wataalamu 2000 nchi nzima,” alinukuliwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Mpoki Ulisubisya.

Continue Reading

Jamii

Waziri Mkuu Majaliwa: Hatutangazi nyongeza ya mshahara hadharani kuepusha athari kwa jamii

Published

on

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameweka wazi kuwa serikali haitatangaza nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa umma hadharani ili kuepusha athari kwa jamii ikiwemo kupanda kwa bei ya bidhaa.

Akizungumza leo Bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalumu (CHADEMA), Susan Lymo ambaye alitaka kufahamu kwanini Serikali imewanyima au imeshindwa kuwalipa watumishi wa umma nyongeza ya mishahara ambayo ni haki yao ya msingi kulingana na miaka waliyokaa kazini.

Akijibu swali la Mbunge huyo, Waziri Mkuu Majaliwa amesema Serikali ina utaratibu wa kutoa nyongeza ya mishahara kwa watumishi wake lakini haitangazi kwa wananchi wote kama ambavyo imekuwa ikifanyika kwenye sherehe za wafanyakazi za Mei Mosi kila mwaka.

Amesema Serikali ikitangaza mishahara hadharani inaweza kusababisha usumbufu kwa watu wasio watumishi wa umma na inaweza kupandisha bei ya bidhaa na kuathiri mwenendo wa mahitaji ya wananchi sokoni.

Nyongeza za mishahara ambazo zinatangazwa hadharani, mara nyingi zina athari yake sio kwamba Serikali haikusudii kutoa nyongeza ya mshahara kwa mwaka, lakini unapotumia Mei Mosi kutangaza nyongeza ya mshahara unaleta athari kwenye jamii kwasababu vitu vinaweza vikapanda bei, vikawasumbua hata na wananchi ambao hawalipwi mshahara,” amesema Waziri Mkuu.

Amebainisha kuwa siyo lazima Serikali itangaze hadharani kila inapoongeza mishahara kwa watumishi wa umma lakini ifahamike kuwa Serikali ina utaratibu wake mzuri wa kuboresha stahiki za wafanyakazi wake kila mwaka.

Suala la nyongeza ya mishahara liko Serikalini na Mhe Rais ameishawahakikishia wafanyakazi atawaongeza mishahara na sio lazima litangazwe hadharani. Mshahara ni suala la mtu binafsi hata ukiongezwa leo kuwa tumeitangaza leo tumeongeza mshahara kwa kiwango hiki. Ukifanya hivi tayari umeleta kupanda kwa gharama’” amebainisha Waziri Mkuu.

Ameongeza kuwa mkakati wa Serikali ni kupunguza gharama za mahitaji kwenye masoko ili kuzuia mfuko wa bei za bidhaa.

Hata hivyo, Waziri Mkuu Mjaliwa amesema Serikali inaendelea kufanya sensa ya watumishi wote nchi nzima na zoezi hilo likikamilika itaboresha nyongeza ya mwaka, nyongeza ya mishahara na upandishaji wa madaraja.

Awali katika swali lake, Mbunge Lyima amesema Serikali inakiuka Sheria ya Utumishi wa Umma ya kuwapatia watumishi stahiki zao na kuwapunguzia motisha ya kufanya kazi kwa ufanisi katika maeneo yao ya kazi na kuathiri mafao baada ya kustaafu.

Hoja ya Mbunge huyo ni muendelezo wa malalamiko ya watumishi dhidi ya Serikali kwamba hawajapata stahiki zao tangu ilipoanza zoezi la ukakiki wa watumishi wa umma mwaka 2015. Katika zoezi hilo watumishi zaidi ya 9,000 walibainika kutokukidhi vigezo vya utumishi na hivyo kuondolewa kazini.

Huenda kauli aliyoitoa Waziri Mkuu leo Bungeni inaweza ikatofautiana na ile ya Rais John Magufuli aliyoitoa wakati wa sherehe za Mei Mosi, 2018 mijini Iringa ambapo alinukuliwa akisema hawezi kutoa nyongeza ya mishahara akidai Serikali haina fedha.

Kwangu mimi ninafikiria hizi pesa tunazotoa kwa ajili ya elimu bure ni nzuri kuliko fedha hizo kuzipeleka kuongezea mishahara, naona bora kuwapa mikopo wanafunzi wa vyuo vikuu kuliko kuongezea wafanyakazi mishahara,

Nikisema nitaongeza hizo pesa mimi nitazitoa wapi? naogopa kusema uongo. Hata mimi napenda kupandishiwa mshahara lakini kwa hali halisi ya sasa hivi lazima niwaeleze ukweli,” alinukuliwa Rais Magufuli.

Hata hivyo alibainisha kuwa kabla ya kuondoka madarakani ataboresha maslahi ya wafanyakazi wa umma, “Nawaahidi, kipindi changu cha urais hakitaisha kabla sijapandisha mishahara kwa wafanyakazi, kupandisha kwangu haitakuwa kwa shilingi elfu kumi, itakuwa ni kupandisha kwelikwel.”

Continue Reading

Jamii

Maaskofu KKKT wapewa siku 10 kufuta waraka

Published

on

Serikali imetoa siku 10 kwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), kuufuta kwa maandishi waraka wao waliotuoa Machi 24 mwaka huu na kisha kuujulisha Umma kwa njia mbalimbali walizotumia kuusambaza.

Kanisa la KKKT kupitia Baraza lake la Maaskofu lilitoa waraka uliopewa jina la ‘Taifa Letu Amani Yetu’ wakati wa Pasaka ambao mbali na masuala ya kiroho, ulibainisha mambo kadhaa yanayogusa mstakabali wa taifa.

Katika mitandao ya kijamii leo imesambazwa barua yenye kumbukumbu no. SO.748/25 inayoonyesha imeandikwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama Wizara ya Mambo ya Ndani kwenda kwa Mwenyekiti /askofu Mkuu wa KKKT iliyoandikwa Mei 30, 2018 ikitoa maelekezo ya kufutwa waraka huo ndani ya siku 10 tangu ilipoandikwa barua hiyo.

Ikiwa na kichwa cha habari ‘Ujumbe wa Baraza la Maaskofu wa KKKT’ barua hiyo inaeleza baraza hilo halitambuliki kisheria katika ofisi ya msajili.

“Unaelekezwa kuufuta waraka husika kwa maandishi na kuujulisha umma kuwa taasisi yako haikuwa na haina uwezo kisheria kufanya kile mlichokifanya. Maandishi hayo yaufikie umma wa Watanzania kwa kupitia vyombo vya habari na njia zingine zilezile zilizotumika kuufikisha waraka ule mliouita ‘Ujumbe wa Baraza la Maaskofu KKKT’.

Hata hivyo, barua hiyo imetoa onyo kali kwa taasisi hiyo dini nchi kutekeleza agizo mara moja la sivyo itachukuliwa hatua za kisheria.

“Maelekezo haya yatekelezwe ndani ya siku kumi tangu kupokea kwa barua hii vinginevyo hatua kali zaidi za kisheria zitachukuliwa dhidi ya taasisi hii,” inasema barua hiyo.

Ikumbukwe kuwa  waraka huo ulisainiwa na maaskofu 27 wa kanisa hilo nchini na kutaja baadhi ya mambo hayo kuwa ni pamoja na utekaji, utesaji, kupotea kwa watu, mashambulizi ya silaha dhidi ya viongozi wa kisiasa, mauaji yenye mwelekeo wa kiitikadi, vitisho, ubambikiziaji wa kesi, na matumizi mabaya ya vyombo vya dola dhidi ya wananchi.ni hali ya kijamii na kiuchumi, maisha ya siasa, na masuala mtambuka likiwamo suala la Katiba Mpya.

Waraka uliongeza pia kwamba uhuru wa kujieleza, kutoa na kupokea habari umeendelea kutoweka nchini huku ukionya kubanwa na hatimaye kuelekea kupungua kwa uhuru wa Bunge, Mahakama, na Tume ya Uchaguzi, ukisema hatua hii ni pamoja na kudhoofishwa kwa serikali za Mitaa.

Lakini kabla ya KKKT kutoa waraka wao, Kanisa Katoliki nalo lilitoa waraka kama huo likionya baadhi ya mambo ikiwemo uminywaji wa misingi ya demokrasia ya vyama vingi na uhuru wa kujieleza.

Baada ya kusambaa kwa waraka huo, yalijitokeza mambo mengi ikiwemo kutofautiana na kwa mawazo ya wananchi kuhusu wajibu wa viongozi wa dini katika kutoa ushauri, kuonya au kukemea pale mambo yanapoenda mrama.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa na Maaskofu wa KKKT

Hata hivyo, barua hiyo imepokelewa kwa hisia tofauti na watumiaji wa mitandao ya kijamii ikizingatiwa kuwa suala hilo lilijadiliwa na kupita, iweje linaibuka tena wakati huu ambapo kuna utulivu na yale mambo waliyoyapigia kelele na maaskofu  yamepungua ikiwemo kuteswa, kupotea kwa watu na vitisho dhidi ya viongozi wa kisiasa.

 

Wananchi bado wanawaamini viongozi wa dini

Wadau mbalimbali wa masuala ya kijamii wamesema kama kweli barua hiyo imetolewa na serikali, inaweza kuchochea taharuki zaidi kwa waumini wa kanisa hilo na wananchi kwasababu linagusa moja kwa moja imani zao.

Amebainisha kuwa bado waumini wengi wana imani na viongozi wao dini na kwamba yale wanayotamka yanakuwa na nia njema kwa jamii yao. Na katika muktadha huo serikali inapaswa kuwa makini ili kuepusha matatizo zaidi yanayoweza kutokea.

Akizungumza na FikraPevu, Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena amesema kama serikali ilibaini kuna tatizo kwenye usajili wa Baraza la Maaskofu la KKKT ingekaa na wahusika na kulimaliza kuliko kujitokeza hadharani na kuendeleza jambo ambalo limepita.

“Mimi namwamini Mungu kuliko serikali na viongozi wangu wa dini hasa Maaskofu. Hivyo serikali inapaswa kuwa makini na mambo yanayogusa imani za watu. Katika hili walipaswa kutafakari sana jinsi ya kushughulika nalo. Vinginevyo halina afya kwa ustawi wa taifa letu,” amesema Meena.

Amesema Maaskofu walitimiza wajibu wao wa kuonya kabla mambo hayajaharibika na serikali inapaswa kuyafanyika kazi yale yalyotajwa kwenye waraka au kukaa kimya ili kuepusha migongano isiyo na faida kwa taifa.

Continue Reading

Muhimu Kusoma

Copyright © 2020 FikraPevu.com