Connect with us

Afya

Watoto wachanga milioni 77 hawapati maziwa ya mama muda mfupi baada ya kuzaliwa, huchangia asilimia 80 ya vifo vyao

Published

on

Shirika la Watoto Duniani (UNICEF) limesema  watoto milioni 77 ambao ni sawa na mtoto 1 kati ya 2 wanaozaliwa hawapati maziwa ya mama  muda mfupi baada ya kuzaliwa ambapo wanakosa virutubisho muhimu, kinga ya mwili na kugusana na mama zao ili kuwakinga na magonjwa na vifo.

Wataalamu wa Afya wanashauri kuwa mtoto apewe maziwa ya mama ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa ili kumkinga na maambukizi ya magonjwa ya utotoni. Kutokana na sababu mbalimbali za kuchelewa kumnyonyesha mtoto baada ya kuzaliwa huwaongezea hatari ya kufa mapema kwa zaidi ya asilimia 80.

“Nilimzaa mtoto wangu nikiwa nyumbani, hakupata chanjo wala sikumyonyesha alipozaliwa”, hayo ni maneno ya Asha Maulid msichana wa miaka 17 mkaazi wa Mtwara ambaye ana mtoto wa miezi 6. Anasema mtoto wake anaumwa mara kwa mara na anatumia gharama kubwa kumtibu lakini hapati nafuu.

“Mwanangu anaumwa mara kwa mara, amedhohofika sina pesa ya kumpeleka hospitali  na mimi nina maisha magumu sina uwezo kumtunza na kumpa lishe kamili”, amesema Asha.

Asha kama walivyo wasichana wengine ambao wanapata mimba za utotoni, wanakabiliwa na changamoto ya uelewa mdogo wa kuwatunza watoto wakiwa wadogo na kuwaweka katika hatari ya kushambuliwa na magonjwa na kufariki katika umri mdogo.

Anasema alikuwa anaishi Mtwara na mama yake lakini baada ya kupata mimba alifukuzwa nyumbani   na alikimbilia Wilaya ya Mkurunga mkoa wa Pwani ambako huko alisaidiwa na dada mmoja aitwaye Monica na kujifungua mwezi Aprili mwaka huu. Kutokana na ugumu wa maisha alijifungulia nyumbani lakini tangu wakati huo mtoto wake hana furaha kwa sababu ya kukosa mlo kamili ana huduma muhimu za afya.

 France Begin, Mshauri Mkuu wa Lishe wa UNICEF, anasema  “Kuwaacha watoto kusubiri muda mrefu kabla ya kugusana na mama zao baada ya kuzaliwa kunapunguza nafasi ya watoto kuishi, kupata maziwa”, anaeleza katika ripoti ya UNICEF 2016 na kuongeza kuwa ikiwa watoto wote watanyonyeshwa maziwa ya mama na sio kitu kingine mpaka miezi sita, basi maisha ya watoto 800,000 yangeokolewa kila mwaka.

Mama akimnyonyesha mtoto wake

Takwimu za UNICEF zinaonyesha kuwa mikakati ya kuwawezesha watoto wanaozaliwa kupata maziwa muda mfupi baada ya kuzaliwa imepungua kwa miaka 15 iliyopita. Mfano katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, vifo vya watoto chini ya miaka 5 vimekuwa kwa kiwango cha juu kuliko maeneo mengine duniani.

 Unyonyeshaji wa watoto muda mfupi baada ya kuzaliwa umeongezeka kwa asilimia 10 tangu mwaka 2000 katika nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika na hazijabadilika katika nchi za Magharibi na Afrika ya Kati.

 Kulingana na ripoti ya  Uchunguzi wa Lishe ya Taifa (NNS 2014) inaeleza kuwa mtoto 1 kati ya 2 walio na miezi 0 hadi 23 wanafaidika na mradi wa kunyonyeshwa maziwa ya mama. Lakini katika baadhi maeneo ya mikoa ya Tabora, Geita, Shinyanga, Rukwa na Katavi, unyonyeshaji wa maziwa kwa watoto uko chini ya 25%.

 Inaelezwa kuwa kadiri mtoto anavyocheleweshwa kunyonyeshwa maziwa ya mama muda mfupi baada ya kuzaliwa hatari ya kufa katika miezi mitano ya maisha yake inaongezeka. Kuchelewa kunyonya kati ya saa 2 hadi 23 baada ya kuzaliwa kunaongeza hatari ya kufa kwa mtoto aliye na siku 28 kwa 40%. Hivyo hivyo kwa saa 24 au zaidi hatari huongezeka hadi asilimia 80.

 UNICEF inasema kuwa maziwa ya mama ni kinga na ulinzi  wa kwanza kwa mtoto dhidi ya udhaifu na magonjwa. Kukosa maziwa ya mama kunachangia karibu nusu ya vifo vyote vya watoto wachanga lakini maziwa ya mama yakiwekewa msisitizo italeta tofauti katika maisha na kifo kwa watoto.

Mila na Desturi, kukosa maarifa na kutoshirikishwa kwa wanawake wa Tanzania kunachangia kwa sehemu kubwa kwa watoto wachanga kutopata maziwa ya mama muda mfupi baada ya kuzaliwa. Pia kuwapa watoto vimiminika na chakula katika kipindi cha kwanza cha miezi sita ni sababu nyingine ya kuchelewa kuwanyonyesha watoto.

Mwakilishi wa UNICEF Tanzania, Maniza Zaman alinukuliwa na vyombo akisema wanaendelea kuweka mikakati madhubuti ili kuhakikisha watoto na mama zao wanafaidika na program ya shirika hilo ya kuwanyonyesha watoto maziwa ya mama ili kuwaepusha na magonjwa na  vifo vya utotoni.

 Hata hivyo, takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 43 ya watoto wote walio chini ya miezi sita wanapata maziwa ya mama duniani kote. Watoto ambao hawapati maziwa ya mama kabisa wana  uwezekano kufa mara 14 zaidi ya wale ambao wanapata maziwa ya mama pekee.

Ripoti ya NNS inaeleza kuwa 41% ya watoto walio chini ya miezi 6 walipata maziwa ya mama kwa mwaka 2014 nchini Tanzania. Katika baadhi ya maeneo ya Ruvuma na Tanga takwimu zinaonyesha kuwa ilikuwa ni chini ya 25%,  huku Zanzibar ikiwa 20% lakini Pemba ikiwa chini ya 10% ya watoto wote waliokuwa wanapata maziwa ya mama kwa mwaka 2014.

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa kiwango chochote cha maziwa ya mama kwa mtoto kinapunguza hatari ya kufa. Watoto ambao hawapati kabisa maziwa ya mama wana uwezekano mara 7 zaidi kufa kutokana na maambukizi ya magonjwa kuliko wale ambao wanapata maziwa ya mama katika kipindi cha miezi 6 ya kwanza ya kuzaliwa kwao.

 Elimu zaidi inatakiwa kutolewa kwa wanawake na wauuguzi katika vituo vya afya na hospitali juu ya umuhimu wa maziwa ya mama kwa mtoto muda mfupi baada ya kuzaliwa. Pia mtoto anatakiwa kugusana na mama yake ili kuimarisha mahusiano na kumkinga na magonjwa ya utotoni

Shirika la Afya Duniani (WHO) linapendekeza:

Linapendekeza kunyonyesha maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya kwanza katika maisha ya mtoto. Mama anatakiwa kupewa vyakula vyenye virutubisho muhimu.

  • Mtoto anapaswa kuanza kunyonya ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa
  • Mtoto lazima anyonye kulingana na mahitaji yake kila mara anapohitaji.
  • Unyonyeshaji wa chupa unatakiwa kuepukwa
Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Afya

Watumishi wa afya 200 kupatiwa mafunzo ya utoaji dawa ya usingizi kuokoa maisha wajawazito

Published

on

Kufuatia upungufu wa wataalamu wa dawa za usingizi (anaesthesia), serikali itatoa mafunzo ya dawa za usingizi kwa watumishi wa afya 200 katika vituo vya afya vya upasuaji wa dharura kwa akina mama wajawazito.

Hatua hiyo inakuja ikiwa imepita miezi 6 baada ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kutangaza kuanza kutoa shahada ya dawa ya usingizi (Bsc. Anaesthesia Nursing).

Katika taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano serikalini cha Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, inaeleza kuwa mafunzo hayo yatatolewa sambamba na uboreshaji wa huduma ya upasuaji wa dharura kwa wajawazito ili kuokoa maisha ya wanawake na watoto ambao hufariki kwa kosa huduma muhimu za uzazi kwenye vituo vya afya.

“Mkakati wa kuhakikisha huduma za afya kwa akina mama wajawazito zinakuwa salama na uhakika kwa kuandaa rasilimali watu, miundombinu ya majengo na vifaa vitakavyowezesha huduma hizi ikiwemo upasuaji wa dharura kwa akina mama wajawazito wakati wa kujifungua,” imeeleza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya, vifo 556 vitokanavyo na uzazi kwa kila viumbe hai 100,000 huripotiwa kila mwaka katika maeneo mbalimbali nchini. Maana yake ni kwamba watoto na wajawazito hufariki hasa wakati wa mama akijifungua.

Aidha, serikali itaboresha vituo vya afya 288 vya serikali vilivyopo nchini ili kuviwezesha kutoa huduma ya dharura ya upasuaji kwa wajawazito ambapo waaguzi katika vituo hivyo watapatiwa mafunzo ya dawa za usingizi ili kuokoa maisha ya akina mama na watoto wachanga.

Utekelezaji wa mafunzo hayo ni matokeo ya ushirikiano wa Wizara ya Afya na Mfuko wa Pamoja wa Afya ambapo zaidi ya sh1,079 bilioni zimepatikana kufakisha mafunzo hayo ya dawa ya usingizi kwa wauguzi na matabibu waliopo kwenye vtuo vya afya nchini.

“Fedha hizo zitasomesha watumishi wapatao 200, kati ya watumishi hao 100 watapata mafunzo yao katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na MOI, watumishi 50 watafanya mafunzo katika hospitali ya KCMC, na 50 watafanya mafunzo hayo kwenye hospitali ya Bugando,” imefafanua taarifa ya wizara.

Lengo la serikali ni kuhakikisha ifikapo 2019 na kabla ya 2020 vituo vyote vya afya vinavyomilikiwa na serikali vinakuwa na watumishi maalum wa kutoa huduma ya dawa ya usingizi kwaajili ya wapasuaji wasiopungua wawili kwa kila kituo.

Mafunzo hayo ya mwaka mmoja ni mpito wakati serikali ikiendelea kukamilisha taratibu za kurasimisha utoaji wa shahada ya kwanza ya kutoa dawa ya usingizi katika Chuo cha MUHAS katka mwaka huu wa 2018/2019.

Hali halisi ya huduma ya dawa za usingizi nchini
Takwimu za wizara ya Afya zinaonyesha kuwa kuna upungufu mkubwa wa madaktari wenye utaalamu wa kutoa dawa ya usingizi hasa wakati wa huduma ya upasuaji ambapo kwa sasa waliopo ni asilimia 1.2 tu ya mahitaji yote.

Ili kuweza kukidhi mahitaji yote ya huduma hiyo wanahitajika madaktari 2000, lakini waliopo sasa ni madaktari 30 pekee.

Kufuatia changamoto hiyo Januari 31, mwaka huu wadau mbalimbali wa afya na elimu walikutana na kujadili namna ya kuondoa changamoto hiyo na kupendekeza mtaala utakaotumika kufundishia kozi ya Aesthesia kabla ya kuupeleka kwa Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU).

” Ni kweli kumekuwepo kwa changamoto hiyo ya watalaamu wa dawa hizo lakini sasa mpango huu ukikamilika maana yake tutaongeza idadi ya madaktari kamili maana hawa waliopo wengi ni wale ambao wamesoma kozi kwa mwaka mmoja au miwili.

” Mafunzo yakianza kutolewa hapa chuoni Muhimbili wataweza kuchukua wanafunzi 200, Bugando 50 na KCMC 50 jambo ambalo litaongeza idadi kubwa ya watalaamu ili kuweza kufikia lengo letu la kuwa na wataalamu 2000 nchi nzima,” alinukuliwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Mpoki Ulisubisya.

Continue Reading

Afya

Vyakula hivi vitakulinda dhidi ya athari za kiafya za uchafuzi wa hewa

Published

on

Tunaishi katika ulimwengu unaokabiliwa na athari kubwa za mabadiliko ya hali ya hewa. Moja ya athari hizo ni kuongezeka kwa joto na kupungua kwa mvua katika maeneo mbalimbali. Athari hizi zinagusa moja kwa moja afya ya binadamu.

Ripoti ya mabadiliko ya hali ya hewa ya mwaka 2017 imeonesha kuwa kuongezeka kwa joto kunaathiri afya ya binadamu kwa kiasi kikubwa. Ripoti hiyo inatoka kundi la vyuo mbalimbali na mashirika tofauti ya Umoja wa Mataifa inasema watu wengi wanaathirika na joto pamoja na mlo hafifu sambamba na kusambaa kwa magonjwa.

Moja ya kisababishi cha mabadiliko ya hali ya hewa ni uchafuzi wa anga. Uchafuzi wa anga ni kuchanganyika kwa hewa asili katika anga na vitu kama vile moshi, majivu, gesi za kemikali katika hali na kiwango ambacho huathiri sifa ya hewa na kusababisha madhara kwa binadamu na viumbe vingine.

Baadhi ya vitu na vitendo huathiri vibaya anga letu. Baadhi ya vitu hivyo ni kama gesi na moshi unaotoka kwenye viwanda, moshi kutoka kwenye magari, marashi, dawa ya kuuwa wadudu shambani na kadhalika.

Lakini umewahi kujiuliza kuwa aina ya chakula unachokula kinaweza kukusaidia kukabiliana na athari za kiafya zinazotokana na uchafuzi wa hewa?

Wanasayansi katika utafiti wao uliotolewa hivi karibuni, wanaeleza ulaji wa chakula cha Mediterania ( Mediterranean diet) chenye matunda mengi, mbogamboga, nafaka isiyokobolewa, samaki, maharage jamii ya soya, mafuta ya mizeituni na mayai yanaweza kuwalinda watu dhidi ya athari za afya zinazotokana na uchafuzi wa hewa.

Wanasayansi hao kutoka Shule kuu ya Udaktari ya NYU ya Marekani, walichambua data za watu takribani 550,000 wenye wastani wa umri wa miaka 62 kwa miaka zaidi ya 17 ambapo waliwapanga watu hao kwenye makundi kulingana na ulaji wao unaoendana na chakula cha Mediterania na kulinganisha na muda waliokaa kwenye hewa iliyochafuliwa.

Walibaini kuwa watu ambao walizingatia kula vyakula vilivyotajwa hapo juu walikuwa na uwezekano mkubwa wa kuepuka magonjwa na vifo vinavyotokana na uchafuzi wa hali ya hewa. Magonjwa hayo ni yale ya mfumo wa upumuaji, moyo na kansa.

                                   Vyakula  jamii ya Mediterania

Vyakula hivyo jamii ya Mediterania vina uwezo mkubwa wa kukabiliana na vimelea vya maambukizi ya magonjwa kwa mtu ambaye atazingatia kwa usahihi kutumia katika maisha yake.

Uchafuzi wa hewa unasababisha athari mbaya za kiafya kupitia hewa ukaa na mlo wa Mediterania una virutubisho muhimu kupambana na vimelea vya magonjwa,” anasema Mwandishi Mtafiti wa utafiti huo, Chris Lim wa Chuo cha NYU.

Lim anasema vyakula vya aina nyingine vinaweza kusaidia kukabiliana na athari hiyo. “Nilipoangalia kila mchanganyiko wa chakula cha Mediterania, kina matunda, mbogamboga na mafuta yanayoweza kupambana na athari za hewa chafu,” anasema.

Utafiti kuhusu ulaji kama unaweza kuzuia athari za kiafya za uchafuzi wa hewa bado haujahakikiwa na kukubalika kisayansi. Lakini utafiti huo sio wa kwanza kutafuta uhusiano wa mlo na athari za kiafya za uchafuzi wa hali ya hewa.

Wakala wa Uhifadhi wa Mazingira wa Marekani (U.S. Environmental Protection Agency (EPA)) unatafiti kama mlo unaweza kumlinda mtu dhidi ya athari za uchafuzi wa mazingira. Pia wanatafiti ili kujiridhisha kama virutubisho hivyo vinaweza kutumika badala ya dawa za kitabibu na kwa kiasi gani mtu anatakiwa apate virutubisho hivyo kumhakikishia usalama dhidi ya uchafuzi huo.

Hata hivyo, bado watu wanashauriwa kutumia zaidi matunda na mbogamboga kwenye milo yao ya kila siku ili kupata faida mbalimbali za kiafya.

Continue Reading

Afya

Ulaji mbaya wa chakula watajwa kusababisha kansa ya matiti kwa wanawake

Published

on

Thamani ya maisha haiko kwenye muonekano wa mtu na vitu vinavyomzunguka bali kwenye chakula anachokula kila siku ili kuwa na afya njema. Lakini umewahi kujiuliza, chakula kinawezaje kupunguza uwezekano wa kufa kutokana na magonjwa ikiwemo kansa?

Utafiti mpya uliofanyika huko Marekani umebaini kuwa kwa sehemu mlo kamili unaweza kupunguza hatari ya kufa kwa kansa.

Mtafiti Dk. Rowan Chlebowski wa Kituo cha Taifa cha Uuguzi cha City of Hope na wenzake walichambua takwimu za wanawake 48,000 waliosajiliwa katika mpango wa Afya ya Mwanamke unaoratibiwa katika vituo 40 nchini Marekani.

Awali wanawake wote walipata vipimo na hakuna aliyegundulika kuwa na kansa ya matiti lakini 20,000 kati yao walishauriwa kubadilisha mlo na kupunguza ulaji wa mafuta kwa asilimia 20 katika milo yao ya kila siku.

Pia waliambiwa wale zaidi matunda, mbogamboga na nafaka zisizokobolewa. Wanawake wengine hawakupewa maelekezo yoyote ya kuzingatia mlo kamili lakini walifundishwa kuhusu lishe nzuri na mlo wenye afya.

Baada ya miaka nane ya kuwafuatilia wanawake hao, watafiti hao waliangalia idadi ya kansa ambazo wanawake hao walitibiwa na zile ambazo zilisababisha vifo. Walibaini kuwa wanawake ambao walitumia kiasi kidogo cha mafuta walikuwa na hatari ndogo ya kufa kwa kansa ya matiti kwa asilimia 22, ukilinganisha na wanawake wengine.

Pia wanawake hao walipunguza kwa asilimia 24 hatari ya kufa kwa kansa zingine ikiwemo kwa 38%  magonjwa ya moyo ikilinganishwa na wanawake wa kundi ambalo walipata elimu ya mlo.

“Tunachokiona ni matokeo halisi,” anasema Dk. Chlebowski. Tafiti za awali ziliangalia madhara kabla ya uchunguzi wa kansa, lakini utafiti huu ulichambua kwa kiasi gani mlo unaweza kumuathiri mtu baada ya uchunguzi.

“Tulichobaini ni kuwa ushauri wa mlo baada ya uchunguzi wa kansa ya matiti ulikuwa muhimu kuliko kabla ya uchunguzi.”

                        Ulaji wa matunda na mboga unasaidia kupunguza hatari ya kupata kansa

Hata hivyo, utafiti huo ulibaini kuwa wanawake ambao wanazingatia kutumia kiasi kidogo cha mafuta katika maisha yao wana nafasi kubwa ya kuepuka kansa ya matiti.

Kutokana na idadi ya watu walioshirikishwa kwenye utafiti huo, Dkt. Chlebowski anasema wazo la kuhusisha mlo katika programu ya matibabu lilikuwa ni muhimu ili kupata matokeo chanya katika kukabiliana na kansa ya matiti kwa wanawake.

Watafiti hao wanaendelea na uchunguzi ili kufahamu kama ulaji wa chakula unaweza kuwa sehemu ya matibabu ya kansa ya matiti. “Inahamasisha kwasababu tunajaribu kuziba pengo kati ya mtindo wa maisha na mchakato wa kibaiolojia uliopo nyuma ya ugonjwa huo.”

 

Kansa ya matiti

Saratani ya matiti ni ugonjwa ambao huwapata wanawake na unatokana na athari za chembe ndogo ama seli kwenye matiti na matokeo yake ni kwamba hubadili mfumo wa kawaida wa kukua na kuongezeka.

Mabadiliko haya huanza polepole na yanaweza yakachukua muda mrefu hadi mtu kuweza kujua kama ana matatizo hayo. Ikiwa katika hatua hizo za mwanzo kwa kawaida huwa hakuna maumivu jambo hilo ni moja ya mambo ambayo huchangia baadhi ya wagonjwa kubaini tatizo hilo wakati tayari limekomaa.

Ni kutokana na sababu hizo, wanawake hutakiwa kuchunguza afya zao mara kwa mara kwasababu ugonjwa huweza kutibiwa kirahisi iwapo utabainika mapema.

Miongoni mwa dalili za saratani ya matiti ni uvimbe kwenye matiti ama makwapani. Titi kubadilika kiumbo, titi kutoa majimaji yaliyochanganyika na damu ama chuchu kuingia ndani.

Zipo aina mbalimbali za tiba na mojawapo ni upasuaji. Upasuaji huu kwa kawaida hufanywa katika hatua za mwanzo. Njia nyingine ni tiba ya mionzi au kupewa dawa. Jambo la kukumbukwa ni kwamba ugonjwa huu unaweza kusababisha kifo iwapo hautabainika mapema na kupatiwa tiba mwafaka.

Njia ambayo mtu aweza kujilinda asiathirike na saratani hii ya matiti ni kujichunguza mara kwa mara ili kubaini mapema na kupatiwa dawa.

Mwanamke anapaswa kuchunguzwa mara moja kwa mwaka ili kuona kama ameathirika na ugonjwa huo au la.

Continue Reading

Muhimu Kusoma

Copyright © 2020 FikraPevu.com