Connect with us

Featured

Ukiona uvuaji gamba ni ovyo, wewe ndiye wa ovyo-Kikwete

Published

on

RAIS Jakaya Kikwete, amekiri wazi kuwepo kwa vuguvugu la upinzani lenye nguvu kubwa hapa nchini, na kuonya kwamba, iwapo Chama cha Mapinduzi (CCM), hakitajirekebisha katika mienendo yake inayoonekana kuwaudhi wananchi, chama hicho kipo hatarini kupoteza hatamu ya kuliongoza Taifa na kusisitiza nia ya chama hicho kuwaondoa mafisadi.

Kadhalika, Rais Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM Taifa, ametetea uamuzi wa kujivua gamba ndani ya chama hicho, uliopewa baraka zote na Halmashauri Kuu ya chama hicho (NEC), dhidi ya viongozi mafisadi kuhakikisha wanajiondoa ndani ya chama kabla hawajaondolewa, na kusema uamuzi huo haukuwalenga watu fulani wanaotuhumiwa kwa ufisadi, bali viongozi wote wasio na maadili mema ndani ya CCM.

Mkuu huyo wa nchi, aliyathibitisha hayo leo Jijini Mwanza, wakati akihutubia maelfu ya wanachama wa CCM katika sherehe za maadhimisho ya miaka 35 ya kuzaliwa kwa CCM, iliyofanyika Kitaifa kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa.

Katika sherehe hizo, CCM ililazimika kutumia mtindo wake wa kukodi mabasi na maroli, kwa ajili ya kusomba watu kutoka maeneo mbali mbali ndani na nje ya mkoa huo, kwa ajili ya kuhudhuria maadhimisho hayo, ambayo hata hivyo yalionekana kughubikwa na imani za kishirikina ndani ya uwanja huo wa CCM Kirumba.

Katika hotuba yake kwa wana CCM, Rais Kikwete alisema kwamba, kwa sasa nchi imekumbwa na mtikisiko mkubwa wa vuguvugu la upinzani, na kwamba viongozi wa CCM na Serikali kwa ujumla wasiwe watu walioganda.

“Wapo wanaobeza mafanikio tuliyofikia, nasema huo ni uroho mbaya. Sisi tuwapuuze. Lakini tutambueni kwamba kwa sasa vuguvugu la upinzani limezidi kuwa na nguv kubwa hapa nchini.

“Kushika ama kuendelea kushika madaraka inatokana na ridhaa ya wananchi wenyewe. Hivyo wana CCM tutambueni hilo kwamba wananchi ndiyo wenye uwezo wa kutupa ama kutukataa kuwaongoza. Tukishindwa hilo tutashindwa”, alisema Rais Kikwete ambaye wakati wa kuingia uwanjani CCM Kirumba wasaidizi wake kitengo cha usalama wa taifa waliona chupa mbili zilizokuwa zimejazwa vitu vilivyodaiwa dawa za kishirikina, kisha mmoja wa saidizi wake hao kuipiga teke chupa moja.

Chupa hizo mbili za kampuni moja ya kutengeneza maji (jina tunalihifadhi), zenye ujazo wa lita 1.5, zilionekana moja kuwekwa upande wa zuria na nyingine upande wa pili wa zuria lililotandikwa uwanjani hapo kwa ajili ya mgeni rasmi na wageni wengine wanapopita kwenda meza kuu (V.I.P), kwa ajili ya shughuli hiyo ya maadhimisho hayo.

Kikundi cha Sungusungu wa Mwanza wakitumbuiza sherehe za miaka 35 ya CCM, Mwanza

Alisema, lazima viongozi wa CCM na Serikali wawajibike kikamilifu katika kusimamia maendeleo ya wananchi, ili kuendelea kuwajengea imani raia hao dhidi ya chama chao tawala na Serikali kwa ujumla, na kwamba chama hicho tawala kimeathiriwa sana na viongozi wake wasiokuwa waaminifu mbele ya jamii ya Kitanzania.

Kuhusu kujivua gamba.
Mwenyekiti huyo wa CCM Taifa alisema: “Hivi karibuni nikiwa na NEC hapo Dodoma, nilitumia neno nyoka kujivua gamba. Usemi huo ulienezwa tofauti kabisa. Kimsingi tulipitisha maazimio mengi, lakini wenzetu wameona azimio moja tu la kujivua gamba.

Alisema, hoja ya kujivua gamba iliyopitishwa na NEC mwaka jana si ya ovyo, hivyo kiongozi na mwanachaa yeyote ndani ya CCM anayeuona uamuzi huo ni wa ovyo, basi yeye ndiyo wa ovyo mbele ya jamii.

“Uamuzi wa kujivua gamba ndani ya CCM si wa ovyo. Ukiuona wa ovyo wewe ndiyo wa ovyo. Haiwezekani tukaendelea kuwa na watu wa ovyo. Lazima chama kijipange na kujiweka sawa ili kisipoteze sifa kwa jamii”, alisema mwenyekiti huyo wa CCM taifa ambaye alipokea wanachama wapya wapatao 1,847.

Kwa mujibu wa Rais Kikwete ambaye alianza kuhutubia saa 8:45 mchana na kumaliza saa 9:37 alasiri, alikiri pia ajenda ya watu ndani ya chama hicho kujivua gamba imegonga mwamba, na amewatupia mzigo wanachama wake kuwawajibisha viongozi hao na wale wanaowaona hawaendani na maadili wala sera za chama hicho tawala.

Alisema, maamuzi ya kujivua gamba hayakulilenga kundi ama watu fulani ndani ya CCM, bali linawahusu wanachama wote wanaojitambua kwamba si waaminifu kujiondoa wenyewe ndani ya chama kwa kuachia nyadhifa za kiuongozi badala ya kusubiri kuondolewa na mamlaka za juu.

“Wito wa kujivua gamba haujapewa mwitikio mzuri. Tumetupa mpira huo kwa wanachama kuwawajibisha viongozi hao, maana tunawafahamu. Sasa kazi kwetu sote”, alisema Rais Kikwete pia alishuhudia uwanja huo wa CCM Kirumba kutokujaa watu kama ilivyokuwa mwaka 2005 wakati alipowasili kwa ajili ya kuomba kura ya kuwa mtawala wa nchi.

Uchaguzi wajumbe wa NEC.
Mwenyekiti huyo na Rais wa nchi alisisitiza kwamba, lazima wajumbe wa Halmashauri kuu ya chama (NEC), wachaguliwe kutoka kwenye wilaya zao, na si vinginevyo, na kusema hiyo itasaidia zaidi kukiimarisha chama chake hicho kinachonyemelewa na vuguvugu kali la upinzani nchini.

Hata hivyo, alikwenda mbali na kuwataka wanachama wasiokuwa wasafi, wenye upeo mfupi, wabakaji na mafisadi wasijidanganye kuomba uongozi huo wa NEC, maana wanachama hawatawachagua kutokana na matendo yao mabaya ndani ya jamii inayowazunguka.

Mwenyekiti huyo wa CCM aliiagiza Taasisi ya Kuzuia Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kuanza kunyemelea nyendo za baadhi ya wanasiasa wanaotaka kugombea UNEC ndani ya chama hicho, kwani wapo baadhi yao wamepanga kutumia rushwa kuwahonga wanachama ili wawachague kushika nafasi hiyo ya juu.

Katiba mpya.
Rais Kikwete aliwapongeza wabunge wa CCM kwa uamuzi wao wa kuitetea Sheria ya Mabadiliko ya Katiba mpya 2011, na kwamba muswaada huo umeshawasilishwa tena bungeni, hivyo ataunda tume ya kukusanya maoni kwa Watanzania, ambapo aliwaomba wana CCM kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao, maana mmbamba ngoma huvutia kwake.

“Hili la Katiba mpya tumechukuwa mapendekezo ya vyama vya upinzani, kikiwemo CCM ambacho nacho kimetoa mapendekezo manane. Nawashukuru sana wabunge wa CCM katika hili, lakini wana CCM jitokezeni kwa wingi kutoa maoni yenu maana mmbamba ngoma huvutia kwake”.

Hata hivyo, Rais Kikwete alikwepa waziwazi kuzungumzia tatizo la mgomo wa Madaktari linaloikumba nchi kwa sasa, na kuahidi kulitolea ufafanuzi na maelezo muda si mrefu.

Alikitaka pia kitengo cha propoganda ndani ya chama hicho kufanya kazi vizuri, maana chama hicho kinaonekana kuzidiwa nguvu na wapinzani ambao wao hutumia propoganda za aina mbali mbali, hivyo wananchi kuanza kuamini maneno ya wapinzani.

Habari hii imeandaliwa na Sitta Tumma – Mwanza.

 

Hotuma kamili ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete:

HOTUBA YA MWENYEKITI WA CCM TAIFA, MHESHIMIWA
JAKAYA MRISHO KIKWETE, KATIKA SHEREHE ZA
KUTIMIZA MIAKA 35 YA CCM, KWENYE UWANJA WA
CCM KIRUMBA,TAREHE 05 FEBRUARI, 2012
Mheshimiwa Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa,
Mhemiwa Pius Msekwa, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara,
Mheshimiwa Wilson Mukama, Katibu Mkuu wa CCM,
Waheshimiwa Wajumbe wa Sekretariat, Kamati Kuu na Halmashauri
Kuu ya Taifa;
Waheshimiwa Waasisi wa TANU, ASP na CCM;
Wanachama wenzangu wa CCM;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Kidumu Chama cha Mapinduzi……..!
Naomba tuanze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa
kutupa afya na uzima na kutuwezesha kukutana tena katika
maadhimisho ya siku hii adhimu na ya kihistoria kwa Chama chetu na
nchi yetu.
Tumekusanyika hapa siku ya leo kusherehekea miaka 35 ya
kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi. Nawashukuru na kuwapongeza
sana viongozi, wana-CCM na wakazi wa Mkoa wa Mwanza kwa
mapokezi mazuri na kwa maandalizi mazuri ya sherehe hizi. Hakika
sherehe zimefana sana. Hongereni wote mlioandaa sherehe hii kwa kazi
nzuri sana mlioifanya. Nawapongeza sana wanachama na wananchi,
kwa kujitokeza kwa wingi katika matembezi ya mshikamano leo
asubuhi na sasa katika kilele cha sherehe. Aidha, nawashukuru kwa
2
burudani mbalimbali na wimbo mzuri wa halaiki ambao umetugusa
sana na kukonga nyoyo zetu. Wahenga walisema “mwenye macho
haambiwi tazama”. Tunawashukuru sana. (Mwabeja sana).
Napenda pia kuwapongeza viongozi, wanachama, makada,
wapenzi na mashabiki wote wa CCM kote nchini kwa kuadhimisha
miaka 35 ya uhai wa Chama chetu. Kama nilivyosema kule Dodoma
mwaka wa jana kwamba tunastahili kujipongeza kwani tumefanikiwa
kwa mengi, na tunazidi kufanikiwa. Wapo wanaotubeza, sisi
tuwapuuze kwa kuendelea kutekeleza ahadi na mipango.
Tuwashangaze kwa kufanikiwa ili wachukie.
Ndugu Wananchi;
Sherehe hizi ni fursa ya kufanya tathmini ya kiasi gani
tumefanikiwa kujenga na kuimarisha Chama chetu na jinsi gani
tumefanikiwa katika kutimiza wajibu wetu kwa taifa na wananchi
ambao tuna dhamana ya kuwaongoza.
Kwa Chama chetu kufanikiwa kudumu na kuwa kimoja kwa
miaka 35, na zaidi ya nusu ya miaka hiyo ikiwa ni ndani ya ushindani
wa vyama vingi, ni mafanikio makubwa ambayo wote hatuna budi
kujivunia. Ni jambo la fahari kubwa kwa Chama cha Mapinduzi
kwamba nchi yetu imesherehekea miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara
wakati Chama chetu kikiwa kinaendelea kushika hatamu za uongozi wa
nchi yetu.
Tumefanikiwa kufanya hivyo kwa miaka yote hiyo kwa sababu
tumetambua na kutimiza wajibu wetu wa uongozi wa taifa kwa namna
na kiwango ambacho kimewaridhisha wananchi wa Tanzania. Ukweli
huo unadhihirishwa na jinsi Chama chetu kilivyoendelea kupata
ushindi katika chaguzi mbalimbali tangu tuanze mfumo wa vyama
vingi mwaka 1992 mpaka sasa. Tumeendelea kupata ushindi mzuri
3
hata katika kipindi hiki ambacho vuguvugu la upinzani nchini
limeongezeka kwa kiasi kikubwa.
Ndugu zangu, Viongozi wenzangu na Wana-CCM wenzangu;
Kama nilivyokwishawahi kusema mara kadhaa kwa wana CCM
siku za nyuma kwamba wakati tunapojipongeza kwa mafanikio
tuliyoyapata, hatuna budi kutambua kuwa ili Chama chetu kiendelee
kupata ushindi na kuongoza taifa letu kwa miaka mingi zaidi, hatuna
budi kwenda na wakati. Lazima tuwe na sera nzuri zinazotambua
matakwa ya raia na matatizo yanayowakabili na kuyatafutia majawabu.
Tuchukue hatua thabiti za kutatua changamoto na matatizo ya
wananchi na kufanya mambo mapya ya kuleta maendeleo. Tukifanya
hayo wananchi wataendelea kuwa na mapenzi na imani na Chama
chetu na kutuwezesha kuendelea kuongoza kwa miaka mingi zaidi.
Bahati nzuri Chama chetu kina sifa ya kutekeleza sera zake na
ahadi zake kwa wananchi pamoja na changamoto mbalimbali
tunazokabiliana nazo. Tumethibitisha ukweli huo kwa jinsi gani
tumetekeleza Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2005 – 2010 na tulivyoanza
kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya 2010 – 2015 katika mwaka wa kwanza
wa ngwe yetu ya pili. Ni ukweli kwa nchi nzima na ukweli kwa Mkoa
wa Mwanza kwamba tumetekeleza ahadi zetu kwa kiwango cha juu
sana. Tunasema tutakayotekeleza na tunatekeleza tuliyoahidi.
Viongozi wenzangu na Wanachama Wenzangu;
Chama chetu kinayo sifa nyingine nzuri nayo ni kufanya tathmini
ya shughuli zake mara kwa mara ili kubaini mafanikio tuliyoyapata na
pale ambapo hatukufanikiwa. Lakini huwa hatuishii hapo bali
hukubaliana juu ya hatua za kuchukua kuimarisha na kuendeleza
tuliyofanikiwa na kusahihisha tulipokosea. Hiyo ndiyo siri ya
mafanikio yetu.
4
Kukamilisha Mageuzi Ndani ya Chama
Ndugu Wana CCM;
Katika hotuba yangu ya mwaka jana pale Dodoma nilieleza haja
ya kufanya tathmini ya uchaguzi uliopita na kufanya mageuzi ndani ya
Chama chetu kwa lengo la kukiimarisha. Shabaha yetu kuu ni
kukihuisha Chama chetu na kukipa taswira mpya na mvuto zaidi mbele
ya jamii. Katika kusisitiza umuhimu wa kufanya hayo nilitoa mfano wa
tabia ya nyoka kujivua gamba. Nilieleza kwa kina faida ya kufanya
hivyo na athari za kutochukua hatua hizo mapema.
CCM ni chama cha siasa ambacho mtaji wetu uko katika kuungwa
mkono na watu. Hivyo basi, hatuna budi kuwa makini, sikivu na
kwenda na wakati. Ni ukweli ulio wazi kuwa uhai na uhalali wa
Chama chetu kushika hatamu za dola unategemea ridhaa ya wananchi.
Hisia zao na mtazamo wao juu ya Chama chetu ndizo zinazowafanya
waamue kutupatia au kutunyima ridhaa hiyo. Hivyo basi, lazima
wakati wote Chama chetu kijitahidi kuhakikisha kuwa kina taswira
nzuri katika mitazamo na hisia za wananchi. Lazima tuwe na sera nzuri
na tufanye mambo mema. Pia lazima Chama chetu kijenge uwezo wa
kupambana na propaganda chafu zinazojenga taswira mbaya ya Chama
kwa jamii. Lazima tujenge uwezo wa kujisemea kwa mema mengi
tunayofanya.
Chama hiki ndio zindiko la nchi hii na matumaini ya wananchi
walio wengi. Kamwe tusikubali sisi viongozi kuwa chanzo cha
kuipoteza tunu hii ya Watanzania kwa kushindwa kuchukua hatua
sahihi. Tukichelea kufanya hivyo, tutachekwa na kulaumiwa sana na
kamwe historia haitotusamehe.
Ndugu Wana-CCM;
Kwa kutambua ukweli huo na wajibu wa kihistoria kwetu wa
Chama chetu, Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama chetu katika kikao
5
cha mwezi Aprili, 2011 kiliazimia kuchukua hatua mbalimbali
zitakazokipa uhai mpya Chama chetu. Miongoni mwa hatua hizo ni
kuiunda upya Kamati Kuu na Sekretariati ya Halmashauri Kuu ya Taifa.
Aidha, kuutazama muundo wa Chama chetu na iliamuliwa kuwa
Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa wachaguliwe kutoka Wilayani
badala ya utaratibu wa sasa wa kuwachagua kutoka Mkoani na Taifa.
Lengo ni kuusogeza uongozi huu wa juu wa Chama chetu utoke karibu
na kule wanachama waliko. Tulikubaliana pia kwamba sote tuelekeze
nguvu zetu katika kuimarisha Matawi na Mashina walipo wanachama.
Hivi sasa nguvu nyingi imeelekezwa Wilayani, Mkoani na Taifa.
Halmashauri Kuu ya Taifa imejadili kwa kirefu nafasi ya viongozi
katika ujenzi wa Chama na sifa yake mbele ya watu na jamii. NEC
imekubaliana kwa kauli moja kwamba, kuwa na viongozi hodari na
wenye mwenendo mwema ni rasilimali yenye tunu kubwa. Kinyume
chake ni kubeba mzigo mkubwa wa lawama na kushusha heshima na
sura ya Chama katika jamii. Halmashauri Kuu ya Taifa ilikubaliana
kwamba sifa na sura ya Chama katika macho ya jamii imeathiriwa sana
na kuwa na viongozi wanaonyooshewa vidole na kutuhumiwa kwa
mwenendo mbaya hasa vitendo vya rushwa, wizi, utovu wa nidhamu
na ubadhirifu. NEC iliamua kuwa viongozi wa namna hiyo hawafai
kuwemo katika safu za uongozi wa Chama chetu. Ikaamuliwa wapime,
watafakari na kuamua kujiondoa katika uongozi na wasipofanya hivyo
waondolewe.
Baada ya kuridhika kuwa wito huo haukuitikiwa ipasavyo, NEC
imeagiza vikao vya Chama vya ngazi zote wawatambue viongozi wa
namna hiyo na kuwachukulia hatua kuwawajibisha. Hayo ndiyo
maelekezo, sasa kazi kwetu sote kwani watu hao wapo katika ngazi
zote, wapo kwenye Matawi, Kata, Wilaya, Mikoa na Taifa. Bahati
mbaya ilijengwa dhana kana kwamba wapo taifa tu.
6
Ndugu Wanachama;
Nafahamu kuwa baadhi ya viongozi na wanachama wenzetu
hawakupendezwa na hawapendezwi na uamuzi huo na mageuzi ya
Chama kwa jumla. Wanataka tubaki tulivyo. Hawa hawakitakii mema
Chama, tuendelee kuwaelimisha. Wako waliotafsiri kuwa mageuzi
haya yanawalenga watu Fulani tu, hayo siyo kweli ni upotoshaji. Kwa
kweli huku kutia fitina kwa jambo ambalo liko dhahiri. Sote tu
mashahidi wa kilio cha wanachama wetu, wapenzi na wananchi kwa
ujumla kuhusu haja ya kukibadili Chama chetu. Tunatambua kilio cha
wanachama na wananchi cha kutaka Chama chao wanachokipenda
kiwe na viongozi waadilifu wasiokuwa na tuhuma za rushwa au
ubadhirifu, wanaotenda maovu.
Kilio hicho ni cha kututakia mema na kinaonyesha kuwa watu
wengi bado wana imani kubwa na CCM na wangependa kuona
tukichukua hatua za kukisafisha na kukijenga upya. Maana wangekuwa
wametuchoka wangejikalia kimya na kusubiri kutunyima kura wakati
wa uchaguzi. Hatuwezi kuzipuuzia sauti hizi za wengi na hatuwezi
kujificha katika visingizio visivyo na msingi. Tusichelee kuudhi
wachache kwa manufaa ya Chama chetu. Mzee wetu Mhe. Benjamin
Mkapa alituusia, “Chama kwanza, mtu baadae”. Chama ni muhimu
zaidi kuliko mtu.
Wana-CCM Wenzangu;
Kazi hii tuliyoianza lazima tuifanye bila ya kuchoka mpaka
tuifikishe ukomo wake. Iwe ni ya kudumu, tusiifanye kuwa ya mara
moja au ya tukio. Iwe ni sehemu ya mila yetu na kila kunapotokea
kiongozi kupoteza sifa achukuliwe hatua. Tuimarishe Kamati za
Usalama na Maadili za ngazi zote ili ziweze kufanya kazi hii. Kusafisha
safu za viongozi na wanachama wetu ni jambo lenye maslahi kwa
Chama chetu.
7
Majukumu yetu kwa 2012
Uchaguzi wa Chama na Jumuiya zake
Ndugu Wana CCM,
Kama tujuavyo, huu ni Mwaka wa Uchaguzi ndani ya Chama
chetu na Jumuiya zake kuanzia ngazi ya Shina hadi Taifa. Tofauti na
chaguzi zilizopita, uchaguzi wa mwaka huu unahusisha Chama na
Jumuiya zake. Huu ni utekelezaji wa moja ya mambo 23
tuliyokubaliana tufanye katika mageuzi ya ndani ya Chama. Sababu
kubwa iliyotufanya tuamue hivyo ni kutaka tupunguze muda
tunaoutumia kwa shughuli za uchaguzi ili tupate muda wa kutosha wa
kushughulikia kazi za ujenzi wa Chama na utekelezaji wa majukumu
yake ya msingi.
Nawasihi viongozi wenzangu na wanachama wenzangu tuitumie
fursa hii vizuri kuchagua viongozi wazuri watakaokiongoza vyema
Chama chetu. Viongozi watakaokijenga na kukiimarisha Chama, siyo
wale watakaokigawa na kukidhoofisha. Tuchague viongozi ambao ni
wabunifu na wana uwezo wa kukisemea na kukitetea Chama chetu na
sera zake badala ya kuwa na viongozi ambao hawana wanalolijua, wana
upeo mfupi wa mawazo, hawana uwezo wa kukisemea na kukitetea
Chama chetu na wakati mwingine hata kupotosha ukweli. Tusichague
viongozi ambao wapo kwa ajili ya kunufaika wao binafsi na siyo Chama
kunufaika na uongozi wao. Tuchague viongozi wenye tabia na
mwenendo mwema na tuepuke kuchagua watu ambao jamii itaguna
kwa sababu ana tabia mbaya, mtenda maovu na asiyekuwa mwadilifu.
Tuchague viongozi wachapakazi hodari, wazalendo wa dhati, wenye
mapenzi mema na nchi yetu, Serikali na Chama chetu.
Ndugu wana CCM;
Nimezieleza sifa hizo kwa kirefu kwa sababu ya umuhimu wa
viongozi kwa uhai na maendeleo ya Chama chetu. Aidha, kwa sababu
8
kiongozi ndiye kioo ambacho huonesha jinsi Chama chetu
kinavyoonekana mbele za watu. Ni ukweli ulio wazi kuwa viongozi
wasiokuwa na sifa njema wamekuwa wanakiathiri Chama chetu katika
chaguzi za dola. Uchaguzi huu unatupa fursa nzuri ya kuachana na
viongozi wasiokuwa na sifa njema za uongozi ndani ya Chama chetu.
Katika kipindi hiki cha mageuzi, wana-CCM mmeona mengi na
mmesikia mengi. Viongozi wachochezi sasa mmewajua, viongozi watoa
na wala rushwa sasa mmewajua, viongozi wenye fitina pia mmewajua,
viongozi wanaokumbatia sera za kibaguzi za ukabila, udini na ukanda
nao mmewajua. Aidha, viongozi waadilifu, wazalendo na
wanaounganisha watu kwa kauli zao na matendo yao mmewajua.
Naomba tutimize wajibu wetu.
Wanachama mmepewa fursa ya kutekeleza mageuzi ya uongozi
katika Chama chetu kupitia Uchaguzi Mkuu wa Chama na Jumuiya
zake. Hii ndiyo maana ya kaulimbiu ya sherehe hii: “CCM imara
Inaanza na Mimi”. Hivyo, tusifanye ajizi katika uchaguzi huo. Ada ya
mja kunena, muungwana ni vitendo. Shime tukatende kwa kupiga
kura za mageuzi ya Chama. Kijua ndio hiki, tusipouanika mpunga
tutaula mbichi’.
Ndugu Wananchi na Viongozi wa CCM;
Ni imani yangu kwamba vikao vya Chama vitakavyoshughulika
na zoezi la kuchuja na kupitisha wagombea katika nafasi mbalimbali
watazingatia sifa za kikatiba nilizozitaja ambazo ni ufafanuzi sahihi wa
Katiba ya Chama. Wale watu wenye kukipunguzia Chama chetu hadhi
na sifa kwa kuwa na tuhuma mbalimbali za rushwa, ubadhirifu, wizi
n.k. wasipitishwe kugombea nafasi za uongozi. Aidha, wana-CCM
tusikubali kuchagua viongozi wetu kwa ushawishi wa fedha. Kufanya
hivyo ni haramu kwani kutakidhoofisha Chama chetu na historia
9
itatuhukumu. Jambo hili limeshusha sana haiba ya Chama chetu mbele
ya macho ya Watanzania, lazima tubadilike.
Vile vile tunapochagua wagombea, ni lazima sasa tuangalie
changamoto zilizo mbele yetu katika uchaguzi mkuu wa 2015.
Tuchague viongozi ambao watakuwa mstari wa mbele kukisemea,
kukitetea na kukipigania Chama chetu katika uchaguzi wa Serikali za
Mitaa 2014 na katika Uchaguzi Mkuu wa 2015. Tusichague watu ambao
ni mzigo na kuwa chanzo cha kukipunguzia Chama chetu sifa na
kutusababishia tusifanye vizuri. Lazima tuwachague viongozi wa
Chama wenye mvuto kwenye makundi yote katika jamii, vijana na
wazee, wanawake na wanaume, maskini na matajiri, wasomi na
wasiokuwa wasomi.
Mwisho naomba wana-CCM wenzangu mjitokeze kwa wingi
kugombea nafasi za uongozi katika ngazi mbalimbali. Hususan
ningependa kuona vijana na wanawake wengi wakijitokeza na naomba
vikao vya kujucha wagombea viwape nafasi wagombee.
Dhima ya CCM katika Mchakato wa Katiba
Ndugu viongozi na wanachama wa CCM;
Mtakumbuka kuwa tarehe 31 Desemba, 2010 katika salamu zangu
za kuuaga mwaka 2010 na kukaribisha mwaka 2011, nilielezea uamuzi
wangu wa kuanzisha mchakato wa kufanya mabadiliko ya Katiba
ambayo hatimaye yatalipatia taifa letu Katiba mpya. Utekelezaji wake
umeshaanza kwa kutungwa Sheria ya mabadiliko ya Katiba. Hivi sasa
Serikali imewasilisha Bungeni mapendekezo ya marekebisho ya baadhi
ya vifungu vya Sheria hiyo kwa nia ya kuiboresha. Mapendekezo hayo
yametokana na sisi wenyewe katika Serikali pamoja na vyama vya siasa
na Baraza la Mashirika ya Kijamii. Kwa upande wa vyama vya siasa
hata Chama cha Mapinduzi kilileta mapendekezo yake tena manane.
10
Baada ya kikao hiki cha Bunge tutaiunda Tume ya Mabadiliko ya
Katiba ili mchakato wa kukusanya maoni uanze. Napenda kutumia
nafasi hii ya kuadhimisha miaka 35 ya kuzaliwa kwa CCM kuwaomba
wana-CCM wote kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao. Viongozi wa
CCM wa ngazi zote wanalo jukumu la msingi la kuhakikisha kuwa
wanachama wetu wanaelimishwa vya kutosha kuhusu Katiba na
Mchakato mzima wa kutoa maoni. Andaeni mikutano ya kutoa elimu
na watafuteni watu wenye ufahamu wa masuala ya Katiba wasaidie
kuwaelimisha wanachama wetu. Katika kikao kilichopita cha Kamati
Kuu tulikubaliana kuwa Chama chetu nacho kitoe mwongozo wa
mafunzo hayo kwa wanachama. Kazi hiyo inaendelea na
itakapokamilika mtaarifiwa ipasavyo. Kwa muhtasari ninachosema ni
kuwa wana-CCM tujipange vizuri ili tuweze kushiriki kwa ukamilifu
katika mchakato wa kutengeneza Katiba mpya.
Ndugu Wanachama, Viongozi wa CCM na Wananchi Wote;
Kuna msemo wa Kiswahili usemao mcheza kwao hutunzwa.
Napenda kwa niaba yenu nitambue na kutoa shukrani maalum kwa
Wabunge wetu wa CCM kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya ya
kuelimisha wananchi kuhusu Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Kulikuwepo na kutokueleweka au hata kupotoshwa kwa Sheria hiyo.
Lakini, kutokana na kazi nzuri waliyofanya sehemu kubwa ya
Watanzania wameelewa. Hata hivyo, kazi hii endeleeni nayo kwani
hatujafika mwisho wa mchakato wenyewe. Hivyo naomba waendelee
kuelimisha sambamba na viongozi wa Chama na watu wenye nia njema
na nchi yetu
Mwisho
Ndugu viongozi na wanachama wa CCM;
Narudia kuwapongeza kwa mara nyingine tena wale wote
waliohusika na maandalizi ya sherehe hizi. Kwa hakika zimefana sana.
11
Zinafanana na hadhi ya mkoa wa Mwanza. Nawapongeza viongozi,
wanachama, makada, wapenzi na mashabiki wa CCM kwa kutimiza
miaka 35 ya uhai wa CCM. Nawaomba tutoke hapa na ari mpya, nguvu
mpya na kasi mpya kwenda kukijenga Chama chetu kote nchini. Na
kwa hapa Mwanza kujiandaa kuyakomboa majimbo ya Ilemela,
Nyamagana na Ukerewe. Kuteleza si kuanguka. Yaliyopita si ndwele,
tugange yajayo.
Ndugu Viongozi, Wanachama na Wananchi;
Kabla ya kumaliza, napenda kusema mambo mawili: Kwanza,
kuhusu vijana Wamachinga. Nimefurahi sana na maneno yenu.
Naahidi kuwa nitawasaidia. Tukutane baadae na uongozi wenu. La
pili, ni kwamba sikuyasemea masuala ya Madaktari na mengineyo kwa
vile katika siku chache zijazo nitapata nafasi ya kufanya hivyo. Kwa ajili
hiyo leo nimeona nizungumzie masuala yahusuyo Chama cha
Mapinduzi.
Mwisho kabisa, napenda kusema kuwa Chama chetu bado imara
na kwamba hatuna budi kuhakikisha kuwa kinazidi kuimarika.
Inawezekana. Timiza Wajibu wako.
.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZIII!
Asanteni sana kwa kunisikiliza!

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Featured

UJASUSI: Jinsi kijana wa kiume kutoka New Zealand alivyojaribu  kumuua Malikia Elizabeth II

Published

on

Shirika la Ujasusi la New Zealand  (SIS) limethibitisha kwa mara ya kwanza kwamba kulikuwa na jaribio la kumuua Malikia Elizabeth II wakati alipotembelea jiji la Kusini la Dunedin mwaka 1981.

Jaribio hilo la kumuua Malikia linalodaiwa kutekelezwa na kijana wa kiume limechochea hamasa ya polisi kutaka kujua ni kwa kiasi gani wanausalama hao walifanikiwa kuzima njama hizo.

Taarifa iliyotolewa na SIS  zinaonesha kuwa kijana huyo, Christopher Lewis (17) alipiga risasi kuelekea kwa Malikia wakati akishuka kwenye gari lake ambapo alikuwa anaenda kushuhudia Maonyesho ya Sayansi yaliyofanyika Oktoba 14, 1981 katika jiji hilo. Tukio hilo lilitokea akiwa katika ziara ya siku 8 kutembelea nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola.

“Lewis alidhamiria kumuua Malikia, hata hivyo hakuwa katika nafasi nzuri ya kurusha risasi, hata silaha iliyotumia haikuwa katika umbali wa kuweza kumfikia mhusika,” imesema taarifa iliyotumwa SIS kwa vyombo vya habari.

Lewis ambaye anatajwa kwenye taarifa ya ujasusi kama ‘kijana msumbufu’ hakuhukumiwa kwa jaribio la kutaka kuua au kosa la uhaini. Tukio hilo lilifanywa kuwa siri ili kuzuia sifa mbaya kwa nchi (New Zealand) ambayo ilitembelewa na mgeni wa heshima. Badala yake Lewis alihukumiwa kwa kumiliki silaha kinyume na sheria na kufyatua risasi.

                       Malikia Elizabeth II akiwa ameambatana na walinzi wake alipotembelea New Zealand

Inaelezwa kuwa watu waliohudhuria tukio la kuwasili kwa Malikia walisikia mlio wa risasi lakini Polisi waliokuwa wanasimamia usalama katika eneo hilo la Dunedin waliwaambia kuwa ilikuwa ni sauti ya kuanguka kwa kitu au magari kugongana.

“Uchunguzi wa sasa wa polisi juu milio iliyosikika umefanywa kwa umakini na wawakilishi wa vyombo vya habari wamepata mrejesho kuwa kelele zilisababishwa na baruti”, inaeleza ripoti kutoka SIS iliyotolewa mwaka 1981 baada ya kutokea tukio hilo.

Kulingana taarifa za ujasusi zinaeleza kuwa polisi wamekuwa wakifuatilia nyendo za Lewis tangu 1986 ambapo Malikia alitembelea tena New Zealand wakiogopa kuwa anaweza kutekeleza tena uhalifu huo. Kuwekwa wazi kwa siri hiyo kumewaibua polisi ambao wameanza kuchunguza upya kesi hiyo.

Zaidi ya muongo mmoja uliopita, Lewis alihukumiwa kwa mauaji ya mwanamke mmoja katika mji wa Auckland na kumteka mtoto wa kike ambapo baadaye alimtupa karibu na kanisa.

Kulingana na taarifa mbalimbali za wakati huo zinaeleza kuwa Lewis alijidhuru kwa umeme akiwa gerezani mnamo 1997 akisubiri hukumu ya kuua. Lakini alikana mashtaka ya kuua kwa ujumbe mfupi wa kifo (suicide note).

New Zealand ilipata uhuru mwaka 1947 kutoka kwa Uingereza lakini inamuheshimu Malikia kama kiongozi wa taifa. Ameitembelea nchi hiyo kama Malikia mara 10 na mara ya mwisho ilikuwa 2002.

Continue Reading

Featured

FREEDOM HOUSE: Tanzania ina uhuru kiasi, kufungiwa vyombo vya habari, kuzuia mikutano ya kisiasa kuididimiza kwenye nchi zisizo na uhuru kabisa

Published

on

Ripoti mpya iliyotolewa na taasisi huru ya Freedom House imesema misingi ya demokrasia ikiwemo uhuru wa vyombo vya habari na haki ya kukusanyika imeendelea kudhoofika nchini Tanzania na hali hiyo isiporekebishwa itaingia kwenye kundi la nchi zisizo na uhuru kabisa duniani.

Kulingana na  Freedom House  ambao walichambua data katika nchi 195 za ulimwenguni katika mwaka 2017 wamebaini kuwa nchi 88 zina uhuru,  58 zimejumuishwa kwenye kundi la nchi zenye uhuru kiasi huku 48 zikiwekwa kwenye kundi la nchi zisizo na uhuru kabisa.

Ripoti hiyo imebainisha kuwa misingi ya demokrasia ikiwemo uchaguzi usio huru na haki, uhuru wa kujieleza umeendelea kushuka kwa mwaka wa 12 mfufululizo duniani kote. Miongoni mwa matokeo yaliyostaajabisha ni kudhoofika kwa  Marekani ambayo ni mama wa demokrasia kutokana na uchunguzi unaofanywa na Mwendesha Mashtaka Maalumu kuhusu Urusi kuingilia uchaguzi mkuu wa mwaka 2016 ambao ulimpa ushindi Rais Donald Trump.

Tanzania imewekwa kwenye nchi 88 ambazo zina uhuru kiasi lakini inatahadharishwa kuwa inaweza kuingia kwenye nchi zisizo na uhuru kabisa. Tahadhari hiyo inatokana na mwenendo wa viongozi wa serikali kufungia vyombo vya habari, kuzuia mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, kushtakiwa kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii kwa tuhuma za uchochezi na kukamatwa kwa wapinzani wa kisiasa ambao wanakosoa na kutoa mawazo yanayotofautiana na serikali.

Pia utekelezaji wa Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015, Sheria ya Huduma ya Habari ya mwaka 2016 na Sheria ya Makosa ya Mtandao  ya mwaka 2015 umekuwa ukilalamikiwa na wadau wa maendeleo kuwa ni mkakati wa kudhoofisha uhuru wa kutoa maoni, uwazi na uwajibikaji.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) nchini hivi karibuni kilitoa tamko la tathmini ya uchaguzi mdogo wa marudio wa kuchagua madiwani uliofanyika katika kata 43 kwenye mikoa 19 ya Tanzania  Novemba 24 mwaka jana ambapo kilibaini mambo mbalimbali ya ukiukwaji wa haki za binadamu.

Tathmini hiyo iliibua mambo mbalimbali ikiwemo matumizi mabaya ya nguvu ya vyombo vya dola, matukio ya watu kutekwa na watu wasiojulikana, watu kupigwa, kujeruhiwa  kwa lengo la kuharibu na kuvuruga uchaguzi  na vilevile kuwatia hofu wapiga kura.

 

Afrika Mashariki hali bado tete

Tanzania inaungana nchi nyingine za Afrika Mashariki ikiwemo Kenya na Uganda ambazo nazo zimewekwa kwenye kundi la nchi zenye uhuru kiasi huku za Rwanda, Burundi na Sudan ya Kusini zimejumuishwa kwenye nchi zisizo na uhuru kabisa.

Awali Uganda ilikuwa kwenye nchi zisizo na uhuru kabisa lakini imepanda hadi kwenye uhuru kiasi kwasababu ya  kuimarika kwa tasnia ya habari na utashi wa wanahabari, blogu na  uhuru wa wananchi kutoa maoni yao licha ya mazingira ya kisiasa kuminywa na utawala wa muda mrefu wa Rais Yoweri Museveni.

Rais Museveni mwenye umri wa miaka 73 amekuwepo madarakani  tangu 1986 amefanikiwa kubadilisha sheria  ya ukomo wa umri wa miaka 75 wa kugombea urais ambapo atapata fursa ya kugombea tena mwaka 2021. Chaguzi nchini Uganda zimekuwa zikitawaliwa na vurugu za polisi na wananchi, kuzimwa kwa intaneti na kuwekwa kizuizini kwa viongozi wa upinzani ikiwemo Kizza Besigye wa chama cha Forum for Democratic Change.

Kwa upande wa Kenya ambayo imekuwa ikisifika kwa kuimarisha misingi ya demokrasia katika ukanda wa Afrika Mashariki ambapo kwa mara ya kwanza mahakama ilifanikiwa kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa Urais yaliyompa ushindi Rais Uhuru Kenyatta uliofanyika Agosti 2018. Uchaguzi ulirudiwa na Rais Kenyatta alichaguliwa tena.

Marudio ya uchaguzi yalilamikiwa na baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa kuwa hayakuzingatia haki za binadamu ambapo watu ambao walipinga uchaguzi huo walikumbana na mkono wa dola. Matendo hayo ndiyo yaliiweka Kenya kwenye kundi la nchi zilizo na uhuru kiasi.

Burundi na Sudan Kusini zimewekwa kwenye kundi la nchi zisizo na uhuru kabisa kutokana na mapigano ya kikabila ambayo yamedhoofisha mfumo wa kisiasa wa kuongoza nchi. Vyombo vya habari na wananchi wanaotoa maoni tofauti na serikali wamekuwa wakiteswa, kufungwa na kuuwawa.

Chanzo: Freedom House           – Nchi zisizo na  uhuru  – Nchi zenye uhuru     – nchi zenye uhuru kiasi   

 

Hali ilivyo Afrika

Afrika kama zilivyo nchi za Afrika Mashariki hali ya demokrasia siyo ya kuridhisha ikizingatiwa kuwa asilimia 11 ya wakazi wapatao bilioni 1.02 wa bara hilo ndio wana uhuru wa kweli, huku 52% wana uhuru kiasi na 37% hawa uhuru kabisa.

Ripoti ya Freedom House inaeleza kuwa waliangazia nchi 49 za Afrika na kugundua kuwa nchi 8 (18%) ndio zina uhuru wa kweli, nchi 22 (43%) zina uhuru kiasi na 19 (39%) hazina uhuru kabisa. Nchi zinazotajwa kuwa na uhuru ni Afrika Kusini, Namibia, Botswana, Ghana, Togo, Senegal na Kisiwa cha Sao Tome.

 Sababu ya nchi nyingi za Afrika kuwepo kwenye kundi la zisizo na uhuru ni matokeo ya viongozi kukaa madarakani muda mrefu, vurugu za kisiasa na kikabila ambazo zimekuwa zikihatarisha haki za binadamu.

 

Demokrasia ya Dunia

Demokrasia ya dunia inakabiliwa na mzozo mkubwa wa kisiasa kuliko wakati mwingine ambapo mwaka 2017 ulishuhudia ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ikiwemo kuminywa kwa  uchaguzi huru na kweli, haki za watu wachache, uhuru wa kujieleza, utawala wa sheria.

Nchi 71 kati ya 195 zimeshuhudiwa zikiteteleka katika kulinda haki za kisiasa na jamii ambapo ni nchi 35 tu ndizo zimeweza kulinda haki hizo. Kudhoofika kwa demokrasia kunaendelea kushuka kwa miaka 12 mfululizo na hatua muhimu zisipochukuliwa amani ya dunia itawekwa rehani.

Marekani ambayo ni bingwa wa demokrasia duniani nayo imeripotiwa na taasisi ya Freedom House kudhoofika katika kulinda haki za kisiasa na kijamii na kuzua mgongano wa mawazo miongoni mwa nchi zinazoibukia katika kujenga demokrasia ya dunia.

Tangu kuisha kwa vita baridi, nchi nyingi ziliachana na utawala wa kiimla na kugeukia demokrasia ya vyama vingi lakini hali hiyo imeanza kujitokeza tena ambapo idadi ya viongozi wanaoongoza kwa udikteta inaongezeka.

 

Uhuru wa nchi moja unategemea uhuru wa nchi zote

Demokrasia itabaki kuwa tunu muhimu kwa jamii zilizostaarabika, ikifungua milango ya uwazi, mawazo na fursa mpya na zaidi ya yote kulinda uhuru wa mtu mmoja mmoja. Ikiwa watu duniani kote wanadai mazingira mazuri ya kisiasa ni dhahiri wanakumbatia misingi ya demokrasia: uchaguzi huru, uhuru wa kujieleza, uwazi na uwajibikaji wa serikali, utawala wa sheria ambao hauingiliwi na polisi, jeshi au taasisi nyingine za nchi.

Hata hivyo, Karne ya 21 imeshuhudia ugumu wa kuifanya demokrasia kuwa endelevu ambapo baadhi ya nchi zinatekeleza lakini zingine zinapuuza. Utawala wa kidekteta wa Urusi na China unatambua wazi ili uendelee kuwepo unahitaji kuimarisha demokrasia katika nchi nyingine ili ziendelee kufaidika na mahusiano ya kidiplomasia. Ukuaji wa  demokrasia ni kulinda haki za watu wote duniani kupitia utandawazi   

Continue Reading

Afya

Is Tanzania’s Adolescent Fertility Rate Three Times Higher Than Global Counterparts?

Published

on

The Comprehensive Community-Based Rehabilitation in Tanzania (CCBRT), an organization ​which works to provide affordable medical and rehabilitative services for mothers and newborns throughout Dar-es-Salaam, marked World Contraception Day on September 26 with a call for more efforts to meet the reproductive health needs of teens between 15 and 19 years old.

The report highlights a worrying statistic — Tanzania’s adolescents are having almost three times as many children on average as their global counterparts, with 135 births per 1000 girls reported in the country, compared to an average of 44 per 1000 girls aged 15–19 worldwide in 2015.

CCRBT attributes the high adolescent fertility rate to a lack of access to contraceptive services, with Technical Advisor for Nursing Bola Abbas saying, that only about 8 per cent of current family planning clients are between the ages of 15 to 19.

On a national scale, Abbas explains, demand for family planning among adolescent girls is still very low, with only one out of every three of those who are sexually active within the 15 to 19 age group using modern contraceptive methods.

So the question is, how does Tanzania’s adolescent fertility rate compare to that of the rest of the world?

Pesacheck investigated the claim that Tanzanian adolescents are having three times as many children as their peers in the rest of the world and found that the statement is TRUE for the following reasons:

Tanzania’s adolescent fertility numbers are rather high, with 4.4% of girls aged 15 having given birth according to the country’s Demographic and Health Survey.

The Sustainable Development Goals call for countries to ensure universal access to sexual and reproductive healthcare services, including family planning, information and education, and the integration of reproductive health into national strategies and programmes by 2030.

The indicators for this goal are the proportion of women of reproductive age (15–49 years) who have their need for family planning satisfied with modern methods, and the adolescent birth rate (10–14 years and 15–19 years) per 1,000 women in that age group.

For several sub-Saharan countries, Tanzania included, access to modern family planning methods is low for this particular age group, and as a result, the regional average is 105 births per 1,000, which is more than double the global average.

Tanzania’s National Bureau of Statistics produced a national fertility and nuptiality report based on data from the 2012 national census, which shows that Adolescent Fertility Rate (AFR) was 81 births per 1,000 women aged 15–19.

The report further shows that in 2012, 23.3% of adolescent girls in the country had given birth to at least one child. Additionally, 42.2% of girls who had never attended school had given birth, compared to just 9% of those who had reached university.

This shows that there is a need for contraceptive access for teenage girls in Tanzania, especially for girls in rural areas and those with limited access to education.

The Tanzania Demographic and Health Survey 2015–16 indicates that 27% of girls aged 15–19 have given birth. Crude birth rates for girls aged 15–19 show that there 135 births per 1,000 girls in Mainland Tanzania and 132 per 1,000 girls in Zanzibar, way above the global average of 44. The data also shows that contraceptive access for this age group is also quite low, with 10.4% of girls aged 15–49 using any form of contraception.

It would therefore appear that the lack of access to contraceptives is contributing to the increased likelihood of adolescent girls getting pregnant.

So the claim by CCBRT that Tanzania’s adolescent fertility rate is almost three times the global average is TRUE. This is driven largely by a lack of access to contraceptives for young people in the 15–19 age group, and the relatively high levels of poverty that have driven many out of school and into early marriage.

As a result, the country is unlikely to meet the Sustainable Development Goal of overall good health and wellbeing of mothers unless it puts measures in place to ensure universal access to sexual and reproductive health-care services for girls and women of all ages.

Do you want us to fact-check something a politician or other public figure has said about public finances? Complete this form, or reach out to us on any of the contacts below, and we’ll help ensure you’re not getting bamboozled.

This report was written by PesaCheck Fellow Belinda Japhet, a Communications Consultant, Online Editor based in Tanzania. The infographics are by PesaCheck Fellow Brian Wachanga, who is a Kenyan civic technologist interested in data visualisation. This report was edited by PesaCheck Managing Editor Eric Mugendi.

Continue Reading

Muhimu Kusoma

Copyright © 2020 FikraPevu.com