Connect with us

Biashara/Uchumi

Polisi wapora maiti walioua kwa risasi mgodini Tarime

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Tarime na Rorya Mkoani Mara, kupitia askari wake wa FFU limelazimika kutumia nguvu pamoja na kuwatisha kwa silaha wananchi na waombolezaji wa marehemu, Mgosi Magasi Chacha (30), aliyekufa baada ya kupigwa risasi ya moto na polisi wanaolinda mgodi wa North Mara uliopo Wilayani hapa.

Published

on

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Tarime na Rorya Mkoani Mara, kupitia askari wake wa FFU limelazimika kutumia nguvu pamoja na kuwatisha kwa silaha wananchi na waombolezaji wa marehemu, Mgosi Magasi Chacha (30), aliyekufa baada ya kupigwa risasi ya moto na polisi wanaolinda mgodi wa North Mara uliopo Wilayani hapa.

Sehemu ya mgodi wa dhahabu wa North Mara, unaomilikiwa na African Barrick Golds

Katika tukio hilo la leo Jumatano saa 5:10 asubuhi, polisi wakiwa kwenye magari manne huku wakiwa wamebeba silaha ikiwamo bunduki aina ya SMG, mabomu ya machozi na marungu, waliwasili kwenye hospitali ya wilaya ya Tarime kuchukuwa mwili wa marehemu Chacha kwa nguvu ili kwenda kuuzika baada ya kuwakamata baadhi ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliokuwa katika msiba huo.

Mgodi wa North Mara unamilikiwa na kampuni kubwa ya uchimbaji madini duniani ya Barrick Gold, na umekuwa katika mgogoro na wenyeji wa eneo hilo mara kwa mara hali inayosababisha kuwapo kwa matukio yanayohatarisha amani mara kwa mara.

Wakati polisi hao wa FFU waliokuwa wametanda aneo kubwa la hospitali hiyo wakitaka kuchukua mwili wa marehemu, mamia ya wananchi, ndugu wa marehemu akiwemo mkewe (jina lake halikupatikana), pamoja na viongozi wa Chadema wilaya ya Tarime, waliwazuia polisi kuuchukuwa mwili huo, wakitaka lazima taratibu za kisheria zifuatwe na si vinginevyo.

Baada ya viongozi hao wa Chadema, wananchi, ndugu na jamaa wa marehemu Chacha kuchachamaa, mke wa marehemu alikuwa akilia kwa uchungu huku akiwa amekaa karibu na mlango wa chumba cha kuhifadhia maiti, akikataa polisi kuchukuliwa mwili wa mumewe kwenda kuuzika bila ndugu na yeye kuridhia, lakini askari kanzu mmoja wa kiume alionekana kuanza kumburuza mke huyo wa marehemu kwa lengo la kumtoa eneo hilo ili polisi wachukuwe mwili huo.

Wakati mke huyo wa marehemu akiburuzwa na mmoja wa askari polisi aliyekuwa akitii amri ya mkubwa wake wa kazi (majina hayakupatikana), mwanamke huyo alikataa katakata kuondoka, lakini polisi nao walionekana kumlazimisha hadi baadhi ya nguo zake alizokuwa amejifunga zikidondoka kisha baadhi ya maeneo ya mwili wake juu ya kiuno yakiwa yanaonekana nje, jambo ambalo lilioelezwa na walioshuhudia  kama ni udhalilishaji.

Mwandishi wa habari hizi alishuhudia vurugu hizo, baina ya polisi na ndugu wa marehemu, ambapo polisi walilazimika kuweka chemba risasi za moto katika bunduki zao za SMG, baada ya kuona wametaka kuzidiwa nguvu, ambapo waliwakamata na kuwaweka ndani mwenyekiti wa Chadema wilayani Tarime, Lucas Ngoto.

Viongozi wengine wa Chadema waliokamatwa na polisi katika tukio hilo ni, Katibu wa Chadema wilaya hiyo, Mroni Mwita pamoja na diwani wa Kata ya Sabasaba, Christopher Chometa, huku mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), wilaya ya Tarime, Chacha Heche akiponea chupuchupu kukamatwa kwa madai ya kutaka kuzuia mwili huo wa marehemu usiondolewe hospitalini hapo kwenda kuzikwa.

Marehemu Chacha mkazi wa Kijiji cha Nkende ambaye alikuwa mwendesha pikipiki wilayani Tarime, aliuawa Juni 4 mwaka huu majira ya saa 1:45 asubuhi, kwa kupigwa risasi ubavuni kisha kutokea tumboni na askari polisi wanaolinda mgodi huo wa North Mara, unaomilikiwa na kampuni ya Barrick, na kwamba jeshi la polisi Kanda maalumu ya Tarime na Rorya imethibitisha askari wake kumuua raia huyo, bila kutaja sababu ya mauaji hayo.

Hata hivyo, baada ya vuta nikuvute hiyo iliyodumu takribani dakika 45, hatimaye polisi walifanikiwa kuuchukuwa mwili huo wa marehemu Chacha na kuuondoa nao hospitalini hapo ukiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi, na kwamba magari yaliyokuwepo eneo hilo yakiwa yamesheheni askari ni PT 2036, PT 1873, PT 1863, T 754 BLF pamoja na pikipiki moja ya doria, huku gari la halmashauri ya wilaya hiyo SM 5241 ndilo lililotumika kuubeba mwili huo wa marehemu.

Taarifa ya jeshi la polisi Kanda hiyo maalumu, iliyotolewa na Kaimu Kamanda wa Kanda hiyo ya Kipolisi, Sebastian Zacharia-SSP ilieleza kwamba awali marehemu alijeruhiwa kwa risasi tumboni na askari polisi, kwa madai ya kumkata panga mguu wa kushoto mlinzi mmoja wa mgodi huo, Winchlaus Petro (26).

“Kabla mauti kumkuta alijeruhiwa kwa kupigwa risasi tumboni na askari polisi waliokuwa doria eneo hilo la mgodi. Marehemu alianza kumshambulia askari kwa panga na kuikata silaha ya askari huyo mara mbili hata baada ya kuonywa kwa kupiga risasi hewani wakati wa kukamatwa”, ilisema sehemu ya taarifa hiyo ya polisi yenye kurasa moja.

Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo ya wilaya ya Tarime, Nagga Marco ilisema, uchunguzi wake umebaini marehemu Chacha alipigwa risasi ubavuni karibu na mgongo, kisha risasi hiyo ikatokea tumboni.

Kwa upande wao familia na ndugu wa marehemu huyo, akiwemo baba yake mkubwa, Charles Matiko waliieleza FikraPevu kwamba, nguvu iliyotumiwa na polisi kuchukuwa mwili wa kijana wao ni ya kinyama, kwani familia ilikuwa haijaridhia kuchukuliwa kwa marehemu kutokana na ukweli kwamba mipango ya maziko ilikuwa haijakamilika.

Mauaji ya watu eneo hilo la mgodi wa Nyamongo, yanaelezwa kushamiri, ambapo inadaiwa mwaka jana vijana wapatao watano waliuawa kwa kupigwa risasi na polisi, Mei 7 mwaka huu kijana mwingine aliyetajwa kwa jina moja la Mwikwabe aliauawa eneo hilo la mgodi, na kwamba Juni 4 mwaka huu marehemu Chacha aliuawa pia kwa kupigwa risasi ya moto na askari polisi wanaolinda mgodi huo wa North Mara ambao unamilikiwa na kampuni ya kigeni ya Barrick.

Habari imeandaliwa na Sitta Tumma, Tarime

Continue Reading
10 Comments

10 Comments

 1. Rwahila

  06/06/2012 at 3:18 pm

  Baada ya Polisi kufanikiwa kuondoka mwili huo wa Chacha toka hospitalini, marehemu alienda kuzikwa na Jeshi la Polisi, Halmashauri, au Ndugu, jamaa na rafiki zake?

 2. Finger Pointer

  06/06/2012 at 4:32 pm

  Stori hii inajaribu kuleta karibu matatizo yanayotokana na kutoelewana kati ya wawekezaji na wananchi (mpokeaji). Sasa swala ni ambayo sijaiona ni kwani huyu kijana alipigwa risasi. Je alikuwa mhalifu? alikuwa mtetea haki ya wachache ( wanyonge)?

  • raphael

   07/06/2012 at 3:20 pm

   du, wawekezaji wanavyohusudiwa! mimi sijui

 3. MJOMBA KALOKOLA

  06/06/2012 at 8:06 pm

  Tunakoelekea ni kubaya.

  Kama polisi wanashindwa kutuliza ghasia kwa njia ambayo si ya kinyama! Mmmh…

 4. Majembe arusha

  06/06/2012 at 9:34 pm

  Cku yao itafika wala haipo mbali na mgodi watafaidi wazawa polen kwa yaliyowakuta

 5. kevoo

  06/06/2012 at 10:18 pm

  Inasikitisha sana kama wewe ni mtanzania lakini uwezi kunufaika na kile kilichopo nchini kwako, poleni sana nduguzani mliopatwa na msiba wa kijana mwenzetu, may holmight god rest his soul in coolest place Amen.

 6. Sekei

  07/06/2012 at 12:04 am

  kama tumefikia hapo…miaka michache baadae kama hatutokuwa makini na kubadilika….tanzania haitokuwa tofauti na DRC

 7. omobhulenimachaba

  07/06/2012 at 8:19 am

  Polisisiem hawa siku zao zinahesabika. Hakiyamama wakati wao utakapofika risasi zao zitageuka kuwa maji na sisi raia tutawakamata kwa mikono yetu na kuwapimia dozi yao. Kiungo kimoja kimoja cha miilini mwao kitacharangwa kwa ustadi mkubwa kabla ya kuvikusanyia katika uchanja maalum kisha kuitia kiberiti. Pambaf zao!!!!

 8. watarime

  07/06/2012 at 8:57 am

  Mtatuuwa lakini mwisho wenu unakaribia!! RIP Mgosi.

  Tunaomba mawakili wakujitolea kusaidia mjane huyu kupata haki zake.

 9. Jamlic mtua

  07/06/2012 at 10:02 am

  Hili tukio linasikitisha sana, kwa wapenda amani hii si dalili njema!!

  Mimi ninashindwa kuelewa, hizi nguvu kubwa zitaendelea kutumika mpaka lini? Serikali ina wataalam wa conflict resolution hivi kweli wanashindwa kukaa na jamii na huyu mwekazaji na kutafuta suluhisho la kudumu juu ya tatizo hili? Mimi napata wasiwasi sana juu ya amani ya sehemu husika na Tanzania kwa ujumla.

  Ninaendelea kusikitika juu ya tukio lenyewe, huyo maiti atazikwa kiserikali au amehamishiwa kwingine wakati taratibu za usalama na mazishi vikiandaliwa??

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Biashara/Uchumi

Ukosefu wa taarifa sahihi za viwango na aina ya samaki wakwamisha ujenzi wa viwanda nchini

Published

on

Tanzania itaanza kufaidika na rasilimali za bahari baada ya kuanza kutekeleza Programu ya Udhibiti na Matumizi Endelevu wa Rasilimali Samaki (EAF-Nansen) kudhibiti mabadiliko ya tabia na uchafuzi wa mazingira yanavyoathiri uzalishaji wa mazingira ya bahari na afya.

Programu ya EAF-Nansen inayofadhiliwa na Norway na kutekelezwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Mambo ya Bahari ya Norway (IMR) itasaidia kutunza mazingira na mifumo ya ikolojia kwa upande mmoja na kutatua mahitaji ya binadamu ya chakula na faida za kiuchumi.

Programu hiyo imekuja siku chache baada ya meli ya kisasa ya utafiti wa samaki na mazingira baharini yenye jina la Dkt. Fridtjof Nansen kukamilisha uchunguzi wake wa rasilimali na mazingira bahari katika maji ya Bahari ya Hindi nchini Tanzania.

Meli hiyo imebaini kuwa Tanzania ina uhaba wa taarifa sahihi za viwango na aina ya samaki, hali inayokwamisha ujenzi wa viwanda vya kusindika samaki nchini.

Chini ya Mpango wa Programu ya EAF-Nansen, meli hiyo inaendesha utafiti wake wa rasilimali bahari na mazingira baharini katika ukanda wa Kusini Mashariki mwa Afrika na Bahari ya Hindi. Nchi thelathini za Kiafrika ikiwemo Tanzania zitapata msaada wa kitaalamu na kisayansi wa namna ya kudhibiti rasilimali zao za samaki na viumbe bahari wengine kwa kutumia na kutekeleza mpango endelevu wa utunzaji wa mazingira.

Akizungumza katika hafla fupi ya kilele cha utafiti huo iliyofanyika ndani ya meli iliyotia nanga katika Bandari ya Dar es Salaam, Katibu mkuu kiongozi, Balozi John Kijazi amesema mpango huo umekuja kwa wakati muafaka kwani utachochea kasi ya uanzishwaji wa viwanda hapa nchini hususani katika sekta ya uvuvi.

Hii ni hatua kubwa sana kwa Tanzania ambayo itafaidika na huduma za utafiti wa kisasa wa meli hii kupitia ushirikiano wa wadau hapa nikizungumzia FAO na Serikali ya Norway, kuweza kujua kwa uhakika aina na kiwango cha samaki na rasilimali bahari nyingine tulizonazo katika maji yetu,” amesema Balozi Kijazi.

Amesema taarifa kuhusu rasilimali bahari yetu ni muhimu sana katika kufanya maamuzi na kupata fursa za ndani na kimataifa za uwekezaji katika sekta ya uvuvi na kutilia maanani mambo muhimu ya utunzaji wa mazingira.

Kwa kutumia taarifa sahihi tunaweza kuwavutia wawekezaji kuja na kujenga viwanda vya kusindika samaki na vingine vinavyohusiana na sekta hii ya uvuvi na hivyo kuongeza kasi kwenye mpango wetu wa kujenga Tanzania ya viwanda,” amesema Balozi Kijazi.

Kwa upande wake,Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Joelson Mpina amesema, mpango huo utaongeza ajira na matumizi ya teknolojia ya kisasa katika sekta ya uvuvi. “Hii itatuwezesha kupata wawekezaji katika eneo hili ambao watajenga viwanda vya kuchakata na kusindika mazao ya samaki ambapo mbali ya kutoa fursa za ajira kwa watu wetu hususani vijana katika mnyororo wa thamani, lakini pia utakuza mapato ya Serikali.”

Wadau wa mazingira wanasema ikiwa mpango huo utatekelezwa kikamilifu unaweza kusaidia kupunguza athari za mabadiliko ya hali ya hewa ambayo yameathiri uhai wa bahari na rasilimali zilizopo.

Mbali ya taarifa ambazo zitawezesha udhibiti bora wa rasilimali kwa matumizi endelevu, utafiti huu utapekelea uelewa mzuri wa athari za mabadiliko ya tabia nchi na athari nyingine za nje, kama vile uchafuzi wa mazingira na mifumo ya uhai baharini.,” amesema Mwakilishi wa FAO nchini Tanzania, Fred Kafeero.

Programu ya Udhibiti na Matumizi Endelevu wa Rasilimali Samaki (EAF) imekuwa ni moja ya marejeo makuu za FAO katika kusaidia nchi katika juhudi zao za kudhibiti na kutekeleza kanuni za maendeleo endelevu.

Kwa mujibu wa FAO, programu ya EAF ni njia ya kutekeleza kanuni sahihi za uvuvi kwa kutoa mwongozo wa namna ya kufikia malengo ya sera ya kiuchumi, kijamii na ikolojia kupitia malengo, viashiria na njia za tathimini. EAF inanuia kuweka uwiano kati ya mambo mawili muhimu; Utunzaji wa mazingira na mifumo ya ikolojia kwa upande mmoja na kuweza kutatua mahitaji ya binadamu ya chakula na faida za kiuchumi upande mwingine.

Uvuvi haramu bado ni changamoto

Utafiti uliotolewa hivi karibuni na Taasisi ya Overseas Development ya nchini Uingereza unaeleza tatizo la uvuvi haramu kwenye bahari kuu ikiwemo bahari ya Hindi kwamba unachochewa zaidi na ukosefu wa miundombinu ya mawasiliano, ushirikiano na teknolojia ya kutunza takwimu za meli za uvuvi kwenye bahari kuu ikiwemo bahari ya Hindi ambayo inaunganisha mataifa mbalimbali duniani.

Tatizo ni kubwa kwa nchi za Afrika ambazo hazina teknolojia ya kisasa na taasisi imara za kusimamia uvuvi ambapo kila mwaka nchi za Afrika Magharibi zinapoteza Dola bilioni 2 za kimarekani huku nchi zinazotumia bahari ya Afrika Mashariki (Kenya, Tanzania, Mauritius, the Comoros, Mozambique, and the Seychelles ) zinapoteza zaidi dola milioni 200 kila mwaka.

Licha ya kila nchi kuwa na taratibu zake katika kupambana na uvuvi haramu, hazijafanikiwa kumaliza tatizo hilo na changamoto inayojitokeza kwenye ukusanyaji wa takwimu na matumizi ya vifaa vya kusimamia mwenendo wa meli katika eneo la bahari kuu.

Utafiti huo unaeleza kuwa ili kufuatilia eneo na safari, meli zinapaswa kuwa na kifaa cha mawasiliano kijulikanacho, ‘Vessel Management Systems (VMS)’. Hata hivyo meli nyingi hazina kifaa hiki hasa katika nchi zinazoendelea ambako teknolojia hiyo haipatikani au wasimamizi wa meli huzima ili kuepuka kufuatiliwa na mamlaka husika.

Licha ya kifaa cha VMS kuwa na uwezo wa kutambua eneo, umbali na mwelekeo wa meli lakini hakiwezi kutambua meli zinazoharibu mazalia ya samaki na viumbe wengine wa baharini

Continue Reading

Biashara/Uchumi

Ushuru wa bidhaa: Kero ya Muungano iliyokosa ufumbuzi wa kudumu

Published

on

Serikali ya Tanzania Bara na ile ya Zanzibar kukutana kujadili kuhusu namna bora ya kupata ufumbuzi wa kudumu wa kero ya ulipaji kodi ya mizigo kutoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara.

Hayo yameelezwa Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Wingwi, Juma Kombo Hamad (CUF) aliyetaka kujua kama Serikali ipo tayari kuunda Kamati Ndogo ya Bunge kwa ajili ya kushughulikia mfumo wa ulipaji kodi ya mizigo kutoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara.

Katika swali la msingi, Hamad ameeleza kuwa mfumo wa ulipaji kodi wa kusafirisha bidhaa kutoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara umekuwa ukilalamikiwa kwa muda mrefu kwamba unawakwaza na kuvunja harakati za ukuaji wa sekta ya biashara Zanzibar na hivyo kusababisha uchumi wa nchi hiyo kushuka.

Akijibu swali hilo Dk. Kijaji, amesema kuwa Serikali hizo mbili zinaendelea kujadiliana ili suala hilo lipatiwe ufumbuzi wa kudumu na kuongeza kuwa Serikali hizo hazijashindwa kutatua changamoto hiyo na hakuna sababu ya kuunda kamati ya kushughulikia suala hilo.

Amesema chimbuko la malalamiko hayo linatokana na kuwepo kwa mifumo tofauti ya kutathmini bidhaa kati ya Zanzibar na Tanzania Bara hali inayosababishwa na viwango tofauti vya ushuru wa forodha vinavyopaswa kulipwa kwa bidhaa ya aina moja kutoka nje ya nchi na kusafirishwa kwenda sehemu ya pili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Dk. Kijaji amesema kuwa Mfumo wa uthaminishaji wa bidhaa zote zinazoingia Tanzania Bara unafanyika kwa kutumia mifumo ya ‘TANCIS’ na ‘Import Export Commodity Database (IECD) inayoratibiwa na kituo cha Huduma za Forodha kilichopo Dar es Salaam, lakini Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haitumii mifumo hiyo na kusababisha kuwepo na tofauti ya kodi kati ya Bara na Zanzibar.

Kutokana na utofauti wa mifumo inayotumika, bidhaa zote za nje zinazoingia Tanzania Bara kupitia Zanzibar hufanyiwa uhakiki licha ya kuwa zimethaminiwa Zanzibar, iwapo uthamini wa Tanzania Bara utakuwa sawa na ule uliofanywa Zanzibar hakuna kodi itakayotozwa Tanzania Bara na ikiwa kodi iliyolipwa Zanzibar ni ndogo, Mamlaka ya Mapato hukusanya tofauti ya kodi iliyozidi”, amesema Dk. Kijaji.

Kulingana na utaratibu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Ushuru wa bidhaa ni kodi inayotozwa kwa bidhaa au huduma maalumu zilizozalishwa ndani ya nchi au kuingizwa nchini kwa viwango tofauti. Kodi hii inatozwa katika viwango maalumu na viwango kulingana na thamani.

Dk. Kijaji amesisitiza kuwa utaratibu wa kukusanya tofauti ya kodi kati ya Zanzibar na Bara kwa kutumia mifumo ya TANCIS na IECD haina lengo la kuua biashara Zanzibar, bali hatua hiyo inalenga kuleta usawa wa gharama za kufanya biashara na ushindani hapa nchini.

Aidha Naibu Waziri huyo amesema kuwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 63 (2) Bunge ni muhimili unaojitegemea na hivyo Serikali haina mamlaka ya kuunda Kamati ndogo ya Bunge kwa ajili ya jambo hilo au jambo lolote.

Ikumbukwe kuwa kodi ya Mapato na ushuru wa bidhaa katika ya nchi hizo mbili umekuwa ni kero ya muda mrefu ya Muungano ambayo haijapatiwa ufumbuzi na kwa nyakati tofauti Wazanzibar wamekuwa wakilalamika kukosa sauti kwenye mapato wakidai hakuna usawa kwenye suala hilo.

Mwanasheria kutoka Zanzibar, Awadh Ali Said, alipokuwa anazungumzia matatizo ya Muungano katika muktadha wa mapato alinukuliwa; “suala la mapato linaanguka katika suala la uchumi huku uchumi ukiwa si suala la muungano”.

Anaongeza kwamba; “kila mmoja (kati ya Tanganyika na Zanzibar) ina uchumi wake na mzigo wa kushughulikia lakini nyenzo kuu za uchumi ambazo ni sera za fedha, sera za kodi, benki kuu, yote hayo yako upande mmoja (Tanzania Bara)”.

Kutokana na hali hiyo upande wa Zanzibar umekuwa ukilalamika kukosa nguvu ya kudhibiti uchumi na sarafu. Suala la kodi limezungumzwa kwa muda mrefu lakini mpaka sasa halijapatiwa ufumbuzi baina ya nchi hizo mbili.

Januari 4, mwaka huu, Rais wa Zanzbar, Dk. Ali Mohammed Shein wakati wa ufunguzi wa jengo la Takwimu mjini Zanzibar, alinukuliwa akisema “si busara kwa mambo ya muungano kufanywa upande mmoja tu au upande mmoja kuonekana unajivutia wenyewe kila kitu, hali hiyo inaweza kuleta madhara makubwa katika utendaji wa masuala ya muungano.”

Continue Reading

Biashara/Uchumi

Mradi wa Stiegler’s Gorge kutua mikononi mwa Kamati ya Urithi wa Dunia

Published

on

Kamati ya Urithi wa Dunia ya Umoja wa Mataifa inatarajia kuamua kama Pori la akiba la Selous liondolewe miongoni mwa maeneo ya urithi wa dunia, kufuatia Serikali ya Tanzania kuanza mchakato wa kujenga bwawa la Stiegler’s Gorge kwa ajili ya kuzalisha umeme wa kilowati 2,100 ndani ya pori hilo.

Kamati hiyo inatarajia kukutana baadaye mwezi Juni katika jiji la Manama, Bahrain na miongoni mwa ajenda zitakazojadiliwa ni uamuzi wa Serikali kujenga mradi mkubwa wa kuzalisha umeme katika pori hilo ambalo ni urithi muhimu wa dunia ambao uko hatarini kutoweka.

Kamati hiyo inakutana kila mwaka na kikao cha mwaka huu kitakuwa cha 42 tangu kuanzishwa kwake na ina kazi moja kubwa ya kujadili maendeleo ya utunzaji wa maeneo ya urithi na kufanya maamuzi ya kufuta au kuendelea kuyaweka maeneo yaliyopewa hadhi ya kuwa kwenye orodha ya Urithi wa dunia ulio katika hatari ya kutoweka.

Akizungumza hivi karibuni na jarida moja la kila wiki la Afrika Mashariki, Meneja wa Programu wa Kituo cha Urithi wa Dunia cha Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Richard Lo Giudice amesema; mradi wa uzalishaji umeme katika pori la Selous utajadiliwa kwenye mkutano wa mwaka wa Kamati ya Urithi wa Dunia na kisha UNESCO itatoa mrejesho.

Suala hilo litajadiliwa katika kikao cha 42 cha Kamati ya Urithi wa Dunia itakayoketi Manama kuanzia Juni 24 hadi Julai 4, wakati inatathmini hali ya uhifadhi wa pori la akiba la Selous,” alinukuliwa Giudice na jarida hilo.

Serikali imetenga Bilioni 700 ambayo ni sawa na asilimia 41 ya bajeti ya Wizara ya Nishati ya mwaka wa fedha wa 2018/2019 inayofikia Trilioni 1.69 kwaajili ya mradi huo, ambapo imesema ni muhimu kwa ajili ya uzalishaji wa umeme ili kuchochea ajenda ya uchumi wa viwanda.

Licha ya tahadhari iliyotolewa na wadau mbalimbali wa mazingira na wanasiasa akiwemo Mbunge wa Kigoma mjini, Zitto Kabwe na Nape Nnauye wa Mtama kuhusu athari zitakazotokea endapo mradi huo utatekelezwa, bado Serikali imeendelea kushikiria msimamo wake wa kujenga mradi huo kwa madai kuwa wanaokosoa hawaitakii nchi mema.

Serikali ilienda mbali zaidi na kutahadharisha mtu yeyote atakayejaribu kuzuia mradi huo atakabiliwa na hatua kali za kisheria ikiwemo kufungwa jela.

Piga ua, garagaza Serikali itatekeleza mradi wa Stiegler’s Gorge. Hawa wanaopinga mradi huu ukiwatazama wanataka umeme ufike vijijini mwao, ukiwatazama wengine ni wachumi wanapinga’” alinukuliwa Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Kangi Lugola wakati akijibu hoja za wabunge Mei 26 mwaka huu.

Kamati ya Urithi wa Dunia inajumuisha wawakilishi 21 ambao wanachaguliwa na Baraza la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuratibu shughuli za ulinzi wa Urithi na Utamaduni wa dunia.

“Hilo litakuwa pigo kwa asili,” limesema shirika la uhifadhi wa asili la World Wildlife Fund (WWF). Bwawa hilo litakuwa na urefu wa mita 130 na upana wa mita 700. Litatengeneza ziwa kubwa la zaidi ya kilomita 1000 za mraba, na maji yatasambaa katika eneo ambalo ni kubwa hata kushinda jiji la Berlin, Ujerumani.

 

Mambo Bayana

Kamati ya Urithi wa Dunia itakutana wakati Serikali kupitia Wakala wa Misitu Tanzania imetoa zabuni ya kukata miti isiyopungua milioni mbili katika eneo la Selous ambalo baadhi ya wabunge wamesema lina ukubwa unaolingana na jiji la Dar es Salaam.

Zabuni hiyo pia itahusisha ukataji na uuzaji wa miti hiyo ili kuiingizia Serikali mapato yatakayotumika katika huduma za kijamii.

Lakini wanaopinga mradi huo, wanaeleza kuwa miti itakayokatwa ni mingi sana na ujenzi wa bwawa hilo utasababisha athari za mazingira zinazoweza kuangamiza wanyama wengi zaidi na kuchangia ongezeko la joto duniani.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Tathmini ya Mazingira juu ya Mradi pendekezwa wa Stiegler’s Gorge iliyotolewa mwaka 2009 na Prof. Raphael Mwalyosi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam imebainisha wazi kuwa kutakuwa na athari kubwa katika eneo la Selous endapo mradi huo utatekelezwa.

Hata hivyo ripoti hiyo inaeleza kuwa mradi huo utazalisha umeme wa kutosha lakini ina mashaka juu ya matokeo ya kijamii na kiuchumi yanayoweza kupatikana.

Wachambuzi wa masuala ya mazingira, wanaeleza kuwa Tanzania ina kibarua kigumu cha kujieleza mbele ya kamati hiyo ikizingatiwa kuwa ni miongoni mwa wanachama wa kamati hiyo muhimu duniani. Nchi zingine za Afrika ambazo zinaingia katika kamati hiyo ni Burkina Faso, Tunisia, Uganda na Zimbabwe.

Kamati hiyo itakuwa na kazi ya kutathmini hali ya utunzaji wa maeneo mbalimbali yaliyoko kwenye urithi wa dunia na kuzitaka nchi wawakilishi kuchukua hatua za kutunza na kuhifadhi urithi huo ili kuhakikisha dunia inakuwa mahali salama pa kuishi.

       Baadhi ya wanyama kuathirika na mradi wa umeme

Historia ya Pori la Selous

Pori la Akiba la Selous ambalo lina eneo la kilomita 50,000 za mraba, ni moja ya mbuga kubwa zaidi barani Afrika, ambayo inajulikana kwa kupatikana kwa tembo, vifaru weusi, duma, twiga, viboko, mamba, na wanyama pori wengine.

Pia pori hilo lina aina nyingi tofauti ya viumbe wa pori, vikiwemo miombo, msitu, sehemu za nyasi, kinamasi, ikisemekana kuwa mbuga hiyo ni maabara ya mabadiliko ya kibaolojia na kiekolojia.

Uwindaji kwa ajili ya biashara unaruhusiwa katika mbuga ya Selous. Ni chanzo cha pato kwa mbuga hiyo na zaidi ya watu milioni 1.2 ambao wanaishi viungani mwa mbuga hiyo. Katika baadhi ya maeneo, uwindaji haukubaliwi kabisa. Watalii wanaweza kuzuru. Lakini kuna watalii wachache ikilinganishwa na mbuga ya kitaifa ya Serengeti, ingawa mbuga ya Selous imeizidi Serengeti mara tatu kwa ukubwa.

Mto Rufiji ni mwokozi wa mbuga hiyo. Ni mto wenye urefu wa kilomita 600 na unaishia katika Bahari ya Hindi kusini mwa Dar es Salaam, lakini maji ya mto kwa sehemu kubwa yatatumika kuzalisha umeme.

Kutokana na umuhimu wake, mwaka 1982, UNESCO lilitangaza na kuiingiza Selous miongoni wa maeneo machache ya urithi wa dunia na kuanza kuhifadhiwa.

Lakini mwaka 2014, Kamati ya Urithi wa Dunia ya UNESCO, iliyokutana mjini Doha, Qatar, iliingiza mbuga ya Hifadhi ya Wanyama ya Selous, iliyopo kusini mashariki mwa Tanzania katika orodha ya Urithi wa Dunia ulio Hatarini kutoweka, kwa sababu ya ujangili wa kupindukia.

Ujangili ulisababisha kupungua kwa idadi ya wanyamapori, hasa kwa upande wa tembo na vifaru, ambao idadi yao imepungua kwa asilimia 90 tangu 1982, wakati mbuga hiyo ilipoorodheshwa kwenye urithi wa dunia.

Continue Reading

Muhimu Kusoma

Copyright © 2020 FikraPevu.com