Connect with us

Siasa

Tarime: Funza wa mabua atesa wakulima wa mahindi

Published

on

NJAA sasa inainyemelea Wilaya ya Tarime, Mara kutokana na mdudu mharibifu wa mahindi.

Ikiwa mavuno ya mahindi hayatakuwa ya kuridhisha msimu, huu, basi wakazi wa wilaya hiyo, wataathirika kwa kukosa chakula na fedha.

Anayesababisha hofu ya kukosekana kwa mavuno ya kutosha msimu huu ni mdudu aitwaye- funza wa mabua. Kwa lugha ya Kiingereza anaitwa Stalk borer.

Mkazi wa Mtaa wa Kebikiri Kata ya Turwa wilayani Tarime Lea Joseph akionesha jinsi mdudu funza wa mabua alivyoharibu mahindi.

FikraPevu imefanya uchunguzi na kutembelea mashamba mbalimbali na kubaini mashamba mengi ya mahindi yakiwa yameliwa na wadudu.

Mashamba yaliyoshambuliwa na wadudu hao hadi sasa, yanakadiriwa kufikia hekta 135 za mahindi, ambayo endapo hatua za haraka hazitachukuliwa, wakulima wataingia hasara.

Katika kukabiliana na wadudu hao, FikraPevu imeshuhudia baadhi ya wakulima wasio na uwezo wa kununua dawa za kuua wadudu, wakitumia njia mbadala za kienyeji kunusuru mazao, kwa kunyunyizia majivu na udongo.

Wakulima hao wanafanya hivyo kwa kuepuka gharama za dawa za dukani (kemikali au viuatilifu), ambapo njia hizo za kienyeji wamedai zimesaidia kuzuia wadudu kuvamia mahindi.

Katika mahojiano yake na FikraPevu, Daniel Chacha mkazi wa Kijiji cha Borega kata ya Ganyange anasema: “Kwakweli wakulima saa hizi tunalia, mahindi yameingiliwa na wadudu wakati huohuo mvua yenyewe ni ya kusuasua. Yaani mwandishi wewe umeshuhudia wadudu walivyoshambulia mahindi ambayo mengi hata hayajaweka watoto,” anasema.

Anaongeza, “mashamba ni makubwa, watu wanaona kununua dawa ni gharama sana, dawa zenyewe unaweka siku chache wadudu wamerudi tunachokifanya tunatibu kwa kienyeji.

Tunayanyunyizia majivu au udongo, kwakweli imesaidia  maana baada ya kugundua wadudu wameingia kwenye mahindi ilibidi sasa tuyawahi mahindi ambayo bado hayajaingiliwa na wadudu na kuyanyunyizia udongo mlaini na majivu na imesaidia.

Tunaomba serikali itusaidie wakulima waone tatizo hili ni kama janga tupatiwe dawa za kuuwa wadudu”.

Lucy John, mkazi wa Sirari anasema kuwa kitendo cha wadudu kuharibu mahindi kimewaingiza hasara, “Tumegharamia uandaaji shamba, kupalilia, dawa bado mazao mengine yamekauka kwa kukosa mvua na ukifanikiwa bado kwenye kuvuna na usafirishaji kutoka shambani ni gharama, bado uyauze kwa bei ya hasara yaani ni shida”.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Matongo, Daniel Irondo ameimbia FikraPevu kuwa chanzo cha kuwepo kwa wadudu hao ni kutokana na ukame wa muda mrefu, ambao umechangia wadudu hao kuingia kwenye mahindi.

Aidha, anasema kuwa kunapokuwepo na mvua za kutosha, wadudu hao huwa hawaonekani.

FikraPevu imebaini baadhi ya mahindi yaliyoliwa na wadudu ni mbegu za mahindi za kutoka nchini Kenya  zinazouzwa sh 12,000 kwa mfuko wenye ujazo wa kilo mbili zinazopandwa na wakulima walio wengi ambazo ni Hybrid Na.H6213, Na. H614, Na. H517, Na. H625, Na. H614, Na. H626, na DK. 8031 pamoja na mahindi mengi yaliyoshambuliwa sana ni mbegu ya kienyeji inayopandwa hususan maeneo ya vijijini iitwayo Maria.

Kushamiri wadudu hao

Perusi Samwel, mkazi wa Kenyamanyori  anasema kuwa serikali isipochukua hatua kuhakikisha utatuzi wa wadudu huo unapatikana, wakulima wengi watakula hasara.

Anasema gharama ya kunyunyizia dawa ambayo ni sh. 9,000 kwa ekari ni kubwa kulinga na ukubwa wa mashamba wananchi waliyolima, kwavile watahitaji madawa mengi na gharama kuwa kubwa.

Recho John anasema kwakuwa wadudu hao wameathiri mashamba mengi ya mahindi, hatua za kunusuru mazao yaliyosalia endapo hazitachukulia, watakosa chakula na pengine bei ya mahindi itapanda zaidi kutokana na mahindi yatakayozalishwa kuwa kidogo.

Kwa upande wake, Paul Mwita, mkazi wa Mtaa wa Gamasara anaiambia FikraPevu kuwa, pamoja na wakulima wengi kutumia majivu na udongo katika kukabilia na wadudu hao, dawa hizo za kienyeji zinafaa tu pale kabla mdudu hajaingia ndani ya mmea, akishaingia tu majivu hayasaidii.

Suluhisho la kuwaondoa kabisa funza wa mabua ni kutumia dawa za kemikali tu ambazo wakulima wengi hawawezi kumudu.

Mtara Marwa, mfanyabiashara wa mahindi mkazi wa Mtaa wa Rebu, Kata ya Turwa anasema “mimi mwenyewe nusu nzima ya heka ya mahindi wameingiliwa na wadudu na sijui ni aina gani za dawa natakiwa kuweka.”

Anauliza, “kwanini serikali isitupatie dawa ili kutunusuru wakulima? Hili walione kama janga kubwa kwa wakulima.”

Anaendelea, “sasa tukisema mkulima mwenyewe anunue dawa, sidhani kama wote watatekeleza hilo maana uchumi ni mgumu, pesa hakuna hata yakula inakosa, hiyo ya dawa itatoka wapi?’’.

Akizungumza na FikraPevu, Kaimu Afisa kilimo wa Halmashauri ya Mji Tarime, Sadock Lundi anasema kuwa katika msimu wa masika uzalishaji wa zao la mahindi  umekumbwa na wadudu aina ya Stalk borer  ambao wameathiri hekta 12.8 na wakulima wameshauriwa kutumia dawa ya maji ya kuuwa wadudu  ambayo ni Supereron na Duducron.

Lundi anasema kuwa Halmashauri iliweka malengo katika mwaka 2016/2017 kulimwa hekta za mahindi 3,663.75, huku mavuno yakikisiwa kuwa tani 13,922.25; hata hivyo zililimwa hekta 1,552, makisio ya mavuno yakiwa tani 5,897.6. Asilimia 20 ya hekta hizo sawa na hekta hekta 310.4 ziliathiriwa na ukame.

Kaimu Afisa kilimo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Stanley Kubalila, anakiri kuwepo kwa  wadudu hao ambao wameharibu hekta 123  katika halmashauri hiyo na kwamba chanzo cha wadudu hao ni ukame na ili kuwaondoa kabisa wakulima wanatakiwa kutumia dawa za kemikali .

“Dawa za kienyeji za udongo na majivu zenyewe ni kinga tu. Husaidia mdudu asiweze kuingia kwenye mahindi maana anapoingia ukaa katikati ya muhindi ndani anapokuwa ameingia kwenye mmea tiba ya kuuwa mdudu huyo ni dawa za kemikali.

Kubalila amewataka wakulima kutumia dawa za kuua wadudu ambazo ni Thiodan dust, Sumithion dust, Thionex dust na Malathion dust zinazouzwa kati ya Sh. 9,000 hadi Sh. 12,000 na kwamba serikali haitoi ruzuku ya dawa za kuua wadudu zaidi ya ruzuku ya pembejeo za kilimo na mbolea.

Kubalila anaiambia FikraPevu kuwa hakuna ruzuku ya dawa za wadudu  kutoka serikalini huku akibainisha hali halisi ya uvunaji wa zao la mahindi kwa msimu wa  vuli 2016/2017  mavuno tegemewa zao la mahindi ilikuwa  hekta 8,115 na kuvuna tani 35,706, lakini  hekta zilizolimwa ni 6,898 huku mavuno halisi yakiwa tani 24,143.0.

“Msimu wa Masika malengo yalikuwa hecta 10,633, huku mavuno yaliyotegemewa ni tani 43,595 katika msimu wa Masika 2016/2017.

Hili la mdudu ameshambulia mazao ya mahindi, nawashauri wakulima ambao wameshindwa kupulizia dawa watumie njia za kienyeji kwa kuweka udongo laini na majivu kwenye mahindi, husaidia kuuaa mdudu,’’ anasema Kubalila.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Siasa

Sakata la waraka wa Maaskofu KKKT lang’oka na Msajili Mambo ya Ndani

Published

on

Waziri wa Mambo ya Ndani Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Usajili wa Jumuiya za Kidini na Vyama vya Kijamii, Merlin Komba ili kupisha uchunguzi wa barua iliyoandikwa ukilitaka Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kufuta waraka ilioutoa Machi mwaka huu.

Barua iisambazwa kwenye mitandao ya kijamii ikiitaka KKKT kuufuta waraka wa Pasaka uliotolewa Machi 24 mwaka huu vinginevyo hatua kali za sheria zitachukuliwa dhidi ya kanisa hilo.

Waraka huo uliopewa jina la ‘Taifa letu amani yetu’ ulisainiwa na maaskofu 27 wa kanisa hilo. Ulijikita kujadili masuala ya jamii, uchumi, siasa, katiba mpya na matukio ambayo yako kinyume na kile lilichokiita tunu na misingi ya Taifa.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Waziri Nchemba amesema Serikali haipingani na dhehebu lolote na pale ambapo kuna uhitaji wa kufanyia kazi jambo kuhusu taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo taratibu huwa zinatumika kuzungumza na sio kama ilivyofanywa taarifa hiyo inayosambaa.

“Serikali inalinda uhuru wa kuabudu na waumini hivyo huo waraka una maudhui kama matatu, ni barua batili na tunaendelea kuchunguza kama imetengenezwa basi imetengenezwaje, kwani haujapita kwetu.” amesema Waziri Mwigulu.

Kutokana na msimamo huo wa serikali, Waziri Nchemba, amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Usajili wa Jumuiya za Kidini na Vyama vya Kijamii, Merlin Komba, kupisha uchunguzi wa barua iliyoandikwa kwa maaskofu wa KKKT.

“Hivyo basi, namsimamisha Msajili wa hizo taasisi kupisha uchunguzi na ikithibitika ni za Wizara tuweze kujua maana jambo hilo halijapita kwa Waziri, Katibu Mkuu na wala si maelekezo ya serikali,” amesema.

Hata hivyo, amewatoa hofu viongozi wa dini kutokana na sakata hilo na kuwataka waendelee na majukumu yao huku ikitahadharisha jamii kuwa makini na taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

“Tunawaomba viongozi wa dini waendelee na kazi zao, nasema jamii iwe macho na taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya jamii na wasifanyie kazi taarifa hizo. Viongozi wa dini wasiwe na taharuki na taarifa hizo, hazina baraka za Serikali na wasisite kuwasiliana na Serikali kujua uhalali wake,” amesema.

Waziri Nchemba amesema waraka wa viongozi wa dini uliotolewa miezi iliyopita ni jambo lililopita na hakukuwa na haja ya kuendeleza malumbano yasiyo na tija kwenye jamii.

Katika waraka wa ujumbe wa pasaka uliosomwa katika makanisa ya Kilutheri kote nchini Tanzania na kusambaa katika mitandao ya kijamii, baraza hilo limeorodhesha mambo kadhaa ambayo wameyataja kuwa ndio tishio la umoja na amani ya nchi hiyo.

Utekwaji wa watu wa hivi karibuni, utesaji, kupotea kwa watu, mashambulizi ya silaha dhidi ya viongozi wa kisiasa, muaji yenye mwelekeo wa kiitikadi, vitisho, ubambikiziaji wa kesi, na matumizi mabaya ya vyombo vya dola dhidi ya wananchi ni baadhi tu ya mambo yaliyotajwa katika waraka huo.

Lakini pia Watanzania wamekuwa na hisia tofauti kuhusu viongozi wa dini kuzungumzia hali ya kisiasa nchini. Waraka wa KKKT ulikuja mwezi mmoja baada ya ule wa maaskofu wa kanisa katoliki ambao nao ulionya juu ya kuminywa kwa haki ya kufanya shughuli za kisiasa kama mikutano ya hadhara na maandamano.

Baada ya nyaraka hizo mbili kutolewa na Maaskofu, baadhi ya mambo yaliyokuwa yakilalamikiwa yalipata ufumbuzi ikiwemo kupungua kwa mauaji na uteswaji wa raia kulikuwa kunafanywa na watu wasiojulikana.

Continue Reading

Jamii

Waziri Mkuu Majaliwa: Hatutangazi nyongeza ya mshahara hadharani kuepusha athari kwa jamii

Published

on

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameweka wazi kuwa serikali haitatangaza nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa umma hadharani ili kuepusha athari kwa jamii ikiwemo kupanda kwa bei ya bidhaa.

Akizungumza leo Bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalumu (CHADEMA), Susan Lymo ambaye alitaka kufahamu kwanini Serikali imewanyima au imeshindwa kuwalipa watumishi wa umma nyongeza ya mishahara ambayo ni haki yao ya msingi kulingana na miaka waliyokaa kazini.

Akijibu swali la Mbunge huyo, Waziri Mkuu Majaliwa amesema Serikali ina utaratibu wa kutoa nyongeza ya mishahara kwa watumishi wake lakini haitangazi kwa wananchi wote kama ambavyo imekuwa ikifanyika kwenye sherehe za wafanyakazi za Mei Mosi kila mwaka.

Amesema Serikali ikitangaza mishahara hadharani inaweza kusababisha usumbufu kwa watu wasio watumishi wa umma na inaweza kupandisha bei ya bidhaa na kuathiri mwenendo wa mahitaji ya wananchi sokoni.

Nyongeza za mishahara ambazo zinatangazwa hadharani, mara nyingi zina athari yake sio kwamba Serikali haikusudii kutoa nyongeza ya mshahara kwa mwaka, lakini unapotumia Mei Mosi kutangaza nyongeza ya mshahara unaleta athari kwenye jamii kwasababu vitu vinaweza vikapanda bei, vikawasumbua hata na wananchi ambao hawalipwi mshahara,” amesema Waziri Mkuu.

Amebainisha kuwa siyo lazima Serikali itangaze hadharani kila inapoongeza mishahara kwa watumishi wa umma lakini ifahamike kuwa Serikali ina utaratibu wake mzuri wa kuboresha stahiki za wafanyakazi wake kila mwaka.

Suala la nyongeza ya mishahara liko Serikalini na Mhe Rais ameishawahakikishia wafanyakazi atawaongeza mishahara na sio lazima litangazwe hadharani. Mshahara ni suala la mtu binafsi hata ukiongezwa leo kuwa tumeitangaza leo tumeongeza mshahara kwa kiwango hiki. Ukifanya hivi tayari umeleta kupanda kwa gharama’” amebainisha Waziri Mkuu.

Ameongeza kuwa mkakati wa Serikali ni kupunguza gharama za mahitaji kwenye masoko ili kuzuia mfuko wa bei za bidhaa.

Hata hivyo, Waziri Mkuu Mjaliwa amesema Serikali inaendelea kufanya sensa ya watumishi wote nchi nzima na zoezi hilo likikamilika itaboresha nyongeza ya mwaka, nyongeza ya mishahara na upandishaji wa madaraja.

Awali katika swali lake, Mbunge Lyima amesema Serikali inakiuka Sheria ya Utumishi wa Umma ya kuwapatia watumishi stahiki zao na kuwapunguzia motisha ya kufanya kazi kwa ufanisi katika maeneo yao ya kazi na kuathiri mafao baada ya kustaafu.

Hoja ya Mbunge huyo ni muendelezo wa malalamiko ya watumishi dhidi ya Serikali kwamba hawajapata stahiki zao tangu ilipoanza zoezi la ukakiki wa watumishi wa umma mwaka 2015. Katika zoezi hilo watumishi zaidi ya 9,000 walibainika kutokukidhi vigezo vya utumishi na hivyo kuondolewa kazini.

Huenda kauli aliyoitoa Waziri Mkuu leo Bungeni inaweza ikatofautiana na ile ya Rais John Magufuli aliyoitoa wakati wa sherehe za Mei Mosi, 2018 mijini Iringa ambapo alinukuliwa akisema hawezi kutoa nyongeza ya mishahara akidai Serikali haina fedha.

Kwangu mimi ninafikiria hizi pesa tunazotoa kwa ajili ya elimu bure ni nzuri kuliko fedha hizo kuzipeleka kuongezea mishahara, naona bora kuwapa mikopo wanafunzi wa vyuo vikuu kuliko kuongezea wafanyakazi mishahara,

Nikisema nitaongeza hizo pesa mimi nitazitoa wapi? naogopa kusema uongo. Hata mimi napenda kupandishiwa mshahara lakini kwa hali halisi ya sasa hivi lazima niwaeleze ukweli,” alinukuliwa Rais Magufuli.

Hata hivyo alibainisha kuwa kabla ya kuondoka madarakani ataboresha maslahi ya wafanyakazi wa umma, “Nawaahidi, kipindi changu cha urais hakitaisha kabla sijapandisha mishahara kwa wafanyakazi, kupandisha kwangu haitakuwa kwa shilingi elfu kumi, itakuwa ni kupandisha kwelikwel.”

Continue Reading

Jamii

Maaskofu KKKT wapewa siku 10 kufuta waraka

Published

on

Serikali imetoa siku 10 kwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), kuufuta kwa maandishi waraka wao waliotuoa Machi 24 mwaka huu na kisha kuujulisha Umma kwa njia mbalimbali walizotumia kuusambaza.

Kanisa la KKKT kupitia Baraza lake la Maaskofu lilitoa waraka uliopewa jina la ‘Taifa Letu Amani Yetu’ wakati wa Pasaka ambao mbali na masuala ya kiroho, ulibainisha mambo kadhaa yanayogusa mstakabali wa taifa.

Katika mitandao ya kijamii leo imesambazwa barua yenye kumbukumbu no. SO.748/25 inayoonyesha imeandikwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama Wizara ya Mambo ya Ndani kwenda kwa Mwenyekiti /askofu Mkuu wa KKKT iliyoandikwa Mei 30, 2018 ikitoa maelekezo ya kufutwa waraka huo ndani ya siku 10 tangu ilipoandikwa barua hiyo.

Ikiwa na kichwa cha habari ‘Ujumbe wa Baraza la Maaskofu wa KKKT’ barua hiyo inaeleza baraza hilo halitambuliki kisheria katika ofisi ya msajili.

“Unaelekezwa kuufuta waraka husika kwa maandishi na kuujulisha umma kuwa taasisi yako haikuwa na haina uwezo kisheria kufanya kile mlichokifanya. Maandishi hayo yaufikie umma wa Watanzania kwa kupitia vyombo vya habari na njia zingine zilezile zilizotumika kuufikisha waraka ule mliouita ‘Ujumbe wa Baraza la Maaskofu KKKT’.

Hata hivyo, barua hiyo imetoa onyo kali kwa taasisi hiyo dini nchi kutekeleza agizo mara moja la sivyo itachukuliwa hatua za kisheria.

“Maelekezo haya yatekelezwe ndani ya siku kumi tangu kupokea kwa barua hii vinginevyo hatua kali zaidi za kisheria zitachukuliwa dhidi ya taasisi hii,” inasema barua hiyo.

Ikumbukwe kuwa  waraka huo ulisainiwa na maaskofu 27 wa kanisa hilo nchini na kutaja baadhi ya mambo hayo kuwa ni pamoja na utekaji, utesaji, kupotea kwa watu, mashambulizi ya silaha dhidi ya viongozi wa kisiasa, mauaji yenye mwelekeo wa kiitikadi, vitisho, ubambikiziaji wa kesi, na matumizi mabaya ya vyombo vya dola dhidi ya wananchi.ni hali ya kijamii na kiuchumi, maisha ya siasa, na masuala mtambuka likiwamo suala la Katiba Mpya.

Waraka uliongeza pia kwamba uhuru wa kujieleza, kutoa na kupokea habari umeendelea kutoweka nchini huku ukionya kubanwa na hatimaye kuelekea kupungua kwa uhuru wa Bunge, Mahakama, na Tume ya Uchaguzi, ukisema hatua hii ni pamoja na kudhoofishwa kwa serikali za Mitaa.

Lakini kabla ya KKKT kutoa waraka wao, Kanisa Katoliki nalo lilitoa waraka kama huo likionya baadhi ya mambo ikiwemo uminywaji wa misingi ya demokrasia ya vyama vingi na uhuru wa kujieleza.

Baada ya kusambaa kwa waraka huo, yalijitokeza mambo mengi ikiwemo kutofautiana na kwa mawazo ya wananchi kuhusu wajibu wa viongozi wa dini katika kutoa ushauri, kuonya au kukemea pale mambo yanapoenda mrama.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa na Maaskofu wa KKKT

Hata hivyo, barua hiyo imepokelewa kwa hisia tofauti na watumiaji wa mitandao ya kijamii ikizingatiwa kuwa suala hilo lilijadiliwa na kupita, iweje linaibuka tena wakati huu ambapo kuna utulivu na yale mambo waliyoyapigia kelele na maaskofu  yamepungua ikiwemo kuteswa, kupotea kwa watu na vitisho dhidi ya viongozi wa kisiasa.

 

Wananchi bado wanawaamini viongozi wa dini

Wadau mbalimbali wa masuala ya kijamii wamesema kama kweli barua hiyo imetolewa na serikali, inaweza kuchochea taharuki zaidi kwa waumini wa kanisa hilo na wananchi kwasababu linagusa moja kwa moja imani zao.

Amebainisha kuwa bado waumini wengi wana imani na viongozi wao dini na kwamba yale wanayotamka yanakuwa na nia njema kwa jamii yao. Na katika muktadha huo serikali inapaswa kuwa makini ili kuepusha matatizo zaidi yanayoweza kutokea.

Akizungumza na FikraPevu, Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena amesema kama serikali ilibaini kuna tatizo kwenye usajili wa Baraza la Maaskofu la KKKT ingekaa na wahusika na kulimaliza kuliko kujitokeza hadharani na kuendeleza jambo ambalo limepita.

“Mimi namwamini Mungu kuliko serikali na viongozi wangu wa dini hasa Maaskofu. Hivyo serikali inapaswa kuwa makini na mambo yanayogusa imani za watu. Katika hili walipaswa kutafakari sana jinsi ya kushughulika nalo. Vinginevyo halina afya kwa ustawi wa taifa letu,” amesema Meena.

Amesema Maaskofu walitimiza wajibu wao wa kuonya kabla mambo hayajaharibika na serikali inapaswa kuyafanyika kazi yale yalyotajwa kwenye waraka au kukaa kimya ili kuepusha migongano isiyo na faida kwa taifa.

Continue Reading

Muhimu Kusoma

Copyright © 2020 FikraPevu.com