Connect with us

Investigative

Mijusi aina ya GECKO hatarini kutoweka

Published

on

MIJUSI aina ya Gecko Williams haipatikani duniani kote, isipokuwa Kimboza kijiji cha Mwarazi wilaya ya Morogoro.

Mijusi hiyo inaweza kuonekana ya kawaida katika macho ya wengi, lakini kwa wale wanaojali mazingira na urithi wa taifa hii ni kesi kubwa.

Lakini, kwa sasa kuna tatizo kubwa ambalo lipo katika msitu wa Kimboza uliopo katika Tao la Mashariki sehemu ya milima ya Uluguru, kilomita chache kutoka Morogoro mjini, njia ya kuelekeaKisaki.

Wataalamu wa wizara ya mali asili na utalii hawapendi kuzungumzia mijusi, hawa ambao kimsingi ni biashara nzuri kwa wale wanaopenda kufuga wadudu, hasa nchi za Ulaya kutokana na kuwa na rangi ya kupendeza.

Kwa nchi za Ulaya mijusi hiyo huuzwa dola 70, sawa na sh 122,500 na ambapo Uingereza bei yake ni paundi 110 kwa mjusi mmoja, ambapo kwa seti ni paundi 200. Kwa maelezo ya wakazi wa jirani na msitu huo, uvunaji wa mijusi umekuwa ukifanyika kwa muda mrefu sasa.

Majangili wamekuwa wakiingia na kuchukua mijusi hiyo na kuwauzia wafanyabiashara kwa bei ya Sh 2,000 hadi Sh 3,000 kwa mjusi mmoja, bei ambayo hailingani na thamani ya mijusi hiyo.

Kwa kuwa mijusi hiyo inatakiwa kuwa jozi (wa kike na wa kiume) ukamataji wake ambao hufanyika sana usiku huhusisha jike na dume.

Wakazi wa jirani hawajui kwa uhakika mijusi hiyo inatakiwa kwa sababu gani na kwa kuwa hawaoni sababu za kuzuia hata wanapofanyakazi hiyo wanaifanya kwa namna ambayo Musa Chande ni mwenyekiti wa kitongoji cha Kibungo kinachozungukwa na hifadhi ya msitu wa Kimboza ambapo mjusi genko ndiomaskani yake alisema kwamba wao hawajui thamani ya mijusi hiyo ambayo kwa kienyeji wanaiita balagaja na hata hao wavunaji wanawaachia tu.

“Zamani kulikuwa na utaratibu wa kufanyika kwa doria katika msitu huu lakini kwa sasa hakuna na watu wamekuwa wakijiingilia kiholela na kufanya wanachotaka” alisema mwenyekiti huyo.

Mwenyekiti huyo alielezea masikitiko yake juu ya mambo yanayofanyika katika msitu huo, mambo ambayo yamesababisha wanyama kadhaa kutoweka na kusema kwamba rasilimali zilizobaki zitaondoka na msitu wenyewe unavyozidi kuondoka na kukosa udhamini.

“Kuna balagaja “mijusi” inachukuliwa sijui wanapeleka wapi na inafanyiwa nini, lakini vitendo vya kukusanya mijusi hiyo na kulipwa ndio siipendi’’ anasema Chande. Mijusi hiyo inayochukuliwa ni sehemu tu ya uharibifu mkubwa unaoendelea katika msitu wa Kimboza ambao pia ndio chanzo cha maji kwa ajili ya mto Ruvu unaolisha jiji la Dar es salaam.

Mijusi hiyo ambayo kiingereza inatambuliwa kama gecko williams na ipo katika aina 2000 za mijusi aina ya gecko duniani miongoni mwa aina 5000 za mijusi yote iliopo dunia. Gecko William ambaye kitaalamu anajulikana kama Lygodactylus jina ambalo lilianza kutumika miongoni mwa wanasayansi mwaka 1952.

Mijusi hiyo yenye urefu usiozidi inchi nne hupendelea kuishi katika miti aina ya pandama na eneo lenye nyuzi joto 25-29°C .Kwa kawaida mijusi hii inarangi tofauti kulingana na jinsia zake ambapo mijusi ya jinsia ya kiume huwa na rangi bluu iliokoza ambapo majike huwa na rangi ya kijani iliochanganyika na rangi ya dhahabu.

Wakati rangi ya watoto wa kiume huwa inafanana na rangi ya mijusi jike ambayo inataga yai moja hadi mawili yanayototolewa katika muda wa siku 100. Mijusi hii haina utaratibu wa kulea mayai badala yake kuyafunika katika takataka hadi yatakapojiengua yenyewe ndani ya siku hizo 100.Mijusi hii inaweza kufugwa na ikifugwa huwa na tabia na mwenendo tofauti.

Mijusi hii yenye tabia ya kusimamisha mkia wake pale inapokimbia au inapohisi hatari pamoja na kutikisa kichwa mara kwa mara huvunwa kwa staili ambayo si sawasawa kwa kuangtushwa kutoka katika miti baada ya kuleweshwa na mwanga wa tochi.

Kutokana na kupendelea kula matunda, asali na wadudu wadogo wadogo wanaopatikana katika miti wanayoishi, wenyeji wa vijiji wamekuwa na kazi ya kuwakamata na kuwapelekea watu wa kati ambao nao husafirisha mijusi hiyo kuipeleka nje.

Mara nyingi mijusi hii hutumika kwa ajili ya kujifunzia masuala ya kisayansi sambamba na mambo ya mazingira ambapo pia hutumika kama mapambo na mifugo katika sehemu mbalimbali za dunia.

Kwa nchi za Ulaya mijusi hiyo huuzwa dola 69.99 ambapo kwa nchi ya uingereza bei yake ni paundi 110 kwa mjusi mmoja ambapo kwa seti ni paundi 200.

Kuvurugika kwa utaratibu wa ulinzi shirikishi unaohusisha maofisa wanyamapori na wananchi,wenyeji wamekuwa wakitumika mwanya huo kuiba mijusi kutoka katika hifadhi na kuwauzia wafanyabiashara wa mijusi kwa bei ya shilingi 2000 hadi 3000.

Kwa namna fulani ukosefu wa uelewa wa thamani ya mijusi hiyo,umaskini na kukosekana kwa mtu wa kusimamia msitu huo wa Kimboza na mali zake wananchi wa kijiji cha Mwarazi ambapo ni moja katika ya vijiji vinne vya Kibangile , Changa na Uponda kusema kuwa hawajui kinachoendelea katika msitu huo japo wanajua wapo wenzao wanaowinda.

Hali hiyo inatokana na kile kilichoonekana kama kukatishwa tamaa ya kulinda rasilimali zilizopo katika msitu huo kwa kuwa hawanufaiki. “Awali kulikuwa na utaratibu wa kupatika fedha na serikali kwa ajili ya kusafisha na kulinda msitu huu lakini kwa sasa utaratibu huo haupo jambo ambalo limetufanya tukate tama’’ alisema Sania Kambi mmoja wa wanakamati ya mazingira kijijini hapo.

Pia mwanakamati huyo alisema jambo lingine linalowakatisha tamaa ya kulinda wanyama na rasilimali zingine katika msitu huo ni pale idara ya maliasili inapotoa vibali vya kuwinda bila kuwashirikisha wananchi wenyewe ambao ndio walinzi .

John Kimario meneja wa hifadhi misitu wilaya ya Morogoro alisema kimsingi kazi ya ulinzi wa rasilimali za msitu wa Kimboza na jukumu la wananchi kwa mujibu wa sheria ndogo za kuhifadhi kuendelea msitu huo.

Aidha, meneja huyo anasema kuwa kwa sasa wanakijiji hao wamekata tamaa ya kuhifadhi msitu huo kutokana na kutopewa fedha kama motisha kutokana na kazi ya ulinzi waliokuwa wakifanya kutoka idara ya misitu tangu mwaka 2007.

Anasema kuwa ofisi ya misitu wilaya ya Morogoro, inamkakati wa kuendelza ushirikiano na vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo ili waweze kulinda kama ilivyokuwa zamani. Hata hivyo, anakanusha kutolewa kwa vibali vya kuwinda wanyama aina yoyote katika msitu huo na kwamba wanaowinda wanyama ni majangili, ambapo wamekuwa wakikamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Tayari mtu mmoja amefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Morogoro, akikabiliwa na shitaka la kukutwa na nyara za serikali. Mshitakiwa huyo alifunguliwa kesi chini ya hakimu Hosan, kesi iliofunguliwa Februari 7 mwaka huu.

Katika mahojiano Mpelelezi wa kesi hiyo anasema mshitakiwa huyo alikamatwa Januari 31 mwaka huu saa 3 asubuhi katika kituo cha mabasi yaendayo mikoani cha Msamvu manispaa ya Morogoro.

Akielezea mazingira ya kumkamata mshitakiwa huyo Lukuba alisema kuwa polisi walipata taarifa kutoka kwa raia wema kuwa kuna mtu huyo alikuwa na mijusi hiyo, akiisafirisha kwenda jijini Dar es Salaam akitumia basi, linalofanya safari zake kati ya Kisaki wilaya ya Morogoro na jijini Dar es Salaam.

Polisi walifanikiwa kuweka mtego katika stendi hiyo na kumkamata mtu huyo, kutokana na tayari walipata taarifa za jinsi alivyo na kwamba baada ya kumkamata walimfikisha katika kituo kidogo cha polisi cha Msamvu ili kuweza kumpekua.

Mtu huyo alikuwa amebeba mfuko wa Rambo, ndani yake kulikuwa na bahasha zile kubwa za kaki, na polisi walipofungua ndani yake walikuta kitenga kinachofanana na mtego wa panya, ambamo ndani yake kulikuwa na mijusi midogo 80.

Mijusi hiyo ilikuwa majike 40 na madume 40 na baada ya hapo walimfikisha katika kituo kikuu cha polisi, kwa ajili ya kuwasiliana na idara ya maliasili mkoani hapa ili kuweza kuweza kumfungulia kesi.

Polisi walibaini kuwa mtu huyo alikuwa na uhusiano mtu mmoja ambaye walipatana kukutana naye Stendi Kuu ya Ubungo, Dar ili kufanya biashara hiyo.

Polisi waliweka mtego kwa ajili ya kwenda Dar pamoja na mshitakiwa na watendaji wa maliasili, lakini cha kushangaza maofisa wa malisili walishindwa kukamilisha taratibu zao za usafiri kwa siku hiyo na hivyo dalali huyo hakuweza kukamatwa kutoa taarifa zaidi wapi wanapopeleka mijusi hiyo na vibali wamevipata wapi.

Taarifa za Kipolisi zinasema mtuhumiwa alikuwa akipewa shilingi 20,000 kwa idadi ya mijusi hiyo jambo ambalo linaongeza maswali kwa kuwa gharama ya kutoka Mkuyuni hadi Dar es Salam inapita gharama ya bidhaa.

Hii ni mara ya pili kwa mtu huyo kuuza mijusi hiyo kwa mteja wake huyo wa Dar, ambaye naye humuuzia mtu mmoja ambaye huisafirishwa kwenda Ujerumani. Jonata Sume ambaye ni Kaimu Afisa Wanyamapori wa Wilaya ya Morogoro, alikiri kuwepo na ujangili na kwamba wao kama idara walipata taarifa hiyo.

Lakini, zoezi hilo lilikwama kutokana na idara ya maliasili kushindwa kutoa posho za watendaji waliotakiwa kwenda Dar es salaam pamoja na usafiri kwa muda. Anasema kuwa hiyo ni changamoto kubwa, inayowakabili idara hiyo na kwamba kushindwa kuwakamata majangili wengi, kunatokana na kutokana na kukosa vitendea kazi.

“Suala la ujangili sio suala la upanga, inatakiwa ukisikia kuna majangili ufanye haraka kama zimamoto, vinginevyo nao watajipanga kupiga haraka na kutoweka’’ anasema Anasema kuwa serikali haijaanza kuuza mijusi hiyo na kwamba thamani ya mijusi yote hiyo iliyokamatwa ni sh 2,240,000, kwani mjusi mmoja ana thamani ya Sh 28,000.

Wananchi wanaozunguka na msitu huo, wanasema kuwa wamekatishwa tamaa ya kulinda rasilimali zilizopo katika msitu huo, kutokana na kutonufaika nazo. “Awali kulikuwa na utaratibu wa serikali kutoa fedha kwa ajili ya kusafisha na kulinda msitu huu, lakini kwa sasa utaratibu huo haupo, jambo ambalo limetufanya tukate tamaa” alisema Sania Kambi, mmoja wa wanakamati ya mazingira kijijini hapo.

John Kimario ni Meneja wa Hifadhi Misitu wilaya ya Morogoro. Anasema kwa mujibu wa sheria ndogo za kuhifadhi kuendeleza msitu huo, kazi ya ulinzi wa rasilimali za msitu wa Kimboza ni jukumu la wananchi wote.

Continue Reading
2 Comments

2 Comments

  1. AVIT MBUYA

    02/06/2012 at 2:58 pm

    JAMANI TUCHUNGE RASILMALI ZETU HASA SISI RAIA

  2. saleh

    04/07/2012 at 3:46 am

    Tanzania imebarikiwa sana lakini wapi tunaelekea?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Investigative

‘UBESHI’: Safari ya Vijana Kuifikia Almasi Mwadui-Shinyanga

Published

on

MAJUZI nilikuwa katika utafiti wa namna gani Madini ya Almas yanayopatikana katika Mji Mdogo wa Maganzo Wilayani Kishapu mkoani Shinyanga umewanufaisha wananchi wanaozunguka Mgodi wa Almasi wa Mwadui.

(more…)

Continue Reading

Investigative

Hofu ya Usalama kwa wafanyakazi GGM Yatanda

Published

on

SIKU chache baada ya moto kuzuka ndani ya mgodi wa Geita (GGM) na kuteketeza mali zenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 25,hofu kubwa ya kupoteza maisha imeibuka kwa uongozi na wafanyakazi wa mgodi huo.

(more…)

Continue Reading

Investigative

If we can’t give people’s priorities the attention they deserve, why ask them to prioritize?

Published

on

In a move intended to empower the citizens and give them mandate to decide on their own development priorities, the government adopted the decentralization policy.

(more…)

Continue Reading

Muhimu Kusoma

Copyright © 2020 FikraPevu.com