Connect with us

Investigative

Ufisadi Chunya unatishia ustawi wa wafugaji

Published

on

“MAISHA yetu ni kama kifaranga aliyekosa mama kwani hali zetu za kiuchumi kila kukicha zinazidi kudhoofika kama mgonjwa wa kwashiakoo’’,anasema Julius Machia  ambaye ni kiongozi wa kikundi cha umoja wa wafugaji wahamiaji bonde la Songwe lililopo wilayani Chunya mkoani Mbeya.

Anabainisha kuwa endapo kiwango cha kupigwa faini ambazo sio halali  kitaendelea ,mifugo yao itamalizika  na watakuwa masikini na mzigo kwa  serikali  kwa  kuwa wanaishi kwa kutegemea mifugo walionayo.

Machia anasema tangu zoezi la kukamata mifugo inayozidi 70 na kutozwa kwa kila mfugo unaozidi shilingi 20,000,kumesababisha matatizo mengi kwa wafugaji yakiwemo baadhi yao kuuwawa na askari kwa kupigwa risasi katika operesheni ya kamata mifugo na wafugaji kudhulumiwa kwa kupigwa faini kubwa hali ambayo inamlazimu mfugaji kuuza mifugo kwa bei ya hasara.

Hii ni risiti ambayo amepewa mfugaji baada ya kupigwa faini ya uharibifu wa mazingira ,hata hivyo mfugaji alitoa shilingi milioni sita ikiwa ni faini ya ng’ombe 300 sawa na kila mmoja shilingi 20,000,hata hivyo mtendaji ameandika shilingi  600,000 tu

“Kwa miaka 10 sasa zoezi la kukamata mifugo, limekuwa  kama mvuta sigara huvuta  sigara anapojisikia kiu kwa kuwa watendaji wa serikali wanaendesha zoezi hili bila mpangilio na limekuwa linafanyika mara kwa mara tena kwa unyanyasaji mkubwa’’,anasisitiza Machia. Julius Machia anasema faini wanayotozwa na serikali kwa kila mfugo unaozidi  imekuwa inafanyika katika mazingira ya kifisadi kwa kuwa kiwango cha faini ni kikubwa na kwamba kinachoandikwa kwenye risiti za malipo ya Halmashauri ya wilaya na hali halisi ni tofauti.

Ngombe wa wafugaji wahamiaji wakisubiri kuuzwa kwa bei ya hasara mnadani ili kuweza kulipa faini ambazo wanatozwa na Halmashauri zikiwemo mazingira, kulisha mashamba na faini nyingine.

Baadhi ya risiti ambazo gazeti hili imepata nakala zake zinaonesha kuwa  mfugaji Materemki Lugola wa kijiji cha Wanzani alilipa faini ya shilingi milioni 4,740,000 mwaka 2001 kwa ajili ya mifugo 948 kula katika mashamba ya wakulima.

Aliyetakiwa kupokea fedha hizo  ni mkulima ambaye shamba lake limeliwa na mifugo kupitia ofisi za vijiji badala yake mpokeaji wa fedha hizo ni Afisa mifugo,kilimo na ushirika wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya ambaye amesaini katika risiti kuwa amepokea kiasi hicho cha fedha.

Risiti nyingine ya mwezi Mei mwaka 2011 inaonesha kuwa mfugaji Julius Machia wa kijiji cha Chang’ombe  alilipa faini ya shilingi milioni sita kwa ajili ya kuzidi mifugo 300 ambapo kila mfugo uliozidi ulitozwa shilingi 20,000,hata hivyo risiti hiyo imeandikwa mfugaji huyo amelipa shilingi laki sita badala ya milioni sita.

“Tumepumzika kwa miezi sita,tu Mei 16 na Juni mosi mwaka huu afisa mifugo akiwa na viongozi wengine wamefika tena kwenye bonde letu safari hii wametoza faini ya uharibifu wa mazingira ng’ombe na mbuzi zinazozidi kila mfugo shilingi 20,000,wamekusanya mamilioni ya shilingi,tumewandikiwa risiti ambazo sio halali tunaomba serikali isikilize kilio chetu, anasema mfugaji Machia.

Wafugaji wahamiaji wengine waliopigwa faini ya kuzidi kwa mifugo na kuandikiwa risiti kuwa  ni faini  kwa ajili ya kulisha mifugo kwenye mashamba ni Misa Njigula wa kijiji cha Totowe ambaye alipigwa faini ya shilingi 1,275,000 kwa ajili ya ng’ombe 255,Masale Gidai wa kijiji cha Magamba alipigwa faini ya shilingi 770,000.

Kiongozi wa kikundi cha wafugaji bonde la Songwe Julius Machia

Masele Julius wa kijiji cha Ifuko alipigwa faini ya shilingi 140,000,Mashala Kwilasa wa kijiji cha Galula  alipigwa faini ya shilingi 115,000 na mfugaji John Kasema wa Totowe ametozwa faini ya shilingi milioni nane kwa ng’ombe 400.

“Tanzania ni nchi  inayosifika kuongoza kwa kufuata utawala wa sheria,sisi wafugaji wahamiaji tumechoka kunyanyaswa, kukandamizwa, kukamatwa ovyo,kutozwa faini zisizo za haki kwanini kama sisi ni wahalifu tusipelekwe mahakamani ili haki itendeke’’,anasema mfugaji Machia.

Sisi wafugaji tulio wengi hatujasoma,tunadhulumiwa mifugo yetu kwa miaka kumi sasa,wewe nenda ukaone maisha ya watumishi wa umma wakiwemo watendaji , madiwani pamoja na viongozi ngazi ya wilaya sisi wenye mifugo tunaonekana masikini,watumishi hao wametajirika kutokana na mifugo yetu’’,anadai  Machia.

Asilimia 90 ya wafugaji wahamiaji  katika Bonde la Songwe hawajui kusoma,kuandika na kuhesabu hali ambayo inawafanya baadhi ya watendaji serikalini kutumia mwanya huo kuwadhulumu kwa kuwapiga faini ambazo sio halali.

Hata hivyo afisa mifugo na kilimo katika Halmashauri ya wilaya ya Chunya Adamu Mbale amekiri kuwepo kwa baadhi ya watendaji kuhusika na utoaji wa risiti ambazo sio halali“Kuna watendaji wawili kutoka vijiji vya Bonde la Songwe ambao wamechunguzwa na TAKUKURU  baada ya kubainika kufanya udanganyifu kwenye risiti za malipo na kesi zao zipo mahakamani’.

Deus Mashalla mfugaji katika kijiji cha Galula anasema kitendo cha kukamata mifugo ya wafugaji wahamiaji kimekuwa kinafanyika sio kwa kuangalia idadi ya mifugo inayozidi 70  badala yake  hata wakikuta mfugaji mhamiaji katika eneo lake kuna ng’ombe mmoja hukamatwa na kupelekwa katika kituo cha polisi  na kumtoza mfugaji huyo kiasi cha shilingi 20,000.

Hata hivyo Mashalla anabainisha  kuwa wanaoendesha operesheni ya kukamata mifugo wamekuwa wanavamia hata katika nyumba za wafugaji wahamiaji na kuwanyang’anya mifugo na kuwatendea  vitendo  vinavyokwenda kinyume na haki za binadamu.

Anavitaja vitendo hivyo kuwa ni kutishiwa risasi hewani ili wenye mifugo wajifiche na kuogopa kuuwawa,kupiga nyumba risasi hadi kubomoa ambapo wametolewa mfano nyumba ya mfugaji Jikolela Mihambo wa kijiji cha Swela nyumba yake iliteketea kwa moto baada ya kupigwa kwa risasi.

Afisa mifugo na kilimo wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya Adamu Mbale

Vitendo vingine ambavyo vinakiuka haki za binadamu ni kuporwa kwa fedha za wafugaji,mgambo na askari kuwakimbiza wafugaji kwa magari na kuwasababishia majeraha wakati wakijitahidi kukimbia ili kujiokoa.

Wafugaji wahamiaji hao wamebainisha zaidi kuwa wafugaji wa bonde la Songwe ndiyo jamii inayooongoza kwa kilimo  kwa kuwa wanazalisha mazao mengi ya chakula kama vile mahindi,mpunga,mtama na viazi vitamu na kwamba wafugaji hawapati tatizo la njaa ukilinganisha na wakulima wenyeji ambao karibu kila mwaka wanapata tatizo la njaa.

Gamaya Bunga  mfugaji katika kijiji cha Chang’ombe anasema  utozwaji wa faini unaonekana kufanyika kwa upendeleo kwa kuwa wakulima wanaovunja sheria na kulima kwenye maeneo ambayo hayaruhusiwi kisheria kama vile kwenye vyanzo vya maji  vya mto Songwe na ziwa Rukwa hawakamatwi.

Bonde la Songwe lenye kata za Galula, Mbuyuni, Totowe, Namkukwe na Khanga lina utajiri mkubwa wa mifugo inayomilikiwa na wafugaji wahamiaji kutoka wa mikoa ya Tabora ,Shinyanga, Mwanza, Singida na Kagera ambapo inakadiriwa  kuna mifugo zaidi ya 727,230 hadi kufikia mwaka jana.

Takwimu ambazo zimetolewa na afisa mifugo,kilimo na ushirika katika Halmashauri ya wilaya ya Chunya Adamu Mbale  zinaonesha kuwa  kati ya mifugo hiyo ng’ombe ni 286,800, mbuzi 46,501, kondoo 24,803, nguruwe 11,223 na kuku wa kienyeji 357,903.

Mbale anabainisha kuwa Kutokana na uwepo wa mifugo mingi serikali mwaka 2002 ilitoa sheria ya Halmashauri ya wilaya ya Chunya  kuhakikisha kila mfugaji katika bonde hilo awe na mifugo isiyozidi 70 na kwamba mfugaji atakayezidisha kiwango hicho cha mifugo anapigwa faini  ya shilingi 20,000 kwa kila mfugo unaozidi.

Operesheni ya kukamata mifugo iliyozidi ilikuwa inafanyika tangu mwaka 2001 hadi 2010 katika Bonde la Songwe kwa kuhusisha wadau mbalimbali wakiwemo watendaji wa serikali, mgambo, na polisi, hata hivyo kuanzia mwaka jana mkuu wa wilaya ya Chunya Deodatus Kinawiro alipiga marufuku operesheni hiyo akitaka wafugaji kwanza wapewe elimu ya kutosha.

Mkuu wa wilaya ya Chunya Deodatus Kinawiro katika kukabiliana na uingizaji wa mifugo ametoa wito kwa   wakuu wa wilaya tisa zinazopakana na wilaya yake wasitishe utoaji wa vibali vya kusafirishia mifugo hasa Ng’ombe wanaoingia wilayani humo.

Wilaya zilizofikia muafaka wa kutotoa vibali vya uingizaji na utoaji wa vibali vya mifugo ni pamoja na Chunya, Mbarali, Mbeya, Mbozi, Mpanda, Sumbawanga, Sikonge, Urambo na Manyoni.


 

 

 

Continue Reading
4 Comments

4 Comments

 1. RASTO JONI SUNGURA

  09/06/2012 at 10:07 am

  HATA KAMA KIOLA MBUZI ANAKULA KWA UREFU WA KAMBA ALIOFUNGWA. HAWA VIONGOZI WAMEZIDI SASA WANALAZIMMISHA HATA KAMBA UVUTIKE KAMA MPIRA WA KUFUNGIA MIZIGO. KAMA RISITI INAANDIKWA 600,000/=, HIYO 6000,000/= INAKWENDA WAPI?

 2. arteta

  23/07/2012 at 2:37 pm

  Afadhalii waandshi wa habari mmeanza kuiona chunya inavyo liwa na wa2 wachachee!!!

 3. michael mbiti

  27/08/2012 at 2:25 pm

  Tanzania yetu hii tunatakiwa tupate wapiganaji kama akina Sokoine, bila hivyo bado tuna wakati mugumu miaka 50 mingine ijayo, Uwajibikaji sufuri hiyo yote viongozi wameona na hakuna atakaye mfunga kengere mwingine, Jamani inakele sana natamani hata kwenye mabadiliko ya katiba tuweke kifungu ukiwa na hasira mtwange hata ngumi tano za uhakika ila usishitakiwe, Huo ni wizi wa kijinga na kumuibia mtu masikini jamani tutafika MUNGU IBARIKI AFRIKA MUNGU IBARIKI TANZANIA NA WATU WAKE AMEE!!!

 4. japhet

  03/09/2012 at 10:52 am

  hivi huyu mbale yeye ni nani katika dunia hii !!tangu tumeanza kusikia habari zake za wizi wa mali za umma!serikali tatizo iko dar tu chunya wezi ni wengi sana ila mmekaa tu huko haya bana sisi kwa sababu hatujasoma mungu awalinde na elimu zenu hizo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Investigative

‘UBESHI’: Safari ya Vijana Kuifikia Almasi Mwadui-Shinyanga

Published

on

MAJUZI nilikuwa katika utafiti wa namna gani Madini ya Almas yanayopatikana katika Mji Mdogo wa Maganzo Wilayani Kishapu mkoani Shinyanga umewanufaisha wananchi wanaozunguka Mgodi wa Almasi wa Mwadui.

(more…)

Continue Reading

Investigative

Hofu ya Usalama kwa wafanyakazi GGM Yatanda

Published

on

SIKU chache baada ya moto kuzuka ndani ya mgodi wa Geita (GGM) na kuteketeza mali zenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 25,hofu kubwa ya kupoteza maisha imeibuka kwa uongozi na wafanyakazi wa mgodi huo.

(more…)

Continue Reading

Investigative

If we can’t give people’s priorities the attention they deserve, why ask them to prioritize?

Published

on

In a move intended to empower the citizens and give them mandate to decide on their own development priorities, the government adopted the decentralization policy.

(more…)

Continue Reading

Muhimu Kusoma

Copyright © 2020 FikraPevu.com