Connect with us

Afya

Mimba za Utotoni: Wasichana wanapogeuka wakimbizi Makumbusho

Published

on

Na Daniel Samson

“Nilipomaliza shule nikaanza mahusiano na huyo mwanaume, basi katika kipindi cha  wiki tano nikajigundua sijielewi kutokana na mabadiliko niliyopata”, hayo ni maneno ya msichana Aisha Juma (17) aliyepata mimba muda mfupi baada ya kumaliza darasa la 7 katika shule moja kata ya Pwani mkoa wa Mtwara.

Aisha (Jina sio halisi) ni miongoni mwa wasichana wengi wanaopata mimba nchini na kukatisha masomo huku wakishindwa kutimiza ndoto zao za kielemu.

Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 , sehemu ya pili (II) ya sheria hiyo inatamka “Mtoto ni mtu aliye na umri chini ya miaka 18”, na kifungu kidogo cha 12 kinatamka kuwa, “Mtu yeyote hataruhusiwa kumfanya mtoto apate mateso, au adhabu ya kikatili, ya kinyama au afanyiwe matendo yenye kumshushia hadhi”.

Mimba za utotoni zinatajwa kuwa miongoni mwa vitendo vya ukatili wa kijinsia ambavyo vinawatesa na kuwadhalilisha watoto wa kike na kuwa kikwazo kwa wao kufikia ndoto zao za kielimu

Baada ya kugundulika kuwa ana mimba, Aisha alifukuzwa myumbani kwao, hata alipomtafuta mwanaume  aliyempa mimba anayejulikana kwa jina la Daudi Mitishamba hakufanikiwa kumpata.   Binti huyo aliondoka Mtwara akiwa mjamzito na kuelekea Dar es Salaam kumtafuta dada yake aitwaye Salma Maulid ambaye alikuwa anaishi Kata ya Makumbusho, Wilaya ya Kinondoni ili aepukane na kile alichodai ni kutengwa na jamii inayomzunguka.

Aisha anasema alikuwa na kiasi kidogo cha fedha ambacho kisingeweza kumfikisha Dar es salaam,na hivyo  safari yake iliishia Mkuranga, hapo alitelemshwa ambapo alikutana na dada mmoja anayeitwa Monica. Dada huyo alimchukua na kukaa naye kwenye chumba kimoja mpaka alipojifungua mtoto wa kiume mwezi Aprili 2017.

 

Ugumu wa maisha wamtoa Mkuranga hadi Dar es Salaam

Kutokana na ugumu wa maisha alikimbilia Dar es salaam kwa dada yake Salma Maulid anae ishi  kata ya Makumbusho lakini hakumkuta kwani alikuwa amehama katika nyumba aliyokuwa anaishi hapo awali.

Watu aliokutana nao walimpeleka kwa Mjumbe wa Mtaa wa Sindano kata ya Makumbusho, Mwanahamisi Majid ambaye alimpokea na kukaa naye wakati mchakato wa serikali ya Mtaa kumrudisha nyumbani kwao Mtwara ukifanyika.

Mwanahamisi  anasema alimpeleka binti huyo Ofisi ya Afisa Ustawi wa Jamii  kata ya Mwananyamala B ambako huko Asha alihojiwa na ameendelea kuishi Makumbusho. Kutokana na madhira yaliyompata binti huyo ameshindwa kuendelea na masomo na sasa anamlea mtoto wake huku akiwa ametengwa na ndugu zake.

                                                      Aisha, msichana aliyepata mimba na kukatiza ndoto za kupata elimu

 

Hali Halisi ya Mimba za Utotoni

Kulingana na utafiti wa Shirika la Afya Duniani (2016), Tanzania inatajwa kuwa ni nchi ya tatu barani Afrika kwa matukio ya ndoa za utotoni na mimba kwa asilimia 28, ambapo kila mwaka wasichana 8,000 hupata mimba na kukatisha masomo.

Tatizo hilo bado ni kubwa katika nchi za Afrika Mashariki. Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Watu na Makazi (UNFPA) linaeleza kuwa msichana 1 kati ya 6 mwenye umri wa miaka 15 hadi 19 hupata mimba katika nchi hizo.

Inakadiriwa kuwa kila mwaka wasichana milioni 15 wanalazimishwa kuolewa katika umri mdogo na kupata ujauzito. Wasichana walio katika hatari ya kupata mimba ni wale wenye umri miaka 10 hadi 13.

 

Mwanaharakati Anena

Kwa msaada wa chama cha wanahabari wanawake TAMWA, mwandishi wa makala haya alifanikiwa kuzungumza na wadau mbalimbali akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi ya Wanawake Katika Jitihada za Kimaendeleo (WAJUKI) ambayo inafanya kazi za kutetea haki za wanawake katika kata ya Makumbusho,  Janeth Mawinza yeye anasema matukio ya wasichana kupewa mimba na kutekelezwa yamekuwa kikwazo kwa wasichana kufikia ndoto zao.

“Kuna uozo huko mitaani, vipigo kwa watoto, vipigo vya majumbani baba na mama, ulawiti, ubakaji. Zaidi ni kushirikiana kuongeza nguvu na tukifanya wote kwa nguvu ya pamoja amani itapatikana na vitendo vya ukatili wa kijinsia havitakuwepo”, amesema.

Hata hivyo anaeleza kuwa ukatili wa kijinsia katika kata yake bado upo lakini sio kwa kiasi kikubwa ikizingatiwa kuwa wanashirikiana na wananchi kupinga vitendo hivyo ikiwemo kutoa elimu na kuwasaidia wale waliothirika warejee katika maisha ya kawaida.

       Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi ya Wanawake Katika Jitihada za Kimaendeleo (WAJUKI), Janeth Mawinza akiwa ofisini Dar es                       Salaam baada ya kufanya mahojiano juu ya ukatili wa kijinsia kata ya Makumbusho, wilaya ya Kinondoni.

 

Athari za Kisaikolojia

Mtaalamu na Mshauri wa Masuala ya Saikolojia kutoka Taasisi ya Ustawi wa Jamii Tanzania, Zainabu Rashidi amesema mimba za utotoni zinaathiri mwenendo na tabia za msichana ambapo asipopata matibabu ya kisaikolojia uwezekano wa kufanya ukatili akiwa mtu mzima ni mkubwa.

“Mimba ina madhara mengi zaidi, msichana anaweza kumtupa au kumkimbia mtoto. Na mara nyingi anapokuwa na yule mtoto uchungu unazidi kwa hiyo anaweza akaendeleza tabia ambazo sio nzuri dhidi ya yule mtoto ikiwemo kumpiga”, anaeleza Mtaalamu wa Saikolojia na kuongeza kuwa hali hiyo husababishwa na mtazamo hasi wa jamii juu ya wasichana waliozaa katika umri mdogo ambapo hujiona ni wakosaji na waliotengwa na jamii yao.

Anasema ikiwa msichana aliyepata mimba akipata matibabu anaweza kurejea katika hali ya kawaida na kuendelea na maisha yake. Anaishauri jamii kutoficha ukatili wa kijinsia lakini wawasaidie waathirika kupata matibabu.

“Kuhakikisha wanapata huduma za kisaikolojia na ushauri ili kurudi katika hali ya kawaida. Ni jukumu la jamii kujua kwamba mtoto anapopata mimba sio kuficha lakini kuhakikisha anapata huduma za kijamii”, amesema, Mtaalamu huyo.

 

Mkakati wa Serikali kutokomeza Mimba za Utotoni

Serikali imezifanyia maboresho Sera na Sheria ili kumlinda mtoto wa kike dhidi ya mimba za utotoni pamoja na marekebisho ya Sheria ya Elimu sura 353 ambayo inatoa adhabu ya kifungo kisichopungua miaka 30 kwa mtu yeyote atakayempa mimba mwanafunzi wa shule ya Msingi na Sekondari.

Katika kutokomeza ndoa na mimba za utotoni Serikali imeanza utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa kutokomeza Ukatili dhidi ya wanawake na watoto unaojumuisha sekta zote zinazohusu wanawake na watoto kwa lengo la kupinga aina zote za ukatili na kupunguza mimba za utotoni kutoka asilimia 47 hadi 10 ifikapo mwaka 2020.

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Katika Lengo la 5 la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s 2030) linasisitiza Usawa wa Kijinsia katika jamii na linakusudia kuondoa aina zote za ukatili dhidi ya wanawake na wasichana katika sekta binafsi na Umma ikiwemo usafirishaji wa watoto, udhalilishaji kingono na aina zote za unyanyasaji.

Ili lengo hilo litimie linazitaka nchi wahisani kutunga na kuimarisha sera madhubuti na sheria zinazolenga kukuza usawa wa kijinsia na kumuwezesha mwanamke na msichana katika nyanja zote.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Afya

Watumishi wa afya 200 kupatiwa mafunzo ya utoaji dawa ya usingizi kuokoa maisha wajawazito

Published

on

Kufuatia upungufu wa wataalamu wa dawa za usingizi (anaesthesia), serikali itatoa mafunzo ya dawa za usingizi kwa watumishi wa afya 200 katika vituo vya afya vya upasuaji wa dharura kwa akina mama wajawazito.

Hatua hiyo inakuja ikiwa imepita miezi 6 baada ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kutangaza kuanza kutoa shahada ya dawa ya usingizi (Bsc. Anaesthesia Nursing).

Katika taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano serikalini cha Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, inaeleza kuwa mafunzo hayo yatatolewa sambamba na uboreshaji wa huduma ya upasuaji wa dharura kwa wajawazito ili kuokoa maisha ya wanawake na watoto ambao hufariki kwa kosa huduma muhimu za uzazi kwenye vituo vya afya.

“Mkakati wa kuhakikisha huduma za afya kwa akina mama wajawazito zinakuwa salama na uhakika kwa kuandaa rasilimali watu, miundombinu ya majengo na vifaa vitakavyowezesha huduma hizi ikiwemo upasuaji wa dharura kwa akina mama wajawazito wakati wa kujifungua,” imeeleza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya, vifo 556 vitokanavyo na uzazi kwa kila viumbe hai 100,000 huripotiwa kila mwaka katika maeneo mbalimbali nchini. Maana yake ni kwamba watoto na wajawazito hufariki hasa wakati wa mama akijifungua.

Aidha, serikali itaboresha vituo vya afya 288 vya serikali vilivyopo nchini ili kuviwezesha kutoa huduma ya dharura ya upasuaji kwa wajawazito ambapo waaguzi katika vituo hivyo watapatiwa mafunzo ya dawa za usingizi ili kuokoa maisha ya akina mama na watoto wachanga.

Utekelezaji wa mafunzo hayo ni matokeo ya ushirikiano wa Wizara ya Afya na Mfuko wa Pamoja wa Afya ambapo zaidi ya sh1,079 bilioni zimepatikana kufakisha mafunzo hayo ya dawa ya usingizi kwa wauguzi na matabibu waliopo kwenye vtuo vya afya nchini.

“Fedha hizo zitasomesha watumishi wapatao 200, kati ya watumishi hao 100 watapata mafunzo yao katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na MOI, watumishi 50 watafanya mafunzo katika hospitali ya KCMC, na 50 watafanya mafunzo hayo kwenye hospitali ya Bugando,” imefafanua taarifa ya wizara.

Lengo la serikali ni kuhakikisha ifikapo 2019 na kabla ya 2020 vituo vyote vya afya vinavyomilikiwa na serikali vinakuwa na watumishi maalum wa kutoa huduma ya dawa ya usingizi kwaajili ya wapasuaji wasiopungua wawili kwa kila kituo.

Mafunzo hayo ya mwaka mmoja ni mpito wakati serikali ikiendelea kukamilisha taratibu za kurasimisha utoaji wa shahada ya kwanza ya kutoa dawa ya usingizi katika Chuo cha MUHAS katka mwaka huu wa 2018/2019.

Hali halisi ya huduma ya dawa za usingizi nchini
Takwimu za wizara ya Afya zinaonyesha kuwa kuna upungufu mkubwa wa madaktari wenye utaalamu wa kutoa dawa ya usingizi hasa wakati wa huduma ya upasuaji ambapo kwa sasa waliopo ni asilimia 1.2 tu ya mahitaji yote.

Ili kuweza kukidhi mahitaji yote ya huduma hiyo wanahitajika madaktari 2000, lakini waliopo sasa ni madaktari 30 pekee.

Kufuatia changamoto hiyo Januari 31, mwaka huu wadau mbalimbali wa afya na elimu walikutana na kujadili namna ya kuondoa changamoto hiyo na kupendekeza mtaala utakaotumika kufundishia kozi ya Aesthesia kabla ya kuupeleka kwa Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU).

” Ni kweli kumekuwepo kwa changamoto hiyo ya watalaamu wa dawa hizo lakini sasa mpango huu ukikamilika maana yake tutaongeza idadi ya madaktari kamili maana hawa waliopo wengi ni wale ambao wamesoma kozi kwa mwaka mmoja au miwili.

” Mafunzo yakianza kutolewa hapa chuoni Muhimbili wataweza kuchukua wanafunzi 200, Bugando 50 na KCMC 50 jambo ambalo litaongeza idadi kubwa ya watalaamu ili kuweza kufikia lengo letu la kuwa na wataalamu 2000 nchi nzima,” alinukuliwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Mpoki Ulisubisya.

Continue Reading

Afya

Vyakula hivi vitakulinda dhidi ya athari za kiafya za uchafuzi wa hewa

Published

on

Tunaishi katika ulimwengu unaokabiliwa na athari kubwa za mabadiliko ya hali ya hewa. Moja ya athari hizo ni kuongezeka kwa joto na kupungua kwa mvua katika maeneo mbalimbali. Athari hizi zinagusa moja kwa moja afya ya binadamu.

Ripoti ya mabadiliko ya hali ya hewa ya mwaka 2017 imeonesha kuwa kuongezeka kwa joto kunaathiri afya ya binadamu kwa kiasi kikubwa. Ripoti hiyo inatoka kundi la vyuo mbalimbali na mashirika tofauti ya Umoja wa Mataifa inasema watu wengi wanaathirika na joto pamoja na mlo hafifu sambamba na kusambaa kwa magonjwa.

Moja ya kisababishi cha mabadiliko ya hali ya hewa ni uchafuzi wa anga. Uchafuzi wa anga ni kuchanganyika kwa hewa asili katika anga na vitu kama vile moshi, majivu, gesi za kemikali katika hali na kiwango ambacho huathiri sifa ya hewa na kusababisha madhara kwa binadamu na viumbe vingine.

Baadhi ya vitu na vitendo huathiri vibaya anga letu. Baadhi ya vitu hivyo ni kama gesi na moshi unaotoka kwenye viwanda, moshi kutoka kwenye magari, marashi, dawa ya kuuwa wadudu shambani na kadhalika.

Lakini umewahi kujiuliza kuwa aina ya chakula unachokula kinaweza kukusaidia kukabiliana na athari za kiafya zinazotokana na uchafuzi wa hewa?

Wanasayansi katika utafiti wao uliotolewa hivi karibuni, wanaeleza ulaji wa chakula cha Mediterania ( Mediterranean diet) chenye matunda mengi, mbogamboga, nafaka isiyokobolewa, samaki, maharage jamii ya soya, mafuta ya mizeituni na mayai yanaweza kuwalinda watu dhidi ya athari za afya zinazotokana na uchafuzi wa hewa.

Wanasayansi hao kutoka Shule kuu ya Udaktari ya NYU ya Marekani, walichambua data za watu takribani 550,000 wenye wastani wa umri wa miaka 62 kwa miaka zaidi ya 17 ambapo waliwapanga watu hao kwenye makundi kulingana na ulaji wao unaoendana na chakula cha Mediterania na kulinganisha na muda waliokaa kwenye hewa iliyochafuliwa.

Walibaini kuwa watu ambao walizingatia kula vyakula vilivyotajwa hapo juu walikuwa na uwezekano mkubwa wa kuepuka magonjwa na vifo vinavyotokana na uchafuzi wa hali ya hewa. Magonjwa hayo ni yale ya mfumo wa upumuaji, moyo na kansa.

                                   Vyakula  jamii ya Mediterania

Vyakula hivyo jamii ya Mediterania vina uwezo mkubwa wa kukabiliana na vimelea vya maambukizi ya magonjwa kwa mtu ambaye atazingatia kwa usahihi kutumia katika maisha yake.

Uchafuzi wa hewa unasababisha athari mbaya za kiafya kupitia hewa ukaa na mlo wa Mediterania una virutubisho muhimu kupambana na vimelea vya magonjwa,” anasema Mwandishi Mtafiti wa utafiti huo, Chris Lim wa Chuo cha NYU.

Lim anasema vyakula vya aina nyingine vinaweza kusaidia kukabiliana na athari hiyo. “Nilipoangalia kila mchanganyiko wa chakula cha Mediterania, kina matunda, mbogamboga na mafuta yanayoweza kupambana na athari za hewa chafu,” anasema.

Utafiti kuhusu ulaji kama unaweza kuzuia athari za kiafya za uchafuzi wa hewa bado haujahakikiwa na kukubalika kisayansi. Lakini utafiti huo sio wa kwanza kutafuta uhusiano wa mlo na athari za kiafya za uchafuzi wa hali ya hewa.

Wakala wa Uhifadhi wa Mazingira wa Marekani (U.S. Environmental Protection Agency (EPA)) unatafiti kama mlo unaweza kumlinda mtu dhidi ya athari za uchafuzi wa mazingira. Pia wanatafiti ili kujiridhisha kama virutubisho hivyo vinaweza kutumika badala ya dawa za kitabibu na kwa kiasi gani mtu anatakiwa apate virutubisho hivyo kumhakikishia usalama dhidi ya uchafuzi huo.

Hata hivyo, bado watu wanashauriwa kutumia zaidi matunda na mbogamboga kwenye milo yao ya kila siku ili kupata faida mbalimbali za kiafya.

Continue Reading

Afya

Ulaji mbaya wa chakula watajwa kusababisha kansa ya matiti kwa wanawake

Published

on

Thamani ya maisha haiko kwenye muonekano wa mtu na vitu vinavyomzunguka bali kwenye chakula anachokula kila siku ili kuwa na afya njema. Lakini umewahi kujiuliza, chakula kinawezaje kupunguza uwezekano wa kufa kutokana na magonjwa ikiwemo kansa?

Utafiti mpya uliofanyika huko Marekani umebaini kuwa kwa sehemu mlo kamili unaweza kupunguza hatari ya kufa kwa kansa.

Mtafiti Dk. Rowan Chlebowski wa Kituo cha Taifa cha Uuguzi cha City of Hope na wenzake walichambua takwimu za wanawake 48,000 waliosajiliwa katika mpango wa Afya ya Mwanamke unaoratibiwa katika vituo 40 nchini Marekani.

Awali wanawake wote walipata vipimo na hakuna aliyegundulika kuwa na kansa ya matiti lakini 20,000 kati yao walishauriwa kubadilisha mlo na kupunguza ulaji wa mafuta kwa asilimia 20 katika milo yao ya kila siku.

Pia waliambiwa wale zaidi matunda, mbogamboga na nafaka zisizokobolewa. Wanawake wengine hawakupewa maelekezo yoyote ya kuzingatia mlo kamili lakini walifundishwa kuhusu lishe nzuri na mlo wenye afya.

Baada ya miaka nane ya kuwafuatilia wanawake hao, watafiti hao waliangalia idadi ya kansa ambazo wanawake hao walitibiwa na zile ambazo zilisababisha vifo. Walibaini kuwa wanawake ambao walitumia kiasi kidogo cha mafuta walikuwa na hatari ndogo ya kufa kwa kansa ya matiti kwa asilimia 22, ukilinganisha na wanawake wengine.

Pia wanawake hao walipunguza kwa asilimia 24 hatari ya kufa kwa kansa zingine ikiwemo kwa 38%  magonjwa ya moyo ikilinganishwa na wanawake wa kundi ambalo walipata elimu ya mlo.

“Tunachokiona ni matokeo halisi,” anasema Dk. Chlebowski. Tafiti za awali ziliangalia madhara kabla ya uchunguzi wa kansa, lakini utafiti huu ulichambua kwa kiasi gani mlo unaweza kumuathiri mtu baada ya uchunguzi.

“Tulichobaini ni kuwa ushauri wa mlo baada ya uchunguzi wa kansa ya matiti ulikuwa muhimu kuliko kabla ya uchunguzi.”

                        Ulaji wa matunda na mboga unasaidia kupunguza hatari ya kupata kansa

Hata hivyo, utafiti huo ulibaini kuwa wanawake ambao wanazingatia kutumia kiasi kidogo cha mafuta katika maisha yao wana nafasi kubwa ya kuepuka kansa ya matiti.

Kutokana na idadi ya watu walioshirikishwa kwenye utafiti huo, Dkt. Chlebowski anasema wazo la kuhusisha mlo katika programu ya matibabu lilikuwa ni muhimu ili kupata matokeo chanya katika kukabiliana na kansa ya matiti kwa wanawake.

Watafiti hao wanaendelea na uchunguzi ili kufahamu kama ulaji wa chakula unaweza kuwa sehemu ya matibabu ya kansa ya matiti. “Inahamasisha kwasababu tunajaribu kuziba pengo kati ya mtindo wa maisha na mchakato wa kibaiolojia uliopo nyuma ya ugonjwa huo.”

 

Kansa ya matiti

Saratani ya matiti ni ugonjwa ambao huwapata wanawake na unatokana na athari za chembe ndogo ama seli kwenye matiti na matokeo yake ni kwamba hubadili mfumo wa kawaida wa kukua na kuongezeka.

Mabadiliko haya huanza polepole na yanaweza yakachukua muda mrefu hadi mtu kuweza kujua kama ana matatizo hayo. Ikiwa katika hatua hizo za mwanzo kwa kawaida huwa hakuna maumivu jambo hilo ni moja ya mambo ambayo huchangia baadhi ya wagonjwa kubaini tatizo hilo wakati tayari limekomaa.

Ni kutokana na sababu hizo, wanawake hutakiwa kuchunguza afya zao mara kwa mara kwasababu ugonjwa huweza kutibiwa kirahisi iwapo utabainika mapema.

Miongoni mwa dalili za saratani ya matiti ni uvimbe kwenye matiti ama makwapani. Titi kubadilika kiumbo, titi kutoa majimaji yaliyochanganyika na damu ama chuchu kuingia ndani.

Zipo aina mbalimbali za tiba na mojawapo ni upasuaji. Upasuaji huu kwa kawaida hufanywa katika hatua za mwanzo. Njia nyingine ni tiba ya mionzi au kupewa dawa. Jambo la kukumbukwa ni kwamba ugonjwa huu unaweza kusababisha kifo iwapo hautabainika mapema na kupatiwa tiba mwafaka.

Njia ambayo mtu aweza kujilinda asiathirike na saratani hii ya matiti ni kujichunguza mara kwa mara ili kubaini mapema na kupatiwa dawa.

Mwanamke anapaswa kuchunguzwa mara moja kwa mwaka ili kuona kama ameathirika na ugonjwa huo au la.

Continue Reading

Muhimu Kusoma

Copyright © 2020 FikraPevu.com