Connect with us

DATA

Tanzania yashika nafasi ya 22 kwa ‘Utumwa wa Kisasa’ duniani. Mimba za utotoni, kusafirisha watu zaigharimu

Published

on

Daniel Samson

Tanzania imetajwa kuwa miongoni mwa nchi 100 duniani zenye idadi kubwa ya watu ambao wanatumikishwa kwenye shughuli za ‘utumwa wa kisasa’ ambapo hali hiyo inatafsiriwa ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Kulingana na ripoti ya utafiti iliyotolewa na taasisi ya Global Slavery Index (GSI-2017) imeitaja Tanzania kushika nafsi ya 22 kati ya nchi 167 zenye idadi kubwa ya watu wanaotumikishwa kwenye aina mbalimbali za utumwa wa kisasa (Modern Slavery).

Ripoti hiyo inaelezwa kuwa inakadiriwa kuwa hadi kufikia mwaka 2016, Tanzania ilikuwa na watu 341,400 ambao wanatumikishwa kwenye shughuli mbalimbali ambazo zinakiuka haki za msingi za binadamu. Idadi hiyo ni sawa na asilimia 0.638 ya wananchi wote waliopo nchini.

‘Utumwa wa kisasa’ unahusisha vitendo vya kulazimishwa kufanya kazi ngumu, kuwaweka watu rehani (bonded labour), usafirishaji watu, utumwa wa watoto, ndoa za kulazimishwa na ndoa za utotoni. Waathirika wakubwa wa utumwa huo ni wanawake na watoto ambao kutokana na hali zao hawawezi kujizuia na matendo maovu yanayofanywa na baadhi ya watu katika jamii.

Tanzania imewekwa nafasi ya 22 kwasababu ya ongezeko la mimba za utotoni na utumikishwaji wa watoto kwenye kazi ngumu za migodini, mashambani na biashara. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tanzania inatajwa kuwa ni nchi ya tatu barani Afrika kwa matukio ya ndoa za utotoni na mimba kwa asilimia 28, ambapo kila mwaka wasichana 8,000 hupata mimba na kukatisha masomo.

Tatizo hilo bado ni kubwa katika nchi za Afrika Mashariki. Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Watu na Makazi (UNFPA) linaeleza kuwa msichana 1 kati ya 6 mwenye umri wa miaka 15 hadi 19 hupata mimba katika nchi hizo.

Kwa upande wa Afrika Mashariki, Tanzania imeshika nafasi ya kwanza ikifuatiwa na Uganda yenye ‘watumwa’ 244,400 ikishika nafasi ya 30 duniani. Nchi ya 3 ni Kenya (188,800) ikiwa nafasi ya 37 ikifuatiwa na Rwanda (74,100) pamoja na Burundi (71,400).

 

Nchi zote za Afrika Mashariki zimeingia kwenye nchi 100 zenye idadi kubwa ya watu wanaotumikishwa kwenye utumwa wa kisasa ambapo vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na wanawake vimeshika kasi kwenye nchi hizo.

GSI ilifanya utafiti katika nchi 167 duniani kuanzia mwaka 2014 na ilipofika 2017 walitoa ripoti hiyo ambayo inaelezwa kuwa licha ya biashara ya utumwa kukomeshwa Karne ya 19, vitendo vya utumwa vinaendelea kufanyika kwa siri na kwa njia mbalimbali ambapo huathiri ustawi wa binadamu na jamii.

Kuwepo au kutokuwepo kwa utumwa katika nchi husika kunapimwa kwa vigezo 4 ambavyo ni ulinzi wa raia na kisiasa, upatikanaji wa haki za kijamii na kiuchumi, ulinzi binafsi, idadi ya wakimbizi na mapigano ya ndani ya nchi.

Duniani kote zaidi ya watu milioni 45.8  wanatumikishwa kwenye aina mbalimbali za utumwa ambapo asilimia 58 ya utumwa huo unatokea kwenye nchi 5 za China, India, Pakistan, Bangladesh na Uzbekistan. Nchi nyingi zinawatumikisha na kuwalipa wafanyakazi ujira mdogo kwenye mashamba na viwanda vinavyotengeneza bidhaa zinazouzwa nchi za Ulaya, Japan, Amerika ya Kaskazini na Australia.

Ripoti hiyo inabainisha kuwa nchi zenye kiwango kikubwa cha  uwiano wa idadi ya watu walio kwenye utumwa wa kisasa ni Korea Kaskazini, Uzbekistan, Cambodia, India na Qatar. Nchini Korea Kaskazini upo ushahidi wa kweli ambao unaonyesha jinsi serikali inavyowalazimisha watu wake kufanya kazi ngumu kwenye kambi za kijeshi na wale wanaokiuka amri hiyo hufungwa jela.

Pia wanawake wanalazimishwa kuolewa na kuingia kwenye biashara na udhalilishaji wa kingono katika nchi ya China na nchi nyingine za jirani. Serikali ya Uzbekistan kila mwaka inawalazimisha wananchi wake kufanya kazi ya kuvuna pamba kwa ujira mdogo.

Hata hivyo, nchi zilizo na kiwango kidogo kabisa cha idadi ya watu walio utumwani ni Luxembourg, Ireland, Norway, Denmark, Switzerland, Austria, Sweden na Ubelgiji. Nchi zingine ni Marekani, Canada, Australia na New Zealand. Kwa ujumla nchi hizo zina uchumi mzuri, sera na sheria nzuri, kiwango kidogo cha mapigano na uthabiti wa kisiasa ambao unapambana na utumwa wa kisiasa.

 

 

Utumwa wa Kisasa nini?

Mtu anahesabika kwamba yuko utumwani ikiwa:

  • Kalazimishwa kufanya kazi – kwa nguvu au kwa vitisho vya kiakili na kimwili.
  • Kumilikiwa au kusimamiwa na mwajiri kwa kudhalilishwa kiakili, kimwili au vitisho
  • Kukosa ubinadamu,  kumchukulia, kumuuza au kumnunua mtu kama bidhaa/mali
  • Vikwazo vya kutembea ikiwemo kwenda popote kwa kuwekewa vikwazo vya kisiasa au usalama.

 

Aina za Utumwa wa Kisasa

Shirika la Kimataifa la Kuzuia Utumwa (Anti-Slavery International) linaeleza kuwa makusudi ya unyanyasaji yanatofautiana kutoka udhalilishaji wa kingono na kazi ngumu mpaka ule wa ndoa za utotoni na ukeketaji. Aina za utumwa wa kisasa zimegawanyika katika matabaka mbalimbali:

  1. Kulazimishwa kufanya kazi – Kazi au huduma yoyote ambayo watu wanalazimishwa kufanya bila hiari yao kwa vitisho au aina fulani ya adhabu.
  2. Rehani ya madeni au kazi – Ni aina ya utumwa ambayo imeshika kasi duniani ambapo watu waliokopa fedha wakashindwa kulipa wanalazimishwa kufanya kazi ili kufidia madeni . Hupoteza utashi na usimamizi wa hali zao ikiwemo ajira na madeni.
  3. Usafirishaji watu – Inahusisha kusafirisha, kuajiri au kuwahodhi watu kwa nia ya kuwatesa, kuwadhalilisha, vitisho au kutumia nguvu.
  4. Utumwa wa Kurithishwa – Inatokea pale ambapo mtu amezaliwa kwenye familia ya watumwa na kwasababu jamaa zake walichukuliwa utumwani na yeye kwa asili anakuwa mtumwa.
  5. Utumwa wa watoto – Watu wengi wanachanganya utumwa wa watoto na kazi ngumu kwa watoto. Kazi ngumu kwa watoto ni hatari na kikwazo kwa maendeleo ya kielimu lakini utumwa wa watoto unatokea pale mtoto anaponyanyaswa na mtu mwingine ambapo inahusisha kusafirishwa, kuingizwa jeshini, ndoa za utotoni na ukatili unaotokea nyumbani.
  6. Ndoa za kulazimishwa na utotoni – Inatokea mtu akiolewa bila ridhaa yake na hawezi kutoka kwenye ndoa hiyo. Ndoa za utotoni zinatajwa kuwa ni utumwa kwasababu watoto hawana utashi wa kufanya maamuzi ya kimahusiano.

 

Hatua zilizochukuliwa 

Serikali kupitia Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba amesema wizara yake imepokea taarifa kuwa wapo watanzania hasa vijana wanaosafirishwa nje ya nchi na kuingia nchini kutumikishwa kwenye shughuli za udhalilishaji na utumwa.

“Tumeona vijana wakiwa wamefungwa miguu juu vichwa chini wamefungwa mikono yote wakitandikwa viboko kwa madai  kwamba miongoni mwao kuna aliyewapeleka akiwaambia kwamba twendeni kuna kazi nzuri ya kufanya lakini wakifika kule wanawekwa rehani pale walipo, wanatumikishwa kitumwa na wengine wananyanyaswa kikatili” amesema Waziri Mwigulu na kuongeza kuwa,

“Lakini wapo raia wanaoingia kwa makundi nchini kwetu na wale wanaowaleta wanatumia sababu tofauti  wanapowaleta na wanapoingia wanawafanyisha shughuli tofauti na walizoombea vibali”.

Amebainisha kuwa wanachukua hatua za kisheria kuwakamata na kuwafikisha mahakamani wale wote wanaowatesa na kuwatumikisha watanzania katika shughuli zisizo halali ili kuhakikisha haki za binadamu zinalindwa na kuendelezwa.

“Lakini wanaohusika na shughuli hizi waendelee kutafutwa, wakamatwe wafike kwenye mkono wa sheria ili sheria iweze kufuata mkondo wake”, ameagiza Waziri Nchemba.

Hata hivyo, shirika la Human Rights Watch limeishauri serikali ya  Tanzania kupitisha mikakati maalumu kuzuia na kukabiliana na unyanyasaji, ikiwa ni pamoja na kuweka kanuni kali na uangalizi wa uajiri, programu za mafunzo ya haki, na msaada wa kujitosheleza  kwa waathirika wa vitendo vya kitumwa vinavyotokea ndani na nje ya nchi. 

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

DATA

Maambukizi  ya Ukimwi yanavyoshamirisha yatima shule za msingi Iringa, Mbeya

Published

on

Mikoa ya Iringa, Mbeya na Njombe imetajwa kuongoza kwa idadi kubwa ya wanafunzi yatima wanaondikishwa katika shule za mingi, jambo linaloweza kuongeza gharama za matunzo kwa watoto hao.

Kulingana na uchambuzi wa takwimu za Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) za mwaka 2016 zinaeleza kuwa mkoa wa Iringa ulishika nafasi ya kwanza kitaifa kwa kuwa na wanafunzi  29,062 yatima sawa na asilimia 14.4% ya wanafunzi wote wa shule za msingi kwa mwaka huo.

Iringa ilikuwa na wanafunzi  wa shule za msingi wapatao 202,113 lakini kati ya hao mwanafunzi 1 kati ya 10 alikuwa ni yatima.

Kulingana na Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009, mtoto anahesabika kuwa ni yatima endapo atafiwa na mzazi mmoja au wote wawili. Kimsingi anakosa matunzo au upendo wa mzazi mmoja au wote wawili ambapo inaweza kuwa ni changamoto kwa ukuaji wake hasa katika upatikanaji wa elimu.

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa siyo Iringa pekee ndiyo yenye idadi kubwa ya wanafunzi yatima lakini mikoa yote inayounda kanda ya Nyanda za Juu Kusini iko kwenye nafasi ya juu kabisa miongoni mwa mikoa 5  ya Tanzania bara yenye yatima wengi.

Nafasi ya pili inashikwa na mkoa wa Njombe ambao ulikuwa na wanafunzi  yatima 19,794 sawa na asilimia 12.7, ikifuatiwa na Mbeya (41,956) sawa na 11.3%. Mkoa wa nne ni Pwani (26,545) sawa na 10.4% na nafasi ya tano ni Kagera (45431) sawa na asilimia 9.8.

Mikoa hiyo mitano inaunda jumla ya asilimia 44.2  ya wanafunzi wote  731,536 yatima waliokuwepo katika shule za msingi kwa mwaka wa 2016. Hiyo ni sawa na kusema kuwa watoto 4 wa mikoa hiyo mitano kati ya 10 ya Tanzania bara ni yatima.

Lakini iko mikoa ambayo imefanikiwa kuwa na idadi ndogo ya wanafunzi  yatima ikiwemo Manyara ambayo ilikuwa na wanafunzi 15,854 sawa na 6.2% ikifuatiwa na Kigoma (6.5%),  Singida na Mtwara ambazo zote kwa pamoja zilikuwa na 6.7 %. Na mkoa wa tano toka chini ni Lindi (6.8%).

Nini kiini cha kuwepo utofauti mkubwa wa kimkoa wa uwepo wa wanafunzi yatima katika shule za msingi za serikali na binafsi nchini?

ASILIMIA ZA WANAFUNZI YATIMA KATIKA SHULE ZA MSINGI KIMKOA- 2016

 

Wadau waelezea dhana hiyo

Wadau wa afya na masuala ya elimu ya jamii wanaeleza kuwa kuna uhusiano mkubwa wa ugonjwa wa UKIMWI na uwepo wa wanafunzi wengi au wachache yatima katika maeneo mbalimbali nchini.

 Kulingana na takwimu za Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) za mwaka 2017 zinaeleza kuwa mikoa ya Mbeya, Njombe na Iringa ambayo ina wanafunzi wengi yatima ndiyo vinara wa maambukizi ya Virusi vya Ukimwi nchini.

Kwa muktadha huo idadi ya wazazi wanaofariki kwa maradhi hayo nayo ni kubwa; uwezekano wa watoto wengi kubaki au kuondokewa na wazazi wote wawili ni mkubwa. VVU husambazwa zaidi kwa njia ya ngono (Uasherati na uzinzi), Matumizi ya pombe na dawa za kulevya, kutakasa wajane na baadhi ya mila na desturi. Ugonjwa huo hauna dawa wala kinga.

TACAIDS inaeleza kuwa  mkoa wa kwanza ni Njombe wenye  asilimia 14.8 ikifuatiwa na Iringa kwa asilimia 9.1 na Mkoa wa Mbeya unashika nafasi ya tatu kwa asilimia 9. Lakini imebainika kuwa mikoa yenye wanafunzi yatima wachache katika shule ina viwango vidogo vya maambukizi ya UKIMWI. Mafano  Manyara (1.5%) na Lindi (2.9%).

Msemaji wa Tacaids, Glory Mziray, wakati akiongea na wanahabari alisema maeneo watanzania walioonesha kuwa na ufahamu sahihi wa elimu kuhusu Virusi vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi wanafikia asilimia 60 jambo linalosababisha kuwepo mwamko mdogo wa kubadili tabia katika maeneo yenye maambukizi makubwa ya maradhi hayo.

Alibainisha kuwa njia mojawapo ya kupunguza maambukizi ya Ukimwi ni tohara kwa wanaume. Njia hiyo napunguza maambukizi ya Ukimwi kwa asilimia 60 na kusisitiza kuwa ipo haja ya kutoa elimu zaidi juu ya uelewa wa ugonjwa huo ili watoto wapate matunzo ya wazazi wote wawili.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi ya Vijana ya YOPOCODE, Alfred Mwahalende amesema mila, ushirikina na kugombania mali ni sababu nyingine inayoongeza watoto yatima shuleni.

“Sababu zingine ni masuala ya kishirikina ambayo hayazungumzwi sana. Katika maeneo ambayo tumekutana na wanavijiji wanaseama baba alirogwa kutokana na mali ili ndugu zake warithi. Wengine wanatafuta utajiri kwa kutoa ndugu zao kafara.” Ameeleza Mwahalende.

Amebainisha kuwa elimu itolewe kwa jamii juu ya kuwatunza watoto yatima na jinsi ya kujikinga na maradhi yote yanayosababisha vifo kwa wazazi ambao wanawajibika kuwalea na kuwasomesha watoto.

“Ninachoweza kusema ni elimu  itolewe lakini pia Asasi zinazoshughulika na masuala ya watoto yatima zione njia ya kuweka sawa kuimarisha na kuwapokea watoto wengi kwenye vituo vyao.” Amesema Mwahalende.

Continue Reading

Afya

Bajeti ya afya 2018/2019 bado tegemezi, yafyekwa kwa asilimia 20

Published

on

Imeelezwa kuwa kuna uwezekano mkubwa kwa watanzania kukosa huduma bora za afya kwa mwaka wa fedha 2018/2019 kutokana na kupunguzwa kwa bajeti ya  Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa asilimia 20.

Hayo yamebainika leo bungeni mjini Dodoma wakati waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akiwasilisha makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019 ambapo amesema wameomba Serikali iwapatie billion 893.4 kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya wizara hiyo.

“Mhe. Mwenyekiti jumla ya fedha kuu ambayo ninaomba Bunge lako tukufu lipitishe katika mafungu yote mawili kwa mwaka 2018/2019 sh. Bilioni 893.4,” amesema Waziri Ummy.

Kiasi hicho cha fedha kilichoombwa kimepungua kutoka trilioni 1.1 za mwaka wa fedha wa 2017/2018 ambapo zimepungua bilioni 171.6  na kufikia bilioni 893.4 mwaka 2018/2019 sawa na asilimia 20.

Waziri Ummy amesema kati ya fedha hizo ambazo wizara yake inaomba, fedha zitakazoelekezwa kwenye matumizi ya miradi ya maendeleo zitakuwa Tsh. bilioni 561.75 sawa na asilimia zaidi 60 ya fedha zote, ambapo matumizi ya kawaida yatagharimu bilioni 304. 47.

“Kwa upande wa matumizi ya kawaida kwa mwaka 2018/2019 wizara ikadiria kutumia kiasi cha sh. Bilioni 304,473,476 (bilioni 304.47) kwa ajili ya matumizi ya kawaida. Kati ya fedha hizo sh. Bilioni 88,465,756 (bilioni 88.46) zitatumika kwajili ya matumizi mengineyo na sh. Bilioni 216,720,000 (bilioni 216.72) zitatumika kwajili ya mishahara ya watumishi,” amesema waziri Ummy na kuongeza kuwa,

“Kwa upande wa miradi ya maendeleo wizara inakadiria kutumia sh. bilioni 4.91 kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Kati ya fedha hizo, sh. Bilioni 1.5 ni fedha za ndani na sh. Bilioni 3.41 ni fedha za nje.” amesema waziri Ummy.

Kwa muktadha huo, bajeti ya afya itategemea fedha za wahisani kwa asilimia 60 kugharimia miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya, zahanati, ukarabati wa majengo na ununuzi wa vifaa tiba na dawa. Hata fedha bilioni 4.91  iliyoelekezwa kwenye miradi ya maendeleo bado ni ndogo.

Changamoto iliyopo ni kwamba fedha za wahisani wakati mwingine huchelewa kufika au zinaweza zisiingie kabisa nchini kutoka na masharti ambayo yanaweza kuathiri utolewaji wa huduma za afya.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii, Peter Serukamba amesema  serikali haina nia ya dhati ya kuinua sekta ya afya kwasababu bajeti inayotengwa kila mwaka ni ndogo na haikidhi mahitaji ya wizara ya afya.

“Uchambuzi wa kamati umebaini fedha zilizotengwa kwaajili ya utekelezaji wa shughuli wizara kwa mwaka wa fedha 2017/18, ni kiasi kidogo ambacho hakiridhishi na kinyume na matarajio ya Mpango wa Bajeti ambao Bunge na Serikali tulikubaliana,” alisema Serukamba.

Licha ya bajeti ya afya kupungua kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019 kwa asilimia 20, fedha za bajeti iliyopita ya 2017/2018 hazikufika zote kwenye wizara hiyo jambo lilikwamishwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya sekta hiyo.

Serukamba amesema, mpaka kufikia Februari mwaka huu, Serikali ilikuwa imetoa Sh. bilioni 576.52 pekee kati ya Sh. trilioni 1.1 zilizokuwa zimetengwa kwaajili ya Bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2017/18,.

Kutokana na bajeti ndogo ya wizara ya afya, wabunge wameshauriwa kuijadili na kuangalia uwezekano wa kuishawishi Serikali kuongeza fedha kwa wizara hiyo ikizingatiwa ni sekta muhimu kwa ustawi wa wananchi ili kuwahakikishia wananchi afya bora.

Continue Reading

Afya

Mgawanyo usio sawa wa hospitali, zahanati unavyokwamisha huduma za afya kwa wananchi

Published

on

Imeelezwa kuwa watanzania watalazimika kusubiri kwa muda mrefu ili kupata huduma bora za afya kutokana na uchache wa vituo vya kutolea huduma hizo ambavyo haviendani na ongezeko la idadi ya watu nchini.

Hali hiyo ni tofauti na matakwa ya Sera ya Afya ya mwaka 2007 ambayo inasisitiza kuwa serikali inawajibika  kuinua hali ya afya ya wananchi wote na hasa wale walioko kwenye hatari zaidi, kwa kuweka mfumo wa huduma za Afya utakaokidhi mahitaji ya wananchi na kuongeza umri wa kuishi wa watanzania.

Lakini watanzania wengi hawafaidiki na tamko la Sera ikizingatiwa kuwa idadi ya watu inaongezeka sana kuliko maboresho na ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya nchini. Vituo hivyo vinajumuisha hospitali, vituo vya afya na zahanati ambazo vinatakiwa kujengwa kwenye vijiji, kata na ngazi ya wilaya na mkoa.

Kwa mujibu wa data za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) za mwaka 2017 zinaonyesha kuwa vituo vya kutolea huduma za afya viliongezeka kutoka 6,321 mwaka 2010 hadi kufikia 7,680 mwaka 2016, ambapo ongezeko hilo ni sawa na vituo 1,359 (14%) tu  kwa miaka saba na wastani wa vituo 194 kila mwaka.

Idadi ya vituo hivyo haiendani na ongezeko kubwa la watu. Kulingana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 Tanzania ilikuwa na watu milioni 45 na hadi kufikia mwaka 2016 inakadiriwa ilikuwa na watu zaidi milioni 50.

Kwa mtazamo wa kawaida ni kwamba karibu nusu ya wananchi hawapati na huduma bora za afya ikiwemo upatikanaji wa vituo vya kutolea huduma za afya, jambo linaloweza kuwaweka katika hatari ya kupoteza nguvukazi ya taifa na hata maisha.

Hata hivyo, bado ziko juhudi mbalimbali zinazofanyika kuhakikisha huduma hizo zinawafikia wananchi katika maeneo yao. Takwimu za NBS zinaeleza kuwa hadi mwaka 2016 kulikuwa na zahanati 6,658 ambazo zilikuwa na kliniki 89 za mama na mtoto. Lakini changamoto ni kwamba zahanati nyingi zinakabiliwa na upungufu wa madaktari, dawa, vifaa tiba na uchakavu wa miundombinu.

Kimsingi Sera ya Afya inaelekeza kuwa kila kijiji kinapaswa kuwa na zahanati yake ili kuhakikisha wananchi hawatembei umbali mrefu kufuata huduma kwasababu afya ni huduma muhimu ya kijamii na inapaswa kupewa kipaombele.

Kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2012, Tanzania ina vijiji 19,200  Ambavyo vinahudumiwa na zahanati 6,658 na hivyo basi kuna upungufu wa zaidi ya zahanati 12,000 ili kukidhi mahitaji ya wakazi wa vijiji vyote.

Kumekuwa na mabadiliko ya kuongezeka na kupungua kwa zahanati nchini. Mathalani mwaka 2013 kulikuwa zahanati 5,680 na mwaka uliofuata wa 2014 zilipungua hadi kufikia 6,002 na sababu kubwa ni  baadhi ya zahanati ni kutotimiza masharti na matakwa ya mwongozo wa matibabu nchini na hivyo kulazimika kufungwa. Juhudi zilifanyika na idadi ya zahanati ziliongezeka hadi kufikia 6,549 mwaka 2015 na mwaka uliofuta wa 2016 zilifikia 6,658.

Kinachotokea ni kwamba wingi wa vituo vya kutolea huduma za afya  unapungua kutoka ngazi ya kijiji, tarafa, wilaya hadi kitaifa. Hali hii inaweza kusababishwa na uhaba wa rasilimali fedha na watu, ubora wa huduma kwenye hospitali husika.

Mwaka 2016, kulikuwa na vituo vya afya 759 nchini kote ambapo ni sawa na kusema kuwa kila mkoa ulikuwa na vituo takribani 29. Kimsingi huduma zinazotolewa kwenye vituo vya afya zina hadhi ya juu ukilinganisha na zahanati kwasababu vinahudumia watu wengi zaidi na vinatakiwa kuwa na vifaa vya kisasa na huduma kama vile upasuaji na kliniki za mama na mtoto.

Idadi ya zahanati zilizoko nchini ni mara 9 ya vituo vya afya ambavyo vinategemewa kuwasaidia wagonjwa ambao hawajapata matibabu ya uhakika kwenye zahanati. Changamoto inayojitokeza ni kuwa vituo hivyo vinaelemewa na idadi kubwa ya wagonjwa wanaotoka ngazi ya chini na kwa vyovyote vile baadhi yake vitakuwa havina huduma bora za matibabu.

Pia vituo vya kutolea huduma za afya hupungua zaidi katika ngazi ya mkoa hadi kitaifa. Mwaka 2016 kulikuwa na hospitali 263 za wilaya, mkoa na rufani. Hizi ndio hospitali pekee zinazotegemewa na watanzania zaidi ya milioni 50 nchi nzima kupata matibabu.

Pengo kati ya vituo vya afya na hospitali sio kubwa sana ukilinganisha na zahanati ambazo ni nyingi lakini huduma zake hazilingani na hospitali nyingine za ngazi ya wilaya na mkoa.

Na utaratibu uliopo ni kwamba mgonjwa anatakiwa kutibiwa ngazi ya juu ikiwa tu zahanati na vituo vya fya vimeshindwa kumpatia matibabu yanayotakiwa. Kwa utaratibu huo vituo vya afya na hospitali nyingi huelemewa na wagonjwa kutokana na uwekezaji mdogo na  huduma zisizoridhisha kwenye zahanati.

Kutokana na hali halisi ya upatikanaji wa huduma za afya nchini, serikali na wadau wanapaswa kuongeza juhudi za kuboresha na kujenga vituo na hospitali ili kukidhi ongezeko la watanzania ambao wanatakiwa kuwa na afya bora zitakazosaidia katika ujenzi wa taifa.

Ujenzi na maboresho hayo ni muhimu yakaenda sambamba na tathmini ya huduma zinazotolewa, idadi ya vituo ili kuyasaidia maeneo yenye uhitaji mkubwa wa huduma za afya.

Continue Reading

Muhimu Kusoma

Copyright © 2020 FikraPevu.com