Connect with us

Siasa

Rais Magufuli anastahili pongezi, na kuungwa mkono

Published

on

Katika moja ya mambo ambayo huwa najiuliza na nashindwa kupata majibu kuhusu sisi watanzania ni kuwa, kama leo akija mgeni na kutuliza swali, tunataka kiongozi wa aina gani? Inawezekana tukashindwa kujibu swali hilo. Na kama tutajaribu kujibu, basi tunaweza kutoa majibu ya kitoto, ambayo muuliza swali anaweza kuishia kucheka na kutuona wajinga. Nimefikia hatua hii baada ya kujaribu kufuatilia maoni ya watanzania wenzangu kuhusu nchi yetu inavyoendeshwa.

Si muda mrefu sana umepita, tangu kelele na purukushani za uchaguzi mkuu zitawale vichwa na masikio yetu. Kila mahali ilikuwa ni kilio, kilio, kilio. Watanzania tulio wengi tulikuwa tunalalamika kuhusu uholela, ubabaishaji, upigaji dili na vingine kama hivyo ambavyo vilikuwa vimefikia hatua ya kuonekana ndio hali ya kawaida.

Uzuri ni kwamba watawala wenye akili na busara, walisikia kilio hicho na kujua watanzania tunataka nini, na Tanzania inataka nini. Yaani serikali na mtawala anaweza kuondoa hayo. Kwa kabwela kama mimi walau nilipata faraja kuona kuwa, kuna mtu mahali alisikia kilio changu, na alisikia kilio cha Tanzania, na akajitolea kukaa na kufanya kazi ya kutafuta hiyo serikali itakayoondoa kilio changu.

Kinachoonekana kwa wengi sisi makabwela ni kuwa, tangu serikali ya awamu ya tano iingie madarakani, kumekuwa na kule kujisikia ni mtanzania ambaye utu na heshima yako vimeanza kuonekana. Nina mifano mingi tu ya kutoa ambayo watanzania sasa tunaichukulia kama ni “granted”, lakini kiuhalisia imetokana na kazi.

Ni muda mrefu kulikuwa na malalamiko kuwa ukienda kuomba huduma, iwe ni hospitali, ofisi za serikali, mashirika ya umma na hata ya binafsi, matokeo yalikuwa ni kunyanyaswa, kupuuzwa na kudharauliwa. Lakini leo hata ukienda ukiwa peku na ukiwa na midabwada, unaheshimiwa na kuhudumiwa kama wakubwa. Hii ni u-turn ya karne, ambayo ilikuwa ni stahili ya vigogo tu, lakini leo sisi makabwela tunaonekana watu. Sikitarajia hili kwa muda mfupi namna hii.

Lililokuwa linakera zaidi ni kuwa, tulifika wazo hata sisi wenyewe kusema nchi yetu imekuwa shamba la bibi. Watu wanajipigia “dili” mchana kweupe na kuihujumu serikali bila hofu, na kutamba mitaani na kututukana juu. Tena na kujiita watu ndio wanaume hasa. Maliasili zetu zilikuwa zinawanufaisha wengine na sio kutunufaisha sisi, tukilalamika tulikuwa tunaonekana washamba. Ni juzi tu tumeona kazi iliyofanyika kwenye suala la usafirishaji wa mchanga. Mbali na hilo sasa sasa tunasikia kabisa wezi wanasema Magufuli amebana sama, sio rahisi tena kuwaibia watanzania kama zamani.

Nchi ilikuwa na mwelekeo wa kuwa pepo ya wauza unga na mateja, lakini sasa tunaona walau kuna watu wanafanya kazi ya kupambana na haya. Unga sasa umeanza kuogopwa. Tofauti na zamani kuwa unga ilikuwa ni sifa.

Kuna lingine ambalo sijui kama kweli tunalifuatilia au la. Muundo wa chama unabadilika, chama kinarudi mikononi mwa wananchi, kinarudi kuwa chama cha kuangalia matatizo ya mtanzania toka ngazi ya chini kabisa, na kumhudumia mwananchi. Na sio mwananchi au mwanachama kumhudumia kiongozi wake.

Haya ni machache tu ambayo nayaona na yananigusa moja kwa moja kama mtanzania wa chini, ambayo yananifanya niseme kweli kuna mtu aliyesikia kilio changu, na sasa anakifanya kazi akiniangalia mimi.

Kinachonisikitisha ni kwamba, kauli zinazotoka kwa baadhi ya watanzania wenzangu, zinasikitisha sana. Sauti hizo zimekuwa ni distraction za ajabu sana, ambazo zinawatoa watu kutoka kwenye kushughulikia mambo ya maana, na kuanza kushughulika na distractions. Hili ndio linanifanya niwe na wasiwasi na mtazamo wa baadhi ya watanzania wenzangu. Na najiuliza hivi tunachotaka watanzania ni nini? Lugha tamu za kuwafurahisha watu, wakati nchi yetu inadorora?

Kuwachekea watu wanaoleta distraction, na kukejeli serikali ambayo inaonekana wazi kabisa ina moyo wa dhati kufanya kazi kwa ajili ya Tanzania na watanzania? Sijui kama maswali haya ni magumu sana, au sijui kama neema ya siku mbili ya sisi makabwela japo kuonekana watu, inatufanya tusahau kilio cha muda mrefu.

Kwenye mkutano mkuu wa chama uliofanyika hivi karibuni, Mh Rais John Magufuli alitoa hotuba yenye akili sana. Ni bahati mbaya sana hotuba yake ni kama iligubikwa na kufunikwa na distraction za ajabu zilizokuwa zinaendelea kwenye vyombo vya habari. Mimi binafsi nilipenda sana ile hotuba, ambayo kwa maoni yangu binafsi ilistahili kuwa “state of the union address”, ichambuliwe na kujadiliwa kwa makini, ili na sisi kama watanzania tushiriki kwenye yale yaliyosemwa.

Mbali na mambo ya mageuzi ndani ya chama, Mh Rais alisema tatizo kubwa la Tanzania na mtanzania ni umaskini. Tunaweza kusema mengine yote, na kuweka porojo nyingi au kupiga siasa nyingi, lakini ukweli ambao kila mtanzania anauona ni kwamba, tatizo kubwa la Tanzania ni umaskini. Kama chama, serikali, na viongozi wanatambua, wanataja bila kuogopa kuwa hilo ndio tatizo, basi bila shaka wanajua kazi iko wapi.

Binafsi naona kujipanga kwa dhati kwa chama na serikali, ili kutoa leadership kwa Tanzania ya sasa. Kweli hii nchi bila kazi haiwezi kwenda popote, ni kuongopeana tu. Sioni kama tutakuwa na busara, kama tutawasumbua viongozi wetu kwa mambo ya kitoto, wakati kuna mengi makubwa ya kuhangaika nayo ili tuishi maisha bora na ya staha.  Kuitukana serikali, kumkejeli Rais na serikali yake, na hata kuwatweza viongozi wetu, sidhani kama kunaweza kusaidia kuondoa matatizo yetu.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Siasa

Sakata la waraka wa Maaskofu KKKT lang’oka na Msajili Mambo ya Ndani

Published

on

Waziri wa Mambo ya Ndani Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Usajili wa Jumuiya za Kidini na Vyama vya Kijamii, Merlin Komba ili kupisha uchunguzi wa barua iliyoandikwa ukilitaka Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kufuta waraka ilioutoa Machi mwaka huu.

Barua iisambazwa kwenye mitandao ya kijamii ikiitaka KKKT kuufuta waraka wa Pasaka uliotolewa Machi 24 mwaka huu vinginevyo hatua kali za sheria zitachukuliwa dhidi ya kanisa hilo.

Waraka huo uliopewa jina la ‘Taifa letu amani yetu’ ulisainiwa na maaskofu 27 wa kanisa hilo. Ulijikita kujadili masuala ya jamii, uchumi, siasa, katiba mpya na matukio ambayo yako kinyume na kile lilichokiita tunu na misingi ya Taifa.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Waziri Nchemba amesema Serikali haipingani na dhehebu lolote na pale ambapo kuna uhitaji wa kufanyia kazi jambo kuhusu taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo taratibu huwa zinatumika kuzungumza na sio kama ilivyofanywa taarifa hiyo inayosambaa.

“Serikali inalinda uhuru wa kuabudu na waumini hivyo huo waraka una maudhui kama matatu, ni barua batili na tunaendelea kuchunguza kama imetengenezwa basi imetengenezwaje, kwani haujapita kwetu.” amesema Waziri Mwigulu.

Kutokana na msimamo huo wa serikali, Waziri Nchemba, amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Usajili wa Jumuiya za Kidini na Vyama vya Kijamii, Merlin Komba, kupisha uchunguzi wa barua iliyoandikwa kwa maaskofu wa KKKT.

“Hivyo basi, namsimamisha Msajili wa hizo taasisi kupisha uchunguzi na ikithibitika ni za Wizara tuweze kujua maana jambo hilo halijapita kwa Waziri, Katibu Mkuu na wala si maelekezo ya serikali,” amesema.

Hata hivyo, amewatoa hofu viongozi wa dini kutokana na sakata hilo na kuwataka waendelee na majukumu yao huku ikitahadharisha jamii kuwa makini na taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

“Tunawaomba viongozi wa dini waendelee na kazi zao, nasema jamii iwe macho na taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya jamii na wasifanyie kazi taarifa hizo. Viongozi wa dini wasiwe na taharuki na taarifa hizo, hazina baraka za Serikali na wasisite kuwasiliana na Serikali kujua uhalali wake,” amesema.

Waziri Nchemba amesema waraka wa viongozi wa dini uliotolewa miezi iliyopita ni jambo lililopita na hakukuwa na haja ya kuendeleza malumbano yasiyo na tija kwenye jamii.

Katika waraka wa ujumbe wa pasaka uliosomwa katika makanisa ya Kilutheri kote nchini Tanzania na kusambaa katika mitandao ya kijamii, baraza hilo limeorodhesha mambo kadhaa ambayo wameyataja kuwa ndio tishio la umoja na amani ya nchi hiyo.

Utekwaji wa watu wa hivi karibuni, utesaji, kupotea kwa watu, mashambulizi ya silaha dhidi ya viongozi wa kisiasa, muaji yenye mwelekeo wa kiitikadi, vitisho, ubambikiziaji wa kesi, na matumizi mabaya ya vyombo vya dola dhidi ya wananchi ni baadhi tu ya mambo yaliyotajwa katika waraka huo.

Lakini pia Watanzania wamekuwa na hisia tofauti kuhusu viongozi wa dini kuzungumzia hali ya kisiasa nchini. Waraka wa KKKT ulikuja mwezi mmoja baada ya ule wa maaskofu wa kanisa katoliki ambao nao ulionya juu ya kuminywa kwa haki ya kufanya shughuli za kisiasa kama mikutano ya hadhara na maandamano.

Baada ya nyaraka hizo mbili kutolewa na Maaskofu, baadhi ya mambo yaliyokuwa yakilalamikiwa yalipata ufumbuzi ikiwemo kupungua kwa mauaji na uteswaji wa raia kulikuwa kunafanywa na watu wasiojulikana.

Continue Reading

Jamii

Waziri Mkuu Majaliwa: Hatutangazi nyongeza ya mshahara hadharani kuepusha athari kwa jamii

Published

on

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameweka wazi kuwa serikali haitatangaza nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa umma hadharani ili kuepusha athari kwa jamii ikiwemo kupanda kwa bei ya bidhaa.

Akizungumza leo Bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalumu (CHADEMA), Susan Lymo ambaye alitaka kufahamu kwanini Serikali imewanyima au imeshindwa kuwalipa watumishi wa umma nyongeza ya mishahara ambayo ni haki yao ya msingi kulingana na miaka waliyokaa kazini.

Akijibu swali la Mbunge huyo, Waziri Mkuu Majaliwa amesema Serikali ina utaratibu wa kutoa nyongeza ya mishahara kwa watumishi wake lakini haitangazi kwa wananchi wote kama ambavyo imekuwa ikifanyika kwenye sherehe za wafanyakazi za Mei Mosi kila mwaka.

Amesema Serikali ikitangaza mishahara hadharani inaweza kusababisha usumbufu kwa watu wasio watumishi wa umma na inaweza kupandisha bei ya bidhaa na kuathiri mwenendo wa mahitaji ya wananchi sokoni.

Nyongeza za mishahara ambazo zinatangazwa hadharani, mara nyingi zina athari yake sio kwamba Serikali haikusudii kutoa nyongeza ya mshahara kwa mwaka, lakini unapotumia Mei Mosi kutangaza nyongeza ya mshahara unaleta athari kwenye jamii kwasababu vitu vinaweza vikapanda bei, vikawasumbua hata na wananchi ambao hawalipwi mshahara,” amesema Waziri Mkuu.

Amebainisha kuwa siyo lazima Serikali itangaze hadharani kila inapoongeza mishahara kwa watumishi wa umma lakini ifahamike kuwa Serikali ina utaratibu wake mzuri wa kuboresha stahiki za wafanyakazi wake kila mwaka.

Suala la nyongeza ya mishahara liko Serikalini na Mhe Rais ameishawahakikishia wafanyakazi atawaongeza mishahara na sio lazima litangazwe hadharani. Mshahara ni suala la mtu binafsi hata ukiongezwa leo kuwa tumeitangaza leo tumeongeza mshahara kwa kiwango hiki. Ukifanya hivi tayari umeleta kupanda kwa gharama’” amebainisha Waziri Mkuu.

Ameongeza kuwa mkakati wa Serikali ni kupunguza gharama za mahitaji kwenye masoko ili kuzuia mfuko wa bei za bidhaa.

Hata hivyo, Waziri Mkuu Mjaliwa amesema Serikali inaendelea kufanya sensa ya watumishi wote nchi nzima na zoezi hilo likikamilika itaboresha nyongeza ya mwaka, nyongeza ya mishahara na upandishaji wa madaraja.

Awali katika swali lake, Mbunge Lyima amesema Serikali inakiuka Sheria ya Utumishi wa Umma ya kuwapatia watumishi stahiki zao na kuwapunguzia motisha ya kufanya kazi kwa ufanisi katika maeneo yao ya kazi na kuathiri mafao baada ya kustaafu.

Hoja ya Mbunge huyo ni muendelezo wa malalamiko ya watumishi dhidi ya Serikali kwamba hawajapata stahiki zao tangu ilipoanza zoezi la ukakiki wa watumishi wa umma mwaka 2015. Katika zoezi hilo watumishi zaidi ya 9,000 walibainika kutokukidhi vigezo vya utumishi na hivyo kuondolewa kazini.

Huenda kauli aliyoitoa Waziri Mkuu leo Bungeni inaweza ikatofautiana na ile ya Rais John Magufuli aliyoitoa wakati wa sherehe za Mei Mosi, 2018 mijini Iringa ambapo alinukuliwa akisema hawezi kutoa nyongeza ya mishahara akidai Serikali haina fedha.

Kwangu mimi ninafikiria hizi pesa tunazotoa kwa ajili ya elimu bure ni nzuri kuliko fedha hizo kuzipeleka kuongezea mishahara, naona bora kuwapa mikopo wanafunzi wa vyuo vikuu kuliko kuongezea wafanyakazi mishahara,

Nikisema nitaongeza hizo pesa mimi nitazitoa wapi? naogopa kusema uongo. Hata mimi napenda kupandishiwa mshahara lakini kwa hali halisi ya sasa hivi lazima niwaeleze ukweli,” alinukuliwa Rais Magufuli.

Hata hivyo alibainisha kuwa kabla ya kuondoka madarakani ataboresha maslahi ya wafanyakazi wa umma, “Nawaahidi, kipindi changu cha urais hakitaisha kabla sijapandisha mishahara kwa wafanyakazi, kupandisha kwangu haitakuwa kwa shilingi elfu kumi, itakuwa ni kupandisha kwelikwel.”

Continue Reading

Jamii

Maaskofu KKKT wapewa siku 10 kufuta waraka

Published

on

Serikali imetoa siku 10 kwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), kuufuta kwa maandishi waraka wao waliotuoa Machi 24 mwaka huu na kisha kuujulisha Umma kwa njia mbalimbali walizotumia kuusambaza.

Kanisa la KKKT kupitia Baraza lake la Maaskofu lilitoa waraka uliopewa jina la ‘Taifa Letu Amani Yetu’ wakati wa Pasaka ambao mbali na masuala ya kiroho, ulibainisha mambo kadhaa yanayogusa mstakabali wa taifa.

Katika mitandao ya kijamii leo imesambazwa barua yenye kumbukumbu no. SO.748/25 inayoonyesha imeandikwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama Wizara ya Mambo ya Ndani kwenda kwa Mwenyekiti /askofu Mkuu wa KKKT iliyoandikwa Mei 30, 2018 ikitoa maelekezo ya kufutwa waraka huo ndani ya siku 10 tangu ilipoandikwa barua hiyo.

Ikiwa na kichwa cha habari ‘Ujumbe wa Baraza la Maaskofu wa KKKT’ barua hiyo inaeleza baraza hilo halitambuliki kisheria katika ofisi ya msajili.

“Unaelekezwa kuufuta waraka husika kwa maandishi na kuujulisha umma kuwa taasisi yako haikuwa na haina uwezo kisheria kufanya kile mlichokifanya. Maandishi hayo yaufikie umma wa Watanzania kwa kupitia vyombo vya habari na njia zingine zilezile zilizotumika kuufikisha waraka ule mliouita ‘Ujumbe wa Baraza la Maaskofu KKKT’.

Hata hivyo, barua hiyo imetoa onyo kali kwa taasisi hiyo dini nchi kutekeleza agizo mara moja la sivyo itachukuliwa hatua za kisheria.

“Maelekezo haya yatekelezwe ndani ya siku kumi tangu kupokea kwa barua hii vinginevyo hatua kali zaidi za kisheria zitachukuliwa dhidi ya taasisi hii,” inasema barua hiyo.

Ikumbukwe kuwa  waraka huo ulisainiwa na maaskofu 27 wa kanisa hilo nchini na kutaja baadhi ya mambo hayo kuwa ni pamoja na utekaji, utesaji, kupotea kwa watu, mashambulizi ya silaha dhidi ya viongozi wa kisiasa, mauaji yenye mwelekeo wa kiitikadi, vitisho, ubambikiziaji wa kesi, na matumizi mabaya ya vyombo vya dola dhidi ya wananchi.ni hali ya kijamii na kiuchumi, maisha ya siasa, na masuala mtambuka likiwamo suala la Katiba Mpya.

Waraka uliongeza pia kwamba uhuru wa kujieleza, kutoa na kupokea habari umeendelea kutoweka nchini huku ukionya kubanwa na hatimaye kuelekea kupungua kwa uhuru wa Bunge, Mahakama, na Tume ya Uchaguzi, ukisema hatua hii ni pamoja na kudhoofishwa kwa serikali za Mitaa.

Lakini kabla ya KKKT kutoa waraka wao, Kanisa Katoliki nalo lilitoa waraka kama huo likionya baadhi ya mambo ikiwemo uminywaji wa misingi ya demokrasia ya vyama vingi na uhuru wa kujieleza.

Baada ya kusambaa kwa waraka huo, yalijitokeza mambo mengi ikiwemo kutofautiana na kwa mawazo ya wananchi kuhusu wajibu wa viongozi wa dini katika kutoa ushauri, kuonya au kukemea pale mambo yanapoenda mrama.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa na Maaskofu wa KKKT

Hata hivyo, barua hiyo imepokelewa kwa hisia tofauti na watumiaji wa mitandao ya kijamii ikizingatiwa kuwa suala hilo lilijadiliwa na kupita, iweje linaibuka tena wakati huu ambapo kuna utulivu na yale mambo waliyoyapigia kelele na maaskofu  yamepungua ikiwemo kuteswa, kupotea kwa watu na vitisho dhidi ya viongozi wa kisiasa.

 

Wananchi bado wanawaamini viongozi wa dini

Wadau mbalimbali wa masuala ya kijamii wamesema kama kweli barua hiyo imetolewa na serikali, inaweza kuchochea taharuki zaidi kwa waumini wa kanisa hilo na wananchi kwasababu linagusa moja kwa moja imani zao.

Amebainisha kuwa bado waumini wengi wana imani na viongozi wao dini na kwamba yale wanayotamka yanakuwa na nia njema kwa jamii yao. Na katika muktadha huo serikali inapaswa kuwa makini ili kuepusha matatizo zaidi yanayoweza kutokea.

Akizungumza na FikraPevu, Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena amesema kama serikali ilibaini kuna tatizo kwenye usajili wa Baraza la Maaskofu la KKKT ingekaa na wahusika na kulimaliza kuliko kujitokeza hadharani na kuendeleza jambo ambalo limepita.

“Mimi namwamini Mungu kuliko serikali na viongozi wangu wa dini hasa Maaskofu. Hivyo serikali inapaswa kuwa makini na mambo yanayogusa imani za watu. Katika hili walipaswa kutafakari sana jinsi ya kushughulika nalo. Vinginevyo halina afya kwa ustawi wa taifa letu,” amesema Meena.

Amesema Maaskofu walitimiza wajibu wao wa kuonya kabla mambo hayajaharibika na serikali inapaswa kuyafanyika kazi yale yalyotajwa kwenye waraka au kukaa kimya ili kuepusha migongano isiyo na faida kwa taifa.

Continue Reading

Muhimu Kusoma

Copyright © 2020 FikraPevu.com