Connect with us

Siasa

Mzimu wa Richmond waendelea kuliumiza taifa

Published

on

KASHFA ya Richmond-Dowans haionyeshi dalili zozote za kumalizika wakati kampuni ya kimarekani (Symbion Power) imeanza kuzalisha umeme.

Sehemu kubwa ya Tanzania inajitahidi kukabiliana na mgawo wa umeme unaochukua hata saa 16 kwa siku wakati serikali inajaribu kutatua mkanganyiko huo uliotokana na kashfa hiyo ya kuingizwa kwa mitambo ya umeme ya Richmond kwa ‘bei mbaya.’

Kampuni ya nishati ya Marekani, Symbion Power sasa imenunua mitambo hiyo ambayo imekuwa haifanyi kazi tangu Agosti 2008. Kiwango chake cha juu za uzalishaji ni megawati 120 na Tanzania inahitaji kiasi cha megawati 350.

Watanzania wanashuku sababu za kuwepo kwa mgawo wa umeme na hawaamini kwa haraka maelezo ya serikali kuwa chanzo ni kukarabati mashine katika mitambo ya umeme inayomilikiwa na kampuni ya Songas, hasa kwa sababu kina cha maji ni kikubwa katika uzalishaji wa umeme kwa maanguko ya maji.

Symbion Power haikueleza ni kiasi gani italipa kwa kununua mitambo hiyo iliyopo Ubungo lakini wataalamu katika sekta ya nishati wanasema ni kiasi cha dola za Marekani milioni 70.

Symbion tayari imekuwepo nchini iliweka miundombinu ya kusambaza umeme, sehemu kubwa ikilipiewa na Millenium Challenge Corporation ya Marekani.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Symbion, Paul Hinks, alisema majadiliano na Dowans yalikuwa na changamoto nyingi, akakubali kuwa taarifa za awali zilifanya Symbion ifanye ukaguzi wa kina kabla ya kuendelea na mpango huo.

Balozi wa zamani wa Marekani Joseph Wilson ambaye, pamoja na mkewe, ofisa wa zamani wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA). Valerie Palme Wilson, anaonyeshwa katika filamu ya Hollywood katika ushindani kisiasa na aliyekuwa Makamu wa Rais wa Marekani, Dick Cheney, analeta ushupavu kiasi chake kama mwenyekiti wa Symbion Power Africa.

Wilson pia ni mkurugenzi wa Jarch Capital,, ambao hivi sasa iko katika shughuli pevu ya kununua maeneo makubwa ya ardhi nchini Sudan Kusini.

Vyanzo vya habari vinasema shirika la umeme nchini, Tanesco ilitaka kununua mitambo hiyo lakini serikali ikaikatalia kwa sababu ambazo bado hazijaelezwa.

Balozi wa Marekani nchini, Meja Jenerali Mstaafu Alfonso E. Lenhardt, alibariki mpango huo. Symbion imetoa taarifa kuwa mtambo huo uko katika hali nzuri, licha ya kuwa hautumiki kwa muda mrefu, na imekubali kutoa umeme wa bure kwa Tanesco wakati inaendelea na zoezi la kuanza tena kuitumia na kuunganisha na gridi ya taifa.

Tanesco katika hali ya kutatanisha ilifikia mkataba wa kutoa umeme wa dharura na Richmond (Development Company) mwaka 2006 baada ya ukame kusababisha upungufu mkubwa wa umeme wa maji.

Baadae Richmond ikaonekana haiwezi kuleta umeme, hivyo ikatoa mkataba huo kwa Dowans Holdings kwa ushawishi wa mawaziri. Richmond ikauza hisa zake (katika mradi huo) kwa Dowans, ambaye mwenye hisa wake mkuu ni raia wa Oman, Brigedia Jenerali Mstaafu Sulaiman Mohamed Yahya al-Adawi.

Waziri Mkuu Edward Lowassa na mawaziri wawili walijiuzulu Januari 2008 kutokana na kufichuliwa kwa uhusika wao katika kufikia mkataba huo, baada ya uchunguzi wa Kamati ya Bunge.

Richmond ilipata kandarasi hiyo katika ushindani na makampuni ya umeme yenye hadhi, licha ya kutokuwa na usajili kamili kama biashara au kuwa na ujuzi wowote katika uzalishaji umeme.

Uchunguzi wa Bunge ulifikia tamati kuwa Richmond ilipewa kandarasi hiyo kutokana na upendeleo wa nguvu wa viongozi waandamizi serikalini.

HAKUNA MASHITAKA

Baada ya Symbion kuafiki kuanza kuwasha mitambo hiyo, maswali bado yanaulizwa kwanini ni machache sana kati ya mapendekezo 23 ya Kamati Teule ya Bunge kuhusu suala la Richmond, yaliyopitishwa na Bunge, yametekelezwa.

Mapendekezo hayo ni pamoja na kutaka serikali kupitia upya mikataba kati ya Tanesco na Richmond-Dowans, Independent Power (T) Ltd, Alstom Power Rentals, Songas na Agrekko.

Pia ilipendekeza kufikishwa mahakamani kwa Richmond na wamiliki wake kwa kuiibia serikali.

Hakuna kati yao, akiwemo Naeem Gire, aliyetia saini mkataba na Tanesco, aliyeshtakiwa. Ripoti ya Kamati Teule iliainisha kuwa Tanesco inawajibika kwa mikataba yake na makampuni ya kufua umeme kulipia gharama za matengenezo, ubadilishaji vifaa, bima, kodi, huduma za kisheria na zaidi, iwe wanatoa umeme kwa gridi ya taifa au la.

Hali hii inaigharimu Tanesco dola milioni 1.3 kwa kampuni kwa mwezi, kwa mujibu wa ripoti hiyo.

Vyazo vya habari ndani ya Chama Cha Mapinduzi vinasema kuwa licha ya kuwa ripoti hiyo ilikuwa ilishtua wengi, haikuivuruga CCM mradi Rais alikuwepo kuzuia kukinga kwa ufuatiliji kiutendaji, na kuzuia mashtaka yoyote.

Hata hivyo uchunguzi huo haukuwa umefurahisha hata kidogo uongozi wa CCM, na minong’ono ikaanza kuhusu nia halisi za wachunguzi Kamati Teule ya Bunge.

Wakasema kuwa Spika, Samuel John Sitta, na mwenyekiti wa Kamati Teule Harrison Mwakyembe walikuwa na nia ya kuanzisha chama kipya cha siasa na kuisuka taarifa ya uchunguzi kuendana na malengo yao hayo.

Wote wawili hata hivyo bado wako CCM. Sitta na Mwakyembe walifikiria kubadilisha utii wao kisiasa lakini iwe ni baada ya viongozi wa CCM, akiwemo Rais Jakaya Kikwete, kujaribu kuwaadhibu kwa kuruhusu uchunguzi huo ufanyike.

Ripoti pia ilipendekeza kusimamisha mkataba na Dowans. Hiyo ilifanyika Agosti 2008 lakini mzozo huo ukatinga baraza la usuluhisho la International Chamber of Commerce, ambako uamuzi wake ulikwenda kwa Dowans mwezi Novemba 2010 na serikiri ikaamriwa kulipa dola milioni 65 kwa kuvunja mkataba.

Kwa vile uamuzi wa ICC umeandikishwa rasmi nchini, Bunge haliwezi kujadili suala hilo. Mlango uko wazi, kwa wahusika wakuu wa mkasa wa Richmond-Dowans kutoka katika sakata hilo wakiwa wamelipwa ipasavyo na kuridhika, na kwa serikali kujitahidi kuondokana na jinamizi hilo.

Mweka Hazina wa zamani wa CCM na rafiki wa miaka mingi wa Rais Kikwete, Rostam Abdulrasul Aziz, anaaminika alikuwa ndiye mfadhili mmiliki wa Richmond, lakini hakuna uhakika ana hisa gani katika Dowans.

Al Adawi alisema mwezi Februari kuwa Aziz hakuwa mmoja wa wenye hisa na kuwa Al Adawi alimpa mamlaka ya uwakili mwaka 2005 kufuatilia suala hilo kwa niaba ya Dowans kwa sababu ‘ni rafiki yake wa miaka mingi na ana nguvu kuwakilisha kampuni yangu.’

Licha ya upinzani kuzuka karibu kila mahali, serikali italipa fidia ya Dowans, kwa mujibu wa vyanzo ndani ya CCM, ikitumia hukumu ya ICC kudai kuwa hakuna njia nyingine iliyobaki.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa serikali, Ludovick Utouh, aliwaambia waandishi wa habari kuwa serikali ichukue jukumu la kulipa ‘baada ya kuingilia mkataba wa Tanesco na masharti yake.’

Migongano kati ya uongozi wa CCM na Sitta na Mwakyembe inaendelea.

Vyanzo vyetu ndani ya CCM vinasisitiza kuwa viongozi hao wawili walivunja maadili kwa kusimamia mashirika ya kitaifa dhidi ya makampuni binafsi ambayo yameisaidia CCM kifedha na hawawezi kutazamia fadhila wakati wamejaribu kuua bata anayetaga yai la dhahabu.

Kuna hisia kuwa sehemu ya pesa ya malipo kutokana na hukumu ya ICC itaingia katika makasha ya CCM kujazia gharama za kampeni za uchaguzi mkuu 2015.

Madai kama hayo kuhusu kampeni ya CCM ya uchaguzi mkuu 2005 katika uporaji wa dola milioni 116 kutoka akaunti ya madeni sugu ya nje, kashfa kubwa iliyotengezwa Benki Kuu.

Jina la Rostam Aziz (aliyekuwa mbunge wa Igunga na aliyejiuzulu ubunge hivi karibuni) pia liliibuka katika sakata hilo. TANESCO na wabunge wanaoitetea wanaamini kuwa imetumiwa tu katika mkabala wa kisiasa na kuwa vitendo vyote ambavyo imekuwa ikilaumiwa vinatokana na amri zilizotoka moja kwa moja kwenye Baraza la Mawaziri.

Continue Reading
1 Comment

1 Comment

  1. Chriss

    25/08/2011 at 12:03 pm

    Kikombe cha Richmond-Dowans hakiwaepuki CCM, serikali na walio na madaraka katika ngazi zote za Tandagiza (Tanzania)

    Ingawa zahama ya matokeo hayo yote yanamuelemea Mtanzania maskini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Siasa

Sakata la waraka wa Maaskofu KKKT lang’oka na Msajili Mambo ya Ndani

Published

on

Waziri wa Mambo ya Ndani Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Usajili wa Jumuiya za Kidini na Vyama vya Kijamii, Merlin Komba ili kupisha uchunguzi wa barua iliyoandikwa ukilitaka Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kufuta waraka ilioutoa Machi mwaka huu.

Barua iisambazwa kwenye mitandao ya kijamii ikiitaka KKKT kuufuta waraka wa Pasaka uliotolewa Machi 24 mwaka huu vinginevyo hatua kali za sheria zitachukuliwa dhidi ya kanisa hilo.

Waraka huo uliopewa jina la ‘Taifa letu amani yetu’ ulisainiwa na maaskofu 27 wa kanisa hilo. Ulijikita kujadili masuala ya jamii, uchumi, siasa, katiba mpya na matukio ambayo yako kinyume na kile lilichokiita tunu na misingi ya Taifa.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Waziri Nchemba amesema Serikali haipingani na dhehebu lolote na pale ambapo kuna uhitaji wa kufanyia kazi jambo kuhusu taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo taratibu huwa zinatumika kuzungumza na sio kama ilivyofanywa taarifa hiyo inayosambaa.

“Serikali inalinda uhuru wa kuabudu na waumini hivyo huo waraka una maudhui kama matatu, ni barua batili na tunaendelea kuchunguza kama imetengenezwa basi imetengenezwaje, kwani haujapita kwetu.” amesema Waziri Mwigulu.

Kutokana na msimamo huo wa serikali, Waziri Nchemba, amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Usajili wa Jumuiya za Kidini na Vyama vya Kijamii, Merlin Komba, kupisha uchunguzi wa barua iliyoandikwa kwa maaskofu wa KKKT.

“Hivyo basi, namsimamisha Msajili wa hizo taasisi kupisha uchunguzi na ikithibitika ni za Wizara tuweze kujua maana jambo hilo halijapita kwa Waziri, Katibu Mkuu na wala si maelekezo ya serikali,” amesema.

Hata hivyo, amewatoa hofu viongozi wa dini kutokana na sakata hilo na kuwataka waendelee na majukumu yao huku ikitahadharisha jamii kuwa makini na taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

“Tunawaomba viongozi wa dini waendelee na kazi zao, nasema jamii iwe macho na taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya jamii na wasifanyie kazi taarifa hizo. Viongozi wa dini wasiwe na taharuki na taarifa hizo, hazina baraka za Serikali na wasisite kuwasiliana na Serikali kujua uhalali wake,” amesema.

Waziri Nchemba amesema waraka wa viongozi wa dini uliotolewa miezi iliyopita ni jambo lililopita na hakukuwa na haja ya kuendeleza malumbano yasiyo na tija kwenye jamii.

Katika waraka wa ujumbe wa pasaka uliosomwa katika makanisa ya Kilutheri kote nchini Tanzania na kusambaa katika mitandao ya kijamii, baraza hilo limeorodhesha mambo kadhaa ambayo wameyataja kuwa ndio tishio la umoja na amani ya nchi hiyo.

Utekwaji wa watu wa hivi karibuni, utesaji, kupotea kwa watu, mashambulizi ya silaha dhidi ya viongozi wa kisiasa, muaji yenye mwelekeo wa kiitikadi, vitisho, ubambikiziaji wa kesi, na matumizi mabaya ya vyombo vya dola dhidi ya wananchi ni baadhi tu ya mambo yaliyotajwa katika waraka huo.

Lakini pia Watanzania wamekuwa na hisia tofauti kuhusu viongozi wa dini kuzungumzia hali ya kisiasa nchini. Waraka wa KKKT ulikuja mwezi mmoja baada ya ule wa maaskofu wa kanisa katoliki ambao nao ulionya juu ya kuminywa kwa haki ya kufanya shughuli za kisiasa kama mikutano ya hadhara na maandamano.

Baada ya nyaraka hizo mbili kutolewa na Maaskofu, baadhi ya mambo yaliyokuwa yakilalamikiwa yalipata ufumbuzi ikiwemo kupungua kwa mauaji na uteswaji wa raia kulikuwa kunafanywa na watu wasiojulikana.

Continue Reading

Jamii

Waziri Mkuu Majaliwa: Hatutangazi nyongeza ya mshahara hadharani kuepusha athari kwa jamii

Published

on

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameweka wazi kuwa serikali haitatangaza nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa umma hadharani ili kuepusha athari kwa jamii ikiwemo kupanda kwa bei ya bidhaa.

Akizungumza leo Bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalumu (CHADEMA), Susan Lymo ambaye alitaka kufahamu kwanini Serikali imewanyima au imeshindwa kuwalipa watumishi wa umma nyongeza ya mishahara ambayo ni haki yao ya msingi kulingana na miaka waliyokaa kazini.

Akijibu swali la Mbunge huyo, Waziri Mkuu Majaliwa amesema Serikali ina utaratibu wa kutoa nyongeza ya mishahara kwa watumishi wake lakini haitangazi kwa wananchi wote kama ambavyo imekuwa ikifanyika kwenye sherehe za wafanyakazi za Mei Mosi kila mwaka.

Amesema Serikali ikitangaza mishahara hadharani inaweza kusababisha usumbufu kwa watu wasio watumishi wa umma na inaweza kupandisha bei ya bidhaa na kuathiri mwenendo wa mahitaji ya wananchi sokoni.

Nyongeza za mishahara ambazo zinatangazwa hadharani, mara nyingi zina athari yake sio kwamba Serikali haikusudii kutoa nyongeza ya mshahara kwa mwaka, lakini unapotumia Mei Mosi kutangaza nyongeza ya mshahara unaleta athari kwenye jamii kwasababu vitu vinaweza vikapanda bei, vikawasumbua hata na wananchi ambao hawalipwi mshahara,” amesema Waziri Mkuu.

Amebainisha kuwa siyo lazima Serikali itangaze hadharani kila inapoongeza mishahara kwa watumishi wa umma lakini ifahamike kuwa Serikali ina utaratibu wake mzuri wa kuboresha stahiki za wafanyakazi wake kila mwaka.

Suala la nyongeza ya mishahara liko Serikalini na Mhe Rais ameishawahakikishia wafanyakazi atawaongeza mishahara na sio lazima litangazwe hadharani. Mshahara ni suala la mtu binafsi hata ukiongezwa leo kuwa tumeitangaza leo tumeongeza mshahara kwa kiwango hiki. Ukifanya hivi tayari umeleta kupanda kwa gharama’” amebainisha Waziri Mkuu.

Ameongeza kuwa mkakati wa Serikali ni kupunguza gharama za mahitaji kwenye masoko ili kuzuia mfuko wa bei za bidhaa.

Hata hivyo, Waziri Mkuu Mjaliwa amesema Serikali inaendelea kufanya sensa ya watumishi wote nchi nzima na zoezi hilo likikamilika itaboresha nyongeza ya mwaka, nyongeza ya mishahara na upandishaji wa madaraja.

Awali katika swali lake, Mbunge Lyima amesema Serikali inakiuka Sheria ya Utumishi wa Umma ya kuwapatia watumishi stahiki zao na kuwapunguzia motisha ya kufanya kazi kwa ufanisi katika maeneo yao ya kazi na kuathiri mafao baada ya kustaafu.

Hoja ya Mbunge huyo ni muendelezo wa malalamiko ya watumishi dhidi ya Serikali kwamba hawajapata stahiki zao tangu ilipoanza zoezi la ukakiki wa watumishi wa umma mwaka 2015. Katika zoezi hilo watumishi zaidi ya 9,000 walibainika kutokukidhi vigezo vya utumishi na hivyo kuondolewa kazini.

Huenda kauli aliyoitoa Waziri Mkuu leo Bungeni inaweza ikatofautiana na ile ya Rais John Magufuli aliyoitoa wakati wa sherehe za Mei Mosi, 2018 mijini Iringa ambapo alinukuliwa akisema hawezi kutoa nyongeza ya mishahara akidai Serikali haina fedha.

Kwangu mimi ninafikiria hizi pesa tunazotoa kwa ajili ya elimu bure ni nzuri kuliko fedha hizo kuzipeleka kuongezea mishahara, naona bora kuwapa mikopo wanafunzi wa vyuo vikuu kuliko kuongezea wafanyakazi mishahara,

Nikisema nitaongeza hizo pesa mimi nitazitoa wapi? naogopa kusema uongo. Hata mimi napenda kupandishiwa mshahara lakini kwa hali halisi ya sasa hivi lazima niwaeleze ukweli,” alinukuliwa Rais Magufuli.

Hata hivyo alibainisha kuwa kabla ya kuondoka madarakani ataboresha maslahi ya wafanyakazi wa umma, “Nawaahidi, kipindi changu cha urais hakitaisha kabla sijapandisha mishahara kwa wafanyakazi, kupandisha kwangu haitakuwa kwa shilingi elfu kumi, itakuwa ni kupandisha kwelikwel.”

Continue Reading

Jamii

Maaskofu KKKT wapewa siku 10 kufuta waraka

Published

on

Serikali imetoa siku 10 kwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), kuufuta kwa maandishi waraka wao waliotuoa Machi 24 mwaka huu na kisha kuujulisha Umma kwa njia mbalimbali walizotumia kuusambaza.

Kanisa la KKKT kupitia Baraza lake la Maaskofu lilitoa waraka uliopewa jina la ‘Taifa Letu Amani Yetu’ wakati wa Pasaka ambao mbali na masuala ya kiroho, ulibainisha mambo kadhaa yanayogusa mstakabali wa taifa.

Katika mitandao ya kijamii leo imesambazwa barua yenye kumbukumbu no. SO.748/25 inayoonyesha imeandikwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama Wizara ya Mambo ya Ndani kwenda kwa Mwenyekiti /askofu Mkuu wa KKKT iliyoandikwa Mei 30, 2018 ikitoa maelekezo ya kufutwa waraka huo ndani ya siku 10 tangu ilipoandikwa barua hiyo.

Ikiwa na kichwa cha habari ‘Ujumbe wa Baraza la Maaskofu wa KKKT’ barua hiyo inaeleza baraza hilo halitambuliki kisheria katika ofisi ya msajili.

“Unaelekezwa kuufuta waraka husika kwa maandishi na kuujulisha umma kuwa taasisi yako haikuwa na haina uwezo kisheria kufanya kile mlichokifanya. Maandishi hayo yaufikie umma wa Watanzania kwa kupitia vyombo vya habari na njia zingine zilezile zilizotumika kuufikisha waraka ule mliouita ‘Ujumbe wa Baraza la Maaskofu KKKT’.

Hata hivyo, barua hiyo imetoa onyo kali kwa taasisi hiyo dini nchi kutekeleza agizo mara moja la sivyo itachukuliwa hatua za kisheria.

“Maelekezo haya yatekelezwe ndani ya siku kumi tangu kupokea kwa barua hii vinginevyo hatua kali zaidi za kisheria zitachukuliwa dhidi ya taasisi hii,” inasema barua hiyo.

Ikumbukwe kuwa  waraka huo ulisainiwa na maaskofu 27 wa kanisa hilo nchini na kutaja baadhi ya mambo hayo kuwa ni pamoja na utekaji, utesaji, kupotea kwa watu, mashambulizi ya silaha dhidi ya viongozi wa kisiasa, mauaji yenye mwelekeo wa kiitikadi, vitisho, ubambikiziaji wa kesi, na matumizi mabaya ya vyombo vya dola dhidi ya wananchi.ni hali ya kijamii na kiuchumi, maisha ya siasa, na masuala mtambuka likiwamo suala la Katiba Mpya.

Waraka uliongeza pia kwamba uhuru wa kujieleza, kutoa na kupokea habari umeendelea kutoweka nchini huku ukionya kubanwa na hatimaye kuelekea kupungua kwa uhuru wa Bunge, Mahakama, na Tume ya Uchaguzi, ukisema hatua hii ni pamoja na kudhoofishwa kwa serikali za Mitaa.

Lakini kabla ya KKKT kutoa waraka wao, Kanisa Katoliki nalo lilitoa waraka kama huo likionya baadhi ya mambo ikiwemo uminywaji wa misingi ya demokrasia ya vyama vingi na uhuru wa kujieleza.

Baada ya kusambaa kwa waraka huo, yalijitokeza mambo mengi ikiwemo kutofautiana na kwa mawazo ya wananchi kuhusu wajibu wa viongozi wa dini katika kutoa ushauri, kuonya au kukemea pale mambo yanapoenda mrama.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa na Maaskofu wa KKKT

Hata hivyo, barua hiyo imepokelewa kwa hisia tofauti na watumiaji wa mitandao ya kijamii ikizingatiwa kuwa suala hilo lilijadiliwa na kupita, iweje linaibuka tena wakati huu ambapo kuna utulivu na yale mambo waliyoyapigia kelele na maaskofu  yamepungua ikiwemo kuteswa, kupotea kwa watu na vitisho dhidi ya viongozi wa kisiasa.

 

Wananchi bado wanawaamini viongozi wa dini

Wadau mbalimbali wa masuala ya kijamii wamesema kama kweli barua hiyo imetolewa na serikali, inaweza kuchochea taharuki zaidi kwa waumini wa kanisa hilo na wananchi kwasababu linagusa moja kwa moja imani zao.

Amebainisha kuwa bado waumini wengi wana imani na viongozi wao dini na kwamba yale wanayotamka yanakuwa na nia njema kwa jamii yao. Na katika muktadha huo serikali inapaswa kuwa makini ili kuepusha matatizo zaidi yanayoweza kutokea.

Akizungumza na FikraPevu, Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena amesema kama serikali ilibaini kuna tatizo kwenye usajili wa Baraza la Maaskofu la KKKT ingekaa na wahusika na kulimaliza kuliko kujitokeza hadharani na kuendeleza jambo ambalo limepita.

“Mimi namwamini Mungu kuliko serikali na viongozi wangu wa dini hasa Maaskofu. Hivyo serikali inapaswa kuwa makini na mambo yanayogusa imani za watu. Katika hili walipaswa kutafakari sana jinsi ya kushughulika nalo. Vinginevyo halina afya kwa ustawi wa taifa letu,” amesema Meena.

Amesema Maaskofu walitimiza wajibu wao wa kuonya kabla mambo hayajaharibika na serikali inapaswa kuyafanyika kazi yale yalyotajwa kwenye waraka au kukaa kimya ili kuepusha migongano isiyo na faida kwa taifa.

Continue Reading

Muhimu Kusoma

Copyright © 2020 FikraPevu.com