Connect with us

Siasa

Siku za Trump zahesabika kabla ya kushitakiwa. Ni kuhusu kashfa ya Russiagate

Published

on

UPO uwezekano mkubwa kwa Rais wa Marekani, Donald Trump, kuondolewa madarakani wakati wowote kuanzia sasa.

Trump (70) anaweza kuondolewa na bunge baada kuibuka dalili za wawakilishi wa wananchi kuanza mchakato wa kumuondoa.

Sababu kubwa inayotajwa na wachambuzi wa siasa na wanazuoni wa taifa hilo tajiri, ni “kupata ushindi kwa kuhusisha taifa la nje kwenye siri za Marekani.”

Rais Donald Trump

Taifa linalonyooshea kidole ni Russia, ambalo kiongozi wake, Rais Vladimir Putin, anatajwa kuhusika kudukua na kusaidia, kwa njia za kijasusi, ushindi wa Trump, dhidi ya mpinzani wake mkubwa, Hillary Clinton.

Taarifa kutoka Marekani zinaeleza kuwa uthibitisho wa Russia kuingilia mchakato wa kupiga kura na hata kutangazwa matokeo ya ushindi wa Trump, umeanza kupatikana.

Kupatikana kwake kutasaidia Trump kushitakiwa na hatimaye kupokwa madaraka yake makubwa nchini Marekani.

Kutokana na kuwepo kwa dalili hizo, Trump ameimarisha “utamaduni wa timuatimua” kwa wote wanaoweza kuwa na ushahidi huo na kuwa tayari kuuanika kwa ngazi husika, kutakapoanza mchakato wa kumng’oa kwenye dhamana ya urais.

Kashfa hii ya Russia kuiingilia kijasusi Marekani katika mchakato wa kumpata kiongozi wa taifa hilo kubwa na lenye nguvu za kivita na kiuchumi duniani, imepachikwa jina na Russiagate.

Trump kama Nixon

 

Richard Nixon, Rais wa zamani wa Marekani

Kama ilivyokuwa kwa Rais wa 37 wa Marekani, Richard Nixon katika kashfa iliyomuondoa madarakani mwaka 1974 baada ya kubainika kufanya hujuma ya kutaka kubaki madarakani kwa kuiba nyaraka na “kudukua” mikakati ya mpinzani wake, George McGovern, alianza kufukuza watendaji wake wa karibu na kuwaondosha ghafla ili wasibaki na ushahidi wnye nguvu.

Rais Nixon kwanza alihakikisha anawaondoa madarakani John Dean, aliyekuwa mwanasheria wa Ikulu,  John Erlichman, mwanasheria na mshauri mahsusi kuhusu uendeshaji wa nchi, Harry Haldeman, mnadhimu mkuu wa majeshi na Chuck Colson, rafiki wa karibu wa rais aliyekuwa mshauri mkuu wa ujasusi.

Mwishoni alimuondoa kwa kumfuta kazi mtu muhimu aliyekuwa akimchunguza, wakili msomi Archibald Cox, akiamini kuwa ungekuwa mwisho wa kuchunguzwa.

Hata hivyo, haikuwa kama alivyokuwa akidhani, kwani hatua za kumuondoa Nixon madarakani ziliendelea na hatimaye kutimuliwa.

Trump katika kuhakikisha anavunjavunja ushahidi, naye ameanza kuwaondoa kwenye nyadhifa zao watendaji wa karibu, ambao ama wanafahamu au kuwa na ushahidi mkubwa juu ya kuhusika kwa Russia kwenye ushindi wake.

Tayari Rais Trump amewafukuza Roger Stone, mshauri mkuu, Carter Page, mshauri wa uhusiano wa nchi za nje na Paul Manafort, aliyekuwa meneja wa kampeni (huyu aliamua kuachia ngazi, lakini baada ya kuoneshwa dalili za kutimuliwa).  

Kana kwamba hiyo haitoshi, ili kumaliza mzizi wa fitina, Trump akamuondoa kazini Mshauri Mwandamizi wa Ulinzi, Michael Flynn na aliyekuwa akikaimu nafasi ya mwanasheria mkuu wa nchi hiyo, Sally Yates.

Baada ya kuwatimua vigogo hao, Trump akaona vyema kumuita na kuzungumza na Mkurugenzi wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI), James Comey ili “kumuweka sawa.”

Januari 27, mwaka huu, Trump alimwalika Comey Ikulu – White House, kwa chakula cha jioni na mazungumzo ya kumshawishi asichangie chochote katika mjadala wa Russiagate.

Hata hivyo, kinyume na matarajio yake, Comey alipoitwa kuhojiwa na Kamati ya Bunge, aliweka wazi kuwa shirika lake linamchunguza Trump na kwamba hataiacha kazi hiyo hadi ukweli upatikane.

Trump, kama ilivyokuwa kwa Nixon, aliamua kumuondoa madarakani kwa kuita wasaidizi wake wa karibu na kuutangazia umma kuwa amemtimua Comey.

Rais Vladimir Putin wa Russia

Kumuondoa Comey madarakani kumeamsha nia ya kuhakikisha Trump anashitakiwa na ikiwezekana, kuondolewa madarakani.

Taratibu za sheria Marekani, pamoja na kwamba haitajwi moja kwa moja katika katiba, zinakataza rais kumfukuza kazi mtu anayemchunguza.

Hatua hii hujulikana kuwa ni “kuzuia haki kutendeka” na inakatazwa na kanuni nyingi ndani ya utendaji wa dhamana za serikali, ikiwamo urais.

Wachambuzi wengi wanaamini kuwa katika hatua hii ya “fukuzafukuza,” Trump hawezi kuchomoka kuhojiwa na hatimaye kumuondoa madarakani.

Hatua za kumshitaki Rais Marekani

Pamoja na ugumu wa kufikia hatua kumshitaki Rais wa Marekani, lakini mambo muhimu huangaliwa kwa umakini mkubwa, ikiwa ni pamoja na kukusanywa kwa ushahidi usiokuwa na chembe ya shaka.

Kwanza, FBI huanza uchunguzi wanapoona kuna ukiukwaji mkubwa wa sheria na taratibu za dhamana Marekani. Miongoni mwa makosa makubwa ni wizi wa kura, kashfa za ngono, usaliti wa kiapo, rushwa na kutoa siri za Marekani.

Baadaye FBI hukabidhi ushahidi huo kwa Baraza la Wawakilishi (House of Represeantatives), ambapo wajumbe wa baraza hilo wa kamati ya sheria na haki hupiga kura.

Idadi ya wajumbe inapokuwa kubwa kuamua kumshiaki rais, basi huteua wajumbe wawili ambao humpelekea barua rasmi rais kumuita mbele ya baraza hilo ili athibitishiwe mashitaka yake na ushahidi.

Mwisho, uamuzi wa kumuondoa au kutomuondoa madarakani hupitishwa na Seneti. Ni katika eneo hili, rais anaweza kusamehewa, kupewa onyo au kuamuriwa kuomba radhi kwa wananchi wa Marekani.

Mfano mzuri wa hatua hizi ni Rais Nixon kutimuliwa na baadaye Rais Bill Clinton kusamehewa kwa kashfa ya ngono. Aliamuriwa kuomba msamaha kwa matendo yasiyofaa akiwa ndani ya Ikulu baada ya kukutwa na makosa ya kuanzisha uhusiano wa mapenzi na mtumishi wa Ikulu, Monica Lewinsky.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Siasa

Sakata la waraka wa Maaskofu KKKT lang’oka na Msajili Mambo ya Ndani

Published

on

Waziri wa Mambo ya Ndani Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Usajili wa Jumuiya za Kidini na Vyama vya Kijamii, Merlin Komba ili kupisha uchunguzi wa barua iliyoandikwa ukilitaka Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kufuta waraka ilioutoa Machi mwaka huu.

Barua iisambazwa kwenye mitandao ya kijamii ikiitaka KKKT kuufuta waraka wa Pasaka uliotolewa Machi 24 mwaka huu vinginevyo hatua kali za sheria zitachukuliwa dhidi ya kanisa hilo.

Waraka huo uliopewa jina la ‘Taifa letu amani yetu’ ulisainiwa na maaskofu 27 wa kanisa hilo. Ulijikita kujadili masuala ya jamii, uchumi, siasa, katiba mpya na matukio ambayo yako kinyume na kile lilichokiita tunu na misingi ya Taifa.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Waziri Nchemba amesema Serikali haipingani na dhehebu lolote na pale ambapo kuna uhitaji wa kufanyia kazi jambo kuhusu taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo taratibu huwa zinatumika kuzungumza na sio kama ilivyofanywa taarifa hiyo inayosambaa.

“Serikali inalinda uhuru wa kuabudu na waumini hivyo huo waraka una maudhui kama matatu, ni barua batili na tunaendelea kuchunguza kama imetengenezwa basi imetengenezwaje, kwani haujapita kwetu.” amesema Waziri Mwigulu.

Kutokana na msimamo huo wa serikali, Waziri Nchemba, amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Usajili wa Jumuiya za Kidini na Vyama vya Kijamii, Merlin Komba, kupisha uchunguzi wa barua iliyoandikwa kwa maaskofu wa KKKT.

“Hivyo basi, namsimamisha Msajili wa hizo taasisi kupisha uchunguzi na ikithibitika ni za Wizara tuweze kujua maana jambo hilo halijapita kwa Waziri, Katibu Mkuu na wala si maelekezo ya serikali,” amesema.

Hata hivyo, amewatoa hofu viongozi wa dini kutokana na sakata hilo na kuwataka waendelee na majukumu yao huku ikitahadharisha jamii kuwa makini na taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

“Tunawaomba viongozi wa dini waendelee na kazi zao, nasema jamii iwe macho na taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya jamii na wasifanyie kazi taarifa hizo. Viongozi wa dini wasiwe na taharuki na taarifa hizo, hazina baraka za Serikali na wasisite kuwasiliana na Serikali kujua uhalali wake,” amesema.

Waziri Nchemba amesema waraka wa viongozi wa dini uliotolewa miezi iliyopita ni jambo lililopita na hakukuwa na haja ya kuendeleza malumbano yasiyo na tija kwenye jamii.

Katika waraka wa ujumbe wa pasaka uliosomwa katika makanisa ya Kilutheri kote nchini Tanzania na kusambaa katika mitandao ya kijamii, baraza hilo limeorodhesha mambo kadhaa ambayo wameyataja kuwa ndio tishio la umoja na amani ya nchi hiyo.

Utekwaji wa watu wa hivi karibuni, utesaji, kupotea kwa watu, mashambulizi ya silaha dhidi ya viongozi wa kisiasa, muaji yenye mwelekeo wa kiitikadi, vitisho, ubambikiziaji wa kesi, na matumizi mabaya ya vyombo vya dola dhidi ya wananchi ni baadhi tu ya mambo yaliyotajwa katika waraka huo.

Lakini pia Watanzania wamekuwa na hisia tofauti kuhusu viongozi wa dini kuzungumzia hali ya kisiasa nchini. Waraka wa KKKT ulikuja mwezi mmoja baada ya ule wa maaskofu wa kanisa katoliki ambao nao ulionya juu ya kuminywa kwa haki ya kufanya shughuli za kisiasa kama mikutano ya hadhara na maandamano.

Baada ya nyaraka hizo mbili kutolewa na Maaskofu, baadhi ya mambo yaliyokuwa yakilalamikiwa yalipata ufumbuzi ikiwemo kupungua kwa mauaji na uteswaji wa raia kulikuwa kunafanywa na watu wasiojulikana.

Continue Reading

Jamii

Waziri Mkuu Majaliwa: Hatutangazi nyongeza ya mshahara hadharani kuepusha athari kwa jamii

Published

on

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameweka wazi kuwa serikali haitatangaza nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa umma hadharani ili kuepusha athari kwa jamii ikiwemo kupanda kwa bei ya bidhaa.

Akizungumza leo Bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalumu (CHADEMA), Susan Lymo ambaye alitaka kufahamu kwanini Serikali imewanyima au imeshindwa kuwalipa watumishi wa umma nyongeza ya mishahara ambayo ni haki yao ya msingi kulingana na miaka waliyokaa kazini.

Akijibu swali la Mbunge huyo, Waziri Mkuu Majaliwa amesema Serikali ina utaratibu wa kutoa nyongeza ya mishahara kwa watumishi wake lakini haitangazi kwa wananchi wote kama ambavyo imekuwa ikifanyika kwenye sherehe za wafanyakazi za Mei Mosi kila mwaka.

Amesema Serikali ikitangaza mishahara hadharani inaweza kusababisha usumbufu kwa watu wasio watumishi wa umma na inaweza kupandisha bei ya bidhaa na kuathiri mwenendo wa mahitaji ya wananchi sokoni.

Nyongeza za mishahara ambazo zinatangazwa hadharani, mara nyingi zina athari yake sio kwamba Serikali haikusudii kutoa nyongeza ya mshahara kwa mwaka, lakini unapotumia Mei Mosi kutangaza nyongeza ya mshahara unaleta athari kwenye jamii kwasababu vitu vinaweza vikapanda bei, vikawasumbua hata na wananchi ambao hawalipwi mshahara,” amesema Waziri Mkuu.

Amebainisha kuwa siyo lazima Serikali itangaze hadharani kila inapoongeza mishahara kwa watumishi wa umma lakini ifahamike kuwa Serikali ina utaratibu wake mzuri wa kuboresha stahiki za wafanyakazi wake kila mwaka.

Suala la nyongeza ya mishahara liko Serikalini na Mhe Rais ameishawahakikishia wafanyakazi atawaongeza mishahara na sio lazima litangazwe hadharani. Mshahara ni suala la mtu binafsi hata ukiongezwa leo kuwa tumeitangaza leo tumeongeza mshahara kwa kiwango hiki. Ukifanya hivi tayari umeleta kupanda kwa gharama’” amebainisha Waziri Mkuu.

Ameongeza kuwa mkakati wa Serikali ni kupunguza gharama za mahitaji kwenye masoko ili kuzuia mfuko wa bei za bidhaa.

Hata hivyo, Waziri Mkuu Mjaliwa amesema Serikali inaendelea kufanya sensa ya watumishi wote nchi nzima na zoezi hilo likikamilika itaboresha nyongeza ya mwaka, nyongeza ya mishahara na upandishaji wa madaraja.

Awali katika swali lake, Mbunge Lyima amesema Serikali inakiuka Sheria ya Utumishi wa Umma ya kuwapatia watumishi stahiki zao na kuwapunguzia motisha ya kufanya kazi kwa ufanisi katika maeneo yao ya kazi na kuathiri mafao baada ya kustaafu.

Hoja ya Mbunge huyo ni muendelezo wa malalamiko ya watumishi dhidi ya Serikali kwamba hawajapata stahiki zao tangu ilipoanza zoezi la ukakiki wa watumishi wa umma mwaka 2015. Katika zoezi hilo watumishi zaidi ya 9,000 walibainika kutokukidhi vigezo vya utumishi na hivyo kuondolewa kazini.

Huenda kauli aliyoitoa Waziri Mkuu leo Bungeni inaweza ikatofautiana na ile ya Rais John Magufuli aliyoitoa wakati wa sherehe za Mei Mosi, 2018 mijini Iringa ambapo alinukuliwa akisema hawezi kutoa nyongeza ya mishahara akidai Serikali haina fedha.

Kwangu mimi ninafikiria hizi pesa tunazotoa kwa ajili ya elimu bure ni nzuri kuliko fedha hizo kuzipeleka kuongezea mishahara, naona bora kuwapa mikopo wanafunzi wa vyuo vikuu kuliko kuongezea wafanyakazi mishahara,

Nikisema nitaongeza hizo pesa mimi nitazitoa wapi? naogopa kusema uongo. Hata mimi napenda kupandishiwa mshahara lakini kwa hali halisi ya sasa hivi lazima niwaeleze ukweli,” alinukuliwa Rais Magufuli.

Hata hivyo alibainisha kuwa kabla ya kuondoka madarakani ataboresha maslahi ya wafanyakazi wa umma, “Nawaahidi, kipindi changu cha urais hakitaisha kabla sijapandisha mishahara kwa wafanyakazi, kupandisha kwangu haitakuwa kwa shilingi elfu kumi, itakuwa ni kupandisha kwelikwel.”

Continue Reading

Jamii

Maaskofu KKKT wapewa siku 10 kufuta waraka

Published

on

Serikali imetoa siku 10 kwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), kuufuta kwa maandishi waraka wao waliotuoa Machi 24 mwaka huu na kisha kuujulisha Umma kwa njia mbalimbali walizotumia kuusambaza.

Kanisa la KKKT kupitia Baraza lake la Maaskofu lilitoa waraka uliopewa jina la ‘Taifa Letu Amani Yetu’ wakati wa Pasaka ambao mbali na masuala ya kiroho, ulibainisha mambo kadhaa yanayogusa mstakabali wa taifa.

Katika mitandao ya kijamii leo imesambazwa barua yenye kumbukumbu no. SO.748/25 inayoonyesha imeandikwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama Wizara ya Mambo ya Ndani kwenda kwa Mwenyekiti /askofu Mkuu wa KKKT iliyoandikwa Mei 30, 2018 ikitoa maelekezo ya kufutwa waraka huo ndani ya siku 10 tangu ilipoandikwa barua hiyo.

Ikiwa na kichwa cha habari ‘Ujumbe wa Baraza la Maaskofu wa KKKT’ barua hiyo inaeleza baraza hilo halitambuliki kisheria katika ofisi ya msajili.

“Unaelekezwa kuufuta waraka husika kwa maandishi na kuujulisha umma kuwa taasisi yako haikuwa na haina uwezo kisheria kufanya kile mlichokifanya. Maandishi hayo yaufikie umma wa Watanzania kwa kupitia vyombo vya habari na njia zingine zilezile zilizotumika kuufikisha waraka ule mliouita ‘Ujumbe wa Baraza la Maaskofu KKKT’.

Hata hivyo, barua hiyo imetoa onyo kali kwa taasisi hiyo dini nchi kutekeleza agizo mara moja la sivyo itachukuliwa hatua za kisheria.

“Maelekezo haya yatekelezwe ndani ya siku kumi tangu kupokea kwa barua hii vinginevyo hatua kali zaidi za kisheria zitachukuliwa dhidi ya taasisi hii,” inasema barua hiyo.

Ikumbukwe kuwa  waraka huo ulisainiwa na maaskofu 27 wa kanisa hilo nchini na kutaja baadhi ya mambo hayo kuwa ni pamoja na utekaji, utesaji, kupotea kwa watu, mashambulizi ya silaha dhidi ya viongozi wa kisiasa, mauaji yenye mwelekeo wa kiitikadi, vitisho, ubambikiziaji wa kesi, na matumizi mabaya ya vyombo vya dola dhidi ya wananchi.ni hali ya kijamii na kiuchumi, maisha ya siasa, na masuala mtambuka likiwamo suala la Katiba Mpya.

Waraka uliongeza pia kwamba uhuru wa kujieleza, kutoa na kupokea habari umeendelea kutoweka nchini huku ukionya kubanwa na hatimaye kuelekea kupungua kwa uhuru wa Bunge, Mahakama, na Tume ya Uchaguzi, ukisema hatua hii ni pamoja na kudhoofishwa kwa serikali za Mitaa.

Lakini kabla ya KKKT kutoa waraka wao, Kanisa Katoliki nalo lilitoa waraka kama huo likionya baadhi ya mambo ikiwemo uminywaji wa misingi ya demokrasia ya vyama vingi na uhuru wa kujieleza.

Baada ya kusambaa kwa waraka huo, yalijitokeza mambo mengi ikiwemo kutofautiana na kwa mawazo ya wananchi kuhusu wajibu wa viongozi wa dini katika kutoa ushauri, kuonya au kukemea pale mambo yanapoenda mrama.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa na Maaskofu wa KKKT

Hata hivyo, barua hiyo imepokelewa kwa hisia tofauti na watumiaji wa mitandao ya kijamii ikizingatiwa kuwa suala hilo lilijadiliwa na kupita, iweje linaibuka tena wakati huu ambapo kuna utulivu na yale mambo waliyoyapigia kelele na maaskofu  yamepungua ikiwemo kuteswa, kupotea kwa watu na vitisho dhidi ya viongozi wa kisiasa.

 

Wananchi bado wanawaamini viongozi wa dini

Wadau mbalimbali wa masuala ya kijamii wamesema kama kweli barua hiyo imetolewa na serikali, inaweza kuchochea taharuki zaidi kwa waumini wa kanisa hilo na wananchi kwasababu linagusa moja kwa moja imani zao.

Amebainisha kuwa bado waumini wengi wana imani na viongozi wao dini na kwamba yale wanayotamka yanakuwa na nia njema kwa jamii yao. Na katika muktadha huo serikali inapaswa kuwa makini ili kuepusha matatizo zaidi yanayoweza kutokea.

Akizungumza na FikraPevu, Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena amesema kama serikali ilibaini kuna tatizo kwenye usajili wa Baraza la Maaskofu la KKKT ingekaa na wahusika na kulimaliza kuliko kujitokeza hadharani na kuendeleza jambo ambalo limepita.

“Mimi namwamini Mungu kuliko serikali na viongozi wangu wa dini hasa Maaskofu. Hivyo serikali inapaswa kuwa makini na mambo yanayogusa imani za watu. Katika hili walipaswa kutafakari sana jinsi ya kushughulika nalo. Vinginevyo halina afya kwa ustawi wa taifa letu,” amesema Meena.

Amesema Maaskofu walitimiza wajibu wao wa kuonya kabla mambo hayajaharibika na serikali inapaswa kuyafanyika kazi yale yalyotajwa kwenye waraka au kukaa kimya ili kuepusha migongano isiyo na faida kwa taifa.

Continue Reading

Muhimu Kusoma

Copyright © 2020 FikraPevu.com